Hazina za Kiroho
Mnapofanyia kazi imani katika Bwana na nguvu Yake ya ukuhani, uwezo wenu wa kuleta hazina hii ya kiroho ambayo Bwana amefanya ipatikane utaongezeka.
Asanteni kwa muziki huo wa kupendeza. Wakati sote tuliposimama kuimba wimbo huo wa katikati, “Asante, Mungu, kwa Nabii,” nilipata mawazo mawili yenye nguvu zaidi yaliyonijia. Moja ni kuhusu Nabii Joseph Smith, nabii wa kipindi hiki cha maongozi ya Mungu. Upendo na uvutiwaji wangu kwake unakua kwa kila siku ipitayo. Wazo la pili lilitokea pale nilipomtazama mke wangu, binti zangu, wajukuu zangu wa kike na vitukuu vyangu vya kike. Nilihisi kama vile ningependa kumchukua kila mmoja wenu kama sehemu ya familia yangu.
Miezi kadhaa iliyopita, katika hitimisho la kipindi cha endaumenti hekaluni, nilimwambia mke wangu Wendy, “natumaini akina dada wanaelewa hazina za kiroho ambazo ni zao ndani ya hekalu.” Akina dada, mara nyingi ninajikuta nikifikiria kuwahusu, ikijumuisha miezi miwili iliyopita wakati mimi na Wendy tulipozuru Harmony, Pennsylvania.
Hii ilikuwa ni safari yetu ya pili huko. Nyakati zote tumepata msukumo wa kina pale tulipotembea juu ya ardhi hiyo takatifu. Ilikuwa karibu na Harmony ambapo Yohana Mbatizaji alimtokea Joseph Smith na kurejesha Ukuhani wa Haruni.
Ilikuwa huko ambapo Mitume Petro, Yakobo, na Yohana walitokea kurejesha Ukuhani wa Melkizedeki.
Ilikuwa huko Harmony ambapo Emma Hale Smith alitumikia kama mwandishi wa kwanza wa mume wake wakati Nabii alipotafsiri Kitabu cha Mormoni.
Ilikuwa pia huko Harmony ambapo Joseph alipokea ufunuo uliodhihirisha mapenzi ya Bwana kwa Emma. Bwana alimwelekeza Emma kuyaelezea maandiko, kushawishi Kanisa, kupokea Roho Mtakatifu, na kutumia muda wake “kujifunza mengi.” Emma alishauriwa pia “kuyaweka kando mambo ya ulimwengu huu, na kuyatafuta mambo ya ulimwengu ulio bora,” na kuyashikilia maagano yake na Mungu. Bwana alihitimisha maelekezo yake kwa maneno haya yenye msukumo: “Hii ni sauti yangu kwa wote.”1
Kila kitu ambacho kilitokea katika eneo hili kina uhusiano mkubwa kwenye maisha yenu. Urejesho wa ukuhani, pamoja na ushauri wa Bwana kwa Emma, vinaweza kumuongoza na kumbariki kila mmoja wenu. Jinsi gani ninavyotamani muelewe kwamba urejesho wa ukuhani unahusika kwako kama mwanamke kama vile ilivyo kwa mwanaume yeyote. Kwa sababu Ukuhani wa Melkizedeki umerejeshwa, wanawake na wanaume watunza maagano wana fursa kwenye baraka “zote za kiroho za kanisa,”2 au, tungeweza kusema, kwenye hazina zote za kiroho Bwana alizonazo kwa watoto Wake.
Kila mwanamke na kila mwanaume anayefanya maagano na Mungu na kutunza maagano hayo, na anayeshiriki kwa kustahili katika ibada za ukuhani, ana fursa ya moja kwa moja kwenye nguvu ya Mungu. Wale ambao wamepokea endaumenti katika nyumba ya Bwana wanapokea kipawa cha nguvu ya ukuhani ya Mungu kwa njia ya agano lao, pamoja na kipawa cha ufahamu wa kujua jinsi ya kuvuta nguvu hiyo.
