Mafundisho ya Kuwa Sehemu Ya
Mafundisho ya kuwa sehemu ya hutokea kwenye hili kwa kila mmoja wetu: Mimi na Kristo tu wamoja katika agano la injili.
Ningependa kuzungumzia kuhusu kile ninachokiita mafundisho ya kuwa sehemu ya Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Fundisho hili lina sehemu tatu: (1) nafasi ya kuwa sehemu ya kuwakusanya watu wa agano wa Bwana, (2) umuhimu wa huduma na dhabihu ukiwa mmoja wa sehemu ya Kanisa na (3) Umuhimu wa Yesu Kristo ukiwa mmoja wa sehemu ya Kanisa.
Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho katika mwanzo wake wa awali liliundwa kwa sehemu kubwa na Watakatifu weupe wa Kimarekani ya Kaskazini na wa Ulaya ya kaskazini na kiasi kidogo cha Wamarekani Wenyeji, Wamarekani wa asili ya Afrika na Watu wa Visiwa vya Pasifiki. Sasa, miaka minane baadaye kutoka kumbukizi ya miaka 200 ya kuanzishwa kwake, Kanisa kwa kiwango kikubwa limeongezeka katika idadi na utofauti katika Amerika ya Kaskazini na vivyo hivyo ulimwenguni kote.
Kama kusanyiko lililongojewa na lililotabiriwa la siku za mwisho la watu wa agano wa Mungu linavyozidi kushika kasi, hakika Kanisa litaundwa na waumini kutoka kila taifa, koo, ndimi na watu.1 Mchanganyiko huu sio wa kimahesabu au wa kulazimishwa bali ni tukio linalotokea kiasili ambalo tungelitarajia, tukitambua kwamba nyavu ya injili inakusanya kutoka kila taifa na kila watu.
Tumebarikiwa kiasi gani kuona siku ile ambayo Sayuni inaanzishwa kwa wakati mmoja kwenye kila bara na katika ujirani wetu. Kama Nabii Joseph Smith alivyosema, watu wa Mungu katika kila zama wametazamia kwa matarajio ya shangwe ya siku hii, na “sisi ni watu waliopendelewa ambao Mungu amefanya uchaguzi wa kuleta utukufu wa Siku za Mwisho.”2
Tukiwa tumepewa heshima hii, hatuwezi kuruhusu ubaguzi wowote, chuki za kikabila au migawanyiko mingine kuwepo katika Kanisa la siku za mwisho la Yesu Kristo. Bwana ametuamuru, “Muwe na umoja; na kama hamna umoja ninyi siyo wangu.3 Tunapaswa kuwa na bidii katika kung’oa chuki na ubaguzi kutoka Kanisani, kutoka majumbani mwetu na zaidi ya yote katika mioyo yetu. Kadiri idadi ya waumini wetu wa Kanisa inavyokua tofauti zaidi, makaribisho yetu lazima yawe ya hiari na yenye ukarimu zaidi. Tunahitajiana.4
Katika waraka wake wa kwanza kwa Wakorintho, Paulo anatangaza kwamba wote wanaobatizwa katika Kanisa ni wamoja katika mwili wa Kristo:
“Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo.
“Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au tu Wayunani, ikiwa tu watumwa, au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja. …
“Ili kusiwe na faraka katika mwili; bali viungo vitunzane.
