Amri Kuu ya Pili
Shangwe yetu kuu huja wakati tunapowasaidia kaka zetu na dada zetu.
Wapendwa kaka zangu na dada zangu, asanteni kwa yote mnayofanya katika kusaidia kukusanya Israeli pande zote za pazia, kuimarisha familia zenu, na kubariki maisha ya wale wenye mahitaji. Asanteni kwa kuishi kama wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo.1 Mnajua na mnapenda kutii amri Zake mbili kuu, kumpenda Mungu na kuwapenda jirani zenu.2
Katika miezi sita iliyopita, mimi na Dada Nelson tumekutana na maelfu ya Watakatifu tulipokuwa tukisafiri Amerika ya Kati na Amerika ya Kusini, visiwa vya Pasifiki, na miji mbali mbali nchini Marekani. Tunaposafiri, tumaini letu ni kujenga imani yenu. Lakini daima tunarudi imani yetu ikiwa imeimarishwa na waumini na marafiki tunaokutana nao. Naweza kushiriki nanyi nyakati tatu zenye tija kutoka kwenye matukio yetu ya hivi karibuni?
Mwezi Mei, mimi pamoja na Dada Nelson tulisafiri na Mzee Gerrit W. na Dada Susan Gong kwenda Pasifiki ya Kusini. Tulipokuwa Auckland, New Zealand, tulipata heshima ya kukutana na maimamu kutoka misikiti miwili huko Christchurch, New Zealand, ambapo miezi miwili tu iliyopita, waabuduo wasio na hatia walikuwa wameuwawa katika vitendo vya vurugu za kutisha.
Tulitoa mkono wetu wa pole kwa ndugu hawa wa imani nyingine na tukasisitiza tena nia yetu ya pamoja katika uhuru wa kidini.
Pia tulijitolea nguvu kazi na msaada wa kifedha wa kujenga upya misikiti yao. Mkutano wetu na viongozi hawa wa Kiislamu ulijawa na hisia nzuri za undugu.
Mnamo Agosti, nikiongozana na Mzee Quentin L. na Dada Mary Cook, mimi na Dada Nelson tulikutana na watu huko Buenos Aires, Argentina—wengi wao siyo wa imani yetu—ambao maisha yao yamebadilishwa na viti vya magurudumu vilivyotolewa na kikundi chetu cha Hisani cha Watakatifu wa Siku za mwisho. Tulitiwa moyo wakati walipokuwa wakielezea shukrani iliyojaa furaha kwa kupata njia yao mpa ya kujongea.
Wakati wa tatu wa thamani ulikuwa wiki chache zilizopita hapa katika Jiji la Salt Lake. Ulikuja kutoka kwenye barua ya kipekee niliyopokea wakati wa kumbukizi yangu ya kuzaliwa kutoka kwa msichana ambaye nitamuita Mary—mwenye umri wa miaka 14.
Mary aliandika juu ya mambo ambayo kwayo mimi na yeye tulifanana: “Una watoto 10. Tuna watoto 10. Unazungumza Kimandarin. Watoto saba katika familia yangu, ikiwa ni pamoja na mimi, waliasiliwa kutoka China, kwa hivyo Mandarin ndiyo lugha yetu ya kwanza. Wewe ni daktari wa moyo. Dada yangu amefanyiwa [upasuaji] wa moyo mara mbili. Unapenda kanisa la masaa mawili. Tunapenda kanisa la masaa mawili. Una sauti nzuri. Kaka yangu ana sauti nzuri pia. Yeye ni kipofu kama mimi.”
Maneno ya Mary yalinigusa sana, yakifunua si tu roho yake kuu bali pia kujiweka wakfu kwa baba na mama yake.
