2010–2019
Kazi ya Umisionari: Kushiriki Kile Kilicho katika Moyo Wako
Mkutano Mkuu wa Aprili 2019


2:3

Kazi ya Umisionari: Kushiriki Kile Kilicho katika Moyo Wako

Popote ulipo hapa duniani, kuna fursa nyingi za kushiriki habari njema ya injili ya Yesu Kristo.

Mwezi uliopita Kumi na Wawili walialikwa na nabii wetu mpendwa, Rais Russell M. Nelson, kusafiri pamoja naye kwenye kuweka wakfu Hekalu la Roma Italia. Tukiwa safarini nilifikiria kuhusu Mtume Paulo na safari zake. Katika siku zake, kutoka Yerusalemu hadi Roma ingechukua karibu siku 40. Leo, katika moja ya ndege nizipendazo, inachukua chini ya masaa 3.

Waandishi wa Biblia wanaamini kwamba Paulo alikuwa Roma wakati alipoandika nyaraka zake kadhaa, ambazo zilikuwa ni kiini cha kuwaimarisha waumini wa Kanisa wakati ule na hata sasa.

Paulo na waumini wengine wa Kanisa la kale, wale Watakatifu wa Mwanzo, walikuwa wakifahamu vyema dhabihu. Wengi waliteswa vibaya, hata kufa.

Katika miaka 200 iliyopita, waumini wa Kanisa la urejesho la Yesu Kristo, la Watakatifu wa Siku za Mwisho , pia wamepitia mateso katika njia nyingi. Lakini licha ya mateso hayo (na wakati mwingine kwa sababu ya mateso hayo), Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho limeendelea kukua na sasa linapatikana ulimwenguni kote.

Kuna Mengi Ya kufanya

Hata hivyo, kabla ya kuoka keki, kutupa confetti, na kujisifu wenyewe juu ya mafanikio haya ya kusifika, tungefanya vizuri kuweka ukuaji huo kwenye mtazamo.

Kwa haraka haraka kuna watu takribani bilioni saba na nusu duniani, ikilinganishwa na waumini milioni 16 wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho—kundi dogo kabisa.1

Wakati huo huo, idadi ya waumini Wakristo katika sehemu fulani za dunia inapungua.2

Hata katika Kanisa la urejesho la Bwana—wakati uumini kwa ujumla unaendelea kukua—kuna wengi sana ambao hawatafuti baraka za ushiriki wa Kanisa wa mara kwa mara.

Kwa maneno mengine, popote ulipo hapa duniani, kuna fursa nyingi za kushiriki habari njema3 ya injili ya Yesu Kristo na watu unaokutana nao, kujifunza nao, na kuishi nao au kufanya nao kazi na kujumuika nao.

Mnamo mwaka uliopita, nimeweza kupata fursa ya kusisimua ya kujihusisha sana na shughuli za kimisionari za Kanisa duniani kote. Mara nyingi nimekuwa nikitafakari na kuomba kuhusu kazi kubwa ya Mwokozi kwa wafuasi Wake—sisi, watoto Wake—ya “enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu.”4

Nimeshindana na swali “Ni kwa jinsi gani sisi, kama waumini na wafuasi wa Kristo, tunaweza kutimiza vizuri kazi hiyo kubwa katika maisha yetu ya kila siku?”

Leo ninakualika kutafakari swali hilo hilo katika moyo wako na akili yako.5

Karama ya Kazi ya Umisionari

Viongozi wa Kanisa wamesisitiza ufafanuzi wa “Kila muumini ni mmisionari!” kwa miongo.6

Waumini wa Kanisa la Yesu Kristo—wote wa kale na wakati wetu—kwa shauku na furaha wameshiriki injili na marafiki na wale wanaojuana nao. Mioyo yao inawaka kwa ushuhuda wa Yesu Kristo, na wanataka wengine wawe na furaha sawa na hiyo waliyoipata katika injili ya Mwokozi.

