Msikilize Yeye
Baba Yetu anajua kwamba pale tunapozingirwa na sintofahamu na woga, kitakachotusaidia hasa ni kumsikiliza Mwana Wake.
Kaka zangu na dada zangu wapendwa, nina shukrani kubwa kwamba kupitia matumizi ya teknolojia tumeweza kukutana pamoja na kuabudu katika asubuhi hii ya Jumapili. Tumebarikiwa kiasi gani kujua kwamba injili ya Yesu Kristo imerejeshwa duniani!
Katika wiki kadhaa zilizopita, wengi wetu tumepitia misukosuko katika maisha yetu binafsi. Matetemeko, moto, mafuriko, tauni, na hatima zake zimevuruga utaratibu na kusababisha upungufu wa chakula, bidhaa muhimu, na akiba.
Katikati ya haya yote, tunawapongeza na kuwashukuru kwa kuchagua kusikiliza neno la Bwana katika muda huu wa msukosuko kwa kujiunga nasi kwa ajili ya mkutano mkuu. Giza linaloongezeka ambalo huambatana na taabu hufanya nuru ya Yesu Kristo kuangaza zaidi siku zote. Hebu fikiria mazuri ambayo kila mmoja wetu anaweza kufanya katika kipindi hiki cha mabadiliko ya ghafla ya ulimwenguni. Upendo wako kwa, na imani kwa Mwokozi vinaweza kuwa vichochezi bora zaidi kwa mtu kugundua Urejesho wa Utimilifu wa injili ya Yesu Kristo.
Katika miaka miwili iliyopita, Dada Nelson pamoja nami tumekutana na maelfu yenu ulimwenguni kote. Tulikutana nanyi katika viwanja vya nje na katika mabwalo ya hoteli. Katika kila eneo, nimehisi kwamba nilikuwa katika uwepo wa wateule wa Bwana na kwamba nilikuwa naona kukusanyika kwa Israeli kukitokea mbele ya macho yangu.
Tunaishi katika siku ambazo “babu zetu wamekuwa wakizisubiri kwa shauku kubwa.”1 Tumekaa viti vya mbele kushuhudia mubashara kile nabii Nefi alichokiona katika ono tu, kwamba “nguvu ya mwanakondoo wa Mungu” itawashukia “watu wa agano wa Bwana, ambao walitawanyika kote usoni mwa dunia; na walikuwa wamejikinga kwa utakatifu na kwa nguvu za Mungu katika utukufu mkuu.”2
Ninyi, kaka zangu na dada zangu, ni miongoni mwa wale wanaume, wanawake, na watoto ambao Nefi aliwaona. Fikiria kuhusu hilo!
Haijalishi unaishi wapi au jinsi hali zako zilivyo, Bwana Yesu Kristo ni Mwokozi wako, na nabii wa Mungu, Joseph Smith, ni nabii wako . Alitawazwa kabla ya misingi ya dunia hii kuwa nabii wa kipindi hiki cha mwisho, ambapo “hakuna kitakachozuiliwa”3 kwa watakatifu. Ufunuo unaendelea kutiririka kutoka kwa Bwana katika kipindi hiki cha muendelezo wa mchakato wa Urejesho.
Inamaanisha nini kwako kwamba injili ya Yesu Kristo imerejeshwa duniani?
Inamaanisha kwamba wewe na familia yako mnaweza kuunganishwa pamoja milele! Inamaanisha kwamba kwa sababu umebatizwa na aliye na mamlaka kutoka kwa Yesu Kristo na kuthibitishwa kuwa muumini wa Kanisa Lake, unaweza kufurahia wenza wa kudumu wa Roho Mtakatifu. Atakuongoza na kukulinda. Inamaanisha kamwe hutaachwa bila faraja au bila msaada wa nguvu za Mungu kukusaidia. Inamaanisha kwamba nguvu za ukuhani zinaweza kukubariki kadiri unavyopokea ibada za muhimu na kufanya maagano na Mungu na kuyatunza. Kweli hizi ni nanga kiasi gani kwa nafsi zetu, hasa nyakati hizi wakati dhoruba inaongezeka.
