Nawezaje Kuelewa?
Wakati kwa dhati, kwa moyo wote, kwa uimara, na kwa moyo wa kweli tunatafuta kujifunza injili ya Yesu Kristo na kufundishana sisi kwa sisi, mafundisho haya yanaweza kubadili mioyo.
Kaka zangu na dada zangu wapendwa, ni furaha kuu iliyoje kukusanyika hapa pamoja nanyi tena katika mkutano huu mkuu wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho chini ya usimamizi wa nabii wetu mpendwa, Rais Russell M. Nelson. Ninawashuhudia kwamba tutakuwa na fursa ya kusikiliza sauti ya Mwokozi wetu, Yesu Kristo, kupitia mafundisho ya wale wanaosali, kuimba, na kuzungumzia mahitaji yetu ya kila siku katika mkutano huu.
Kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Matendo ya Mitume, Filipo Mwinjilisti alimfundisha injili mtu fulani wa Kushi ambaye alikuwa towashi mwenye mamlaka juu ya hazina yote ya malkia wa Kushi.1 Alipokuwa akirejea kutoka Yerusalemu alipokuwa amekwenda kuabudu, alisoma kitabu cha Isaya. Akiwa amepata msukumo wa Roho, Filipo alisogea karibu naye akanena, “Je! Yamekuelea haya unayosoma?
“Na [towashi] akasema, Nitawezaje kuelewa, mtu asiponiongoza? …
“Filipo akafunua kinywa chake, naye, akianza kwa andiko lilo hilo, akamhubiri habari njema za Yesu.”2
Swali lililoulizwa na mwanaume huyu wa Kushi ni ukumbusho wa agizo la kiungu tulilo nalo sote kutafuta kujifunza na kufundishana sisi kwa sisi injili ya Yesu Kristo.3 Hakika, katika muktadha wa kujifunza na kufundisha injili, wakati mwingine sisi ni kama yule mtu wa Kushi—tunahitaji usaidizi wa mwalimu mwaminifu aliyetiwa msukumo; na wakati mwingine sisi ni kama Filipo—tunahitaji kufundisha na kuimarisha wengine katika uongofu wao.
Lengo letu tunapotafuta kujifunza na kufundisha injili ya Yesu Kristo lazima liwe ni kuongeza imani katika Mungu na mpango Wake mtakatifu wa furaha na katika Yesu Kristo na dhabihu Yake ya upatanisho na kufikia uongofu wa kudumu. Ongezeko la imani na uongofu wa aina hii vitatusaidia kufanya na kutunza maagano na Mungu, hivyo kuimarisha tamaa yetu ya kumfuata Yesu na kuleta badiliko la kweli ndani yetu—kwa maneno mengine, kutubadili kuwa kiumbe kipya, jinsi alivyofundisha Mtume Paulo katika waraka wake kwa Wakorintho.4 Mabadiliko haya yatatuletea maisha yenye furaha zaidi, mafanikio, na afya bora na kutusaidia kudumisha mtazamo wa milele. Je, hiki sicho kilichomtokea towashi wa Kushi baada ya yeye kujifunza kuhusu Mwokozi na kuongolewa katika injili Yake? Maandiko yanasema kwamba “alikwenda zake akifurahi.”5
Amri ya kujifunza injili na kufundishana sisi kwa sisi si ngeni; daima imerudiwa toka mwanzo wa historia ya mwanadamu.6 Katika tukio moja, wakati Musa na watu wake walipokuwa katika ardhi tambarare za Moabu kabla ya kuingia katika nchi ya ahadi, Bwana alimtia msukumo awashauri watu wake kuhusu wajibu wao kujifunza sheria na maagano ambayo walikuwa wamepokea kutoka kwa Bwana na kufundisha uzao wao,7 wengi wao ambao binafsi hawakuwa wamepata uzoefu wa kuvuka bahari ya Shamu au ufunuo ulitolewa katika mlima Sinai.
