Mkutano Mkuu
Yesu Kristo Ni Nguvu kwa Wazazi
Mkutano mkuu wa Aprili 2023


15:13

Yesu Kristo Ni Nguvu kwa Wazazi

Wasaidie watoto wako wajenge imani katika Yesu Kristo, wapende injili Yake na Kanisa Lake; wajiandae kwa maisha yote ya chaguzi za haki.

Hapo zamani za kale, baba mmoja alikuwa karibu kuondoka kwenda kwenye mkutano wa jioni wa uaskofu. Binti yake mwenye umri wa miaka minne alisogea mbele yake, akiwa amevalia nguo za kulalia na kushikilia nakala ya Hadithi za Kitabu cha Mormoni.

“Kwa nini inakubidi uende kwenye mkutano?” binti aliuliza.

“Kwa sababu mimi ni mshauri katika uaskofu,” baba akajibu.

“Lakini wewe ni baba yangu!” binti yake alipinga.

Baba alipiga magoti mbele yake. “Kipenzi,” alisema, “Ninajua unataka nikusomee na nikusaidie ulale, lakini usiku wa leo nahitaji kumsaidia askofu.”

Binti yake akajibu, “Je, askofu hana baba wa kumsaidia kwenda kulala?”

Tunashukuru milele kwa waumini wasiohesabika wanaohudumu kwa bidii katika Kanisa la Yesu Kristo kila siku. Hakika dhabihu yenu ni takatifu.

Lakini kama msichana huyu alivyoonekana kuelewa, kuna jambo takatifu pia—jambo lisiloweza kuwa na mbadala—kuhusu mzazi kumlea mtoto. Linaakisi mfano wa mpangilio mbinguni.1 Baba yetu wa Mbinguni, Mzazi wetu wa Kiungu, hakika hufurahi wakati watoto Wake wanapofundishwa na kulelewa na wazazi wao duniani.2

Wazazi, asanteni kwa kila kitu mnachofanya katika kuwalea watoto wenu. Na watoto, asanteni kwa kila kitu mnachofanya kuwalea wazazi wenu, kwa sababu kama kila mzazi ajuavyo, mara nyingi tunajifunza mengi kutoka kwa watoto wetu kuhusu imani, tumaini, na hisani wakati wanapojifunza kutoka kwetu!3

Wazazi Wana Wajibu Mtakatifu

Je, umewahi kufikiria kuhusu tahadhari kubwa ambayo Baba yetu wa Mbinguni huchukua kila wakati Anampomleta mtoto duniani? Hawa ni wana na mabinti zake wa kiroho. Wana uwezekano usio na kikomo. Wamekusudiwa kuwa viumbe watukufu wa wema, rehema na ukweli. Na bado wanakuja duniani wakiwa hoi kabisa, hawana uwezo wa kufanya lolote zaidi ya kulilia msaada. Kumbukumbu ya wakati wao katika uwepo wa Mungu imefunikwa, pamoja na ufahamu wa wao ni nani hasa na wanaweza kuwa nani. Wanajenga ufahamu wao juu ya maisha, upendo, Mungu na mpango Wake kutokana na kile wanachokiona kutoka kwa watu wanaowazunguka—hasa wazazi wao, ambao, kwa uaminifu, bado wanajaribu kutambua mambo hayo wao wenyewe.

Mtoto mchanga

Mungu amewapa wazazi “wajibu mtakatifu wa kuwalea watoto wao katika upendo na haki, kukidhi mahitaji yao ya kimwili na ya kiroho, na kuwafundisha … kuzingatia amri za Mungu.”4

Hiyo inatosha kuwaweka macho usiku hata wazazi bora zaidi.

Ujumbe wangu kwa wazazi wote ni huu:

Bwana anawapenda.

Yeye yu pamoja nanyi.

Yeye anasimama kando yenu.

Yeye ndiye nguvu yenu katika kuwaongoza watoto wenu wafanye maamuzi ya haki.

Kubalini fursa hii na wajibu huu kwa ujasiri na kwa shangwe. Msikabidhi chanzo hiki cha baraka za mbinguni kwa mtu mwingine yeyote. Ndani ya mfumo wa maadili na kanuni za injili, ninyi ndiyo mnapaswa kuwapa mwongozo watoto wenu katika vipengele vya maisha ya kila siku. Wasaidie watoto wako wajenge imani katika Yesu Kristo, wapende injili Yake na Kanisa Lake; wajiandae kwa maisha yote ya chaguzi za haki. Kwa kweli, huo ndiyo mpango wa Mungu kwa wazazi.