Baadhi ya Waumini wa Kanisa inaonekana wana karama hii. Wanapenda kuwa mabalozi wa injili. Wanatumikia kwa ujasiri na furaha na kuongoza kazi kama wamisionari waumini.

Hata hivyo, wengine kati yetu wanasita sana. Wakati kazi ya umisionari inapojadiliwa katika mikutano ya Kanisa, vichwa vinainamishwa polepole mpaka vinafichwa nyuma ya kiti, macho yakifokasi kwenye maandiko au yakifumbwa kwa tafakari ya kina ili kuepuka mgongano wa macho na waumini wengine.

Kwa nini hivi? Labda tunahisi hatia kwa kutofanya zaidi kwenye kushiriki injili. Pengine tunahisi kutokuwa na uhakika jinsi ya kuifanya. Au tunaweza kuhisi wasiwasi kuhusu kwenda nje ya eneo la faraja yetu.

Ninalielewa hili.

Lakini kumbuka, Bwana hajawahi kuhitaji juhudi za kitaalamu, zisizo na dosari za kimisionari. Badala yake, “Bwana anahitaji moyo na akili yenye kukubali.”7

Kama tayari unafanya kazi ya umisionari kwa furaha, tafadhali endelea, na simama kama mfano kwa wengine. Bwana atakubariki.

Kama, hata hivyo, unahisi kwamba miguu yako inakuwa mizito inapokuja kwenye kushiriki ujumbe wa injili, naomba nipendekeze mambo matano yasiyoleta hatia ambayo mtu yeyote anaweza kufanya katika kazi kubwa ya Mwokozi ili kusaidia kukusanya Israeli?

Mapendekezo Matano Rahisi

Kwanza, mkaribie Mungu. Amri kuu ya kwanza ni kumpenda Mungu.8 Ni sababu ya msingi ya kwa nini tupo hapa duniani. Jiulize mwenyewe, “Je kweli ninamwamini Baba wa Mbinguni?”

“Je ninampenda na kumwamini Yeye?”

Kadiri unavyomkaribia Baba yetu wa Mbinguni, ndivyo nuru na furaha Yake vitang’ara kati yako. Wengine watagundua kwamba kuna kitu cha thamani na cha kipekee kuhusu wewe. Nao watakuuliza kuhusu kitu hicho.

Pili, jaza moyo wako na upendo kwa wengine. Hii ndiyo amri ya pili iliyo kuu.9 Jaribu kiukweli kumuona kila anayekuzunguka kama mtoto wa Mungu. Wahudumie—bila kujali iwapo majina yao yanaonekana kwenye orodha yako ya huduma kwa dada au kaka.

Cheka nao. Shangilia nao. Lia nao. Waheshimu. Ponya, inua, na waimarishe.

Jitahidi kuiga upendo wa Kristo na kuwa na huruma kwa wengine—hata kwa wale ambao siyo wakarimu kwako, ambao wanakucheka na wanataka kukuumiza. Wapende na kuwachukulia kama watoto wenzako wa Baba wa Mbinguni.

Tatu, jitahidi kutembea katika njia ya ufuasi. Kadiri upendo wako kwa Mungu na kwa watoto Wake unavyoongezeka, ndivyo kutakavyokuwa kujitolea kwako kumfuata Yesu Kristo.

Unajifunza kuhusu njia Zake kwa kusherehekea neno Lake na kusikiliza na kutumia mafundisho ya manabii na mitume wa siku hizi. Unakua katika kujiamini na kuwa na ujasiri wa kufuata njia Yake pale unapowasiliana na Baba wa Mbinguni kwa moyo unaofundishika, mnyenyekevu.

Kuenenda katika njia ya ufuasi kunahitaji mazoezi—kila siku, kidogo kidogo, “neema juu ya neema,”10 “mstari juu ya mstari.”11 Wakati mwingine hatua mbili mbele na moja nyuma.

