Ushindi wa Tumaini
Tumaini ni zawadi hai, zawadi inayokua wakati tunapoongeza imani yetu katika Yesu Kristo.
Akina kaka na dada zangu wapendwa kote ulimwenguni, tunapoanza muda huu maalumu wa mkutano mkuu macho ya mbinguni bila shaka yatafokasi kwetu. Tutasikia sauti ya Bwana kupitia watumishi Wake; tutahisi ushawishi wenye “kuongoza, kuelekeza na kufariji” wa Roho Mtakatifu, na imani yetu itaimarishwa.
Miaka mitatu iliyopita, Rais Russell M. Nelson alifungua mkutano mkuu kwa maneno haya: “Ufunuo halisi kwa ajili ya maswali katika moyo wako utafanya mkutano huu kuwa wenye thawabu na usiosahaulika. Kama bado hujatafuta kuhudumiwa na Roho Mtakatifu ili akusaidie kusikia kile ambacho Bwana angetaka usikie katika siku hizi mbili, ninakualika kufanya hivyo sasa. Tafadhali fanya mkutano huu kuwa muda wa kusherehekea katika jumbe kutoka kwa Bwana kupitia watumishi Wake.”
Maandiko huunganisha kwa nguvu maneno matatu: imani, tumaini na hisani. Zawadi ya tumaini ni endaumenti ya thamani mno kutoka kwa Mungu.
Neno tumaini linatumika kwa ajili ya vitu vingi tunavyotaka vitokee. Kwa mfano, “Natumaini mvua haitanyesha,” au “Natumaini timu yetu ishinde.” Lengo langu ni kuzungumza kuhusu matumaini yetu matakatifu na ya milele katika Yesu Kristo na injili ya urejesho, na “[ma]tarajio ya ujasiri ya … baraka zilizoahidiwa za utakatifu.”
Tumaini Letu kwa ajili ya Uzima wa Milele
Tumaini letu la uzima wa milele limehakikishwa kupitia neema ya Kristo na chaguzi zetu wenyewe, likiruhusu baraka kuu ya kurudi kwenye makazi yetu ya mbinguni na kuishi milele katika amani pamoja na Baba wa Mbinguni, Mwanawe Mpendwa, familia zenye uaminifu na marafiki wapendwa, na wanaume na wanawake wenye haki kutoka kila bara na kila karne.
Duniani tunapitia shangwe na huzuni wakati tukijaribiwa na kuthibitishwa. Ushindi wetu huja kupitia imani katika Yesu Kristo wakati tunaposhinda dhambi zetu, magumu, majaribu, kukosa haki, na changamoto za maisha haya ya duniani.
Tunapoimarisha imani yetu katika Yesu Kristo, tunatazama zaidi mahangaiko yetu hadi kwenye baraka na uzima wa milele. Kama vile kwa mwanga ambao uangavu wake hukua, tumaini huangaza ulimwengu wa giza na tunaona siku zetu tukufu za baadaye.
Tumaini Hutoka kwa Mungu
Tangu mwanzo, Baba yetu wa Mbinguni na Mwanawe Mpendwa kwa dhati wamekuwa wakiwabariki wenye haki kwa zawadi za thamani kuu ya tumaini.
Baada ya kuondoka bustanini, Adamu na Hawa walifundishwa na malaika kuhusu ahadi za Yesu Kristo. Zawadi ya tumaini iliangaza maisha yao. Adamu alitangaza, “Macho yangu yamefunguliwa, na katika maisha haya nitakuwa na shangwe.” Hawa alizungumza kuhusu “shangwe ya ukombozi [wao], na uzima wa milele ambao Mungu huutoa kwa wote walio watiifu.”
Kama vile Roho Mtakatifu alivyoleta tumaini kwa Adamu, nguvu ya Roho wa Bwana huwaelimisha waaminifu leo hii, ikiangazia uhalisia wa uzima wa milele.
Mwokozi humtuma kwetu Mfariji, Roho Mtakatifu, mwenza kuleta imani, tumaini, amani “si kama ile ulimwengu utoayo.”
“Ulimwenguni,” Mwokozi alisema, “mnayo dhiki: lakini jipeni moyo [shikilieni mwangaza wa tumaini]; mimi nimeushinda ulimwengu.”
Katika nyakati za magumu, tunachagua kumwamini Bwana kupitia imani. Kimya kimya tunasali, “Si Mapenzi Yangu, bali Yako Yatendeke.” Tunahisi uthibitisho wa Bwana juu ya utayari wetu wa unyenyekevu na tunasubiria amani iliyoahidiwa ambayo Bwana ataituma kwa muda Wake aliouchagua.
