Nia ya Mungu ni Kukuleta Nyumbani
Kila kitu kuhusu mpango wa Baba kwa ajili ya watoto Wake wapendwa kimesanifiwa kumleta kila mtu nyumbani.
Ningependa kutoa shukrani kwa ajili ya sala zenu ninapoanza mchakato wa kuzoea wito, kupitia Rais Nelson, wa kutumikia kama Mtume wa Bwana Yesu Kristo. Unaweza kupata taswira ya jinsi hili lilivyo la kunyenyekeza, na umekuwa muda usio wa kawaida wa mabadiliko na kwa umakini kujichunguza mwenyewe. Hata hivyo, kwa kweli ni heshima kubwa sana ya kumtumikia Mwokozi, katika wadhifa wowote, na kujishughulisha nanyi katika kushiriki habari njema za injili Yake ya tumaini.
Zaidi ya hapo, imesemekana kwamba nyumba ya kila Mtume husimama mama mkwe wa kipekee. Sijui kama hilo hasa limesemwa, lakini katika hali hiyo, kwa kweli inawezekana. Na ninadhani kwamba ukweli kwamba mama mkwe wangu hayupo pamoja nasi haipunguzi upekee wake.
Miezi kadhaa iliyopita, wakati mimi na mke wangu tukiwa tunazuru nchi nyingine kwa ajili ya kazi tofauti ya Kanisa, niliamka mapema asubuhi moja na kutazama nje kwa macho ya usingizi kutokea dirisha la hotelini. Huko chini kwenye mtaa wenye shughuli nyingi, niliona kizuizi barabarani kimewekwa na polisi akiwa karibu ili kugeuza magari yalipofika kwenye kizuizi. Hapo mwanzo, ni magari machache yalipita barabarani na kugeuza kurudi. Lakini wakati uliposonga na magari kuongezeka, foleni ya magari ikaanza kuongezeka.
Kutoka hapo juu dirishani, nilimtazama polisi akionekana kuridhika na nguvu zake za kuzuia mtiririko wa magari na kuwageuza watu. Kwa kweli, alionekana kuongeza hatua zake, kana kwamba yeye angeanza kukimbia, wakati kila gari likisogelea kizuizi. Kama dereva angeudhika kuhusu kizuizi, polisi hakuonekana kuwa na msaada au huruma. Yeye alitingisha tu kichwa chake mara kwa mara na kuonyesha mwelekeo mwingine.
Marafiki zangu, wanafunzi wenzangu kwenye hii barabara ya maisha ya duniani, mpango mzuri wa Baba yetu, hata mpango Wake wa “kupendeza,” uliosanifiwa kukuleta wewe nyumbani, siyo kukuzuia nje. Hakuna mtu aliyejenga kizuizi na kumweka mtu pale wa kukugeuza na kufukuza. Hakika, ni kinyume kabisa. Mungu yuko katika kukutafuta wewe bila kusita. Yeye anataka watoto Wake wote wachague kurudi Kwake, na Yeye anatumia kila njia inayowezekana kukurudisha Kwake.
Baba yetu mwenye upendo alisimamia Uumbaji wa huu ulimwengu kwa ajili ya dhumuni la kutoa nafasi kwa ajili yako na kwa ajili yangu kuwa na uzoefu wenye kukuza na kukuboresha wa duniani, fursa ya kutumia haki yetu ya kujiamulia tuliyopatiwa na Mungu kumchagua Yeye ili kujifunza, na kukua, kufanya makosa, kutubu, kumpenda Mungu na jirani yetu, na siku moja kurudi nyumbani Kwake.
Yeye alimtuma Mwanawe Mpendwa kwenye ulimwengu ulioanguka ili kuishi uzoefu mpana wa binadamu, kutoa mfano kwa ajili ya watoto Wake wengine kufuata, na kupatanisha na kukomboa. Kipawa kikubwa cha upatanishi cha Kristo huondoa kila kizuizi cha kifo cha kimwili na kiroho ambacho kingetutenganisha sisi na nyumba yetu ya milele.
Kila kitu kuhusu mpango wa Baba kwa ajili ya watoto Wake wapendwa kimesanifiwa kumleta kila mtu nyumbani.
Ni nini wajumbe wa Mungu, manabii Wake, wanauita mpango huu katika maandiko yaliyorejeshwa? Wanauita mpango wa ukombozi, mpango wa rehema, mpango mkuu wa furaha, na mpango wa wokovu ambao ni kwa wote, “kupitia damu ya Mwanangu wa Pekee”
Nia ya mpango mkuu wa furaha wa Baba ni furaha yako, hapa sasa, sasa hivi, na katika milele yote. Siyo kuzuia furaha yako na kukusababishia wewe wasiwasi na hofu.
Nia ya mpango wa ukombozi wa Baba kwa kweli ni ukombozi wako, kukombolewa kwako kupitia kuteseka na kifo cha Yesu Kristo, kuwekwa huru kutokana na ufungwa wa dhambi na kifo. Siyo kukuacha kama ulivyo.
Nia ya mpango wa rehema wa Baba ni kutoa rehema unaporudi Kwake na kuheshimu agano lako la uaminifu Kwake. Siyo kukatalia rehema na kuweka uchungu na huzuni.
Nia ya mpango wa wokovu wa Baba kwa kweli ni wokovu wako katika utukufu wa ufalme wa selestia pale unapopokea “ushuhuda wa Yesu” na kutoa nafsi yako yote Kwake. Siyo kukuzuia nje.