Kitu muhimu ni kwamba haukati tamaa; enaendelea kujaribu ili upatie. Hatimaye utakuwa mzuri, mwenye furaha, na mkweli zaidi. Kuongea na wengine kuhusu imani yako litakuwa jambo la kawaida na la asili. Kwa kweli, injili itakuwa sehemu muhimu sana, sehemu ya thamani ya maisha yenu kwamba mtahisi vibaya kuacha kuizungumzia kwa wengine. Hiyo huenda isitokee mara moja—ni juhudi ya maisha yote. Lakini itatokea.

Nne, shiriki Kile Kilicho katika moyo wako. Sikuambii kwamba ukasimame kwenye kona ya mtaa ukiwa na kipaza sauti na kusoma kwa sauti mistari ya Kitabu cha Mormoni. Ninachokuomba ni kwamba mara zote tafuta fursa za kuongelea imani yako katika njia za asili na za kawaida unapokutana na watu—iwe uso kwa uso au mtandaoni. Ninaomba kwamba “msimame kama mashahidi”12 wa nguvu ya injili nyakati zote—na inapohitajika, tumia maneno.13

Kwa sababu “injili ya Kristo … ni uweza wa Mungu uletao wokovu,” unaweza kujiamini, kuwa na ujasiri, na unyenyekevu unapoishiriki.14 Kujiamini, ujasiri, na unyenyekevu vinaweza kuonekana kama tabia zinazopingana, lakini siyo. Zinaonyesha mwaliko wa Mwokozi wa kutoficha maadili na kanuni za injili chini ya pishi bali kuifanya nuru yako iangaze, ili matendo yako mema yamtukuze Baba yako wa Mbinguni.15

Kuna njia nyingi za kawaida na za asili za kufanya haya, kutoka kwenye matendo mema ya kila siku hadi kwenye shuhuda zetu binafsi kwenye You Tube, Facebook, Instagram, au Twitter mpaka kwenye maongezi rahisi na watu unaokutana nao. Mwaka huu tunajifunza kutoka katika Agano Jipya katika nyumba zetu na kwenye Shule ya Jumapili. Ni nafasi nzuri kiasi gani kuwaalika marafiki na majirani kuja kanisani na nyumbani kwenu kujifunza kuhusu Mwokozi pamoja nanyi. Shiriki nao Gospel Library app, ambako wanaweza kupata Njoo, Unifuate. Kama unawajua vijana na familia zao, wapatie kijitabu cha Kwa Nguvu ya Vijana na waalike waje na kuona jinsi vijana wetu wanavyo jitahidi kuishi kanuni hizo.

Kama mtu anakuuliza kuhusu wikiendi yako, usisite kuongelea juu ya uzoefu wa kanisani. Eleza kuhusu watoto wadogo waliosimama mbele ya umati na kuimba kwa shauku jinsi wanavyojaribu kuwa kama Yesu. Zungumza kuhusu kundi la vijana wanaotumia muda wao kuwasaidia wazee kwenye nyumba za kupumzika ili kukusanya taarifa zao binafsi. Zungumza kuhusu mabadiliko ya hivi karibuni ya ratiba za mikutano ya Jumapili na jinsi yanavyobariki familia yako. Au elezea kwa nini tunasisitiza kwamba hili ni Kanisa la Yesu Kristo na kwamba sisi ni Watakatifu wa Siku za Mwisho, kama vile waumini wa kale wa Kanisa walivyoitwa Watakatifu.

Kwa njia yoyote inayoonekana ya asili na ya kawaida kwako, shiriki na watu kwanini Yesu Kristo na Kanisa Lake ni muhimu kwako. Waalike “kuja na kuona.”16 Kisha wahimize kuja na kusaidia. Kuna fursa nyingi za watu kusaidia katika Kanisa letu.

