Tembea katika Nuru ya Mwokozi
Unapokuja kwa Yesu Kristo na kutubu, nguvu Yake ya uponyaji na kuimarisha itakuongoza utoke gizani.
Nikiwa katika safari moja ndefu kwa ndege kama kapteni wa shirika la ndege, ningeweza kuruka kutoka Ujerumani saa 5:00 asubuhi, na kutua huko California saa 7:00 mchana siku hiyo hiyo. Ukilinganisha muda wa kuondoka na muda wa kuwasili, inaweza kuonekana kama safari ya ndege kuvuka Bahari ya Atlantiki na bara la Amerika ya Kaskazini imechukua kama saa mbili tu.
Ndege Boeing 747 ina mwendo kasi, lakini sio kasi hivyo! Katika uhalisia, safari imechukua takribani saa 11, inategemeana na upepo, kusafiri maili 5,600 (kilometa 9,000)
Kwa sababu tulikuwa tukisafiri kuja magharibi, jua halizami wakati wa safari yetu. Tulikuwa tukifurahia mwangaza wa siku njia nzima kutokea Ujerumani hadi California. Kurudi Ujerumani hata hivyo, ilikuwa ni hadithi tofauti kabisa. Tulipokuwa tukisafiri mashariki, jua lilizama haraka zaidi kuliko kawaida, na kabla hatujajua, usiku ulikuwa umetufunika.
Hata wakati wa kusafiri usiku, katika giza totoro, nilijua kwa uhakika kwamba jua limebaki lisobadilika, thabiti, na la kutegemewa. Nilijua kwamba mwishowe jua lingechomoza, na nuru angavu ingerudi kuleta joto na uzima kwa siku mpya kabla ya mwisho wa safari yetu.
Wakati mwingine mambo yanayotuzunguka yanaweza kuonekana sio thabiti, yasiyotabirika, na kiza. Nina shukrani jinsi gani kwa sababu ya Yesu Kristo. Yeye ni nuru na uzima wa ulimwengu. Kwa sababu Yake, tunalo tumaini la siku zijazo, njia ya kufikia nuru Yake ya kiungu, na ahadi ya hatima ya ushindi juu ya dhambi na mauti.
Upendo na Nguvu ya Mwokozi
Kwa sababu ya upendo Wake kwetu, Yesu Kristo alitoa uhai Wake kwa ajili ya watoto wote wa Mungu na kufungua lango la maisha ya milele na uzima wa milele.
Licha ya kile Shetani anachotaka wewe uamini, wewe hauko ng’ambo ya pili ya uwezo wa Mwokozi wa kuokoa. Kamwe hauko mbali kuwa “umezingirwa milele katika mikono ya upendo wake” (2 Nefi 1:15).
Hii iliyo kuu kuliko zawadi zote inatoka kwenye nguvu inayowezesha na kukomboa ya Upatanisho wa Yesu Kristo. Kwa sababu ya mateso ya Mwokozi katika Gethsemani na Golgota, Yeye anajua jinsi ya kukusaidia katika changamoto yoyote na zote zinazo kukabili (ona Alma 7:11–12).
Rais Russell M. Nelson amesema: “Wakati Mwokozi alipotoa [dhabihu hii ya kulipia dhambi] kwa wanadamu wote, Yeye alifungua njia ambayo wale wanaomfuata Yeye wanaweza kufikia nguvu Yake ya uponyaji, uimarishaji na ukombozi.”
Nguvu hiyo, kama vile jua, daima ipo hapo. Kamwe haiyumbi. Kufuata katika hatua za Mwokozi ni kama kutembea nje ya vivuli na ndani ya mwangaza wa jua, mahali unapoweza kupokea baraka za nuru ya Mungu, joto, na upendo.
