Maongezi Muhimu
Hatuwezi kusubiri kwa kuongoka kutokea kiepesi tu kwa watoto wetu. Kuongoka kwa bahati mbaya sio kanuni ya injili ya Yesu Kristo.
Umewahi kujiuliza kwa nini tunaliita darasa la Msingi “Msingi”? Wakati jina linamaanisha mafunzo ya kiroho ambayo watoto wanayapata katika miaka yao ya awali, kwangu mimi pia ni kumbukumbu ya ukweli wenye nguvu. Kwa Baba yetu wa Mbinguni, watoto hawajawahi kuwa upili—wamekuwa daima ni “msingi.”1
Anatuamini sisi katika kuwathamini, kuwaheshimu, na kuwalinda kama watoto wa Mungu. Hii inamaanisha kamwe tusiwadhuru kimwili, kwa maneno, au kihisia kwa namna yoyote ile, hata wakati migogoro na mashinikizo vinapoongezeka. Badala yake tuthamini watoto, na kufanya yote tunayoweza kupambana na maovu ya udhalilishaji. Matunzo yao ni ya msingi kwetu—kama ilivyo kwa Mungu.2
Mama mmoja kijana na baba walikaa kwenye meza yao ya jikoni wakitafakari siku yao. Ndipo kutoka chumbani, walisikia mshindo. Mama akauliza, “Hicho kilikuwa nini?”
Kisha walisika sauti nyororo ya kilio ikitoka kwenye chumba cha mtoto wao wa kiume mwenye umri wa miaka minne. Walikimbia kuelekea chumbani. Alikuwa pale, amelala sakafuni karibu na kitanda chake. Mama alimnyanyua na kumuuliza nini kilikuwa kimetokea.
Alisema, “nilianguka kutoka kitandani.”
Mama akamuuliza,“Kwa nini ulianguka kutoka kitandani?”
Alipandisha mabega juu na kushusha na kusema, “Sijui. Nadhani sikuwa nimesonga mbali vya kutosha.”
Ni kuhusu hili la “kusonga mbali vya kutosha” ambako ningependa kuzungumzia asubuhi ya leo. Ni fursa na wajibu kwetu kuwasaidia watoto “kusonga mbali vya kutosha” kwenye injili ya Yesu Kristo. Na ni muhimu kuanza mapema mno.
Kuna wakati maalum katika maisha ya watoto wanapokuwa wamekingwa dhidi ya ushawishi wa Shetani. Ni wakati wanapokuwa hawana hatia na huru kutokana na dhambi.3 Ni wakati mtakatifu wa mzazi na watoto. Watoto lazima wafundishwe, kwa neno na mfano, kabla na baada ya “kufikia miaka ya kuwajibika kwa Mungu.”4
Rais Henry B. Eyring alifundisha: “Tunayo fursa kubwa zaidi kwa wadogo hawa. Wakati bora wa kufundisha ni wawapo wadogo, wakati bado wana kinga ya majaribu ya adui wa hapa duniani, na mapema kabla maneno ya kweli hayajawa magumu kwao kusikia katika kelele ya mapambano yao ya kibinafsi.”5 Mafundisho kama hayo yatawasaidia kutambua asili yao ya kiungu, lengo lao, na baraka tele zinazowasubiria pale wanapofanya maagano matakatifu na kupokea ibada takatifu katika njia ya agano.
Hatuwezi kusubiri kwa kuongoka kutokea kiepesi tu kwa watoto wetu. Kuongoka kwa bahati mbaya sio kanuni ya injili ya Yesu Kristo. Kuwa kama Mwokozi wetu hakutatokea tu bila mpangilio. Kuwa mwenye kusudi katika kupenda, kufundisha, na kushuhudia kunaweza kuwasaidia watoto kuanza katika umri mdogo kuhisi ushawishi wa Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu ni wa muhimu kwa shuhuda za watoto wetu na kuongoka katika Yesu Kristo; tunatamani kwamba wao “daima wamkumbuka yeye, ili Roho wake apate kuwa pamoja nao.”6
Fikiria thamani ya mazungumzo ya familia juu ya injili ya Yesu Kristo, mazungumzo muhimu ambayo yanaweza kumwalika Roho. Tunapokuwa na mazungumzo kama hayo pamoja na watoto wetu, tunawasaidia kujenga msingi, “ambao ni msingi imara, msingi ambako watu wote wakijenga hawataanguka.”7 Tunapomuimarisha mtoto, tunaimarisha familia.
