Mkutano Mkuu
Furahia Katika Zawadi ya Funguo za Ukuhani
Mkutano mkuu wa Aprili 2024


19:3

Furahia Katika Zawadi ya Funguo za Ukuhani

Funguo za ukuhani huongoza jinsi ukuhani wa Mungu unavyoweza kutumika ili kutimiza lengo la Bwana na kuwabariki wale wanaokubali injili ya urejesho.

Wapendwa wangu akina kaka na akina dada, leo ni siku ya kihistoria kwangu na kwa Rais Dallin H. Oaks Ilikuwa ni miaka 40 iliyopita, mnamo Aprili 7, 1984, wakati tulipokubaliwa kwenye Akidi ya Mitume Kumi na Wawili. Tumefurahia kwenye kila mkutano mkuu tokea hapo, ikiwa ni pamoja na huu. Tumebarikiwa tena kuwa na wingi wa uwepo mtakatifu wa Roho. Ninatumaini mtajifunza mara kwa mara kutoka kwenye jumbe za mkutano huu kote katika miezi ijayo.

Nilipozaliwa, kulikuwa na mahekalu sita ya Kanisa yaliyokuwa yakitumika—yakiwa huko St. George, Logan, Manti, na Salt Lake City, Utah; pamoja na huko Cardston, Alberta, Canada; na Laie, Hawaii. Mahekalu mawili yalikuwa yametumika kwa uchache huko Kirtland, Ohio, na Nauvoo, Illinois. Wakati Kanisa likielekea magharibi, Watakatifu walilazimika kuyaacha mahekalu hayo.

Hekalu la Nauvoo liliharibiwa kwa moto wa makusudi. Lilijengwa upya na kisha kuwekwa wakfu na Rais Gordon B. Hinckley. Hekalu la Kirtland lilitiwa unajisi na maadui wa Kanisa. Baadaye Hekalu la Kirtland lilinunuliwa na dhehebu la Community of Christ, ambalo limekuwa likilimiliki kwa miaka mingi.

Mwezi uliopita, tulitangaza kwamba Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho limenunua Hekalu la Kirtland, pamoja na baadhi ya maeneo muhimu ya kihistoria huko Nauvoo. Tunashukuru kwa dhati kwa majadiliano mazuri na yenye manufaa ambayo tulikuwa nayo na viongozi kutoka Community of Christ ambayo yalipelekea makubaliano haya.

Hekalu la Kirtland.

Hekalu la Kirtland lina umuhimu usio wa kawaida kwenye Urejesho wa injili ya Yesu Kristo. Matukio kadhaa ambayo yalitokea hapo yalikuwa yametolewa unabii kwa milenia na yalikuwa muhimu kwa Kanisa liliorejeshwa la Bwana ili kutimiza kazi yake ya siku za mwisho.

Muhimu zaidi ya yote kati ya matukio hayo lilitokea siku ya Jumapili ya Pasaka, Aprili 3, 1836. Katika siku hiyo, Joseph Smith na Oliver Cowdery walipata uzoefu usio na kifani wa mfululizo wa kutembelewa. Kwanza, Bwana Yesu Kristo alitokea. Nabii aliandika kwamba “macho ya Mwokozi yalikuwa kama mwale wa moto; nywele za kichwa chake zilikuwa nyeupe kama theluji safi; uso wake ulingʼara kupita mngʼaro wa jua; na sauti yake ilikuwa kama sauti ya maji mengi yakimbiayo.”

Wakati wa matembezi haya, Bwana alitilia mkazo utambulisho Wake. Alisema, “Mimi ni kwanza na mwisho; Mimi ni yeye aliye hai, Mimi ni yule aliyeuawa; Mimi ni mtetezi wenu kwa Baba.”

Yesu Kristo kisha alitangaza kwamba Yeye alikuwa amelikubali hekalu kama nyumba Yake na alitoa ahadi hii ya kupendeza: “nami nitajionyesha kwa watu wangu kwa rehema katika nyumba hii.”

Ahadi hii kuu ni kwa kila hekalu hivi leo lililowekwa wakfu. Ninawaalika kutafakari ahadi ya Bwana inamaanisha nini kwenu binafsi.

Baada ya matembezi ya Mwokozi, Musa alitokea. Musa alitunuku kwa nabii Joseph Smith funguo za kukusanya Israeli na urejesho wa makabila kumi.

Wakati ono hili lilipofungwa, “Elia alitokea, na kukabidhi kipindi cha nyakati cha injili cha Ibrahimu” kwa Joseph.

