Ujumbe wa kila Mwezi wa Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana, Desemba 2024
Kuzaliwa kwa Yesu Kristo
Jifunze kuhusu tukio hili la Krismasi lililozoeleka na jinsi linavyotusaidia kufokasi kwa Mwokozi.
Bethlehemu
Bethlehemu inamaanisha “nyumba ya mkate” katika Kiebrania. Wakati mwingine unaitwa mji wa Daudi, ambao ukoo wake Masiya alitabiriwa kuja (ona Yeremia 23:5; Yohana 7:42). Samweli alimtawaza Daudi mfalme huko Bethlehemu (ona 1 Samweli 16:1–13). Ilitabiriwa kwamba Masiya angezaliwa hapo (ona Mika 5:2).
Nyumba ya Wageni
Neno la Kigiriki la nyumba ya wageni linaweza kumaanisha makazi yoyote ya muda, ikiwa ni pamoja na chumba cha wageni. Mariamu “alimweka [Mtoto Kristo] katika hori; kwa kuwa hapakuwa na nafasi katika nyumba ya wageni” (Luka 2:7). (Tafsiri ya Joseph Smith inasema “nyumba za wageni.”) “Hakuna nafasi” inaweza kumaanisha walifukuzwa au kwamba hakuna mahali ambapo wangeweza kukaa palikuwa na nafasi ya kumzaa mtoto. Kwa hali yoyote, walikwenda sehemu fulani ambapo kulikuwa na hori.
Hori
Hori ni kisanduku kilichoinuliwa au beseni ambalo linabeba chakula kwa ajili ya wanyama. Katika Yuda ya kale, haya hasa yalitengenezwa kwa mawe. Nyumba za Wageni zilikuwa na viwanja vyenye mahori, na nyumba nyingi pia zilikuwa na mahori katika chumba kikuu ili wanyama waweze kuwekwa huko kwa usiku mmoja.
Mavazi ya Kitoto
Akina mama wamekuwa wakiwafunika watoto wachanga kwa mavazi ya kitoto (kuwafunga kwa blanketi au nguo) kwa maelfu ya miaka. Hii inawatuliza na kuwafariji baada ya mshtuko wa kutoka tumboni. Nguo ambazo Mariamu alitumia huenda zilikuwa na alama maalumu ya kipekee kwa familia.
Mariamu na Yusufu
Walikuwa watu wema na wenye haki, na wote walikuwa uzao wa Daudi. Kila mmoja alikuwa ametembelewa na malaika katika maandalizi ya kuzaliwa kwa Mwokozi ( ona Mathayo 1:18–25; Luka 1:26–38). Walisafiri kwa kilomita 100–140 (maili 60–90) kwenda Bethlehemu. Mariamu alikuwa mjamzito wakati wa safari.
Wachungaji
Wachungaji walikuwa wakichunga mifugo yao karibu na Bethlehemu. Kulingana na baadhi ya wasomi, kondoo waliokusudiwa kwa ajili ya dhabihu za hekaluni pekee ndiyo waliruhusiwa kufugwa karibu na mji. Kwa hiyo wachungaji hawa yaweza kuwa walikuwa wakichunga kondoo ambao wangewakilisha dhabihu ya Yesu Kristo kwa ajili yetu (ona Musa 5:6–7). Waliacha mifugo yao ili kumwona Masiya, ambaye dhabihu yake ya upatanisho ingeondoa dhabihu ya wanyama.
Mtoto Yesu
Yesu Kristo ni kiini cha tukio la Kuzaliwa kwa Yesu—na maisha yetu.
© 2024 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Limepigwa chapa Marekani. Idhini ya Kiingereza: 6/19. Idhini ya kutafsiri: 6/19. Tafsiri ya Monthly For the Strength of Youth Message, December 2024. Swahili. 19346 743