Mbingu ziko wazi kwa wanawake ambao wamepokea endaumenti ya nguvu ya Mungu ikitiririka kutoka kwenye maagano yao ya ukuhani kama ilivyo kwa wanaume ambao wana ukuhani. Ninaomba kwamba ukweli uweze kujiandika juu ya mioyo ya kila mmoja wenu kwa sababu ninaamini utabadili maisha yenu. Akina dada, mna haki ya kuleta kwa ukarimu nguvu za Mwokozi ili kuzisaidia familia zenu na wengine mnaowapenda.
Sasa, yaweza kuwa unajiambia mwenyewe, “Hili linaonekana la kupendeza, lakini ninalifanikishaje? Ni kwa jinsi gani ninaleta nguvu ya Mwokozi kwenye maisha yangu?”
Huwezi kukuta mchakato huu umeelezewa kwenye kitabu chochote cha kiada. Roho Mtakatifu atakuwa mwalimu wako binafsi pale unapotafuta kuelewa kile ambacho Bwana angependa ujue na ufanye. Mchakato huu si wa haraka wala rahisi, lakini ni wa kuimarisha kiroho. Nini kingeweza kuwa cha kufurahisha sana zaidi ya kufanya kazi na Roho ili kuelewa nguvu ya Mungu—nguvu ya ukuhani?
Kile ninachoweza kuwaambia ni kwamba kufikia nguvu ya Mungu katika maisha yako kunahitaji mambo sawa na yale ambayo Bwana alimwelekeza Emma na kila mmoja wenu kufanya.
Hivyo, ninawaalika kujifunza kwa sala sehemu ya 25 ya Mafundisho na Maagano na kugundua kile Roho Mtakatifu atakachokufundisha wewe. Juhudi zako binafsi za kiroho zitakuletea shangwe pale unapopokea, unapoelewa, na unapotumia nguvu ambayo kwayo umepokea endaumenti.
Sehemu ya jitihada hii itakuhitaji kuweka kando mambo mengi ya ulimwengu huu. Wakati mwingine tunazungumza kwa kawaida sana kuhusu kuwa mbali na ulimwengu pamoja na mabishano yake, majaribu yaliyoenea, na filosofia za uongo. Lakini kwa kweli kufanya hivyo kunakuhitaji utathmini maisha yako kwa uangalifu sana na mara kwa mara. Unapofanya hivyo, Roho Mtakatifu atakuvuvia kuhusu kile ambacho hakiitajiki tena, kile ambacho hakistahili tena muda na nguvu zako.
Unapoondosha fokasi yako kutoka kwenye vurugu za ulimwengu, baadhi ya mambo yanayoonekana ya muhimu kwako sasa yatarudi nyuma katika kipaumbele. Utahitaji kusema hapana kwa baadhi ya mambo, hata kama yanaweza kuonekana hayana madhara. Unapojiingiza na kuendelea katika mchakato huu wa maisha yote wa kuweka wakfu maisha yako kwa Bwana, mabadiliko katika mtazamo wako, hisia, na nguvu yako ya kiroho yatakushangaza!
Sasa neno dogo la tahadhari. Kuna wale ambao watafanya duni uwezo wako wa kuita nguvu ya Mungu. Kuna baadhi ambao watakufanya ujionee shaka na kupunguza uwezo wako wa mtandao wa kiroho kama mwanamke mwadilifu.
Kwa hakika hasa, mjaribu hataki uelewe agano ulilofanya kwenye ubatizo au endaumenti kubwa ya ufahamu na nguvu uliyopokea au utakayopokea ndani ya hekalu—nyumba ya Bwana. Na Shetani kwa hakika hataki uelewe kwamba kila muda unapotumikia na kuabudu kwa kustahili hekaluni, unaondoka ukiwa na ulinzi wa nguvu ya Mungu pamoja na malaika Zake “wakikulinda ” wewe.3
Shetani na watumishi wake daima watabuni vikwazo ili kukuzuia kuelewa vipawa vya kiroho ambavyo umeweza na unaweza kubarikiwa navyo. Kwa bahati mbaya, baadhi ya vikwazo vinaweza kuwa matokeo ya tabia mbaya za mtu mwingine. Inanihuzunisha kufikiria kwamba yeyote kati yenu amehisi kutengwa au kutoaminiwa na kiongozi wa ukuhani, au amenyanyaswa au kusalitiwa na mume, baba, au rafiki aliyeonekana mwema. Ninahisi huzuni nyingi kwamba yeyote kati yenu amehisi kuwekwa kando, kutoheshimiwa, au kuhukumiwa kimakosa. Maudhi kama hayo hayana nafasi katika ufalme wa Mungu.
