Mkutano Mkuu
“Hii Ni Injili Yangu”—“Hili Ni Kanisa Langu”
Mkutano mkuu wa Oktoba 2024


13:49

“Hii Ni Injili Yangu”—“Hili Ni Kanisa Langu”

Hii ni injili ya Mwokozi, na hili ni Kanisa Lake (ona 3 Nefi 27:21; Mosia 26:22; 27:13). Muunganiko wa hivi viwili ni wenye nguvu na unabadilisha.

Kwa karne nyingi, poda nyeusi ilikuwa ndicho kitu chenye mlipuko wenye nguvu zaidi kilichoweza kupatikana. Ingeweza kurusha matufe ya mizinga, lakini haikuwa na ufanisi kwenye miradi ya uchimbaji wa madini na ujenzi wa barabara. Ilikuwa dhaifu sana katika kuvunjavunja mawe.

Mnamo 1846, mtaalamu wa kemia Muitaliano aliyeitwa Ascanio Sobrero alisanisi mlipuko mpya, nitroglycerin. Kimiminika hiki chenye mafuta mafuta angalau kilikuwa chenye nguvu mara elfu moja kuliko poda nyeusi. Kwa urahisi kilivunjavunja mawe. Kwa bahati mbaya, nitroglycerin haikuwa thabiti. Kama ungeidondosha kutoka kimo kifupi, ingelipuka. Kama ingepata joto kali, ingelipuka. Kama ingepata baridi kali, ingelipuka. Hata kama ingewekwa kwenye chumba cha nyuzi joto la kawaida chenye giza na kuachwa peke yake, hatimaye ingelipuka. Nchi nyingi zilipiga marufuku usafirishwaji wake, na nyingi zilipiga marufuku kutengenezwa kwake.

Mnamo 1860 mwanasayansi Mswidi aliyeitwa Alfred Nobel alianza kujaribu kuiimarisha nitroglycerin. Baada ya majaribio ya miaka saba, alitimiza malengo yake kwa kuifyonza nitroglycerin kuwa kitu kinachokaribia kukosa thamani kinachojulikana kama diatomaceous earth au kieselguhr. Kieselguhr ni mawe yanayofyonza unyevunyevu na ambayo yanaweza kusagwa na kuwa poda laini. Ikichanganywa na nitroglycerin, kieselguhr hufyonza nitroglycerin na uji uji unaotokea unaweza kuumbwa katika umbile la “vijiti.” Katika umbile hilo, nitroglycerin ilikuwa thabiti zaidi. Ingeweza kuhifadhiwa kwa usalama zaidi, kusafirishwa, na kutumika kwa mlipuko wenye nguvu isiyopungua. Nobel aliuita mchanganyiko huo wa nitroglycerin na kieselguhr kama “baruti”.

Baruti iliubadilisha ulimwengu. Pia ilimfanya Nobel kuwa tajiri. Pasipokuwa na kidhibiti, nitroglycerin ilikuwa kitu hatarishi sana kwa matumizi ya kibiashara, kama vile Ascanio Sobrero alivyogundua. Kikiwa chenyewe, kama nilivyosema, kieselguhr kilikuwa na thamani ndogo. Lakini muunganiko wa vijenzi hivyo viwili vimeifanya baruti kuleta mabadiliko na thamani.

Katika njia sawa na hiyo, muunganiko wa injili ya Yesu Kristo na Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho hutoa mabadiliko yenye nguvu na faida kwetu sisi. Injili ni kamilifu, lakini kanisa lililopewa mamlaka kiungu linahitajika kuihubiri, kudumisha usafi wake na kusimamia ibada zake takatifu kwa nguvu na mamlaka ya Mwokozi.