Omba si tu kwa ajili ya wamisionari kuwapata wateule. Omba kila siku kwa moyo wako wote kwamba uwapate wale wote ambao watakuja na kuona, watakuja na kusaidia, na watakuja na kubaki. Wajumuishe wamisionari. Wao ni kama malaika, walio tayari kusaidia!

Unaposhiriki habari njema, injili ya Yesu Kristo, fanya hivyo kwa upendo na uvumilivu. Ikiwa tunachangamana na watu wenye matumaini pekee ya kwamba hivi karibuni watavaa mavazi meupe na kuomba maelekezo ya kwenda kwenye kisima cha karibu cha ubatizo, tunafanya isivyostahili.

Baadhi ambao wanakuja na kuona, huenda, wasijiunge na Kanisa kamwe; baadhi watajiunga hapo baadaye. Huo ni uamuzi wao. Lakini hilo halibadilishi upendo wetu kwao. Na halibadili jitihada zetu za shauku za kuendelea kuwaalika watu na familia, kuja na kuona, kuja na kusaidia, na kuja na kubaki.

Tano, mwamini Bwana kutenda miujiza Yake. Elewa kwamba siyo kazi yetu kuwaongoa watu. Huo ni wajibu wa Roho Mtakatifu. Wajibu wako ni kushiriki yaliyo moyoni mwako na kuishi kulingana na imani yako.

Hivyo, usikatishwe tamaa mtu asipokubali ujumbe wa injili mara moja. Sio kushindwa binafsi.

Hiyo ni kati ya mtu binafsi na Baba wa Mbinguni.

Kazi yako ni kumpenda Mungu na jirani zako, watoto Wake.

Amini, penda, tenda.

Fuata njia hii, na Mungu atatenda miujiza kupitia wewe ili kuwabariki watoto Wake wa thamani.

Mapendekezo haya matano yatakusaidia kufanya yale ambayo wafuasi wa Yesu Kristo wamefanya tangu nyakati za kale. Injili Yake na Kanisa Lake ni sehemu muhimu ya maisha yako na sehemu ya wewe ni nani na kile unachokifanya. Kwahiyo, waalike wengine waje na waone na waje na wasaidie, na Mungu atafanya kazi Yake ya kuokoa, na watakuja na kukaa.

Lakini Vipi kama ni Vigumu?

“Lakini,” unaweza kuuliza, “vipi kama ninafanya yote haya na watu hawaitikii? Vipi kama wanasema mabaya kuhusu Kanisa? Vipi kama wananitenga?

Ndio, hayo yanaweza kutokea. Toka nyakati za kale, wafuasi wa Yesu Kristo mara nyingi wamekuwa wakiteswa.17 Mtume Petro alisema, “Furahini … mnaposhiriki mateso ya Kristo.”18 Watakatifu wa mwanzo walifurahi “kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuaibishwa kwa ajili ya Jina hilo.”19

Kumbuka, Bwana hufanya kazi kwa njia za ajabu. Inawezekana kwamba majibu yako kama ya Kristo kwenye kujibu kukataliwa moyo mgumu unaweza kulainika.

Kama Mtume wa Bwana Yesu Kristo, ninawabariki na kujiamini kuwa ushuhuda ulio hai wa maadili ya injili, pamoja na ujasiri ili mara zote muweze kutambuliwa kama waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, pamoja na unyenyekevu ili kusaidia kazi Yake kwa kuonyesha upendo wako kwa Baba wa Mbinguni na watoto Wake.

Rafiki zangu wapendwa, mtafurahi katika kujua kwamba ninyi ni sehemu muhimu ya unabii ulionenwa wa kukusanyika kwa Israeli, kujiandaa kwa ujio wa Kristo katika “nguvu na utukufu mkubwa; pamoja na malaika wote watakatifu.”20

Baba wa Mbinguni anawajua ninyi. Bwana anawapenda. Mungu atawabariki. Kazi hii imetakaswa na Yeye. Unaweza kufanya hili. Sote tunaweza kufanya hili pamoja.