Shetani atakupinga, atakuvuruga, atajaribu kukukatisha tamaa.

Lakini kila mtoto amepokea Nuru ya Kristo kama simu ya moja kwa moja hadi mbinguni. Na Mwokozi atakusaidia, atakuongoza na kukutia moyo. Tafuta msaada Wake. Uliza kwa Bwana!

Bwana Yesu Kristo

Kama vile Yesu Kristo alivyo nguvu kwa vijana, Yesu Kristo pia ni nguvu kwa wazazi.

Yeye Anakuza Upendo

Wakati fulani tunaweza kujiuliza kama mtu mwingine anaweza kuwa na sifa bora zaidi za kuwaongoza na kuwafundisha watoto wetu. Lakini bila kujali jinsi unavyoweza kuhisi kuwa umepungukiwa, una kitu fulani cha pekee ambacho kinakustahilisha: upendo wako kwa mtoto wako.

Upendo wa mzazi kwa mtoto ni mojawapo ya kani zenye nguvu zaidi katika ulimwengu. Ni mojawapo ya mambo machache hapa duniani ambayo hakika yanaweza kuwa ya milele.

Sasa, labda unahisi kwamba uhusiano wako na mtoto wako haufai. Hapo ndipo nguvu za Mwokozi zinapoingia. Yeye huponya wagonjwa, na anaweza kuponya uhusiano. Yeye huzidisha mkate na samaki, na Anaweza kuzidisha upendo na furaha katika nyumba yako.

Upendo wako kwa watoto wako unatayarisha mazingira mazuri ya kufundisha ukweli na kujenga imani. Ifanye nyumba yako kuwa nyumba ya sala, ya kujifunza, na ya imani; nyumba ya kumbukumbu za furaha; mahali pa kuwa sehemu ya; nyumba ya Mungu.5 Na “sali kwa Baba kwa nguvu zote za moyo, ili [wewe] ujazwe na upendo [Wake], ambao [anautoa] kwa … wafuasi wa Mwana Wake, Yesu Kristo.”6

Yeye Anakuza Juhudi Ndogo na Rahisi

Nguvu nyingine uliyonayo, kama mzazi, ni fursa ya ushawishi endelevu wa kila siku. Makundi rika, walimu na washawishi wa vyombo vya habari huja na kuondoka. Lakini wewe unaweza kuwa ushawishi thabiti, na endelevu katika maisha ya mtoto wako.

Juhudi zako zinaweza kuonekana kuwa ndogo ikilinganishwa na sauti kubwa ambazo watoto wako husikia ulimwenguni. Wakati fulani unaweza kuhisi hufanikishi mengi. Lakini kumbuka kwamba “kwa njia ndogo Bwana anaweza kuleta mambo makubwa.”7 Jioni moja ya nyumbani, mjadala mmoja wa injili, au mfano mmoja mzuri unaweza usibadilishe maisha ya mtoto wako kwa muda mfupi, kama tone moja la mvua lisivyoweza kusababisha mmea ukue kwa haraka. Lakini uendelevu wa mambo madogo na rahisi, siku baada ya siku, huwarutubisha watoto wako vizuri zaidi kuliko mafuriko ya hapa na pale.8

Hiyo ndiyo njia ya Bwana. Anazungumza na wewe na mtoto wako kwa sauti ndogo ya utulivu, siyo kwa sauti ya radi.9 Alimponya Naamani si kupitia “jambo fulani kubwa” bali kupitia tendo rahisi la kurudia kujiosha.10 Wana wa Israeli walifurahia karamu ya kware jangwani, lakini kilichowafanya waendelee kuishi ni muujiza mdogo na rahisi wa mana—mkate wao wa kila siku.11

Akina kaka na akina dada, mkate wa kila siku hutayarishwa vyema na kuliwa vyema nyumbani. Imani na ushuhuda vinalelewa vyema kwa njia za kawaida na za asili, kitafunwa kimoja kwa wakati mmoja, katika nyakati ndogondogo na rahisi katika mtiririko wa kila siku wa maisha ya kila siku.12

Kila wakati ni wakati wa kufundisha. Kila neno na tendo vinaweza kuwa mwongozo wa kufanya chaguzi.13

Huenda usione matokeo ya haraka ya juhudi zako. Lakini usikate tamaa. “Mambo yote lazima yatimie kwa wakati wake,” Bwana alisema. “Kwa hiyo, msichoke katika kutenda mema, kwa maana [ninyi] mnaweka msingi wa kazi kubwa.”14 Ni kazi gani inayoweza kuwa kubwa kuliko kuwasaidia watoto wa thamani wa Mungu wajifunze wao ni nani hasa na wajenge imani yao katika Yesu Kristo, injili Yake na Kanisa Lake? Yesu Kristo atabariki na kukuza juhudi zako endelevu.