Kitabu cha Mormoni kinaelezea kuinuka na kuanguka kwa tamaduni mbili kuu. Historia yao inaonesha jinsi ilivyo rahisi kwa watu wengi kumsahau Mungu, kukataa maonyo ya manabii wa Bwana, na kutafuta mamlaka, umaarufu, na anasa za mwili.4 Mara kwa mara, manabii wa kale wametangaza “vitu vikubwa na vya ajabu kwa watu, ambao hawakuamini.”5
Hakuna tofauti katika siku yetu. Kwa miaka mingi, vitu vikubwa na vya ajabu vimesikika kutoka katika mimbari zilizotukuka duniani kote. Lakini bado watu wengi hawakumbatii kweli hizi—huenda kwa sababu hawajui wapi pa kuzipata6 au kwa sababu wanawasikiliza wale wasio na ukweli wote au kwa sababu wamekataa ukweli kwa kupendelea mambo ya ulimwengu.
Adui ni mjanja. Kwa milenia, amekuwa akifanya jema lionekane baya na baya lionekane jema.7 Ujumbe wake huwa wa kelele, kishujaa, na wa kujisifu.
Hata hivyo, ujumbe kutoka kwa Baba yetu wa Mbinguni ni wa tofauti sana. Anawasiliana kwa njia nyepesi, kwa utulivu, na uwazi mzuri sana kwamba hatuwezi kukosa Kumuelewa.8
Kwa mfano, wakati wowote Alipomtambulisha Mwana Wake wa Pekee kwa wanadamu duniani, amefanya hivyo kwa maneno machache yasiyo na kifani. Katika Mlima wa Kugeuzwa sura kwa Petro, Yakobo, na Yohana, Mungu alisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa: Msikilizeni.”9 Maneno yake kwa Wanefi katika Nchi ya Neema ya kale yalikuwa “Tazama Mwana wangu Mpendwa ninayependezwa naye, ambaye ndani yake nimetukuza jina langu—msikilizeni yeye.”10 Na kwa Joseph Smith, katika lile tangazo kuu lililofungua kipindi hiki, Mungu alisema kwa urahisi, “Huyu ni Mwanangu Mpendwa. Msikilize Yeye!”11
Sasa, Kaka zangu na dada zangu wapendwa, fikiria ukweli kwamba katika matukio haya matatu yaliyotajwa, kabla Baba hajamtambulisha Mwana, watu waliohusika walikuwa katika hali ya woga na, kwa kiasi fulani, kukata tamaa.
Mitume waliogopa walipomuona Yesu Kristo amezungukwa na wingu katika Mlima wa Kugeuzwa Sura.
Wanefi waliogopa kwa sababu walikuwa wamepitia maangamizo na giza kwa siku kadhaa.
Joseph Smith alikuwa kwenye mshiko wa nguvu ya giza kabla ya mbingu kufunguka.
Baba Yetu anajua kwamba pale tunapokuwa tumezingirwa na sintofahamu na woga, kitakachotusaidia hasa ni kumsikiliza Mwana Wake.
Kwa sababu tunapotafuta kumsikiliza—kumsikiliza kwa dhati—Mwana Wake, tutaongozwa kujua nini cha kufanya katika hali yoyote.
Neno la Kwanza kabisa katika Mafundisho na Maagano ni sikilizeni.12 Likimaanisha “kusikiliza kwa nia ya kutii.”13 Kusikiliza inamaanisha “Kumsikiliza Yeye”— kusikiliza kile Mwokozi anachosema na kisha kufuata ushauri Wake. Katika maneno hayo mawili—“Msikilize Yeye”—Mungu anatupatia mpangilio wa mafanikio, furaha, na shangwe katika maisha haya. Inatubidi kusikiliza maneno ya Bwana, kuyasikiliza hayo, na kufuata kile Alichotuambia!
Tunapotafuta kuwa wafuasi wa Yesu Kristo, jitihada zetu za kumsikiliza Yeye zinatakiwa ziwe za dhati zaidi. Inahitaji juhudi za kujitambua na thabiti kujaza maisha yetu ya kila siku kwa maneno Yake, mafundisho Yake, kweli Zake.
Hatuwezi tu kutegemea taarifa tunayokutana nayo katika mitandao ya kijamii. Kwa maneno bilioni mtandaoni na katika ulimwengu uliojazwa na elimu ya masoko siku zote ukijaa kelele, juhudi mbaya za mwovu, wapi tunaweza kwenda ili kumsikiliza Yeye?
