Kuvunja Mzunguko wa Ponografia
Nilihisi upweke na nisiyejiweza. Lakini askofu wangu alinikumbusha juu ya baadhi ya funguo za kupata tumaini na usaidizi.
Kwa mara ya kwanza nilionyeshwa ponografia nikiwa na umri wa miaka 13. Niliiona kwa bahati mbaya kwenye mitandao ya kijamii, pasipo kujua ilikuwa kitu gani na bila kuelewa. Nilikwenda kutoka kuona pasipo kusudia na udadisi wa makusudi wa kuitafuta.
Kwa wakati huo, jumbe za viongozi kuhusu ponografia zilionekana zikisema kwamba ni kitu ambacho wavulana tu ndio waliokuwa wakipambana nacho. Hii iliniacha mimi kuhisi aibu nyingi. Nilidhani kamwe sitaweza kumwambia mtu ye yote kuhusu changamoto yangu. Nilijua kuhusu Upatanisho wa Yesu Kristo, lakini kwa sababu nilidhani kwamba nilikuwa msichana pekee aliye na changamoto hii, nilihisi hali yangu ni kama ilikuwa nje ya ufikiaji wa Mwokozi. Nilihisi kama jambo lisilo la kawaida.
Ofisi ya Askofu
Kwa miaka hiyo, katika mahali pa seminari au mikutano ya ibada fupi—po pote Roho alipokuwepo—mara kwa mara nilihisi kusukumwa kuomba kukutana na askofu wangu. Kwa muda mrefu, kitu kilichonizuia kufanya hili ilikuwa wazo nililokuwa nalo kwamba mimi ninayo hadhi ya kuwa mtoto mzuri kutoka familia inayohudhuria kikamilifu kanisani. Nilifikiria angeniona mimi kama jinsi nilivyo—na sikuamini kwamba mtu huyo alikuwa anapendeka. Nilidhani ningekutana na adhabu za papo hapo.
Wakati mwishowe nilipopanga mkutano huo, ilikwenda kinyume kabisa na jinsi nilivyotegemea. Badala ya kunipa adhabu, askofu wangu aliniambia: “Wewe bado ni binti wa Mungu. Bado unapendwa, na bado ni wa thamani.”
Ninakumbuka kuhisi kulemewa na upendo. Hiyo ilikuwa ni mara yangu ya kwanza nilipohisi nguvu ya Upatanisho wa Mwokozi kwa nguvu sana katika maisha yangu. Nikitazama nyuma, ninaelewa kwa nini maneno yale askofu wangu aliyosema yalikuwa muhimu sana.
Binti wa Mungu
Unapopambana na ponografia, unakwenda kupitia mzunguko wa aibu. Kwangu mimi, ningehisi kuwa nje ya mguso wa utambulisho wangu mwenyewe na kisha kutumia ponografia kushughuilika na hisia hiyo hasi. Kisha ningehisi aibu na kujitenga mwenyewe mbali na wengine, na mzunguko ungejirudia.
Kwa muda mrefu, nilijaribu kutegemea uwezo wangu mwenyewe wa “kuacha tu.” Lakini sikuweza kufanya hivyo mwenyewe. Askofu wangu alinisaidia kukumbuka utambulisho wangu—kwamba mimi ni binti mpendwa wa Mungu. Nilipokutana naye na kukumbuka ukweli huo, nilianza kufanya maendeleo ya dhati.
Ukweli kuhusu Mungu na Mwokozi
Mwanzoni nilikuwa ninaogopa kusali. Nilimwona Baba wa Mbinguni ni Mungu wa haki na wa hasira. Lakini kuendelea na mchakato wa toba endelevu kumenisaidia kuelewa asili ya Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo. Kujua kwamba kutubu mara moja hakunifanyi niwe na kinga dhidi ya changamoto hii kumeniruhusu kuendelea kutegemea usaidizi Wake wa kiungu. Baba wa Mbinguni tayari alijua kuhusu na alielewa majaribu yangu; nilihitaji tu kumfikia Yeye.
Nilijifunza kwamba wote wawili Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo ni wenye rehema na wenye kuelewa. Unapowageukia Wao, Watatembea pamoja nawe na kukushika mkono kila hatua njiani.
Kupigana na Mbinu za Shetani
Kuelewa asili ya Mungu pia kulinisaidia kumwelewa Shetani na zana zake na jinsi zinavyofanya kazi kwa upinzani na Mungu moja kwa moja. Mojawapo ya zana za Shetani yenye nguvu zaidi ni aibu, ambayo ni tofauti na hatia au “huzuni ya kiungu” (2 Wakorintho 7:10). Unapohisi hatia, unatambua umefanya kosa. Lakini aibu inaunganisha hisia hasi ulizonazo wewe mwenyewe unapotenda dhambi kinyume na utambulisho wako, kana kwamba wewe ni hisia hizo.
Shetani alitaka mimi niamini kwamba ningeweza kushinda changamoto hizo mimi mwenyewe. Uongo huu ulikuwa kitu ambacho kilinizuia kuzungumza na askofu wangu kuhusu changamoto yangu ya ponografia. Nilihisi kama nisingeweza kukutana naye hadi pale nitakapoweza kusema kilikuwa kitu nilichokuwa nahangaika nacho wakati uliopita. Shetani anatumia udhaifu wako binafsi kukufanya ujisikie hustahili kutafuta nguvu ya Mwokozi ya uponyaji.
Nilijifunza kwamba Shetani anafanya kazi juu yetu tunapokuwa tumejitenga, hivyo basi ulinzi wetu bora zaidi ni muunganisho. Wakati mwingine ni rahisi tu kama kuwafikia wengine na kutumia muda wa maana na marafiki wema. Kujiunganisha na Baba wa Mbinguni, na wewe mwenyewe, na watu wengine (hususani wale wanaokuona kama Baba wa Mbinguni anavyokuona) ni njia iliyo bora kwako kukumbuka utambulisho wako wa kweli: mwana wa Mungu mwenye kuthaminiwa.
Dhumuni la Juu
Hatimaye nilianza kupata misukumo ya kuwasaidia wasichana wengine wenye changamoto na ponografia. Nilihisi dhumuni la juu zaidi. Niliamua kujali zaidi kuhusu kile Baba wa Mbinguni anachofikiria kuliko kile watu wengine walionizunguka wanachoweza kufikiria, hivyo basi nilianza kusema kwa uwazi zaidi kuhusu uzoefu wangu.
Mara unapohisi shangwe isiyokanushika ya toba endelevu, unataka kushiriki na wengine. Sasa ninaendelea kushiriki shangwe hii ninapohudumu kama mmisionari.
Ujumbe Wangu
Kamwe hauko peke yako, na kuna tumaini.
Changamoto hii ni kitu unachoweza kushinda kwa usaidizi wa Mwokozi, wapendwa unaowaamini na viongozi, na zana sahihi. Toka huko ulikojitenga na mfikie mtu anayekuona wewe kupitia macho ya Mungu. Waulize wanaona kitu gani ndani yako!
Bila kujali kitu unachopigana nacho, wewe katu hauko ng’ambo ya ufikiaji wa Mwokozi na Upatanisho Wake. Baba wa Mbinguni anakupenda kikamilifu, na inastahili kuendelea kutubu.