“Je, Ninaishi ‘kwa Furaha’?,” Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana, Feb. 2024.
Ujumbe wa kila mwezi wa Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana, Februari 2024
Je, Ninaishi “Kwa Furaha”?
Hapa kuna baadhi ya mawazo kwa ajili ya kukuwezesha kuishi kama vile Nefi alivyosema watu wake waliishi.
Muda mfupi baada ya kujitenga na Walamani, Nefi alisema watu wake “waliishi kwa furaha” (2 Nefi 5:7). Kwa kuzingatia kwamba kulikuwa na kundi la watu ambao walitaka kuwaua (ona 2 Nefi 5:1–6, 14), hiyo ingeweza kushangaza. Ingewezekana vipi kila mmoja kuwa na furaha katika mazingira kama haya?
Awali ya yote, tambua kwamba “tuliishi kwa furaha” haimaanishi kwamba “kila Mnefi alikuwa na furaha 24/7.” Inamaanisha waliishi katika njia ya wema, na walifanya aina ya mambo, ambayo kwa ujumla yaliongoza kwenye furaha. Kwa ujumla, licha ya changamoto zao, ulikuwa ni muda wa furaha.
Kwa hiyo “hali ya furaha ni nini”? Je, tunawezaje kuiendeleza katika maisha yetu wenyewe, ambayo pia yana changamoto? Acha tuone!
-
Kuwa mtiifu. “Tuliendelea kutii … amri za Bwana” (2 Nefi 5:10).
Kuishi ijnili ni Hatua ya 1. Waweza kuwa na furaha ya muda mfupi ukiwa kwenye dhambi, lakini haiwezi kudumu. Kuacha kumtii Mungu kwa makusudi siyo “hali ya furaha” (ona Alma 41:10).
-
Pekua maandiko. “Na mimi, Nefi, nilikuwa … nimeleta maandishi yaliyokuwa yamechorwa kwenye bamba za shaba” (2 Nefi 5:12). “Tuliyachunguza … na tukagundua kwamba yalikuwa ya kupendeza; ndio, hata yenye thamani kubwa kwetu sisi” (1 Nefi 5:21).
Watu wa Nefi walikuwa na maandiko. Na hawakuwa nayo tu— waliyachunguza maandiko.
-
Wasikilize viongozi wenye msukumo wa kiungu. “Mimi, Nefi, niliwatenga Yakobo na Yusufu, kwamba wawe makuhani na walimu juu ya … watu wangu” (2 Nefi 5:26).
Hawa walimu waliyatumia maandiko kama mwongozo wao (ona 2 Nefi 4:15; 6:4).
-
Nenda Hekaluni (na maeneo mengine matakatifu). “Mimi, Nefi, nilijenga hekalu” (.2 Nefi 5:16).
Ni muhimu kuwa na maeneo matakatifu kama vile nyumba za mikutano na mahekalu kwa ajili ya wafuasi kukutana na kuabudu. (Tunaweza kufikiri kwamba watu wa Nefi hawakuwa tu na hekalu—hakika walilitumia.) Kama huwezi kufika kwenye hekalu wewe binafsi, mara zote unaweza kufanya kazi ya historia ya familia.
-
Kuwa mwenye manufaa. “Niliwafundisha watu wangu kujenga majengo, na kufanya kazi. … [Nilisababisha] watu wangu wawe wenye bidii, na kutenda kazi kwa mikono yao” (2 Nefi 5:15, 17)
“Sehemu ya hali ya furaha” ni kuwa na kazi ya kufanya! Jukumu, kazi, wajibu—kitu fulani ambacho kinakupa wewe fokasi na lengo (pamoja na muda sahihi wa kupumzika, kwa hakika). Ni vigumu kuwa na furaha kama umekwazika wakati wote.
Je, unaweza kusema kwamba kwa sasa unaishi kwa furaha? Kama hapana, pengine mfano wa Nefi unaweza kukupa mawazo ya jinsi ya kuwa bora.
© 2024 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Limepigwa chapa Marekani. Idhini ya Kiingereza: 6/19. Idhini ya kutafsiri: 6/19. Tafsiri ya Monthly For the Strength of Youth Message, February 2024. Language. 19276 743