Yeye Anatoa Ufunuo

Njia nyingine yenye nguvu ambayo Bwana huwasaidia wazazi ni kupitia karama ya ufunuo binafsi. Mungu anatamani sana kumwaga Roho wake ili awaongoze wazazi.

Unapokuwa katika maombi na usikivu kwa Roho, Yeye atakuonya juu ya hatari zilizofichika.15 Atafichua vipaji vya watoto wako, uwezo wao na mahangaiko ambayo hayajasemwa.16 Mungu atakusaidia uwaone watoto wako jinsi Yeye anavyowaona—zaidi ya sura yao ya nje na ndani ya mioyo yao.17

Kwa msaada wa Mungu, unaweza kujifunza kuwajua watoto wako kwa njia safi na ya kimbingu. Ninakualika ukubali mwaliko wa Mungu wa kuongoza familia yako kupitia ufunuo binafsi. Tafuta mwongozo wake katika maombi yako.18

Mabadiliko Makuu

Pengine msaada muhimu zaidi ambao Yesu Kristo huutoa kwa wazazi ni “mabadiliko makuu” ya moyo.19 Ni muujiza ambao kila mmoja wetu anauhitaji.

Kwa muda, fikiria hali hii: Uko kanisani, ukisikiliza mahubiri kuhusu familia. Mzungumzaji anaelezea nyumba yenye ukamilifu na hata familia yenye ukamilifu zaidi. Mume na mke hawagombani kamwe. Watoto huacha kusoma maandiko yao pale tu unapofika wakati wa kufanya kazi za nyumbani. Na muziki wa “Niwapendavyo”20 unasikika kwa sauti ya chini. Kabla ya mzungumzaji kufikia sehemu kuhusu kila mtu kujiunga ili kusafisha bafuni kwa furaha, tayari unafikiri, “Familia yangu haina matumaini.”

Wapendwa akina Kaka na akina Dada, tulieni! Kila mtu katika kusanyiko anafikiria jambo lile lile! Ukweli ni kwamba, wazazi wote wana wasiwasi kuhusu kutokuwa wazuri vya kutosha.

Kwa bahati nzuri, kuna chanzo cha kiungu cha msaada kwa wazazi: Ni Yesu Kristo. Yeye ndiye chanzo chetu cha badiliko kuu la moyo.

Unapofungua moyo wako kwa Mwokozi na mafundisho Yake, Yeye atakuonesha udhaifu wako. Kama ukimtumainia Yesu Kristo kwa moyo mnyenyekevu, Yeye atafanya vitu dhaifu kuwa vyenye nguvu.21 Yeye ni Mungu wa miujiza.

Je, hiyo inamaanisha kuwa wewe na familia yako mtakuwa na picha kamili? Hapana. Lakini utapata kuwa bora zaidi. Kupitia neema ya Mwokozi, kidogo kidogo, utakuza sifa zaidi ambazo wazazi wanahitaji: upendo kwa Mungu na watoto Wake, subira, kutokuwa na ubinafsi, imani katika Kristo na ujasiri wa kufanya chaguzi za haki.

Yesu Kristo Anatoa Msaada kupitia Kanisa Lake

Jitihada zetu za kujenga imani katika Yesu Kristo zimejikita nyumbani, zikifokasi kwa mtu binafsi. Na zinaungwa mkono na Kanisa. Kando na maandiko matakatifu na maneno ya manabii, Kanisa la Mwokozi hutoa nyenzo nyingi ili kuwasaidia wazazi na watoto wafanye maamuzi ya haki:

Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana: Mwongozo wa Kufanya Chaguzi
  • Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana: Mwongozo wa Kufanya Chaguzi haikupatii orodha ya cha kufanya au cha kutofanya. Hufundisha kweli za milele ili kusaida kufanya chaguzi zinazolenga kwenye maisha na mafundisho ya Yesu Kristo. Kisome pamoja na watoto wako. Waruhusu wazungumze kukihusu. Wasaidie wawe na kweli hizi za milele na takatifu ili ziongoze chaguzi zao.22

  • Mikutano ya KNV ni nyenzo nyingine nzuri. Natumaini kila kijana atahudhuria. Ninawaalika vijana waseja kujiunga na mikutano hii kama wanasihi na kama washauri. Ninawaalika wazazi kujenga juu ya kasi ya kiroho ambayo vijana wao huleta nyumbani kutoka kwenye mikutano ya KNV.

