Jina Sahihi la Kanisa
Yesu Kristo alituagiza kuliita Kanisa kwa jina Lake kwa sababu ni Kanisa Lake, lililojazwa na nguvu Zake.
Akina kaka na dada zangu wapendwa, kwenye sabato hii njema tunafurahia kwa pamoja baraka zetu nyingi kutoka kwa Bwana. Tuna shukrani kwa ajili ya shuhuda zenu za Injili iliyorejeshwa ya Yesu Kristo, kwa dhabihu mliyotoa ili kubaki au kurudi katika njia Yake ya agano, na kwa huduma mliyojitolea kwa Kanisa Lake.
Leo ninahisi kujadili nanyi jambo lenye umuhimu mkubwa. Wiki kadhaa zilizopita, nilitoa taarifa kuhusu kurekebisha mwendo kwa ajili ya jina la Kanisa.1 Nilifanya hivi kwa sababu Bwana aliishawishi akili yangu kwenye umuhimu wa jina alilotamka kwa ajili ya Kanisa Lake, hata Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.2
Kama mnavyoweza kutarajia, mwitikio kwa taarifa hii na mwongozo wa mtindo uliorekebishwa3 yamekuwa ya mchanganyiko. Waumini wengi walirekebisha mara moja jina la Kanisa kwenye blogu na kurasa zao za mitandao ya kijamii. Wengine walijiuliza kwa nini, pamoja na yote yanayoendelea ulimwenguni, ilikuwa ni muhimu kusisitiza kitu “kisicho kuwa na umuhimu.” Na wengine wakasema haiwezi kufanyika, kwa nini basi kujaribu? Acha nieleze kwa nini tunajali sana kuhusu suala hili. Lakini acha kwanza niseme juhudi hii si kwa ajili ya nini:
-
Si ya kubadili jina.
-
Si ya kutengeneza upya.
-
Si ya kurembesha.
-
Si ya wazo la ghafla
-
Na si isiyo ya umuhimu.
Badala yake, ni rekebisho Ni amri ya Bwana. Joseph Smith hakulipa jina Kanisa lililorejeshwa kupitia yeye; hata Mormoni. Ilikuwa ni Mwokozi Mwenyewe aliyesema, “kwani ndivyo kanisa langu litakavyoitwa katika siku za mwisho, hata Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.”4
Hata hapo awali mnamo miaka 34 Baada ya Kristo, Bwana wetu aliyefufuka alitoa maagizo sawa na haya kwa waumini wa Kanisa Alipowatembelea kule Amerika. Wakati huo alisema:
“Mtaliita kanisa katika jina langu. …
“Na linawezaje kuwa kanisa langu isipokuwa liitwe kwa jina langu? Kwani kanisa likiitwa kwa jina la Musa, hapo litakuwa kanisa la Musa; au likiitwa kwa jina la mtu, basi litakuwa kanisa la yule mtu; lakini likiitwa katika jina langu, hapo basi litakuwa kanisa langu.”5
Hivyo, jina la Kanisa si jambo la mjadala. Wakati Mwokozi anaposema wazi jinsi jina la Kanisa lake Linavyopasa kuwa na hata kutanguliza tangazo lake kwa “Kwani ndivyo kanisa langu litakavyoitwa,” Anamaanisha. Na tukikubali majina ya utani kutumiwa na kuyaasili au hata sisi wenyewe kudhamini majina hayo, Yeye huchukizwa.
Ni nini kilicho katika jina, au katika suala hili, jina la utani? Linapokuja suala la majina ya utani ya Kanisa, kama vile “kanisa la WSM,” “Kanisa la Mormoni,” au “Kanisa la Watakatifu wa Siku za Mwisho,” kitu cha muhimu zaidi katika majina hayo ni kutokuwepo kwa jina la Mwokozi. Kuondoa jina la Bwana kutoka Kanisa la Bwana ni ushindi mkubwa kwa Shetani. Tunapoondoa jina la Mwokozi, kwa werevu tunapuuza yote ambayo Yesu Kristo alifanya kwa ajili yetu—Hata upatanisho Wake.