Majadiliano haya muhimu yanaweza kuwaongoza watoto kwenye:
-
Kuelewa mafundisho ya toba.
-
Kuwa na imani katika Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.
-
Kuchagua ubatizo na kipawa cha Roho Mtakatifu wafikapo umri wa miaka nane.8
-
Na kusali na “kutembea katika haki mbele za Bwana”.9
Mwokozi aliasa, “Kwa hiyo ninakupeni amri, kuyafundisha mambo haya kwa uhuru kwa watoto wenu.”10 Na ni kitu gani Alitutaka sisi tufundishe kwa uhuru sana?
-
Anguko la Adamu
-
Upatanisho wa Yesu Kristo
-
Umuhimu wa kuzaliwa mara ya pili11
Mzee D. Todd Christofferson alisema, “Kwa hakika adui anapendezwa wakati wazazi wanapopuuza kuwafundisha na kuwafunza watoto wao kuwa na imani katika Kristo na kuzaliwa tena kiroho.”12
Kinyume chake, Mwokozi anatutaka sisi kuwasaidia watoto “kuweka matumaini [yao] katika Roho yule anayeongoza kutenda mema.”13 Ili kufanya hivyo, tunaweza kuwasaidia watoto kutambua wakati wanapohisi Roho na katika kutambua ni matendo yapi husababisha Roho kuondoka. Hivyo hujifunza kutubu na kurejea katika nuru kwa kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo. Hii husaidia kuhamasisha uthabiti wa kiroho.
Tunaweza kufurahia kuwasaidia watoto wetu kujenga uthabiti wa kiroho katika umri wowote. Haitakiwi kuwa jambo gumu au la kutumia muda mwingi. Mazungumzo ya kawaida, na yenye kujali yanaweza kuwaongoza watoto kujua sio tu kile wanachokiamini, ila cha msingi, kwa nini wanakiamaini. Mazungumzo yenye kujali, yafanyikayo kwa hali ya kawaida na mara kwa mara, huweza kupelekea katika uelewa mzuri na majibu. Tusiruhusu uwepo wa vifaa vya kielektroniki kutuondoa katika kufundisha na kuwasikiliza watoto wetu na kuwaangalia machoni mwao.
Fursa za ziada kwa ajili ya mazungumzo muhimu zinaweza kutokea kupitia kuigiza tukio. Wanafamilia wanaweza kuigiza hali za kujaribiwa au kusukumwa kufanya uchaguzi mbaya. Igizo kama hilo linaweza kuwaimarisha watoto kujiandaa katika hali za changamoto. Kwa mfano, tunaweza kuigiza na pia kuzungumzia igizo hilo wakati tunawauliza watoto ni nini wangefanya:
-
Ikiwa wamejaribiwa kuvunja Neno la Hekima.
-
Kama wamekumbana na picha za ponografia.
-
Kama wanajaribiwa kudanganya, kuiba, au kutokuwa waaminifu.
-
Ikiwa watasikia jambo kutoka kwa rafiki au mwalimu shuleni ambalo linapingana na imani yao au maadili.
Kadiri wanavyoigiza na kulizungumzia igizo, kuliko kukutwa bila kujiandaa katika mazingira ya kundi rika ovu, watoto wanaweza kulindwa na “ngao ya imani ambayo kwa hiyo [wao] wataweza kuizima mishale yote yenye moto ya adui.”14
Rafiki binafsi wa karibu alijifunza somo hili muhimu akiwa na umri wa miaka 18. Alijiandikisha katika jeshi la Marekani wakati wa mgogoro kati ya Marekani na Vietinam. Alipangwa katika mafunzo ya msingi ya jeshi la watembea kwa miguu. Alielezea kwamba mafunzo yalikuwa magumu. Alimwelezea mkufunzi wake wa mazoezi kama mtu mkatili na asiye na ubinadamu.