“Na kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia nacho, na kiungo kimoja kikitukuzwa, viungo vyote hufurahi pamoja nacho.”5
Hisia za kuwa sehemu ya ni muhimu kwa ustawi wetu wa kimwili, kiakili na kiroho. Bado, yawezekana kabisa kwamba nyakati zingine kila mmoja wetu anaweza akahisi kutokuwa sehemu ya. Katika nyakati za kukata tamaa, yawezekana tukahisi kwamba kamwe hatuwezi kufikia kwenye viwango vya juu vya Bwana au matarajio ya wengine.6 Huenda pasipo kujua tukaweka matarajio kwa wengine—au hata kwetu wenyewe—ambayo siyo matarajio ya Bwana. Yawezekana tukaongea kwa hila kwamba thamani ya nafsi inategemea mafanikio fulani au miito, lakini hivi sivyo kipimo cha thamani yetu machoni pa Bwana. “Bwana anautazamo moyo.”7 Yeye anajali matamanio yetu na hamu zetu na kile tunachokuwa.8
Dada Jodi King aliandika uzoefu wake wake mwenyewe juu ya miaka iliyopita:
“Kamwe sikuwahi kuhisi kama sikuwa sehemu ya Kanisa hadi pale mume wangu, Cameron, pamoja nami tulipoanza kuhangaika na ugumba. Watoto na familia ambazo ndizo walikuwa wameniletea furaha kanisani sasa walianza kunisababishia huzuni na uchungu.
“Nilihisi nisiye na faida pasipo mtoto mikononi mwangu au begi la nepi mkononi. …
“Jumapili ngumu zaidi ilikuwa ile ya kwanza katika kata yetu mpya. Kwa sababu hatukuwa na watoto, tuliulizwa kama tumeoana hivi karibuni na lini tunapanga kuanzisha familia. Nilikuwa nimekuwa hodari sana katika kujibu maswali haya bila kuruhusu yaniathiri—nilijua hayakukusudiwa kuwa ya kuniumiza.
“Hata hivyo, katika Jumapili hii mahsusi, kujibu maswali hayo ilikuwa ngumu mno. Ndio tulikuwa tumegundua, baada ya kuwa wenye matumaini, kwamba nilikuwa—bado tena—sina ujauzito.
“Nilitembea kuingia mkutano wa sakramenti nikihisi kuchoka, na kujibu hayo maswali ya ‘kutaka kukujua’ ilikuwa ngumu kwangu. …
“Lakini ilikuwa Shule ya Jumapili ambayo hakika iliuvunja moyo wangu. Somo—lilikusudiwa kuwa nafasi takatifu ya akina mama—kwa haraka mwelekeo ukabadilika na kuwa kikao cha kutoa vinyongo. Nilivunjika moyo na machozi kimya kimya yakinitiririka huku nikisikia wanawake wakilalamika kwamba ni baraka ambayo angetoa kitu chochote kuipata.
“Haraka nilitoka nje ya kanisa. Mwanzoni, sikutaka kurudi tena. Sikutaka kupitia hisia ile ya kutengwa tena. Lakini usiku ule, baada ya kuongea na mume wangu, tulijua kuwa tungeendelea kuhudhuria kanisani siyo tu kwa sababu Bwana ametutaka kufanya hivyo bali pia kwa sababu tulijua kwamba shangwe ambayo huja kutokana na kufanya upya maagano na kumhisi Roho kanisani inapita huzuni niliyoihisi siku ile. …
“Katika Kanisa, kuna wajane, watalikiwa na waumini waseja; wale wenye wanafamilia walioteleza mbali na injili; watu wenye magonjwa ya kudumu, au mahangaiko ya kifedha; waumini wanaopitia mvuto wa jinsia moja; waumini wanaopambana na uraibu au mashaka, waongofu wapya, wahamiaji wapya; wazazi waishio peke yao; na orodha inaendelea. …
“Mwokozi anatualika tuje Kwake—bila kujali hali zetu. Tunaenda kanisani ili kufanya upya maagano yetu, kuongeza imani yetu, kupata amani na kufanya kama Yeye alivyofanya kwa ukamilifu katika maisha Yake—kuwatumikia wengine wanaohisi kutokuwa sehemu ya.”9
Paulo alielezea kwamba Kanisa na maafisa wake wameitwa na Mungu “kwa ajili ya kuwakamilisha watakatifu, kwa ajili ya kazi ya huduma, kwa ajili ya kuujenga mwili wa Kristo:
“Hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo.”10
Ni kejeli ya kuhuzunisha, pale, wakati mtu anapohisi hafikii viwango katika vipengele vyote vya maisha, kuhitimisha kwamba wao siyo sehemu ya mfumo uliosanifiwa na Mungu ili kutusaidia sisi kukua kufikia viwango hivyo.