Fikiria hili katika msimamo wake: Kabla ya maisha ya duniani alikuwa Yehova, Mungu wa Agano la Kale. Chini ya uelekezi wa Baba Yake, Alikuwa Muumbaji wa dunia hii na dunia zingine.6 Alichagua kujiweka chini ya matakwa ya Baba Yake na kufanya kitu kwa ajili ya watoto wote wa Mungu ambacho hakuna mwingine ambaye angekifanya! Akijishusha hadhi kuja ulimwenguni kama Mwana wa Pekee wa Baba katika mwili, alidharauliwa kikatili, alidhihakiwa, akatemewa mate na kupigwa. Kwenye Bustani la Gethsemane, Mwokozi wetu alijuchukulia juu yake kila maumivu, kila dhambi, na uchungu na masumbuko yote tuliyowahi kupata wewe na mimi na kila mtu aliyewahi au atakayewahi kuishi. Chini ya mzigo wa uchungu mkali, alitokwa damu katika kila kinyweleo.7 Mateso haya yote yalizidi wakati alipoangikwa kikatili kwenye Msalaba wa Kalvari.
Kupitia kwa uzoefu huu wa machungu na Ufufuko Wake baadaye—Upatanisho wake usio na Mwisho—Alitoa kutokufa kwa wote, kumfidia kila mmoja wetu kutokana na athari za dhambi, kwa sharti la kutubu kwetu.
Kufuatia Ufufuko wa Mwokozi na kufa kwa Mitume Wake, dunia iliangukia katika karne za giza. Kisha mnamo mwaka 1820 ,Mungu Baba na Mwanae, Yesu Kristo, walimtokea Nabii Joseph Smith ili kuanzisha Urejesho wa Kanisa la Bwana.
Baada ya yote aliyovumilia—na baada ya yote aliyofanya kwa ajili ya wanadamu— ninatambua kwa majuto makubwa kwamba bila kufikiria tumekubali Kanisa la Bwana lililorejeshwa kuitwa kwa majina mengine, ambayo kila moja huondoa jina takatifu la Yesu Kristo!
Kila jumapili tunaposhiriki sakramenti kwa kustahili, tunafanya upya ahadi yetu kwa Baba yetu wa Mbinguni kwamba tuko radhi kujichukulia juu yetu jina la Mwanae, Yesu Kristo.8 Tunaahidi kumfuata Yeye, kutubu, kushika amri Zake na daima kumkumbuka Yeye.
Tunapoondoa jina Lake kutoka Kanisa Lake, tunamuondoa Yeye bila kuwa waangalifu kama kiini cha maisha yetu.
Kujichukulia jina la Mwokozi juu yetu kunajumuisha kutangaza na kushuhudia kwa wengine—kupitia matendo na maneno yetu—kwamba Yesu ndiye Kristo. Je, tumekuwa wenye uoga sana kumuudhi mtu aliyetuita “Wamormoni” kwamba tumeshindwa kumtetea Mwokozi Mwenyewe, kusimama imara kwa ajili Yake hata kwa jina ambalo kwalo Kanisa Lake linaitwa?
Ikiwa sisi kama watu binafsi tutataka kufikia nguvu ya Upatanisho wa Yesu Kristo—ili kututakasa na kutuponya , ili kuimarisha na kutukuza, na hatimaye kutuinua—ni lazima tumtambue Yeye bayana kama chanzo cha nguvu hizo. Tunaweza kuanza kwa Kuliita Kanisa Lake kwa jina Aliloamrisha.
Kwa sehemu kubwa ya ulimwengu, Kanisa la Bwana limefichwa kama “Kanisa la Mormoni.” Lakini sisi kama waumini wa Kanisa la Bwana tunafahamu ni nani anayesimama kwenye kichwa chake: Yesu Kristo Mwenyewe. Kwa bahati mbaya, wengi wanaosikia neno Mormoni wanaweza kufikiri kuwa tunamwabudu Mormoni. Si hivyo! tunataadhima na heshima kwa huyo nabii wa Marekani ya Kale.9 Lakini sisi si wafuasi wa Mormoni. Sisi ni Wafuasi wa Bwana.
Katika siku za mwanzo za Kanisa lililorejeshwa, maneno kama vile “Kanisa la Mormoni” na Wamormoni 10 mara nyingi yalitumiwa kama wasifu—kama maneno ya kikatili, ya kutusi—yaliyokusudiwa kuangamiza mkono wa Mungu katika kurejesha Kanisa la Yesu Kristo katika siku hizi za mwisho.11
Akina kaka na akina dada, kuna ubishi mwingi wa kiulimwengu dhidi ya kurejesha jina sahihi la Kanisa. Kwa sababu ya ulimwengu wa kidijitali tunamoishi na kwa ubora wa viperuzi vya kusaka habari vinayotusaidia kupata taarifa tunayoihitaji mara moja— ikijumuisha habari kuhusu Kanisa la Bwana wakosoaji wanasema kuwa rekebisho kwa wakati huu si hekima. Wengine wanahisi kuwa kwa sababu tunajulikana sana kama “Wamormoni” na kama “Kanisa la Mormoni”, tunapaswa kutumia hayo zaidi.