Kisha Eliya nabii alitokea. Ujio wake ulitimiza ahadi ya Malaki kwamba kabla ya Ujio wa Pili, Bwana angemtuma Eliya ili “kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao, na mioyo ya watoto iwaelekee baba zao.” Eliya kisha alitunuku funguo kwa Joseph Smith za nguvu ya kuunganisha.

Umuhimu wa kurejeshwa kwa funguo hizi duniani na wajumbe watatu wa kimbingu chini ya maelekezo ya Bwana ni wa kusisitizwa sana. Funguo za ukuhani hujumuisha mamlaka na nguvu za urais. Funguo za ukuhani huongoza jinsi ukuhani wa Mungu unavyoweza kutumika ili kutimiza lengo la Bwana na kuwabariki wale wanaoikubali injili ya urejesho ya Yesu Kristo.

Ni muhimu kuzingatia kwamba kabla ya kurejeshwa kwa Kanisa, wajumbe kutoka mbinguni walikuwa wamempa Nabii Jospeh Smith ukuhani wa Haruni na wa Melkizedeki na kumpa funguo za kuhani zote mbili. Funguo hizi zilimpa Joseph Smith mamlaka ya kurejesha Kanisa mnamo 1830.

Kisha kwenye Hekalu la Kirtland mnamo 1836, utunukiaji wa funguo hizi tatu za ziada—ambazo ni, funguo za kukusanya Israeli, funguo za injili ya Ibrahimu na funguo za nguvu ya kuunganisha—ulikuwa ni wa muhimu. Funguo hizi zilimpa idhini Joseph Smith—na Marais wote waliofuatia wa Kanisa la Bwana—kuikusanya Isareli pande zote mbili za pazia, kubariki watoto wote wa agano kwa baraka za Ibrahimu, kuweka muhuri wa uthibitisho kwenye ibada za kikuhani na maagano na kuziunganisha familia milele. Nguvu ya funguo hizi za ukuhani haina mwisho na ni ya kushangaza.

Fikiria jinsi ambavyo maisha yako yangekuwa tofauti kama funguo za ukuhani zisingerejeshwa duniani. Bila funguo za ukuhani, usingeweza kupata endaumenti yenye nguvu za Mungu. Bila funguo za ukuhani, Kanisa lingeweza kutoa mafundisho kiasi na shughuli kadhaa tu za kibinadamu na si zaidi ya hapo. Bila funguo za ukuhani, hakuna kati yetu ambaye angeweza kufikia ibada muhimu na maagano ambavyo hutuunganisha sisi na wapendwa wetu milele na kuturuhusu hatimaye kuishi na Mungu.

Funguo za ukuhani hutofautisha Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho na taasisi nyingine duniani. Nyingi ya taasisi zingine zinaweza na hufanya maisha yako kuwa bora hapa duniani. Lakini hakuna taasisi nyingine inaweza na itaweza kuathiri maisha yako baada ya kifo.

Funguo za ukuhani hutupatia mamlaka ya kutoa baraka zote zilizoahidiwa kwa Ibrahimu kwa kila mwanamume au mwanamke mshika maagano. Kazi ya Hekaluni hufanya baraka hizi muhimu kupatikana kwa watoto wote wa Mungu bila kujali wapi au wakati gani waliishi, au wanapoishi sasa. Acha tufurahie kwamba funguo za ukuhani zipo tena duniani kwa mara nyingine.

Ninawaalika kutafakari kwa umakini matamko haya matatu:

  1. Kukusanyika kwa Israeli ni uthibitisho kwamba Mugu anawapenda watoto Wake wote kila mahali.

  2. Injili ya Ibrahimu ni uthibitisho zaidi kwamba Mungu anawapenda watoto wake wote kila mahali. Anawaalika wote kwenda Kwake—“weusi kwa weupe, wafungwa na walio huru, waume kwa wake; … wote ni sawa mbele za Mungu.”

  3. Nguvu hizi za kuunganisha ni uthibitisho upitao maelezo wa jinsi Mungu anavyowapenda watoto wake wote kila mahali na kutaka kila mmoja wao kuchagua kurudi nyumbani Kwake.

Funguo za ukuhani zilizorejeshwa kupitia Nabii Joseph Smith hufanya iwezekane kwa kila mwanamume na mwanamke mshika maagano kufurahia fursa binafsi za thamani za kiroho. Hapa pia, kuna mengi tunaweza kujifunza kutoka kwenye historia takatifu ya Hekalu la Kirtland.