Watakatifu wa Siku za Mwisho, kama ilivyo kwa wafuasi wengine wa Yesu Kristo, daima wanatafuta njia za kusaidia, kuinua, na kupenda wengine. Wale walio radhi kuitwa watu wa Bwana “wapo radhi “kubeba mizigo ya mmoja na ya mwingine, … kuomboleza na wale wanaoomboleza, na kuwafariji wale ambao wanahitaji kufarijiwa.”3
Kwa dhati wanatafuta kuishi amri kuu ya kwanza na ya pili. Tunapompenda Mungu kwa mioyo yetu yote, Yeye hubadilisha mioyo yetu kwa ustawi wa wengine katika mzunguko mzuri, wa wema.
Haiwezekani kuhesabu kiasi cha huduma ambayo Watakatifu wa Siku za Mwisho hutoa ulimwenguni kote kila siku ya kila mwaka, lakini inawezekana kuhesabu mazuri ambayo Kanisa kama taasisi hufanya ili kubariki waume kwa wake—wavulana na wasichana—ambao wanahitaji mkono wa usaidizi.
Msaada wa kibinadamu wa Kanisa ulianzishwa mnamo 1984. Kisha mfungo wa Kanisa lote ulifanywa ili kupata fedha za kuwasaidia wale walioathirika na ukame wa kutisha huko mashariki ya Afrika. Washiriki wa Kanisa walichanga dola millioni 6.4 katika siku hiyo moja ya mfungo.
Kisha Mzee M. Russell Ballard na Kaka Glenn L. Pace walipelekwa Ethiopia kuangalia jinsi ambavyo pesa hizo zilizowekwa wakfu zingeweza kutumiwa vyema. Juhudi hii ilithibitisha kuwa mwanzo wa kile ambacho baadaye kilijulikana kama Misaada ya Hisani ya Watakatifu wa Siku za Mwisho.
Tangu wakati huo, Misaada ya Hisani ya Watakatifu wa Siku za Mwisho imetoa zaidi ya dola bilioni mbili katika kusaidia wenye mahitaji ulimwenguni kote. Msaada huu hutolewa kwa wapokeaji bila kujali uhusiano wao na Kanisa, utaifa, rangi, mwelekeo wa kijinsia, jinsia, au ushawishi wa kisiasa.
Lakini hiyo si yote. Ili kuwasaidia washiriki wa Kanisa la Bwana ambao wana shida, tunapenda na kuishi sheria ya zamani ya mfungo.4 Tunashinda njaa ili kuwasaidia wengine wenye njaa. Siku moja kila mwezi, tunashinda bila kula na tunatoa gharama ya chakula hicho (na zaidi) ili kusaidia wale walio na uhitaji.
Sitasahau kamwe safari yangu ya kwanza huko Afrika Magharibi mnamo mwaka 1986. Watakatifu walikuja kwenye mikutano yetu kwa idadi kubwa. Ingawa walikuwa na kidogo kwenye upande wa umiliki wa vitu, wengi walikuja wamevaa mavazi meupe yasiyo na mawaa.
Nilimuuliza rais wa Kigingi ni kwa jinsi gani yeye aliwatunza waumini ambao walikuwa maskini. Akajibu kuwa maaskofu wao waliwajua watu wao vizuri. Ikiwa washiriki wangeweza kumudu milo miwili kwa siku, hakuna msaada uliohitajika. Lakini ikiwa wangeweza kumudu mlo mmoja tu au chini ya hapo—hata kwa msaada wa familia—maaskofu walitoa chakula, kilicholipiwa kutokana na matoleo ya mfungo. Kisha akaongeza ukweli huu wa kushangaza: michango yao ya matoleo ya mfungo mara nyingi huzidi gharama zao. Matoleo ya ziada ya mfungo yalipelekwa kwa watu sehemu zingine ambao mahitaji yao yalizidi matoleo yao. Watakatifu wale waaminifu wa Kiafrika walinifundisha somo kubwa juu la nguvu ya sheria na roho ya mfungo.