Kinyume chake, inanisisimua wakati ninapojifunza juu ya viongozi wa ukuhani ambao kwa shauku wanatafuta ushiriki wa wanawake katika mabaraza ya kata na vigingi. Ninavutiwa na kila mume ambaye anaonesha kwa mfano kwamba jukumu lake la muhimu zaidi la ukuhani ni kumtunza mkewe.4 Ninamsifu mwanaume yule ambaye kwa dhati anaheshimu uwezo wa mkewe wa kupokea ufunuo na kumthamini kama mwenza sawa katika ndoa yao.
Wakati mwanaume anapoelewa nguvu na ukuu wa mwanamke Mtakatifu wa Siku za Mwisho mwadilifu, anayeomba, aliyepokea endaumenti, je si ni ajabu yoyote kwamba anahisi kusimama wakati mwanamke huyo anapoingia chumbani?
Toka mwanzo wa nyakati, wanawake wamebarikiwa kwa dira ya kipekee ya maadili—uwezo wa kutofautisha jema na baya. Karama hii inakuzwa kwa wale wanaofanya na kutunza maagano. Na inafifia kwa wale ambao kwa makusudi wanapuuzia amri za Mungu.
Ninaharakisha kuongeza kwamba siwaepushi wanaume katika njia yoyote kutoka kwenye vigezo vya Mungu kwa ajili yao pia kutofautisha kati ya jema na baya. Lakini dada zangu wapendwa, uwezo wenu wa kutambua ukweli kutoka kwenye kosa, kuwa walinzi wa maadili wa jamii, ni muhimu katika siku hizi za mwisho. Na tunawategemea muwafundishe wengine kufanya vivyo hivyo. Acha niwe wazi kuhusu hili: ikiwa ulimwengu unapoteza unyofu wa maadili wa wanawake wake, ulimwengu kamwe hautapona.
Sisi Watakatifu wa siku za Mwisho si wa ulimwengu; sisi ni wa Israeli ya agano. Tumeitwa kuwaandaa watu kwa Ujio wa Pili wa Bwana.
Sasa, naweza kufafanua vipengele kadhaa vya ziada katika kuzingatia wanawake na ukuhani. Wakati unaposimikwa kutumikia katika wito chini ya maelekezo ya yule anayeshikilia funguo za ukuhani—kama vile askofu wako au rais wa kigingi—unapewa mamlaka ya ukuhani kufanya kazi katika wito huo.
Kadhalika, ndani ya hekalu takatifu unapewa mamlaka ya kufanya na kusimama kwa niaba katika ibada za ukuhani kila mara unapohudhuria. Endaumenti yako ya hekaluni inakuandaa kufanya hivyo.
Ikiwa umepokea endaumenti na kwa sasa hujaolewa na mwanaume aliye na ukuhani na mtu anakuambia, “ninahisi vibaya kwamba huna ukuhani nyumbani kwako,” tafadhali elewa kwamba kauli hiyo si sahihi. Unaweza usiwe na mwenye ukuhani nyumbani kwako, lakini umepokea na kufanya maagano matakatifu na Mungu ndani ya hekalu Lake. Kutoka kwenye maagano hayo inatiririka endaumenti ya nguvu ya ukuhani Wake juu yako. Na kumbuka, ikiwa mume wako angekufa, wewe ungesimamia katika nyumba yako.
Kama mwanamke Mtakatifu wa Siku za Mwisho, mwadilifu, aliyepokea endaumenti, unazungumza na kufundisha kwa nguvu na mamlaka kutoka kwa Mungu. Iwe ni kwa kuonya au mazungumzo, tunahitaji sauti yako kufundisha mafundisho ya Kristo. Tunahitaji mchango wako katika mabaraza ya familia, kata, na kigingi. Ushiriki wako ni muhimu na kamwe si wa mapambo!