Sala ya Joseph Smith ya kuweka wakfu Hekalu la Kirtland ni mafunzo kuhusu jinsi gani hekalu katika hali ya kiroho hututia nguvu wewe na mimi ili kukabiliana na changamoto za maisha kwenye siku hizi za mwisho. Ninawahamasisha mjifunze sala hiyo iliyoko kwenye Mafundisho na Maagano sehemu ya 109. Sala hiyo ya kuweka wakfu, ambayo ilipokelewa kwa ufunuo, hufundisha kwamba hekalu ni “nyumba ya sala, nyumba ya mfungo, nyumba ya imani, nyumba ya mafundisho, nyumba ya utukufu, nyumba ya utaratibu, nyumba ya Mungu.”

Orodha ya sifa hizi ni zaidi ya ufafanuzi wa hekalu. Ni ahadi kuhusu kitakachotokea kwa wale ambao wanatumikia na kuabudu kwenye nyumba ya Bwana. Wanaweza kutegemea kupokea majibu ya sala, ufunuo binafsi, imani kuu, nguvu, faraja, ongezeko la maarifa na nguvu.

Kutumia muda hekaluni kutakusaidia ufikirie selestia na uelewe wewe ni nani hasa, unaweza kuwa nani na aina ya maisha ambayo unaweza kuwa nayo milele. Kuabudu hekaluni mara kwa mara kutadumisha jinsi unavyojiona na jinsi ulivyo sehemu ya mpango mtukufu wa Mungu. Ninakuahidi hilo.

Pia tunaahidiwa kwamba ndani ya hekalu tunaweza “kupokea utimilifu wa Roho Mtakatifu.” Fikiria ni kipi ahadi hiyo inachomaanisha kwa maana ya mbingu kufunuliwa kwa kila mtafutaji wa dhati wa ukweli wa milele.

Tunaelekezwa kwamba wale wote wanaoabudu hekaluni watakuwa na nguvu za Mungu na malaika “wakiwahudumia.” Ni kwa kiasi gani hii huongeza kujiamini kwako kujua kwamba, kama mwanamume au mwanamke uliyepokea endaumenti yenye nguvu za Mungu, huitaji kukabiliana na maisha peke yako? Ni utiwaji moyo kiasi gani hili huleta kwako kwa kujua kwamba malaika kweli watakusaidia?

Hatimaye, sote tunaahidiwa kwamba “hakuna muunganiko wa uovu” utawashinda wale wanaoabudu kwenye nyumba ya Bwana.

Kuelewa fursa za kiroho ambazo hufanywa ziwezekane hekaluni ni muhimu kwa kila mmoja wetu hivi leo.

Wapendwa wangu akina kaka na akina dada, hii ni ahadi yangu kwenu. Hakuna kitakachokusaidia kushikilia kwa nguvu zaidi fimbo ya chuma kuliko kuabudu hekaluni mara nyingi kadiri hali zinavyoruhusu. Hakuna kitakachokulinda zaidi wakati unapokumbana na ukungu wa giza wa duniani. Hakuna kitakachoimarisha ushuhuda wako juu ya Bwana Yesu Kristo na Upatanisho Wake au kukusaidia uelewe zaidi mpango mtakatifu wa Mungu. Hakuna kitakachoipa faraja zaidi roho yako nyakati za maumivu. Hakuna kitakachofungua mbingu zaidi. Hakuna!

Hekalu ni lango kuelekea baraka kuu za Mungu alizonazo kwa ajili ya kila mmoja wetu, kwani hekalu ni sehemu pekee duniani ambapo tunaweza kupokea baraka zote zilizoahidiwa kwa Ibrahimu. Hii ndiyo sababu tunafanya kila lililo ndani ya uwezo wetu, chini ya maelekezo Bwana, kufanya baraka za hekaluni zipatikane zaidi kwa waumini wa Kanisa. Hivyo, tunayo furaha kutangaza kwamba tunapanga kujenga hekalu jipya kwenye kila sehemu hizi 15 zifuatazo:

  • Uturoa, French Polynesia

  • Chihuahua, Mexico

  • Florianópolis, Brazil

  • Rosario, Argentina

  • Edinburgh, Scotland

  • Eneo la kusini la Brisbane, Australia

  • Victoria, British Columbia

  • Yuma, Arizona

  • Houston eneo la kusini la Texas

  • Des Moines, Iowa

  • Cincinnati, Ohio

  • Honolulu, Hawaii

  • West Jordan, Utah

  • Lehi, Utah

  • Maracaibo, Venezuela

Wapendwa wangu akina kaka na akina dada, ninashuhudia kwamba hili ni Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Yeye ndiye mkuu wa Kanisa. Sisi ni wafuasi Wake.

Acha tufurahie kwenye urejesho wa funguo za ukuhani ambazo hufanya iwezekane kwangu na kwako kufurahia kila baraka ya kiroho ambayo tuko tayari na tunastahili kuipokea. Ninashuhudia hivyo katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.