Kama waumini wa Kanisa, tunajisikia kuwa ndugu pamoja na wale wanaoteseka kwa njia yoyote ile.5 Kama wana na mabinti wa Mungu, sisi sote ni kaka na dada. Tunatii maagizo kutoka Agano la Kale: “Utafungua mkono wako kwa kaka yako, kwa maskini wako, na kwa mhitaji wako.”6
Pia tunajitahidi kuishi mafundisho ya Bwana Yesu Kristo kama yalivyoandikwa katika Mathayo 25:
“Kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula: nalikuwa na kiu, mkaninywesha: nalikuwa mgeni, mkanikaribisha:
“Nalikuwa uchi, mkanivika: Nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama. …
“… Kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.”7
Acha nitoe mifano michache tu juu ya jinsi Kanisa linavyofuata mafundisho haya ya Mwokozi.
Ili kusaidia kupunguza njaa, Kanisa linaendesha maghala 124 ya akiba ya askofu ulimwenguni kote. Kupitia hayo, takriban misaada 400,000 ya chakula hutolewa kila mwaka kwa watu wenye uhitaji. Katika maeneo ambayo hakuna ghala la akiba, maaskofu na marais wa tawi huchukua kutoka kwenye mfuko wa matoleo ya mfungo ya Kanisa ili kutoa chakula na mahitaji kwa waumini wao wenye uhitaji.
Hata hivyo, changamoto ya njaa huenda mbali zaidi ya mipaka ya Kanisa. Inaongezeka ulimwenguni kote. Ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa ilionesha kuwa idadi ya watu wasio na lishe bora ulimwenguni sasa inazidi milioni 820—au karibu mtu mmoja kati ya tisa ya wakaazi duniani.8
Ni takwimu za kutisha kiasi gani! Tunashukuru sana kwa michango yenu. Asanteni kwa ukarimu wenu wa moyo, mamilioni kote ulimwenguni watapata chakula kinachohitajika, mavazi, malazi ya muda, viti vya magurudumu, dawa, maji safi, na zaidi.
Magonjwa mengi ulimwenguni huja kwa sababu ya maji yasiyo safi. Hadi leo, juhudi za kibinadamu za Kanisa zimesaidia kutoa maji safi katika mamia ya jamii katika nchi 76.
Mradi huko Luputa, katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ni mfano mzuri. Ukiwa na idadi ya watu zaidi ya 100,000, mji haukuwa na maji ya bomba. Raia walilazimika kutembea umbali mrefu kupata vyanzo safi vya maji. Chemichemi ya mlima iligunduliwa umbali wa maili 18 (km 29), lakini wenyeji hawakuweza kupata maji hayo mara kwa mara.
Wakati wamisionari wetu wa huduma za kibinadamu walipopata habari juu ya changamoto hii, walifanya kazi na viongozi wa Luputa kwa kusambaza vifaa na mafunzo ya kutumia mabomba kupeleka maji kwenye jiji. Watu wa Luputa walitumia miaka mitatu kuchimba mfereji wa mita moja kupitia kwenye mwamba na msitu. Kwa kufanya kazi pamoja, siku ya furaha hatimaye ilifika wakati maji yatiririkayo, na safi yalipopatikana kwa wote katika kijiji hicho.
Kanisa pia husaidia wakimbizi, iwe ni kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe, majanga ya asili, au mateso ya kidini. Zaidi ya watu milioni 70 sasa wamefurushwa kutoka kwenye nyumba zao.9
Katika mwaka 2018 pekee, Kanisa lilitoa vifaa vya dharura kwa wakimbizi katika nchi 56. Kwa kuongezea, waumini wengi wa Kanisa hujitolea muda wao kusaidia wakimbizi kujumuika katika jamii mpya. Tunamshukuru kila mmoja wenu ambaye anajitahidi kuwasaidia wale ambao wanajaribu kuanzisha makazi mapya.
Kupitia matoleo ya ukarimu kwenye maduka ya Viwanda vya Deseret nchini Marekani, mamilioni ya nguo hukusanywa na kuchambuliwa kila mwaka. Huku maaskofu wa eneo wakitumia orodha hii kubwa kusaidia waumini wenye uhitaji, sehemu kubwa hutolewa kwenye mashirika mengine ya hisani ambayo husambaza vitu ulimwenguni kote.