Zingatia muunganiko wa injili ya Mwokozi na Kanisa Lake kama lilivyoanzishwa na nabii Alma wa Kitabu cha Mormoni. Kanisa liliwajibika kuhubiri “si kingine isipokuwa toba na imani kwa Bwana, ambaye [angewakomboa] watu wake.” Kutumia mamlaka ya Mungu, Kanisa lillikuwa na wajibu wa kusimamia ibada ya ubatizo “katika jina la Bwana, kama ushahidi [wa kuingia] katika agano na Yeye kumtumikia yeye na kushika amri zake.” Watu ambao walibatizwa walijichukulia juu yao wenyewe jina la Yesu Kristo, walijiunga na Kanisa Lake, na waliahidiwa uwezo mkubwa kupitia mbubujiko wa Roho.

Watu walikusanyika kwenye maji ya Mormoni kumsikiliza Alma akihubiri injili. Ingawa waliyaheshimu maji hayo na msitu uliozunguka, Kanisa la Bwana halikuwa eneo au jengo, wala sio hivyo leo. Kanisa ni watu tu wa kawaida, wanafunzi wa Yesu Kristo, waliokusanyika pamoja, wakiwekwa katika muundo ulioteuliwa kiungu ambao unamsaidia Bwana kutimiza maadhumuni Yake. Kanisa ni chombo ambamo ndani yake tunajifunza nafasi muhimu ya Yesu Kristo katika mpango wa Baba wa Mbinguni. Kanisa linatoa njia za kimamlaka kwa watu binafsi ili kushiriki katika ibada na kufanya maagano ya kudumu na Mungu. Kushika maagano hayo kunatusogeza sisi karibu na Mungu, kunatupa sisi ufikiaji wa nguvu Zake, na kutubadilisha sisi katika kuwa wale Yeye anao kusudia tuwe.

Kama tu vile kwa baruti pasipo nitroglycerin haikuwa na umuhimu, Kanisa la Mwokozi ni maalumu tu endapo litakuwa limejengwa juu ya injili Yake. Pasipo injili ya Mwokozi na mamlaka Yake ya kusimamia ibada zake, Kanisa halingekuwa la kipekee.

Pasipo matokeo ya udhibiti ya kielselguhr, nitroglycerin ilikuwa na thamani yenye ukomo kama kilipuzi. Kama historia inavyoonyesha, pasipo Kanisa la Bwana, uelewa wa mwanadamu juu ya injili pia haukuwa thabiti—ukihatarishwa na anguko la mafundisho na kuwa kwenye ushawishi wa dini tofauti tofauti, tamaduni na falsafa. Munganiko wa ushawishi huo umekuwa ukidhihirika kwenye kila kipindi cha urejesho wa injili ulioongoza kwenye hiki cha mwisho. Ingawa mwanzoni injili ilifunuliwa katika usafi wake, uelewa na matumizi ya injili hiyo pole pole ulichukua sura ya uchamungu uliokosa nguvu kwa sababu muundo wa kiungu ulioidhinishwa haukuwepo.

Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho linawezesha ufikiwaji wa nguvu za Mungu kwa sababu limeruhusiwa na Yeye katika vyote kufundisha mafundisho ya Kristo na kutoa ibada okozi na kuinuliwa za injili. Mwokozi anatamani kutusamehe dhambi zetu, kutusaidia kufikia nguvu Zake na kutubadilisha. Yeye aliteseka kwa ajili ya dhambi zetu na anasubiri kwa hamu kutusamehe kutokana na adhabu ambayo vinginevyo tungestahili. Yeye anatutaka tuwe watakatifu na kukamilishwa katika Yeye.

Yesu Kristo anao uwezo wa kufanya hivyo. Yeye hakutuhurumia tu kwa mapungufu yetu na kuomboleza hali zetu za milele kama matokeo ya dhambi. Hapana, Yeye alifanya zaidi ya hayo, zaidi ya hayo pasipo ukomo, na alirejesha Kanisa Lake ili kuwezesha ufikiwaji wa nguvu Zake.