Mwanzo Mpya Angavu
Kitabu cha Mormoni kinatuambia jinsi gani Wanefi walikuwa siku tatu katika giza nene kufuatia kusulubiwa kwa Mwokozi. Giza lililowazunguka lilikuwa ishara ya giza la kiroho tunalopitia kwa sababu ya dhambi. Kisha walisikia sauti ya Kristo ikiwaalika watoke nje ya lile giza nene na kuja ndani ya nuru Yake.
“Je, hamtarudi kwangu sasa, na kutubu dhambi zenu, na kugeuka, ili niwaponye?” (3 Nefi 9:13)
“Na mtatoa kwangu dhabihu ya moyo uliopondeka na roho iliyovunjika” (3 Nefi 9:20).
“Mtatubu na kunirudia kwa lengo moja la moyo” (3 Nephi 10:6).
Mwokozi anatoa mialiko hiyo hiyo kwako unapojiona umepotea gizani. Kama vile kila kuchomoza kwa jua kunaashiria mwanzo wa siku mpya, kila wakati unapotubu, unapata mwanzo mpya, mwanzo mpya angavu.
Kupitia toba yako ya dhati, Yesu Kristo “atabadilisha hatia yako kwa amani na shangwe. Hatakumbuka dhambi zako tena. Katika nguvu Zake, hamu yako ya kushika amri Zake itaongezeka.
Mara uchukuapo hatua ya kwanza ya kutubu, Mwokozi ataanza kuubadilisha moyo wako na maisha yako. Kidogo kidogo, utakua na kuwa zaidi kama Yeye” na “Atakuletea njia kuu ya kufikia Nguvu Yake.”
Tafuta Uponyaji wa Kudumu
Mwokozi ni Mponyaji Mkuu. Mojawapo ya madhihirisho mazuri zaidi ya nguvu Yake ya uponyaji yanapatikana katika huduma Yake binafsi katika Kitabu cha Mormoni.
“Mnao wowote ambao ni wagonjwa miongoni mwenu?” Yeye aliwauliza. “Mnao wowote ambao wame … sumbuka katika namna yo yote ile? Waleteni hapa na nitawaponya, kwani ninayo huruma juu yenu. …
“Na ikawa kwamba wakati alipokuwa amesema hivyo, umati wote, kwa lengo moja, ulisonga mbele … ; na aliwaponya wote kila mmoja kadiri walivyoletwa kwake” (3 Nefi 17:7, 9).
Kila wakati Mwokozi alipomponya mtu, kabla na baada ya Ufufuko Wake, alishuhudia juu ya nguvu Yake ya msingi ya kuponya nafsi zetu. Kila uponyaji wa kimuujiza ulielekeza kwenye ahadi Yake ya uponyaji wa kudumu wa kimwili na kihisia ambao utakuja kwetu katika Ufufuko.
Nyakati zingine, sala zako kwa ajili ya uponyaji yawezekana zisijibiwe katika njia unayotumainia, lakini kamwe hazipuuzwi. Wakati wa uponyaji hatimaye utafika katika njia na muda wa Baba wa Mbinguni mwenyewe, kama vile tu giza la usiku daima litatoa njia kiutukufu kwa kuchomoza kwa jua.
Rafiki yangu mpendwa, ninashuhudia kwamba Yesu Kristo ndiye Mponyaji katika maisha haya na katika milele. Rehema zake zatosha kuponya majeraha yako, kuosha dhambi zako, kukuimarisha katika majaribu yako, na kukubariki wewe kwa tumaini, hekima, na amani. Nguvu Yake siku zote iko hapo—daima na ya kutegemewa—hata wakati wewe, kwa muda fulani, unahisi kuwa mbali na upendo, nuru, na joto Lake.
Naomba kamwe usipoteze hisia za heshima na shukrani yako ya kina kwa yale yote Yesu Kristo aliyokutendea. Tafadhali fahamu kuwa unapendwa kiukamilifu. Kumbuka kitu ambacho umeahidiwa milele. Na “Mungu akubali kwamba mizigo yako ipate kuwa miepesi, kupitia shangwe ya Mwanawe,” Yesu Kristo (Alma 33:23).