Musa aliwashauri watu wake:
“Na sasa, Ee Israeli, zisikilizeni amri na hukumu niwafundishazo, ili mzitende; mpate kuishi, na kuingia na kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wa baba zenu. …
“… Uwajulishe watoto wako na watoto wa watoto wako.”8
Kisha Musa alihitimisha, akisema, “Basi, zishike sheria zake, na amri zake, ninazokuamuru leo, upate kufanikiwa, wewe na watoto wako baada yako, na siku zako ziwe nyingi katika nchi ile akupayo Bwana, Mungu wako, milele.”9
Manabii wa Mungu daima wametufundisha kwamba tunahitaji kulea familia zetu “katika adabu na maonyo ya Bwana”10 na “katika nuru na kweli.”11 Rais Nelson hivi karibuni alisema, “Katika nyakati hizi za uovu uliokithiri na kutawaliwa na ponografia, wazazi wana wajibu mtakatifu kuwafundisha watoto wao umuhimu wa Mungu [na Yesu Kristo] katika maisha yao.”12
Akina kaka na akina dada, onyo la nabii wetu mpendwa ni ukumbusho wa ziada wa wajibu wetu binafsi wa kutafuta kujifunza na kufundisha familia zetu kwamba kuna Baba Mbinguni ambaye anatupenda na ambaye ametengeneza mpango mtakatifu wa furaha kwa ajili ya watoto Wake; kwamba Yesu Kristo, Mwana Wake, ni Mkombozi wa ulimwengu; na kwamba wokovu huja kupitia imani katika jina Lake.13 Maisha yetu yanapaswa kuwa imara juu ya mwamba wa Mkombozi wetu, Yesu Kristo, ambao unaweza kutusaidia kama watu binafsi na kama familia kuwa na misukumo yetu binafsi ya kiroho ikiwa imeandikwa mioyoni mwetu, kutusaidia kubaki imara katika imani yetu.14
Waweza kukumbuka kwamba wanafunzi wawili wa Yohana Mbatizaji walimfuata Yesu Kristo baada ya kumsikia Yohana akishuhudia kwamba Yesu alikuwa Mwanakondoo wa Mungu, Masiya. Watu hawa wema walikubali mwaliko wa Yesu “njoni muone”15 na wakakaa kwake siku ile. Walikuja kufahamu kwamba Yesu alikuwa Masiya, Mwana wa Mungu, na walimfuata siku zote za maisha yao.
Kadhalika, wakati tunapokubali mwaliko wa Mwokozi wa “njoni muone,” tunahitaji kukaa kwake, tukizama katika maandiko, tukiyafurahia, tukijifunza mafundisho Yake, na kujitahidi kuishi jinsi Alivyoishi. Ndipo hapo tutakuja kumjua Yeye, Yesu Kristo, na kutambua sauti Yake, tukijua kwamba tunapokuja Kwake na kumwamini Yeye, kamwe hatutaona njaa wala kiu.16 Tutaweza kutambua ukweli katika nyakati zote, jinsi ilivyotokea kwa wale wanafunzi wawili ambao walikaa na Yesu.
Akina kaka na akina dada, hilo halitokei kwa bahati. Kujituni sisi wenyewe na vishawishi vikuu zaidi vya kiungu si jambo rahisi; kunahitaji kusali na kujifunza namna ya kuleta injili ya Yesu Kristo kwenye kiini cha maisha yetu. Kama tutafanya hivyo, ninaahidi kwamba ushawishi wa Roho Mtakatifu utaleta ukweli katika mioyo yetu na akili zetu na atashuhudia juu ya ukweli huo,17 akifundisha vitu vyote.18
Swali la mtu wa Kushi, “Nitawezaje [kuelewa] mtu asiponiongoza?” pia lina maana maalumu katika muktadha wa wajibu wetu kufanyia mazoezi kanuni za injili ambazo tumejifunza katika maisha yetu. Katika swala la mtu wa Kushi, kwa mfano, alitenda kulingana na ukweli aliojifunza kutoka kwa Filipo. Aliomba kubatizwa. Alikuja kufahamu kwamba Yesu Kristo alikuwa Mwana wa Mungu.19
Akina kaka na akina dada, vitendo vyetu lazima vidhihirishe kile tunachojifunza na kufundisha. Tunahitaji kuonyesha imani yetu kupitia vile tunavyoishi. Mwalimu bora zaidi ni mfano mwema wa kuigwa. Kufundisha kitu tunachokiishi kwa dhati, kunaweza kuleta mabadiliko katika mioyo ya wale tunaowafundisha. Ikiwa tunawataka watu, iwe ni wanafamilia au la, kwa shangwe wasome maandiko na mafundisho ya mitume na manabii walio hai, wanahitaji kuona nafsi zetu zikifurahishwa katika hayo. Kadhalika, ikiwa tunataka wafahamu kwamba Rais Russell M. Nelson ni nabii, muonaji, na mfunuzi katika siku yetu, wanahitaji kutuona tukiinua mikono yetu ili kumkubali na kutambua kwamba tunafuata mafundisho yake yenye msukumo wa kiungu. Jinsi msemo maarufu wa Marekani unaosema, “Vitendo vinazungumza zaidi kuliko maneno.”
Pengine baadhi yenu hivi sasa mnajiuliza, “Mzee Soares, Nimekuwa nikifanya haya yote na nimekuwa nikifuata mtindo huu kibinafsi na kama familia, lakini cha kusikitisha, baadhi ya marafiki zangu na wapendwa wangu wamejitenga na Bwana. Nini napaswa kufanya? Kwa baadhi yenu ambao wakati huu mnapitia hisia hizi za majonzi, maumivu makubwa, na pengine majuto, tafadhali fahamuni kwamba hawajapotea kabisa kwa sababu Bwana anajua walipo na anawalinda. Kumbuka, ni watoto Wake pia!