  • Watoto na vijana katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho wana walimu, washauri na wanasihi. Mara nyingi unaingia katika maisha ya kijana katika wakati muhimu ili kujenga na kuunga mkono imani na ushuhuda. Baadhi yenu ni watu wazima waseja. Wengine hamkujaliwa kupata watoto wenu wenyewe. Huduma yako yenye shangwe kwa watoto wa Mungu ni huduma takatifu machoni pa Mungu.23

Usikate Tamaa kwenye Muujiza

Rafiki zangu wapendwa, wapendwa akina kaka na akina dada, kujenga imani kwa mtoto ni sawa na kusaidia ua kukua. Huwezi kuvuta shina ili kulifanya liwe refu zaidi. Huwezi kufungua kichipukizi ili lichanue haraka. Na huwezi kupuuzia ua na kutarajia likue au kustawi kwa ghafla.

Unachoweza kufanya na lazima ufanye kwa ajili ya kizazi kinachoinukia ni kutoa udongo wenye rutuba ulio na upatikanaji wa maji ya mbinguni yanayotiririka. Ondoa magugu na kitu chochote ambacho kingezuia mwanga wa jua. Tengeneza mazingira bora zaidi kwa ajli ya ukuaji. Kisha kwa subira ruhusu kizazi kinachoinukia wafanye chaguzi zenye mwongozo wa kiungu na mruhusu Mungu atende muujiza Wake. Matokeo yatakuwa mazuri zaidi na ya kustaajabisha na ya kufurahisha zaidi kuliko kitu chochote ambacho ungeweza kutimiza mwenyewe.

Katika mpango wa Baba wa Mbinguni, uhusiano wa familia unakusudiwa kuwa wa milele. Hii ndiyo sababu, kama mzazi, hukati tamaa, hata kama huoni fahari jinsi mambo yalivyokuwa huko nyuma.

Ukiwa na Yesu Kristo, Mponyaji Mkuu na Mwokozi, daima kunaweza kuwa na mwanzo mpya; Yeye daima hutoa tumaini.

Yesu Kristo ni nguvu kwa familia.

Yesu Kristo ni nguvu kwa vijana.

Yesu Kristo ni nguvu kwa wazazi.

Juu ya hili ninashuhudia katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. “Asili karibu kwa kila mzazi ni tamaa ya kufundisha watoto wake maadili mema. Hii ni sehemu ya muujiza wa mpango wa Baba wa Mbinguni. Anataka watoto Wake waje duniani, wakifuata mtindo wa milele wa familia zilizopo mbinguni. Familia ni kitengo cha msingi cha taasisi ya ulimwengu wa milele, na hivyo Yeye anakusudia wao pia wawe kitengo cha msingi duniani. Ingawa familia za kidunia ziko mbali na ukamilifu, zinawapa watoto wa Mungu nafasi nzuri zaidi ya kukaribishwa ulimwenguni kwa upendo wa pekee duniani unaokaribia kile tulichohisi mbinguni—upendo wa mzazi. Familia pia ni njia bora ya kuhifadhi na kupitisha maadili mema na kanuni za kweli ambazo zina uwezekano mkubwa wa kuturudisha kwenye uwepo wa Mungu” (Henry B. Eyring, “Kukusanya Familia za Mungu,” Liahona, Mei 2017, 20).

  2. Bila shaka, tunajua kwamba siku zote mapenzi ya Mungu hayatimizwi “duniani, kama huko mbinguni” (Mathayo 6:10). Uzazi wa duniani kwa hakika ni mdogo kwa kulinganisha na bora ya Mungu. Hakika analiona hilo. Lazima alie juu ya huzuni zote na maumivu ya moyo katika mahusiano ya familia. Na bado hajakata tamaa juu ya familia. Na hatakata tamaa, kwa sababu Mungu anao mpango mtukufu kwa ajili ya hatma ya milele ya watoto Wake. Na kwenye kiini cha mpango huo ni familia.