Tunaweza kwenda kwenye maandiko. Yanatufundisha kuhusu Yesu Kristo na injili Yake, uzito wa Upatanisho Wake, na mpango mkuu wa Baba yetu wa furaha na ukombozi. Kuzama kila siku kwenye neno la Mungu ni muhimu kwa uhai wa kiroho, hasa katika siku hizi za ongezeko la mabadiliko ya ghafla. Tunaposherehekea katika maneno ya Kristo kila siku, maneno ya Kristo yatatuambia jinsi ya kukabiliana na ugumu ambao hatukutegemea kuupata.
Tunaweza pia kumsikiliza Yeye katika hekalu. Nyumba ya Bwana ni nyumba ya kujifunza. Huko, Bwana hufundisha katika njia zake Mwenyewe. Huko kila ibada inafundisha kuhusu Mwokozi. Huko, tunajifunza jinsi ya kutenganisha pazia na kuwasiliana kwa uzuri zaidi na mbingu. Huko, tunajifunza jinsi ya kumkemea adui na kuita nguvu za ukuhani wa Bwana kutuimarisha sisi na wale tunaowapenda. Ni hamu kubwa kila mmoja wetu anapaswa kuwa nayo ya kutafuta kimbilio huko.
Wakati vikwazo hivi vya muda vya COVID-19 vitakapoondolewa, tafadhali panga muda maalum wa kuabudu na kuhudumu hekaluni. Kila dakika ya muda huo itakubariki wewe na familia yako katika njia ambayo kingine chochote hakitaweza. Chukua muda kutafakari kile unachosikia na kuhisi utakapokuwa huko. Muombe Mungu akufundishe jinsi ya kufungua mbingu zibariki maisha yako na maisha ya wale wote unaowapenda na kuwatumikia.
Wakati kuabudu hekaluni kwa sasa hakuwezekani, ninawaalika kuongeza ushiriki wenu katika historia ya familia, ikijumuisha kutafiti historia ya familia na kufanya faharisi. Ninaahidi kwamba kadiri unavyoongeza muda wako katika hekalu na kazi ya historia ya familia, utaongeza na kuboresha uwezo wako wa kumsikiliza Yeye.
Pia Tunamsikiliza Yeye kwa uzuri zaidi tunaporekebisha uwezo wetu wa kutambua minong’ono ya Roho Mtakatifu. Haijawahi kuwa muhimu sana kujua jinsi Roho anavyoongea nawe kama ilivyo sasa. Katika Uungu, Roho Mtakatifu ni mjumbe. Atakuletea mawazo katika akili zako ambayo Baba na Mwana wanakutaka uyapokee. Yeye ni Mfariji. Ataleta hisia ya amani katika moyo wako. Anashuhudia ukweli na atathibitisha kilicho kweli, kadiri unavyosikiliza na kusoma neno la Bwana.
Ninarudia upya ombi langu la ninyi kufanya chochote kinachowezekana kuongeza uwezo wenu wa kiroho ili kupokea ufunuo binafsi.
Kufanya hivyo kutakusaidia kujua jinsi ya kusonga mbele katika maisha yako, nini cha kufanya wakati wa hali ya wasiwasi, na jinsi ya kutambua na kuepuka vishawishi na uongo wa adui.
Na, hatimaye, tunamsikiliza Yeye wakati tunapofuata maneno ya manabii, waonaji, na wafunuzi. Mitume waliotawazwa wa Yesu Kristo siku zote humshudia Yeye. Wanaelekeza njia wakati tunapoanza kutembea katika safari ya kuchosha moyo ya uzoefu wa hapa duniani.
Nini kitatokea kama ukijitoa kwa makusudi kusikiliza, na kufuata kile Mwokozi alichosema, na kile Anachokisema sasa kupitia manabii wake? Ninakuahidi kwamba utabarikiwa kwa nguvu ya ziada ya kupambana na majaribu, ugumu, na udhaifu. Ninaahidi miujiza katika ndoa yako, mahusiano yako ya familia, na kazi zako za kila siku. Na ninaahidi kwamba uwezo wako wa kuhisi shangwe utaongezeka hata kama misukosuko itaongezeka katika maisha yako.
