Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana
Je, Kanisa linajali kuhusu siasa na serikali?
Septemba 2024


Kwenye Hoja

Je, Kanisa linajali kuhusu siasa na serikali?

watu mbalimbali

Siasa na serikali zinagusa maisha yetu, ikijumuisha uwezo wetu wa kuabudu, na Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho linahimiza waumini wake kushiriki katika hili. Kupitia manabii wake, Bwana ametupatia sisi kanuni za kweli, na ni juu ya kila mmoja wetu kutumia kanuni hizo katika vipengele tofauti vya maisha yetu, ikijumuisha ushiriki wetu kuhusu siasa na serikali. Mahali tofauti pana sheria tofauti, na Kanisa linatuhimiza kushiriki vyo vyote tuwezavyo.

Kanisa lenyewe haliungi mkono vyama vya siasa, majukwaa, au wagombea. Kisiasa halifungamani na yeyote. Na Kanisa halituambii jinsi ya kupiga kura. Kwa urahisi linatukumbusha tu kwamba Bwana ametuambia tuwatafute na kuwaunga mkono viongozi walio waaminifu, wema, na wenye hekima (ona Mafundisho na Magano 98:10). Na wakati mwingine linatoa taarifa rasmi kwa umma juu ya mambo ya kisiasa yanayohusiana na masuala ya kimaadili au desturi za Kanisa.

Kanisa pia linawahimiza waumini kusaidia kufanya jumuiya zao ziwe mahala pazuri pa kuishi na kulea familia. Kuna mambo mema mengi tunayoweza kushiriki katika kusaidia kuboresha mambo mahali po pote tulipo.

Ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 38.8.30, Maktaba ya Injili; Makala ya Imani 1:11–12.