Kama huu ungekuwa mjadala kuhusu utengenezwaji upya wa taasisi iliyoundwa na binadamu, ubishi huu ungeweza kufaulu. Lakini katika jambo hili muhimu, tunamtazama Yeye ambaye hili ni Kanisa Lake na kutambua kuwa njia za Bwana kamwe si, wala hazitakuwa njia za mwanadamu. Ikiwa tutakuwa wavumilivu na kufanya sehemu yetu vyema, Bwana atatuongoza kupitia kazi hii muhimu. Kwani, tunajua kuwa Bwana huwasaidia wale wanaotafuta kufanya mapenzi yake, kama vile alivyomsaidia Nefi kutimiza kazi ya kujenga merikebu ya kuvuka bahari.12
Tutataka kuwa wapole na wavumilivu katika juhudi zetu kurekebisha makosa haya. Vyombo vya habari vinavyowajibika vitakuwa vyenye kuelewa vinapojibu ombi letu.
Kwenye Mkutano mkuu uliopita, Mzee Benjamín De Hoyos alizungumzia tukio kama hili. Alisema:
“Miaka kadhaa iliyopita nikihudumu kwenye ofisi wa Masuala ya umma ya Kanisa huko Mexico, [mwenza wangu pamoja nami] tulialikwa kushiriki katika majadiliano redioni. … [Mmoja wa wasimamizi wa kipindi] [alituuliza], ‘Kwa nini Kanisa lina jina refu hivyo? …’
“Mwenza wangu pamoja nami tukatabasamu kwa swali hilo zuri, kisha tukaendelea kuelezea kuwa jina la Kanisa halikuchaguliwa na mwanadamu. Ilitolewa na Mwokozi. … Msimamizi wa kipindi kisha akajibu mara moja na kwa heshima, ‘Basi tutalirudia kwa Furaha tele.’”13
Ripoti hii inaonyesha mwelekeo. Mmoja mmoja, juhudi zetu bora kama watu binafsi zitahitajika kurekebisha makosa yaliyonyemelea kwa miaka mingi.14 Ulimwengu unaweza au kutoweza kufuata maongozi yetu kwa kutuita kwa jina sahihi. Lakini ni ulaghai kwetu kukasirishwa ikiwa wengi duniani huliita Kanisa na waumini wake majina yasiyo sahihi ikiwa nasi tunafanya vivyo hivyo.
Staili yetu elekezi iliyopitiwa upya inasaidia. Inasema: “Katika rejeo la kwanza, jina kamili lililopendekezwa la Kanisa: ‘Kanisa La Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.’ wakati rejeo fupi [la pili] linahitajika, maneno ‘Kanisa’ au ‘Kanisa la Yesu Kristo’ yanahimizwa. ‘Kanisa la Yesu Kristo Lililorejeshwa’ pia ni sahihi na linahimizwa.”15
Ikiwa mtu atauliza, “Wewe ni mmormoni?” ungeweza kujibu, “kama unauliza ikiwa mimi ni muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, ndio, mimi ndiye!”
Ikiwa mtu atauliza “Wewe ni Mtakatifu wa Siku za Mwisho?”16 Unaweza kujibu “Ndiyo, mimi ndiye. Ninaamini katika Yesu Kristo na ni muumini wa Kanisa Lake lililorejeshwa.”
Akina kaka na dada zangu wapendwa, Ninawaahidi kuwa kama tutafanya bidii kurejesha jina sahihi la Kanisa la Bwana, Yeye ambaye hili Kanisa ni Lake atatoa nguvu zake na baraka juu ya vichwa vya Watakatifu wa Siku za Mwisho,17 ambazo hatujapata kuona. Tutapata uelewa na nguvu za Mungu kutusaidia kupeleka baraka za injili ya urejesho ya Yesu Kristo katika kila taifa, ukoo, ndimi, na watu, kusaidia kuuandaa ulimwengu kwa Ujio wa Pili wa Bwana.
Hivyo, kuna nini kwenye jina? Linapokuja suala la jina la Kanisa la Bwana, jibu ni “Kila kitu!” Yesu Kristo alituagiza kuliita Kanisa kwa jina Lake kwa sababu ni Kanisa Lake, lililojazwa na nguvu Zake.
Ninajua kwamba Mungu anaishi. Yesu ndiye Kristo. Analiongoza Kanisa Lake hivi leo. Nashuhudia hivi, katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.