Ni vigumu kuelewa sababu zote kwa nini baadhi ya watu huchagua njia tofauti. Kilicho bora kufanya katika hali hii ni kuwapenda na kuwakumbatia, kusali kwa ajili ya usalama wao, na kutafuta msaada wa Bwana kujua cha kufanya na kusema. Sherehekea nao kwa dhati katika mafanikio yao; kuwa rafiki yao na tafuta wema ndani yao. Kamwe tusikate tamaa juu yao bali tutunze mahusiano yetu. Kamwe usiwakane au kuwahukumu vibaya. Wapende tu! Fumbo la mwana mpotevu hutufundisha kwamba wakati watoto wanapojirudi, mara nyingi wanatamani kurudi nyumbani. Ikiwa hilo litafanyika kwa wapendwa wetu, jazeni mioyo yenu na huruma, wakimbilieni, waangukieni shingoni, na muwabusu, kama baba wa mwana mpotevu.20
Hatimaye, endelea kuishi maisha yanayostahili, kuwa mfano mwema kwao kwenye kile unachokiamini, na mkaribie Mwokozi wetu Yesu Kristo. Anajua na anaelewa huzuni zetu na uchungu wetu mkubwa, na atabariki juhudi zako na kujitolea kwako kwa wapendwa wako ikiwa haitakuwa katika maisha haya, itakuwa katika maisha yajayo. Kumbukeni daima akina kaka na akina dada, kwamba tumaini ni sehemu muhimu ya mpango wa injili.
Kwa kipindi cha miaka mingi ya huduma katika Kanisa, nimewaona waumini waaminifu ambao kwa uaminifu wametumia kanuni hizi maishani mwao. Hii ni hali ya kweli ya mama asiye na mwenza ambaye nitamrejelea kama “Mary.” Cha kusikitisha, Mary alipitia talaka ya majonzi. Kwa wakati ule, Mary alitambua kwamba uamuzi muhimu zaidi aliohitaji kufanya kwa familia yake ulikuwa wa kiroho. Je, kusali, kujifunza maandiko, kufunga, na kuhudhuria kanisani na hekaluni kungeendelea kuwa muhimu kwake?
Mary daima alikuwa mwaminifu, na kwa hali hii muhimu ya mambo yalivyokuwa, aliamua kushikilia kile ambacho tayari alifahamu kuwa cha kweli. Alipata nguvu katika “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu,” ambalo, miongoni mwa kanuni nyingi nzuri, linafundisha kwamba “Wazazi wana jukumu takatifu la kulea watoto wao katika upendo na utakatifu” na kuwafundisha daima kutii amri za Mungu.21 Daima alitafuta majibu kutoka kwa Bwana na kuyashiriki na watoto wake wanne katika kila mkutano wa familia. Walijadiliana injili mara kwa mara na walishiriki uzoefu wao na shuhuda wao kwa wao.
Licha ya huzuni waliyopitia, watoto wake walijenga upendo kwenye injili ya Kristo na hamu ya kuhudumu na kuishiriki na wengine. Watatu miongoni mwao walitumikia misheni kwa uaminifu, na mdogo wao sasa anatumikia kule Amerika Kusini. Binti yake mkubwa, ambaye ninamjua vizuri sana, ambaye ameolewa na yuko imara katika imani Yake, alishiriki, “Kamwe sikuhisi kana kwamba mama yangu alitulea peke yake kwa sababu daima Bwana alikuwa nyumbani kwetu. Wakati alipotushuhudia juu ya Bwana, kila mmoja wetu alianza kumgeukia Bwana kwa maswali yetu wenyewe. Nina shukrani alifanya injili kuwa hai.”
Akina kaka na akina dada, mama huyu mzuri aliweza kufanya nyumbani kwake kuwa kituo cha mafunzo ya kiroho. Sawa na lile swali la mtu wa Kushi, Mary alijiuliza mara kadhaa, “Watoto wangu wanawezaje kujifunza isipokuwa mama awaongoze?”
Wenzangu wapendwa katika injili, ninatoa ushuhuda kwenu kwamba Wakati kwa dhati, kwa moyo wote, kwa uimara, na kwa moyo wa kweli tunatafuta kujifunza injili ya Yesu Kristo na kufundishana sisi kwa sisi kwa kusudi la dhati na chini ya uelekezi wa Roho, mafundisho haya yanaweza kubadili mioyo na kuchochea nia ya kuishi kulingana na kweli za Mungu.
Ninashuhudia kwamba Yesu Kristo ni Mwokozi wa ulimwengu. Yeye ndiye Mkombozi, na Yuko hai! Ninajua kwamba Anaongoza Kanisa Lake kupitia manabii Wake, waonaji, na wafunuzi. Ninashuhudia pia kwenu kwamba Mungu yu hai, kwamba anatupenda. Anatutaka turudi katika uwepo Wake—sisi sote. Yeye anasikiliza maombi yetu. Ninatoa ushuhuda wangu juu ya kweli hizi katika jina la Yesu Kristo, amina.