Na tuache hukumu mikononi mwa Bwana na wale aliowapa mamlaka na sisi tuwe radhi kupendana na kutendeana mema kadiri tuwezavyo. Na tumwombe Yeye atuonyeshe njia, siku hata siku, ili “tuwalete ndani … maskini, na waliolemazwa, na wenye kuchechemea, na vipofu”11—hiyo ni, kila mmoja wetu—kwenye karamu kuu ya Bwana.
Upande wa pili wa mafundisho ya kuwa sehemu ya unahusiana na michango yetu wenyewe. Ingawa mara chache tunafikiria kuhusu hili, sehemu kubwa ya sisi kuwa sehemu ya, hutokana na huduma yetu na dhabihu tunazofanya kwa ajili ya wengine na kwa ajili ya Bwana. Kufokasi kupita kiasi kwenye mahitaji yetu binafsi au faraja zetu wenyewe kunaweza kuvuruga hisia ya kuwa sehemu ya.
Tunajitahidi kufuata mafundisho ya Mwokozi:
“Yule atakaye kuwa mkuu kwenu, na awe mtumishi wenu. …
“Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa; bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.”12
Kuwa sehemu ya hakuji tu kwa kusubiria bali kwa kujitoa ili kusaidiana.
Leo, kwa bahati mbaya, kujitoa kwa kusudi fulani au kutoa dhabihu ya chochote kwa ajili ya mwingine inakuwa kinyume na utamaduni. Katika sehemu ya Gazeti la Deseret mwaka jana, mwandishi Rod Dreher alirejea maongezi yake na mama kijana huko Budapest:
“Mimi niko kwenye treni ya Budapest pamoja na … rafiki umri wake ni wa miaka ya 30—acha tumwite Kristina—wakati tukiwa njiani kwenda kumhoji mwanamke mzee [Mkristo] ambaye, pamoja na mumewe aliyekuwa amefariki, walistahimili mateso kutoka serikali ya kikomunisti. Tunapokatisha mitaa ya jiji, Kristina anaongelea jinsi ilivyo vigumu kuwa mwaminifu kwa marafiki wa umri wake kuhusu matatizo anayokabiliana nayo kama mke na mama mwenye watoto wadogo.
“Magumu ya Kristina ni ya kawaida kabisa kwa mwanamke kijana anayejifunza kuwa mama na mke—lakini mtazamo ulioko miongoni mwa kizazi chake ni kwamba magumu ya maisha ni tishio kwa ustawi wa mtu na yanapaswa kuondolewa. Je, yeye na mumewe wanabishana nyakati zingine? Basi anapaswa kumwacha, wao wanasema. Je, watoto wake wanamsumbua? Basi anapaswa kuwapeleka kituo cha kulelea watoto.
“Kristina anahofia kwamba marafiki zake hawafahamu kwamba majaribu, na hata mateso, ni sehemu ya kawaida ya maisha—na yawezekana hata kuwa sehemu ya maisha mazuri, kama mateso hayo yanatufundisha jinsi ya kuwa na subira, wakarimu na wenye kupenda. …
“… Mwanasosholojia wa dini wa Chuo Kikuu cha Notre Dame, Christian Smith aligundua katika mafunzo yake ya watu wazima [umri] miaka18 hadi 23 kwamba wengi wao wanaamini kwamba jamii siyo kitu zaidi ya mkusanyiko wa watu wanaojitegemea ili kufurahia maisha.’”13
Kwa falsafa hii, kitu chochote ambacho mtu anakiona kuwa kigumu “ni aina ya ukandamizaji.”14
Kinyume chake, mababu zetu waanzilishi walipata hisia nyingi za kuwa sehemu ya, umoja na matumaini katika Kristo kwa dhabihu walizozitoa ili kutumikia misheni, kujenga mahekalu, kuacha nyumba zao nzuri kwa shinikizo na kuanza upya, na katika njia nyingine nyingi walijitoa wenyewe na mali zao kwa sababu ya Sayuni. Walikuwa radhi kutoa dhabihu hata uhai wao kama ikibidi. Na sisi sote tu wanufaika wa uvumilivu wao. Hilo ni kweli kwa wengi hivi leo ambao huenda wakapoteza uhusiano wa familia na marafiki, kuporwa fursa za ajira, au vinginevyo kubaguliwa au kunyanyaswa kama matokeo ya kubatizwa. Tuzo yao, hata hivyo, ni hisia imara ya kuwa miongoni mwa watu wa agano. Dhabihu yoyote tufanyayo kwa kusudi la Bwana husaidia kutuweka katika nafasi pamoja naye aliyetoa uhai Wake kama fidia kwa ajili ya wengi.