Ninashuhudia hivyo katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Nabii mkuu Nefi aliona katika ono kwamba japokuwa Kanisa la Mwanakondoo wa Mungu litaenea “katika uso wote wa dunia,” kwa sababu ya uovu wa ulimwengu “idadi kwa ujumla [itakuwa] ndogo”(1 Nefi 14:12; ona pia Luka 12:32).

  2. Kwa mfano, uchunguzi wa hivi karibuni na Kituo cha Utafiti cha Pew kiligundua kwamba huko Marekani, “asilimia ya watu wazima (wenye umri wa miaka 18 na zaidi) ambao wanajielezea kuwa Wakristo imeshuka kwa pointi karibu asilimia nane katika miaka saba tu, kutoka78.4% katika … 2007 mpaka 70.6% mwaka 2014. Katika kipindi hicho hicho, asilimia ya Wamarekani ambao hawajihusishi na dini—wakijielezea wenyewe kuwa hawana Mungu, agnostic au ‘chochote hasa’—imeongezeka kwa zaidi ya pointi sita, kutoka 16.1% hadi 22.8%” (“America’s Changing Religious Landscape,” Pew Research Center, Wednesday, May 12, 2015, pewforum.org/2015/05/12/americas-changing-religious-landscape).

  3. Neno injili linamaanisha “habari njema.” Habari njema ni kwamba Yesu Kristo amefanya Upatanisho kamili ambao utawakomboa watu wote kutoka kaburini na kumlipa kila mtu kwa kadiri ya kazi zake. Upatanisho huu ulianza kwa kuteuliwa kwake katika maisha kabla ya kuja duniani, uliendelea wakati wa maisha Yake duniani, na kukamilishwa na Ufufuo Wake wenye utukufu. Kumbukumbu za kibiblia za maisha yake ya duniani, huduma, na dhabihu huitwa Injili: Mathayo, Marko, Luka, na Yohana.

  4. Mathayo 28:19

  5. “Amini ninawaambia, marafiki zangu, ninayaacha maneno haya kwenu ili muyatafakari katika mioyo yenu” (Mafundisho na Maagano 88:62).

    “Tazama, ninakuambia, kwamba unalazimika kulichunguza katika akili yako; ndipo uniulize kama ni sahihi, na kama ni sahihi nitaufanya moyo wako uwake ndani yako; kwa njia hiyo, utahisi kuwa hiyo ni sahihi” (Mafundisho na Maagano 9:8).

  6. Rais David O. McKay alihimiza “kila muumini [kuwa] mmisionari” wakati aliposimamia misheni ya Ulaya kuanzia 1922 mpaka 1924, na alishiriki ujumbe sawa na huo pamoja na Kanisa lote katika mkutano mkuu mapema kama 1952 (ona “’Kila muumini ni Mmisionari’ Kaulimbiu Inayosimama Imara Leo,” Habari za Kanisa, Feb. 20, 2015, news.

  7. Mafundisho na Maagano 64:34.

  8. Ona Mathayo 22:37–38.

  9. Ona Matayo 22:39.

  10. Mafundisho na Maagano 93:12.

  11. Isaya 28:10.

  12. Mosia 18:9

  13. wazo hili mara nyingi huasisiwa kwa Mtakatifu Francis wa Assisi; ona pia Yohana 10:36–38.

  14. Warumi 1:16.

  15. Ona Mathayo 5:15-16.

  16. Yohana 1:46; msisitizo umeongezwa.

  17. Ona Yohana 3:18.

  18. 1 Petro 4:13, Toleo la Kiingereza; ona pia mistari 1–19 kwa mengi ya jinsi wafuasi wa Kristo wanavyopaswa kutazama mateso kwa ajili ya injili.

  19. Matendo ya Mitume 5:41.

  20. Mafundisho na Maagano 45:44.