Siku moja mahsusi kundi lake lilikuwa limevalia mavazi kamili ya kivita, wakipanda mlima katika joto kali. Mkufunzi wa mazoezi ghafla alitoa amri za kuanguka chini na kutosogea. Mkufunzi alikuwa anaangalia hata hatua ndogo tu. Mtikisiko wa aina yoyote ule ungepelekea kwenye matokeo mabaya baadae. Kundi lilitaabika kwa zaidi ya saa mbili katika joto na hasira na chuki iliongezeka dhidi ya kiongozi wao.
Miezi mingi baadaye, rafiki yetu alijikuta akiongoza kikosi chake kupitia misitu ya Vietinam. Hii ilikuwa ni kweli, na sio mafunzo tu. Milio ya risasi ilianza kusikika kutokea juu katika miti iliyowazunguka. Mara moja kikosi chote kilianguka ardhini.
Adui alikuwa anatafuta nini? Mienendo yao. Hatua yoyote ile ingeleteleza moto. Rafiki yangu alinambia kwamba alivyokuwa amelala akitokwa jasho na bila kusogea katika sakafu ya msitu, akisubiria giza kwa masaa mengi, mawazo yake yalirejelea nyuma katika mafunzo ya msingi. Alikumbuka alivyokuwa hampendi mkufunzi wake. Sasa, alihisi shukrani kubwa—kwa kile alichokuwa amemfundisha na jinsi alivyokuwa amemwandaa kwa ajili ya nyakati hizi ngumu. Mkufunzi wa mazoezi kwa hekima alikuwa amemhami rafiki yetu na kikosi chake na uwezo wa kujua nini cha kufanya wakati mapigano yakiendelea. Alikuwa, kimsingi, ameokoa maisha ya rafiki yetu.
Je, ni kwa namna gani sisi tunaweza kufanya vivyo hivyo kiroho kwa watoto wetu? Mapema kabla ya kuingia katika uwanja wa vita ya maisha, kwa jinsi gani tunaweza kujitahidi zaidi kuwafunza, kuwaimarisha na kuwaandaa?15 Ni kwa jinsi gani tunaweza kuwaalika “kusonga mbali vya kutosha”? Si tungeweza kuwafanya “watoe jasho” katika mazingira salama ya kujifunza ya nyumbani kuliko kuvuja damu katika uwanja wa vita wa maisha?
Ninapotazama nyuma, kuna nyakati wakati mume wangu na mimi tulijihisi kama wakufunzi wa mazoezi katika bidii yetu ya kuwasaidia watoto wetu kuiishi injili ya Yesu Kristo. Nabii Yakobo alionekana kutamka hisia kama hizi aliposema: “ninajali ustawi wa nafsi zenu. Ndio, wasiwasi wangu ni mkubwa kwenu; na nyinyi mnajua imekuwa hivyo tangu mwanzo.”16
Kadiri watoto wanavyojifunza na kukua, imani yao itajaribiwa. Lakini kama watalindwa vizuri, wanaweza kukua kiimani, kiujasiri, na kujiamini, hata katikati ya upinzani mkubwa.
Alma alitufundisha sisi “kutayarisha akili [za] watoto.”17 Tunakiandaa kizazi kinachoinukia kuwa walinzi wa baadaye wa imani, kuelewa “kwamba mko huru kujitendea—kuchagua njia ya kifo kisicho na mwisho au njia ya uzima wa milele.”18 Watoto wanastahili kuelewa ukweli huu mkuu: ni jambo baya kutojua kuhusu umilele.
Basi mazungumzo yetu ya kawaida lakini ya muhimu na watoto wetu yawasaidie “kufurahia maneno ya uzima wa milele” sasa, ili waweze kufurahia “uzima wa milele katika ulimwengu ujao, hata utukufu usio na mwisho.”19
Kadiri tunavyowatunza na kuwaandaa watoto wetu, tunaruhusu uhuru wao wa kuchagua, tunawapenda kwa moyo wetu wote, tunawafundisha amri za Mungu na Zawadi Yake ya toba, na kamwe, hata siku moja, hatutawaacha. Hata hivyo, hii si ndio njia ya Bwana kwa kila mmoja wetu?
Acha “tusonge mbele tukiwa imara katika Kristo,” tukijua kwamba tunaweza kuwa na “mng’aro halisi wa tumaini”20 kupitia kwa Mwokozi wetu mpendwa.
Ninashuhudia kwamba daima Yeye ni jibu. Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.