Mkutano huu mkuu wa Aprili 2020 ni muda wetu wa kukumbuka tukio lililobadilisha ulimwengu. Tulipokuwa tukitazamia kumbukizi hii ya miaka 200 ya Ono la Kwanza la Joseph Smith, Urais wa Kwanza na Baraza la Mitume Kumi na Wawili walitafakari kile sisi tunachoweza kufanya ili kukumbuka kikamilifu tukio hili moja.
Kuonekana huko kwa Mungu kulianzisha Urejesho wa utimilifu wa injili ya Yesu Kristo na kukaribisha kipindi cha utimilifu wa nyakati.
Tulijiuliza ikiwa mnara ungepaswa kuinuliwa. Lakini tulipofikiria matokeo ya kipekee ya kihistoria na ya kimataifa ya Ono hilo la Kwanza, tulipata msukumo wa kutengeneza mnara usio wa itale au jiwe bali wa maneno—maneno ya tangazo la dhati na takatifu—yaliyoandikwa, si kuwekwa nakshi katika “vibao vya mawe” bali kuchorwa katika “vibao laini” vya mioyo yetu.14
Tangu Kanisa lilipoanzishwa, ni matangazo matano tu yamekwishatolewa, la mwisho likiwa “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu,” lililotambulishwa na Rais Gordon B. Hinckley mnamo 1995.
Sasa tunapotafakari kipindi hiki muhimu katika historia ya ulimwengu na agizo la Bwana la kukusanya Israeli iliyotawanyika katika maandalizi ya Ujio wa Pili wa Yesu Kristo, sisi, Urais wa Kwanza na Baraza la Mitume Kumi na Wawili, tunatoa tangazo lifuatalo. Kichwa chake cha habari ni “Urejesho wa Utimilifu wa Injili ya Yesu Kristo: Tangazo la Miaka Mia Mbili kwa Ulimwengu.” Limepewa mamlaka na Urais wa Kwanza na Baraza la Mitume Kumi na Wawili wa Kanisa La Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. limetolewa Aprili 2020. Kujiandaa kwa ajili ya leo, nilirekodi tangazo hili kabla katika Msitu Mtakatifu, ambapo Joseph Smith mwanzo alimwona Baba na Mwana.
“Kwa dhati tunatangaza kwamba Mungu anawapenda watoto wake katika kila taifa la ulimwengu. Mungu Baba ametupatia uzao mtakatifu, maisha yasiyolinganishwa, na dhabihu ya upatanisho usio na mwisho wa Mwana Wake Mpendwa, Yesu Kristo. Kwa nguvu ya Baba, Yesu alifufuka tena na kupata ushindi juu ya kifo. Yeye ni Mwokozi wetu, Mfano wetu, na Mkombozi wetu.
“Miaka mia mbili iliyopita, katika asubuhi nzuri ya majira ya kuchipua mnamo 1820, kijana Joseph Smith, akitafuta kujua kanisa lipi ajiunge nalo, alikwenda msituni kuomba karibu na nyumba yake huko upstate New York, Marekani. Alikuwa na maswali kuhusu wokovu wa nafsi yake na kuamini kwamba Mungu angemwongoza.
“Kwa unyenyekevu, tunatangaza kwamba katika kujibu sala yake, Mungu Baba na Mwana Wake, Yesu Kristo, walimtokea Joseph na kuzindua ‘kufanywa upya vitu vyote’ (Matendo ya Mitume 3:21) kama ilivyotabiriwa katika Biblia. Katika ono hili, alijifunza kwamba kufuatia kifo cha Mitume wa mwanzo, Kanisa la Kristo la Agano Jipya lilipotea duniani. Joseph angekuwa chombo katika kurejeshwa kwake.
“Tunathibitisha kwamba chini ya maelekezo ya Baba na Mwana, wajumbe wa mbinguni walikuja kumwelekeza Joseph na kuanzisha tena Kanisa la Yesu Kristo. Yohana Mbatizaji aliyefufuka alirejesha mamlaka ya ubatizo kwa kuzamisha majini kwa ajili ya ondoleo la dhambi. Watatu kati ya Mitume wa mwanzo—Petro, Yakobo, na Yohana—walirejesha utume na funguo za mamlaka ya ukuhani. Wengine pia walikuja, ikiwa ni pamoja na Eliya, aliyerejesha mamlaka ya kuunganisha familia pamoja milele katika mahusiano yasiyo na mwisho ambayo yanavuka mipaka ya kifo.