Mtume Paulo alifundisha, “Mungu wa tumaini [atawajaza] ninyi na … furaha … , mpate kuzidi sana kuwa na tumaini,” “kwa tumaini, mkifurahi; katika dhiki, mkisubiri;” “katika nguvu za Roho Mtakatifu.”
Somo la Tumaini
Nabii Moroni alijua hapo kabla kuhusu kuwa na tumaini katika Kristo wakati wa dhiki. Alifafanua hali ya yake kuhuzunisha:
“Niko peke yangu. …” Sina … popote pa kwenda.”
“Na sitaki kujionyesha … wasije wakaniangamiza.”
Cha kushangaza, kwenye wakati huu wa kiza na wa upweke, Moroni aliandika maneno ya baba yake ya tumaini:
“Ikiwa mtu ana imani lazima ahitaji kuwa na tumaini; kwani bila imani hakuwezi kuwepo na tumaini lolote.”
“Na ni kitu gani mtakachotumainia? … Mtakuwa na tumaini kupitia upatanisho wa Kristo na nguvu ya ufufuko Wake, kuinuliwa kwenye maisha ya milele.”
Akina kaka na akina dada, tumaini ni zawadi hai, zawadi inayokua wakati tunapoongeza imani yetu katika Yesu Kristo. “Imani ni hakika ya mambo yatarajiwayo.” Tunajenga hakika hii—tofali za ushahidi wa imani yetu kupitia sala, maagano ya hekaluni, kushika amri, kuendelea kusherehekea maandiko na maneno ya manabii walio hai, kupokea sakramenti na kuabudu kila wiki pamoja na Watakatifu wenzetu.
Nyumba ya Tumaini
Ili kuimarisha tumaini letu katika nyakati za ongezeko la uovu, Bwana amemuelekeza nabii Wake kuijaza dunia kwa makehalu Yake.
Tunapoingia katika nyumba ya Bwana, tunahisi Roho wa Mungu, akithibitisha tumaini letu.
Hekalu hushuhudia kuhusu kaburi lililo wazi na maisha ambayo huendelea kupita pazia kwa ajili ya wote.
Kwa wale ambao hawana mwenza wa milele, ibada kwa nguvu huthibitisha kwamba kila mtu mwenye haki atapokea kila baraka iliyoahidiwa.
Kuna tumaini kuu wakati wanandoa vijana wanapopiga magoti kwenye madhabahu ili kuunganishwa, si tu kwa muda bali kwa milele yote.
Kuna wingi wa tumaini kwetu katika ahadi zilizowekwa kwa ajili ya kizazi chetu, bila kujali hali zao za sasa.
Hakuna maumivu, ugonjwa, ukosefu wa haki, mateso wala chochote ambacho kinaweza kutia giza tumaini letu wakati tunapoamini na kushikilia kwa nguvu maagano yetu na Mungu katika nyumba ya Bwana. Ni nyumba ya nuru, nyumba ya tumaini.
Wakati Tumaini Linapotupwa
Tunatokwa machozi ya huzuni wakati tunapoona huzuni na ukiwa wa wale ambao hawana tumaini katika Kristo.
Hivi karibuni kwa mbali niliwaona wanandoa ambao awali walikuwa na imani katika Kristo lakini baadae wakaamua kuitupa imani yao. Walikuwa na mafanikio ya kiulimwengu, na walijivunia uwezo wao wa kiakili na kuikataa imani yao.
Yote yalionekana kuwa sawa mpaka mume, akiwa bado kijana na mwenye nguvu, ghafla alipougua na kufa. Kama vile kupatwa kwa jua, walikuwa wameziba mwangaza wa Mwana, matokeo yake ilikuwa ni kupatwa kwa tumaini lao. Mke, katika kutoamini kwake, sasa akihisi kutojua cha kufanya, kwa uchungu akiwa hajajiandaa, alishindwa kuwafariji watoto wake. Uwezo wake wa akili ulikuwa umemwambia kwamba maisha yake yalikuwa katika mpangilio mzuri mpaka pale ambapo ghafla hakuweza kuiona kesho. Kukata tamaa kwake kulileta giza na mkanganyiko.
Tumaini katika Janga la Kuvunja Moyo
Acha nionyeshe tofauti kati ya majonzi yake na tumaini kwa Kristo la familia nyingine kwenye wakati wa kuvunjika moyo.