Dada zangu wapendwa, nguvu yenu itaongezeka pale mnapowatumikia wengine. Sala zenu, kufunga, muda katika maandiko, huduma ndani ya hekalu na kazi ya historia ya familia vitafungua mbingu kwenu.
Ninawasihi mjifunze kwa sala kweli zote mnazoweza kupata kuhusu nguvu ya ukuhani. Mngeweza kuanza na Mafundisho na Maagano 84 na 107. Sehemu hizo zitawaongoza kwenye vifungu vingine. Maandiko na mafundisho ya manabii, waonaji, na wafunuzi wa siku hizi yamejaa kweli hizi. Pale ufahamu wenu unapoongezeka na pale mnapofanyia kazi imani katika Bwana na nguvu Yake ya ukuhani, uwezo wenu wa kuleta hazina hii ya kiroho ambayo Bwana amefanya ipatikane utaongezeka. Mnapofanya hivyo, mtajikuta mkiweza vizuri zaidi kusaidia kujenga familia za milele ambazo zina umoja, zimeunganishwa ndani ya hekalu la Bwana, na zimejaa upendo kwa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo.
Juhudi zetu zote za kuhudumiana, kutangaza injili, kuwakamilisha Watakatifu, na kuwakomboa wafu zinakutana ndani ya hekalu takatifu. Kwa sasa tuna mahekalu 166 ulimwenguni kote, na zaidi yanakuja.
Kama mjuavyo, Hekalu la Salt Lake, Temple Square, na uwanda unaopakana karibu na Jengo la Ofisi ya Kanisa yatarekebishwa katika mradi ambao utaanza mwishoni mwa mwaka huu. Hili hekalu takatifu lazima litunzwe na kuandaliwa ili kuvutia vizazi vijavyo, kama vile lilivyotushawishi sisi katika kizazi hiki.
Wakati Kanisa linapokua, mahekalu zaidi yatajengwa ili kwamba familia nyingi ziweze kufikia baraka ile kuu kuliko zote, ile ya uzima wa milele.5 Tunachukulia hekalu kama jengo takatifu zaidi katika Kanisa. Wakati mipango inapotangazwa ya kujenga hekalu jipya, linakuwa sehemu ya historia yetu takatifu. Kama tulivyojadili hapa usiku huu, ninyi akina dada ni muhimu kwenye kazi ya hekalu, na hekaluni ni mahala ambapo mtapokea hazina zenu kubwa za kiroho.
Tafadhali sikilizeni kwa makini na kwa unyenyekevu wakati sasa ninatangaza mipango ya kujenga mahekalu mapya manane. Ikiwa moja linatangazwa katika eneo ambalo ni maalumu kwako, ninapendekeza kwamba uinamishe tu kichwa chako kwa sala pamoja na shukrani katika moyo wako. Tunafurahia kutangaza mipango ya kujenga mahekalu katika maeneo yafuatayo: Freetown, Sierra Leone; Orem, Utah; Port Moresby, Papua New Guinea; Bentonville, Arkansas; Bacolod, Philippines; McAllen, Texas; Cobán, Guatemala; na Taylorsville, Utah. Asanteni, dada zangu wapendwa. Tunashukuru kwa dhati mapokezi yenu ya mipango hii na mwitikio wenu wa unyenyekevu.
Sasa, katika hitimisho, ningependa kuacha baraka juu yenu, kwamba muweze kuelewa nguvu ya ukuhani ambayo kwayo mmepokea endaumenti na kwamba mtaongeza nguvu hiyo kwa kufanyia kazi imani yenu katika Bwana na katika nguvu Yake.
Wapendwa akina dada, kwa heshima na shukrani kubwa, ninaelezea upendo wangu kwenu. Kwa unyenyekevu, ninatangaza kwamba Mungu yu hai! Yesu ndiye Kristo. Hili ni kanisa Lake. Nashuhudia hivyo, katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.