  3. Ona Mathayo 18:1–5; Mosia 3:19.

  4. Familia: Tangazo kwa Ulimwengu,” ChurchofJesusChrist.org; ona pia Mafundisho na Maagano 68:25–28.

  5. Ona “Kujifunza Nyumbani Kunatokana na Mahusiano,” Kujifunza katika Njia ya Mwokozi: Kwa Wote Ambao Wanafundisha Nyumbani na Kanisani (2022), 30–31; ona pia Mafundisho na Maagano 109:8.

  6. Moroni 7:48.

  7. 1 Nefi 16:29; ona pia Alma 37:6–7.

  8. Ona “Kujifunza Nyumbani Hujumuisha Jitihada Ndogo, Rahisi, Thabiti,” Kufundisha katika Njia ya Mwokozi, 31. Rais David O. McKay alifundisha: “Tusifikiri kwamba, kwa sababu baadhi ya [mambo] … yanaonekana kuwa madogo na yasiyo na maana, [kwamba] si muhimu. Maisha, hata hivyo, yanaundwa na vitu vidogo vidogo. Maisha yetu, utu wetu, kimwili, umeundwa na mapigo madogo madogo ya moyo. Hebu moyo huo mdogo uache kupiga, na maisha katika ulimwengu huu hukoma. Jua kuu ni nguvu kuu katika ulimwengu, lakini tunapokea baraka za miale [yake] kwa sababu hutujia kama miale midogo, ambayo, ikichukuliwa kwa jumla, hujaza ulimwengu wote kwa mwanga wa jua. Usiku wa giza unapendezeshwa na mwangaza wa kile kinachoonekana kuwa nyota ndogo; na hivyo maisha ya Kikristo ya kweli yanafanyizwa na matendo madogo kama ya Kristo yanayofanywa saa hii, dakika hii—nyumbani” (Teachings of Presidents of the Church: David O. McKay [2003], 219).

  9. Ona Helamani 5:30.

  10. Ona 2 Wafalme 5:9–14.

  11. Ona Kutoka 16.

  12. Ona “Kuwatayarisha Watoto Wako kwa Maisha Yote Katika Njia ya Agano ya Mungu,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya 2023, kiambatisho (kidigitali pekee).

  13. Ona “Kujifunza Nyumbani Kwaweza Kupangwa lakini Pia Bila Kupangwa, Kufundisha katika Njia ya Mwokozi, 31; 1 Petro 3:15.

  14. Mafundisho na Maagano 64:32–33.

  15. Ona Mathayo 2:13.

  16. Ona Alma 40:1; 41:1; 42:1.

  17. Ona 1 Samweli 16:7.

  18. Ona 1 Nefi 15:8.

  19. Alma 5:13.

  20. Ona “Niwapendavyo,” Nyimbo za Dini, na. 185.

  21. Ona Etheri 12:27.

  22. “Kwa upande wa watoto, jukumu la kutoa mwongozo wa kimaadili ni la wazazi. Wanajua tabia, uelewaji, na akili ya kila mtoto. Wazazi hutumia maisha yao yote kutafuta na kudumisha mawasiliano mazuri na kila mmoja wa watoto wao. Wako katika nafasi nzuri zaidi ya kufanya maamuzi ya mwisho ya kimaadili kuhusu ustawi wa watoto wao” (James E. Faust, “The Weighter Matters of the Law: Judgment, Mercy, and Faith,” Ensign, Nov. 1997, 54).

  23. Nyenzo nyingine mbili zinazostahili kutajwa: Toleo la kidijitali la mwaka huu la Njoo, Unifuate nyenzo hujumuisha sehemu mpya yenye kichwa cha habari “Kutayarisha Watoto Wako kwa Maisha Yote Katika Njia ya Agano ya Mungu.” Hupendekeza mawazo rahisi, yanayolenga nyumbani kwa ajili ya kuwasaidia watoto kujiandaa kwa ubatizo na maagano na ibada zingine. Na Kufundisha katika Njia ya Mwokozi iliyosasishwa hivi karibuni ina sehemu yenye kichwa cha habari “Nyumba na Familia” ambayo inaeleza jinsi kanuni za mafundisho kama ya Kristo zinavyotumika nyumbani (ona ukurasa wa 30–31).