Je, hii inamaanisha kwamba kila kitu huendana na jinsi tunavyoishi maisha yetu? Kwamba haijalishi jinsi tunavyochagua kutumia haki yetu ya kujiamulia ? Kwamba tunaweza kushika au kukataa amri za Mungu? Hapana, si hivyo. Hakika mojawapo ya mialiko na kusihi kwa Yesu kuliko thabiti sana wakati wa huduma Yake duniani ilikuwa kwamba tubadilike na kutubu na kuja Kwake. Kinachojitokeza kimsingi katika mafundisho Yake yote ya kuishi kwenye uwanda wa juu zaidi wa tabia ya maadili ni wito wa maendeleo binafsi, imani katika Kristo yenye kugeuza, badiliko kuu la moyo.
Mungu anataka kutoka kwetu mageuzi makali ya ubinafsi na misukumo ya kiburi, kufurushwa kwa mtu wa asili, ili tuweze “kwenda, na kutotenda dhambi tena.”
Kama tunaamini nia ya mpango wenye ufikiaji wa Baba ni kutuokoa sisi, kutukomboa, kutupatia rehema, na kwa hiyo kutuletea sisi furaha, ni ipi nia ya Mwana na kupitia nani mpango huu mkubwa unatolewa?
Mwana alituambia Mwenyewe: “Kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenipeleka.” ().
Mapenzi ya Yesu ndiyo mapenzi ya ukarimu ya Baba! Yeye anataka kufanya iwezekane kwa ajili ya kila mmoja wa watoto wa Baba kupokea lengo la mwisho la mpango—uzima wa milele pamoja Nao. Hakuna aliyezuiwa kutokana na uwezo huu mtakatifu.
Kama una wasiwasi kwamba kamwe hautaweza kufikia kipimo, au kwamba mfuko wa upendo wa Upatanisho wa Kristo usio na mwisho kwa rehema unamjumuisha kila mtu mwingine, bali siyo wewe, basi huelewi. Isiyo na mwisho humaanisha isiyo na mwisho. Isiyo na mwisho hujumuisha wewe na wale unaowapenda.
Nefi alieleza ukweli huu mzuri: “Hafanyi chochote ila tu kwa manufaa ya ulimwengu; kwani anaupenda ulimwengu, hata kwamba anayatoa maisha yake ili awavute wanadamu wote kwake. Kwa hivyo, hamwamuru yeyote kwamba asipokee wokovu wake.”
Mwokozi, Msamaria Mwema, anaenda akiwatafuta kondoo wake waliopotea mpaka anapowapata. Yeye “hayuko tayari kwamba yeyote aangamie.”
“Tazama, mkono wangu wa rehema umenyoshwa kwenu, na yeyote atakayekuja, nitampokea.”
“Mnao wowote ambao ni wagonjwa miongoni mwenu? Waleteni hapa. Mnao wowote ambao ni viwete, au vipofu, au wa kupooza, au vilema, au wenye ukoma, au walionyauka au ni viziwi, au ambao wanateseka kwa njia yoyote? Waleteni hapa na nitawaponya, kwani ninayo huruma juu yenu.”
Yeye hakumfukuza yule mwanamke aliyekuwa anatokwa na damu, Yeye hakurudi nyuma kutokana na mkoma; Yeye hakumkataa mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi; Yeye hakuwakataa wenye nia ya kutubu—bila kujali dhambi yao. Na Yeye hakukatai wewe au wale unaowapenda pale mnapoleta Kwake mioyo yenu iliovunjika na roho zilizopoendeka. Hiyo siyo nia Yake au usanifu Wake, wala mpango Wake, dhumuni, matakwa au tumaini Lake.
Hapana, Yeye haweki vizuizi na vikwazo; Yeye huviondoa. Hakuachi wewe nje; Yeye anakualika wewe ndani. Huduma Yake yote ilikuwa ni tangazo hai la nia hii.
Kisha bila shaka kuna dhabihu Yake ya upatanisho yenyewe, ambayo ni vigumu sana kwetu kuielewa, zaidi ya uwezo wetu wa ufahamu. Lakini, na hii ni muhimu “lakini,” tunaelewa, tunaweza kufahamu, nia takatifu ya kuokoa ya dhabihu ya upatanisho Wake.
Pazia la hekalu lilipasuka mara mbili wakati Yesu alipofariki msalabani, kuashiria kwamba kufika tena kwenye uwepo wa Baba kulikuwa kumefunguliwa wazi kabisa—kwa wale wote ambao watamgeukia Yeye, kumtumainia Yeye, kutupa mizigo yao Kwake na kujichukulia nira Yake juu yao katika kifungo cha agano.
Kwa maneno mengine, mpango wa Baba siyo kuhusu vizuizi. Kamwe haujawahi kuwa hivyo; kamwe hautakuwa hivyo. Je, kuna mambo yoyote ambayo tunahitaji kufanya, amri za kushika, vipengele vya asili yetu vya kubadilisha. Ndiyo. Lakini kwa neema Yake, hayo yapo ndani ya uwezo wetu, sio mbali nasi.
Hii ndiyo habari njema! Mimi nina shukrani isiyo na kifani kwa ajili ya kweli hizi rahisi. Usanifu wa Baba, mpango Wake, dhumuni Lake, nia Yake, matakwa Yake, na matumaini Yake yote ni kukuponya, kukupa wewe amani, kukuleta wewe na wale unaowapenda nyumbani. Juu ya hili, ninatoa ushahidi katika jina la Yesu Kristo, amina.