Na mwaka jana tu, Kanisa lilitoa huduma ya macho kwa watu zaidi ya 300,000 katika nchi 35, huduma kwa watoto wachanga kwa maelfu ya akina mama na watoto wachanga katika nchi 39, na viti vya magurudumu kwa watu wenye ulemavu zaidi ya 50,000 wanaoishi katika nchi kadhaa.
Kanisa linajulikana vyema kwa kuwa miongoni mwa waitikiaji wa kwanza wakati janga linapotokea. Hata kabla ya kimbunga kutokea, viongozi na wafanyakazi wa Kanisa katika maeneo yaliyoathiriwa wanapanga mipango ya jinsi ya kufikisha vifaa vya misaada na msaada wa kujitolea kwa wale ambao wataathirika.
Mwaka jana pekee, Kanisa lilifanya miradi zaidi ya 100 ya kusaidia katika maafa ulimwenguni kote, likisaidia waathiriwa wa vimbunga, moto, mafuriko, matetemeko ya ardhi, na majanga mengine. Wakati wowote inapowezekana, waumini wetu wa Kanisa wakiwa na vizibao vya njano vya Mikono ya Usaidizi hukusanyika kwa idadi kubwa ili kusaidia wale walioathiriwa na janga. Aina hii ya huduma, inayotolewa na wengi wenu, ndiyo kiini hasa cha kuhudumu.
Akina kaka na dada zangu wapendwa, shughuli ambazo nimeelezea ni sehemu ndogo tu ya kuongezeka kwa ustawi na ufikiaji wa kibinadamu wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.10 Na ninyi ndiyo mnaowezesha haya kufanyika. Kwa sababu ya maisha yenu ya mfano, mioyo yenu ya ukarimu, na mikono yenu ya usaidizi, haishangazi kwamba jamii nyingi na viongozi wa serikali wanasifu juhudi zenu.11
Tangu nimekuwa Rais wa Kanisa, nimeshangazwa na jinsi marais wengi, mawaziri wakuu, na mabalozi walivyonishukuru kwa dhati kwa msaada wetu wa kibinadamu kwa watu wao. Na wameelezea pia shukrani kwa ajili ya nguvu ambayo waumini wetu waaminifu huleta katika nchi yao kama raia waaminifu, na wanaochangia.
Nimeshangazwa pia wakati viongozi wa ulimwengu walipotembelea Urais wa Kwanza wakielezea matumaini yao kwa ajili ya Kanisa kuanzishwa nchini mwao. Kwa nini? Kwa sababu wanajua Watakatifu wa Siku za Mwisho watasaidia kujenga familia na jamii imara,wakifanya maisha kuwa mazuri zaidi kwa wengine popote wanapoishi.
Bila kujali ni wapi tunapaita nyumbani, waumini wa Kanisa wanahisi shauku juu ya ubaba wa Mungu na undugu wa binadamu. Kwa hivyo, shangwe yetu kuu huja wakati tunapowasaidia kaka na dada zetu, bila kujali ni wapi tunaishi katika ulimwengu huu wa kupendeza.
Kutoa msaada kwa wengine—kufanya bidii ya kuwajali wengine kama vile au zaidi ya sisi tunavyojijali—ni shangwe yetu. Hasa, naweza kuongeza, wakati ambapo si muafaka na wakati ambapo kufanya hivyo hututoa katika eneo letu la faraja. Kuishi amri hiyo ya Pili ni kiini cha kuwa mfuasi wa kweli wa Yesu Kristo.
Kaka zangu na dada zangu wapendwa, ninyi ni mifano hai ya matunda ambayo hutokana na kufuata mafundisho ya Yesu Kristo. Ninawashukuru! Ninawapenda!
Ninajua kwamba Mungu anaishi. Yesu ndiye Kristo. Kanisa Lake limerejeshwa katika siku hizi za mwisho ili kutimiza malengo yake ya matakatifu. Ninashuhudia hivyo katika jina la Yesu Kristo, amina.