“Tunashuhudia zaidi kwamba Joseph Smith alipewa kipawa na nguvu ya Mungu ili kutafsiri kumbukumbu ya kale: Kitabu cha Mormoni—Ushuhuda mwingine wa Yesu Kristo. Kurasa za maandishi haya matakatifu zinajumuisha maelezo ya huduma binafsi ya Yesu Kristo kati ya watu wa Amerika ya Kaskazini na Kusini punde baada ya Ufufuko Wake. kinafundisha juu ya lengo la maisha na kuelezea mafundisho ya Kristo, ambayo ni kiini cha lengo hilo. Kama maandiko mwenza ya Biblia, Kitabu cha Mormoni kinashuhudia kwamba wanadamu wote ni wana na mabinti za Baba wa Mbinguni mwenye upendo, kwamba Yeye ana mpango mtakatifu kwa ajili ya maisha yetu, na kwamba Mwana Wake, Yesu Kristo, anazungumza leo kama vile ilivyokuwa katika siku za kale.
“Tunatangaza kwamba Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, lililoanzishwa mnamo Aprili 6, 1830, ni Kanisa la Kristo lililorejeshwa la Agano Jipya. Kanisa hili lina nanga katika maisha makamilifu ya jiwe lake kuu la pembeni, Yesu Kristo, na katika Upatanisho Wake usio na mwisho na Ufufuko wake halisi. Yesu Kristo kwa mara nyingine tena amewaita Mitume na amewapa mamlaka ya ukuhani. Anatualika sote kuja Kwake na kwenye Kanisa Lake, ili kupokea Roho Mtakatifu, ibada za wokovu, na kupata shangwe ya kudumu.
“Miaka mia mbili sasa imepita tangu Urejesho huu ulipoanzishwa na Mungu Baba na Mwana Wake Mpendwa, Yesu Kristo. Mamilioni kote ulimwenguni wamekumbatia ufahamu wa matukio haya yaliyotabiriwa.
“Kwa furaha tunatangaza kwamba Urejesho ulioahidiwa unasonga mbele kupitia ufunuo unaoendelea. Dunia kamwe haitabaki kama ilivyo, kwani Mungu ‘atavijumlisha vitu vyote katika Kristo’ (Waefeso 1:10).
“Kwa unyenyekevu na shukrani, sisi kama Mitume Wake tunawaalika wote mjue—kama tunavyojua—kwamba mbingu ziko wazi. Tunathibitisha kwamba Mungu anafanya yajulikane mapenzi Yake kwa wana wake na mabinti Zake wapendwa. “Tunashuhudia kwamba wale wote ambao kwa sala wanajifunza ujumbe wa Urejesho na kutenda kwa imani watabarikiwa kupata ushahidi wao wenyewe wa utakatifu wake na wa lengo lake la kuuandaa ulimwengu kwa Ujio wa Pili ulioahidiwa wa Bwana wetu na Mwokozi, Yesu Kristo.”15
Akina kaka na akina dada wapendwa, hilo ndilo tangazo letu la miaka mia mbili kwa ulimwengu kuhusiana na Urejesho wa injili ya Yesu Kristo katika utimilifu wake. Limetafsiriwa katika lugha 12. Lugha zingine zitafuatia baadaye. Litapatikana mara moja kwenye tovuti ya Kanisa, ambapo unaweza kupata nakala. Lisome kwa faragha na pamoja na wanafamilia yako na marafiki. Tafakari kweli na fikiria athari ambazo kweli hizo zitakuwa nazo katika maisha yako ikiwa utazisikiliza, na kufuata amri na maagano ambayo yanaambatana nazo.
Ninajua kwamba Joseph Smith ni nabii aliyetawazwa tangu mwanzo ambaye Bwana alimchagua kufungua kipindi hiki cha mwisho cha maongozi ya Mungu. Kupitia kwake, Kanisa la Bwana lilirejeshwa duniani. Joseph alitia muhuri ushuhuda wake kwa damu yake. Jinsi gani ninampenda na Kumheshimu!
Mungu yu hai! Yesu ndiye Kristo! Kanisa lake limerejeshwa! Yeye na Baba Yake, Baba yetu wa Mbinguni, wanatulinda. Nashuhudia hivyo, katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.