Msingi wa injili ambao Kanisa linafundisha ni kwamba Yesu Kristo alibeba “huzuni zetu na alichukua majonzi yetu.” Yeye “alijitweka juu yake uovu wetu sisi sote.” Yeye “aliuvumilia msalaba,” alikata “kamba za mauti,” “akapaa mbinguni, na … amekaa mkono wa kuume wa Mungu, ili kuchukua haki zake za rehema toka kwa Baba.” Mwokozi alifanya haya yote kwa sababu Yeye anampenda Mungu na anatupenda sisi. Yeye tayari ameshalipia bei isiyo na mwisho ili Yeye aweze “[kudai] haki juu ya wale wote ambao wana imani katika Yeye [na] huomba” kwa ajili yao—na sisi. Yesu Kristo hataki chochote zaidi ya sisi kutubu na kuja Kwake ili kwamba Yeye aweze kutuhalalisha na kututakasa. Katika hamu hii, Yeye hatetereki na hayumbishwi.

Njia ya kufikia nguvu ya Mungu ya kimaagano na upendo Wake wa kimaagano ni kupitia Kanisa Lake. Muunganiko wa injili ya Mwokozi na Kanisa Lake hubadilisha maisha yetu. Uliwabadilisha mababu zangu upande wa mama. Babu yangu Oskar Andersson, alifanya kazi katika yadi ya kutengeneza meli huko Högmarsö, kisiwa katika Stockholm archipelago. Mke wake, Albertina, na watoto wao waliishi Uswidi bara. Mara moja katika wiki mbili, siku ya Jumamosi, Oskar alipiga makasia boti yake kurudi nyumbani kwa ajili ya wikiendi kabla ya kurudi kwenda Högmarsö siku ya Jumapili jioni. Siku moja, akiwa huko Högmarsö, aliwasikia wamisionari wawili wa Kiamerika wakihubiri injili ya urejesho ya Yesu Kristo. Oskar alihisi kwamba kitu alichokisikia kilikuwa ukweli msafi, na alijawa na shangwe isiyoelezeka.

Wakati mwingine aliporudi nyumbani, Oskar kwa shauku alimwambia Albertina yote kuhusu wamisionari wale. Alimwelezea kwamba alisadiki kile walichofundisha. Alimwomba asome kipeperushi ambacho walikuwa wamempatia, na akamwelezea kwamba hafikirii kwamba mtoto wao yeyote atakayezaliwa siku za usoni anapaswa kubatizwa akiwa mtoto mchanga. Albertina aligadhabika na kutupa kipeperushi kwenye rundo la takataka. Hakuna mengi yaliyozungumzwa kabla ya Oskar kurudi kazini Jumapili jioni.

Mara alipokuwa ameondoka, Albertina alivitoa tena vile vipeperushi. Kwa uangalifu alilinganisha mafundisho yake na mafundisho yaliyoko kwenye Biblia Yake chakavu. Alistaajabu kuhisi kwamba kile alichokisoma kilikuwa cha kweli. Muda uliofuata Oskar kurudi nyumbani, alipokelewa kwa upendo mkuu, kama vile kwa nakala ya Kitabu cha Mormoni aliyokuwa amekuja nayo. Albertina kwa hamu alikisoma, akilinganisha tena mafundisho yake na yale katika Biblia yake. Kama ilivyokuwa kwa Oskar, naye aligundua ukweli ulio safi na akajawa na shangwe isiyoelezeka.

Oskar, Albertina na watoto wao walihamia Högmarsö ili kuwa karibu na waumini wachache waliokuwepo huko. Wiki moja baada ya Oskar na Albertina kubatizwa mnamo 1916, Oskar aliitwa kuwa kiongozi wa kikundi huko Högmarsö. Kama waongofu wengi, Oskar na Albertina walikabiliwa na ukosoaji kwa sababu ya imani yao mpya. Wakulima wa eneo lao walikataa kuwauzia maziwa, hivyo Oskar alipiga makasia kuvuka kisiwa kila siku ili kununua maziwa kutoka kwa mkulima aliye mvumilivu zaidi.

Hata hivyo wakati wa miaka iliyofuata, waumini wa Kanisa huko Högmarsö waliongezeka, kwa sehemu ni kwa sababu ya ushuhuda wenye nguvu wa na ari kubwa ya umisionari ya Albertina. Kikundi kilipokuja kuwa tawi, