2010–2019
Nyumba Ambapo Roho wa Bwana Hukaa
Mkutano Mkuu wa Aprili 2019


2:3

Nyumba Ambapo Roho wa Bwana Hukaa

Mtapata baadhi ya shangwe zenu kuu katika juhudi zenu za kufanya nyumba zenu sehemu ya imani katika Bwana Yesu Kristo na sehemu ambayo imejaa upendo.

Kaka zangu na dada zangu wapendwa, nina shukrani kuwa nimealikwa kuzungumza nanyi katika Mkutano huu Mkuu wa 189 wa mwaka wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Katika tarehe kama hii mwaka 1830, Joseph Smith aliunda Kanisa chini ya uelekezi wa Bwana. Ilifanyika katika nyumba ya familia ya Whitmer huko Fayette, New York. Kulikuwa na waumini sita na takribani watu wengine 50 waliovutiwa siku hiyo.

Ingawa sijui ni nini Nabii Joseph smith alikisema au jinsi alivyoonekana wakati aliposimama mbele ya kundi lile dogo, najua jinsi watu wale wenye imani katika Yesu Kristo walivyohisi. Walimhisi Roho Mtakatifu, na walihisi kwamba walikuwa katika sehemu takatifu. Walihisi hakika kwamba walikuwa wamoja.

Hisia hizo za kimiujiza ndicho kile ambacho sote tunakitaka katika nyumba zetu. Ni hisia ambayo huja kutokana na kuwa na, kama Paulo alivyoelezea, “nia ya kiroho.”1

Lengo langu leo ni kufundisha kile ninachojua kuhusu jinsi tunavyoweza kustahili kupata hisia hiyo mara kwa mara na kuialika kukaa kwa muda mrefu katika familia zetu. Kama mjuavyo kutokana na uzoefu, kwamba si rahisi kufanya hivyo. Mabishano, majivuno, na dhambi vinatakiwa kuwekwa kando. Upendo msafi wa Kristo lazima uje katika mioyo ya wale walio katika familia zetu.

Adamu na Hawa, Lehi na Saria, na wazazi wengine tunaowajua kutoka katika maandiko walipata kwamba hii ilikuwa ni changamoto ngumu. Lakini kuna mifano ya kutia moyo ya furaha ya kudumu katika familia na nyumba inayotuondolea hofu. Na mifano hiyo hutufanya tuone jinsi inavyoweza kutokea kwetu na katika familia zetu. Mnakumbuka tukio katika 4 Nefi:

“Na ikawa kwamba hakukuwa na ubishi katika nchi, kwa sababu ya mapenzi ya Mungu ambayo yaliishi katika mioyo ya watu.

“Na hakukuwa na wivu, wala ubishi, wala misukosuko, wala ukahaba, wala uwongo, wala mauaji, wala uzinifu wa aina yoyote; na kwa kweli hakujakuwa na watu ambao wangekuwa na furaha zaidi miongoni mwa watu wote ambao waliumbwa na mkono wa Mungu.

“Hakukuwa na wanyang’anyi, wala wauaji, wala hakukuwa na Walamani, wala aina yoyote ya vikundi; lakini walikuwa kitu kimoja, watoto wa Kristo, na warithi wa ufalme wa Mungu.

“Na jinsi gani walibarikiwa! Kwani Bwana aliwabariki kwa matendo yao yote; ndio, hata walibarikiwa na kufanikiwa mpaka miaka mia moja na kumi ikapita; na kizazi cha kwanza kutoka Kristo kilikuwa kimepita, na hakukuwa na ubishi katika nchi yote.”2

Kama mjuavyo, kwamba wakati huo wa furaha haukudumu milele. Tukio katika 4 Nefi huelezea dalili za baadaye za kufifia kiroho kati ya kundi la watu wazuri. Ni mpangilio ambao umetokea kwa nyakati nyingi kwa watu wote, katika mikusanyiko, na mbaya zaidi, katika familia. Kwa kujifunza mpangilio huu, tunaweza kuona jinsi tunavyoweza kulinda na hata kuongeza hisia za upendo katika familia yetu.

Hapa kuna mpangilio wa kufifia ambao ulitokea baada ya miaka 200 ya kuishi katika amani kamilifu iletwayo na injili:

Majivuno yaliingia.

Watu waliacha kushiriki na wengine vile walivyokuwa navyo.

Walianza kujiona katika hali za juu au chini wao kwa wao.

Walianza kufifia kwenye imani yao katika Yesu Kristo.

Walianza kuchukia.

Walianza kutenda dhambi za kila namna.

Wazazi wenye busara watakuwa makini zaidi kujua dalili hizo wakati zikitokea kati ya wanafamilia wao. Bila shaka, watakuwa na wasiwasi. Lakini watajua kwamba kisababishi cha msingi ni ushawishi wa Shetani akijaribu kuwaongoza watu wazuri chini katika njia ya kutenda dhambi na hivyo kupoteza ushawishi wa Roho Mtakatifu. Kwa hivyo mzazi mwenye busara ataona kwamba fursa ipo katika kumuongoza kila mtoto, na wao wenyewe, kukubali kikamilifu zaidi mwaliko wa Bwana wa kuja Kwake.

Ungeweza kuwa na mafanikio kidogo kwa kumwita mtoto kutubu, kwa mfano, kwenye majivuno. Ungeweza kujaribu kuwashawishi watoto kushiriki kile walichonacho kwa ukarimu. Ungeweza kuwaomba kuacha kuhisi kuwa wao ni bora zaidi ya mwingine yoyote katika familia. Lakini kisha unakuja kwenye dalili niliyoelezea awali kama “Walianza kufifia imani katika Yesu Kristo.”

Kuna umuhimu wa kuongoza familia yako kuinuka kufika sehemu hiyo ya kiroho ambayo unataka wao wafike—na kwa ajili yako kuwa pale pamoja nao. Wakati unapowasaidia wao kukua katika imani kwamba Yesu Kristo ni Mkombozi wao mpendwa, watahisi hamu ya kutubu. Wanapofanya hivyo, unyenyekevu utaanza kuchukua nafasi ya majivuno. Wanapoanza kuhisi kile ambacho Bwana amewapa, watataka kushiriki kwa ukarimu zaidi. Ushindani kwa ajili ya umaarufu na kutambulika utapungua. Chuki itaondolewa na upendo. Na mwishowe, kama ilivyotendeka kwa watu walioongolewa na Mfalme Benyamini, hamu ya kutenda wema itawaimarisha dhidi ya jaribu la kutenda dhambi. Watu wa Mfalme Benyamini walishuhudia kwamba “hawakuwa na hamu tena ya kutenda maovu.”3

Hivyo kujenga imani katika Yesu Kristo ni mwanzo wa kutatua kufifia kiroho katika familia yako na nyumbani kwako. Imani hiyo inaweza kwa kiasi kikubwa kuleta toba kuliko mahubiri yako dhidi ya kila dalili ya kufifia kiroho.

Utaongoza vizuri zaidi kwa mfano. Wanafamilia pamoja na wengine lazima wakuone ukikua katika imani yako mwenyewe katika Yesu Kristo na katika injili Yake. Hivi karibuni umepewa msaada mkubwa sana. Wazazi katika Kanisa wamebarikiwa kwa mtaala wenye msukumo wa kiungu kwa ajili ya familia na watu binafsi. Unapoutumia, utajenga imani yako na imani ya watoto wako katika Bwana Yesu Kristo.

Kukua katika Imani

Imani yako katika Mwokozi imekua wakati ulipofuata pendekezo la Rais Russell M. Nelson la kusoma tena Kitabu cha Mormoni. Uliwekea alama vifungu na maneno ambayo yalimzungumzia Mwokozi. Imani yako katika Yesu Kristo ilikua. Lakini kama mmea mchanga, imani hiyo katika Yesu Kristo itanyauka isipokuwa upate suluhisho endelevu kutafakari na kusali ili kuiongeza.

Mfano wako wa kukua katika imani unaweza usifuatwe na wanafamilia wako wote kwa sasa. Lakini jipe moyo kutoka katika uzoefu wa Alma Mdogo. Katika maumivu yake makali ya hitaji la toba na msamaha, alikumbuka imani ya baba yake katika Yesu Kristo. Watoto wako wanaweza kukumbuka imani yako katika Mwokozi wakati kwa dhati wanapohitaji toba. Alma alisema kuhusu wakati kama huo:

“Na ikawa kwamba wakati nilipoteseka na maumivu mabaya, wakati nilihuzunishwa na ufahamu wa dhambi zangu nyingi, tazama, nilikumbuka pia nikisikia baba yangu akitoa unabii kwa watu kuhusu kuja kwa mmoja aitwaye Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, kulipia dhambi za ulimwengu.

“Sasa, nilipofiikiria wazo hili, nililia ndani ya moyo wangu: Ee Yesu, wewe Mwana wa Mungu, nihurumie, mimi ambaye nina uchungu, na nimezungukwa na minyororo ya kifo kisicho na mwisho.

“Na sasa, tazama, nilipofikiri hivi, sikukumbuka uchungu wangu tena; ndio, sikuteseka na ufahamu wa dhambi zangu tena.”4

Kusali kwa Upendo

Kwa kuongezea katika mfano wako wa kukua katika imani, kusali kwenu kama familia kunaweza kuwa sehemu muhimu sana katika kutengeneza nyumba kuwa sehemu takatifu. Mtu mmoja mara nyingi huchaguliwa kuwa mnenaji kusali kwa ajili ya familia. Wakati sala inapokuwa dhahiri kwa Mungu kwa niaba ya watu waliopiga magoti na kusikiliza, imani hukua ndani yao wote. Wanaweza kuhisi hisia za upendo kwa Baba wa Mbinguni na Mwokozi. Na wakati mtu anayesali anapowataja wale waliopiga magoti katika mduara huo wa familia ambao wana mahitaji, wote wanaweza kuhisi upendo kwao na kwa kila mwanafamilia.

Hata kama wanafamilia hawaishi nyumbani, sala inaweza kujenga mahusiano ya upendo. Sala katika familia inaweza kuvuka mipaka ya ulimwengu. Zaidi ya mara moja nimejifunza kwamba mwanafamilia aliye mbali sana alikuwa akisali wakati uleule na kwa ajili ya kitu kilekile kama nilivyokuwa nikifanya mimi. Kwangu mimi, msemo wa zamani “Familia ambayo husali pamoja hukaa pamoja” ungeweza kuongezwa kuwa “Familia ambayo husali pamoja ina umoja, hata wakati wako mbali na kila mmoja wao.”

Kufundisha Toba ya Mapema

Kwa sababu hakuna kati yetu ambaye ni mkamilifu na hisia huumizwa kirahisi, familia zinaweza kuwa tu mahali patakatifu tunapotubu mapema na kwa dhati. Wazazi wanaweza kuwa mfano. Maneno makali au mawazo yasiyo ya ukarimu yanaweza kufanyiwa toba haraka na kwa dhati. Neno rahisi “samahani” linaweza kuponya vidonda na kualika vyote msamaha na upendo.

Nabii Joseph Smith alikuwa ni mfano kwetu wakati alipokabiliana na mashambulizi makali, wasaliti, na hata kutokuelewana katika familia yake. Alisamehe haraka, hata kama alijua mshambuliaji angeshambulia tena. Aliomba msamaha, na yeye aliutoa bure.5

Kujenga Roho ya Kimisionari

Wana wa Mosia walidhamiria kutoa injili kwa kila mtu. Hamu hii ilikuja kutokana na uzoefu wao binafsi wa toba. Hawakuweza kuvumilia wazo kwamba mtu yoyote anasumbuka kwa madhara ya dhambi kama ilivyokuwa kwao. Hivyo walikumbana na miaka mingi ya kukataliwa, ugumu, na hatari katika kutoa injili ya Yesu Kristo kwa adui zao. Katika mchakato huo, walipata shangwe katika wengi wa waliotubu na kupata shangwe ya msamaha kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo.

Wanafamilia wetu watakua katika hamu yao ya kushiriki injili wakati wanapohisi shangwe ya msamaha. Hiyo inaweza kuja hata wanapokuwa wakifanya upya maagano wakati wanaposhiriki sakramenti. Roho ya kimisionari itakuwa katika nyumba zetu wakati watoto na wazazi wanapohisi shangwe ya msamaha katika huduma ya sakramenti. Kwa mfano wao wa utulivu, wote wazazi na watoto wanaweza kusaidiana kuhisi shangwe hiyo. Shangwe hiyo inaweza kwenda mbali zaidi katika kugeuza nyumba zetu kuwa vituo vya mafunzo ya umisionari. Si wote wanaweza kutumikia misheni, lakini wote watahisi hamu ya kushiriki injili, ambayo imewafanya wao kuhisi msamaha na amani. Na hata kama kwa sasa wanatumikia muda wote au hawatumikii, wote wanaweza kuhisi shangwe katika kushiriki injili na wegine.

Kwenda Hekaluni

Kwa wote wazazi na watoto, hekalu ni fursa nzuri zaidi ya kupata hisia kwa ajili ya na upendo wa sehemu za kimbingu. Hiyo ni kweli hasa wakati watoto ni wadogo. Watoto wanazaliwa wakiwa na Nuru ya Kristo. Hata mtoto anaweza kuhisi kwamba hekalu ni takatifu. Kwa sababu wazazi wanawapenda watoto wao, hekalu huwasilisha kwao tumaini kwamba wanaweza kuwa na watoto wao kuwapenda katika familia zao za milele—daima.

Baadhi yenu mna picha za mahekalu katika nyumba zenu. Wakati mahekalu yakiwa yanaongezwa duniani kote, inawezekana kwa wazazi wengi kutembelea ardhi ya hekalu pamoja na familia zao. Baadhi wanaweza hata kuhudhuria shughuli ya ufunguzi wakati mahekalu yanajengwa. Wazazi wanaweza kuwauliza watoto jinsi walivyohisi kwa kuwa karibu na hekalu au ndani ya hekalu.

Kila mzazi anaweza kutoa ushuhuda wa nini hekalu humaanisha kwake. Rais Ezra Taft Benson, ambaye aliyapenda mahekalu, aliongea mara nyingi kuhusu kumuona mama yake kwa umakini akinyoosha nguo zake za hekaluni.6 Aliongea kuhusu kumbukumbu yake kama kijana mdogo akiiona familia yake wakati wakiondoka nyumbani kwao kwenda kuhudhuria hekaluni.

Wakati alipokuwa Rais wa Kanisa, alihudhuria hekaluni siku ile ile kila wiki. Mara zote alifanya kazi ya hekaluni kwa ajili ya mababu. Ilitokana hasa na mfano wa wazazi wake.

Ushuhuda Wangu

Mtapata baadhi ya shangwe zenu kuu katika juhudi zenu za kufanya nyumba zenu sehemu ya imani katika Bwana Yesu Kristo na sehemu ambayo hujazwa kwa upendo, upendo msafi wa Kristo. Urejesho wa injili ulianza kwa swali la dhati lililotafakariwa katika nyumba nyenyekevu, na inaweza kuendelea katika kila nyumba zetu wakati tukiendelea kujenga na kutumia kanuni za injili huko. Hili limekuwa ni tumaini langu na nia ya dhati tangu nilipokuwa kijana mdogo. Nyote mmewahi kwa muda kupata taswira ya nyumba za namna hiyo. Wengi wenu, kwa msaada wa Bwana, mmezitengeneza.

Baadhi mmejaribu kwa moyo wa dhati kwa ajili ya baraka hiyo, lakini bado haijatolewa. Ahadi yangu kwenu ni moja ambayo mshiriki wa akidi ya Mitume Kumi na Wawili aliwahi kuitoa kwangu. Nilikuwa nimemwambia kwamba kwa sababu ya chaguzi ambazo baadhi katika familia yetu kubwa wamezifanya, nilikuwa na shaka kwamba tungeweza kuwa pamoja katika ulimwengu ujao. Alisema, vile ninavyoweza kukumbuka, “Una wasiwasi juu ya tatizo ambalo si sahihi. Wewe ishi tu kwa kustahili ufalme wa selestia, na mipangilio ya familia itakuwa mizuri ajabu kuliko unavyofikiria.”

Ninaamini kwamba angetoa tumaini hilo la furaha kwa yoyote kati yetu katika maisha haya ya duniani ambao tumefanya yote tunayoweza kustahili sisi wenyewe na familia zetu kwa ajili ya uzima wa milele. Ninajua kwamba mpango wa Baba wa Mbinguni ni mpango wa furaha. Ninashuhudia kwamba mpango Wake unafanya iwezekane kwa kila mmoja wetu ambaye amefanya yote tunayoweza kuunganishwa katika familia milele.

Ninajua kwamba funguo za ukuhani zilizorejeshwa kwa Joseph smith zilitolewa katika mtiririko usio na kikomo kwa Rais Russell M. Nelson. Funguo hizo zinawezesha kuunganishwa kwa familia leo hii. Ninajua kwamba Baba wa Mbinguni anatupenda sisi, watoto Wake wa kiroho, kwa upendo mkamilifu. Ninajua kwamba kwa sababu ya Upatanisho wa Yesu Kristo, tunaweza kutubu, kusafishwa, na kuwa wastahiki kuishi katika familia zenye upendo milele pamoja na Baba yetu wa Mbinguni na Mwana Wake Mpendwa, Yesu Kristo. Ninashuhudia hivyo katika jina la Yesu Kristo, amina.