Kitu cha mwisho na cha muhimu zaidi cha mafundisho ya kuwa sehemu ya ni nafasi muhimu ya Yesu Kristo. Hatujiungi na Kanisa kwa ajili ya ushirika peke yake, japo hilo ni muhimu. Tunajiunga kwa ajili ya ukombozi kupitia upendo na rehema ya Yesu Kristo. Tunajiunga ili kupata ibada za wokovu na kuinuliwa kwa ajili yetu wenyewe na wale tuwapendao kwenye pande zote mbili za pazia. Tunajiunga ili kushiriki katika mradi mkubwa wa ujenzi wa Sayuni kwa matayarisho ya kurudi kwa Bwana.
Kanisa ni mlinzi wa maagano ya wokovu na kuinuliwa ambayo Mungu hutupatia sisi kupitia ibada za ukuhani mtakatifu.15 Ni kwa kushika maagano haya kwamba tunapata hisia ya juu na ya kina zaidi ya kuwa sehemu ya. Rais Russell M. Nelson aliandika hivi karibuni:
Mimi na wewe tukiwa tayari tumefanya agano na Mungu, uhusiano wetu na Yeye unakuwa wa karibu sana kuliko kabla ya agano letu. Sasa tumeunganishwa pamoja. Kwa sababu ya agano letu na Mungu, Yeye kamwe hatachoka katika juhudi Zake za kutusaidia, na kamwe hatuwezi kumaliza subira Yake ya rehema kwetu. Kila mmoja wetu ana sehemu maalumu katika moyo wa Mungu. …
“… Yesu Kristo ni mdhamini wa maagano hayo (ona Waebrania 7:22; 8:6).”16
Kama tutalikumbuka hili, matumaini ya juu ya Bwana kwetu sisi yatatuhamasisha na siyo kutuvunja moyo.
Tunaweza kuhisi shangwe tunapofuatilia kibinafsi au kijumuiya “kipimo cha kimo cha utimilifu wa Kristo.”17 Licha ya kukatishwa tamaa na vikwazo njiani, hili ni tamanio kubwa. Tunainuana na kutiana moyo katika kufuata njia iliyoinuka, tukijua kwamba bila kujali dhiki na bila kujali kuchelewa katika baraka zilizoahidiwa, sisi tunaweza “kujipa moyo; [kwani Kristo] ameushinda ulimwengu,”18 na sisi tuko pamoja Naye. Kuwa wamoja pamoja na Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu pasipo shaka ndio kilele cha kuwa sehemu ya.19
Hivyo, mafundisho ya kuwa sehemu ya hutokea hapa—kila mmoja wetu anaweza kuthibitisha: Yesu Kristo alikufa kwa ajili yangu; aliniwazia mimi kuwa mwenye kustahili damu Yake. Ananipenda na anaweza kuleta utofauti katika maisha yangu. Ninapotubu, neema Yake itanibadilisha. Mimi na Yeye tu wamoja katika agano la injili; mimi ni wa Kanisa Lake na ufalme Wake; na niko katika kusudi Lake la kuleta ukombozi kwa watoto wote wa Mungu.
Ninashuhudia kwamba wewe ni sehemu Yake, katika jina la Yesu Kristo, amina.