Miaka ishini na moja iliyopita mpwa wangu, mwana mpya wa kiume wa Ben Andersen na Robbie, mkewe, alisafirishwa akiwa mahututi kutoka kwao Idaho kuja Jiji la Salt Lake. Nilifika hospitali, na Ben akaelezea hali ya hatari, ya kutishia maisha iliyoko kwenye moyo wa mtoto wao mchanga. Tuliweka mikono yetu kwenye kichwa kidogo cha Trey. Bwana alimbariki kwa kuendeleza maisha yake.
Trey alifanyiwa upasuaji wa moyo wiki ya kwanza ya maisha yake, upasuaji zaidi ulifuata. Kadiri miaka ilivyopita, ilionekana kwamba Trey angehitaji kupandikizwa moyo. Ingawa shughuli zake za kimwili zilikuwa na ukomo, imani yake iliongezeka. Aliandika “Sijawahi kuhisi kujionea huruma kwa sababu mara zote nimejua umuhimu wa kuwa na imani katika Yesu Kristo na ushuhuda wa mpango wa wokovu.”
Trey aliweka nukuu hii maarufu kutoka kwa Rais Nelson kwenye simu yake: “Furaha tunayoihisi inahusiana kwa kiasi kidogo na hali za maisha yetu na inahusiana na kila kitu kinachohusu fokasi ya maisha yetu.”
Trey aliandika: “Mara zote nimekuwa nikitazamia kutumikia kama mmisionari, lakini … madaktari wasingeniruhusu kutumikia misheni mpaka mwaka mmoja baada ya kupandikizwa moyo. … Nimeweka imani yangu katika Yesu Kristo.”
Trey alifurahi kwa kukubaliwa kujiunga na digrii ya uhasibu huko BYU kuanzia muhula huu, lakini furaha zaidi ni kuhusu mwishoni mwa mwezi wa Julai ambapo alipokea simu aliyoitarajia kwa hamu ya kwenda hospitali kupandikizwa moyo.
“Mwaka mmoja” Trey alisema, “Nitakuwa kwenye misheni yangu.”
Kulikuwa na matazamio makubwa wakati alipoingia kwenye chumba cha upasuaji. Hata hivyo, wakati wa upasuaji kulikuwa na changamoto za kukatisha tamaa, na Trey hakuweza kuzinduka.
Robbie, mama yake, alisema: “Ijumaa ilikuwa siku ya kuvunja moyo … tunajaribu tu kuweka mawazo yetu sawa kuihusu. … Nilikaa mpaka usiku sana nikijaribu kutafakari kila kitu. … Lakini Jumamosi, niliamka na hisia ya shangwe kabisa. Haikuwa tu amani; haikuwa kukataa. Nilihisi shangwe kwa ajili ya mwanangu, na nilihisi shangwe kama mama yake. … Ben alikuwa ameamka mapema kuliko mimi, na wakati hatimaye tulipopata nafasi ya kuzungumza, Ben alikuwa pia ameamka na hisia sawa na zangu.”
Ben alifafanua: “Uelewa ulikuja nafsini mwangu wakati Mungu akinifundisha kupitia Roho Wake. Niliamka mnamo saa 10 alfajiri na nilijawa na amani na shangwe isiyoelezeka. Hii inawezekanaje? … Kifo cha Trey ni cha kueleta huzuni sana, ninamkumbuka sana. Lakini Bwana hatuachi bila faraja. … Ninatazamia kwenye muunganiko wenye shangwe.”
Ahadi ya Tumaini
Trey alikuwa ameandika kwenye shajara yake maneno haya ya Rais Nelson kutoka kwenye ujumbe wake wa mkutano mkuu: “Haionekani kuwezekana kuwa na furaha wakati mtoto wako anapokuwa na maradhi yasiyotibika au unapopoteza kazi yako, au mwenza wako anapokusaliti. Hata hivyo hiyo ndiyo furaha anayotoa Mwokozi. Furaha Yake ni endelevu, ikituhakikishia kwamba ‘mateso yetu yatakuwa kwa muda’ [Mafundisho na Maagano 121:7]na yatatakaswa kwa ajili yetu.”
Akina kaka na akina dada, amani muitafutayo inaweza isije kwa haraka kama mnavyotamani, lakini ninawaahidi kwamba mnapomtumainia Bwana, amani Yake itakuja.
Na tuikuze imani yetu, tukisonga mbele kwa mng’aro mkamilifu wa tumaini. Ninashuhudia kwamba tumaini letu ni Mwokozi wetu Yesu Kristo. Kupitia Yeye, ndoto zote za haki zitatimizwa. Yeye ni Mungu wa tumaini—ushindi wa tumaini. Yeye Yu hai na Yeye anakupenda. Katika jina la Yesu Kristo, amina.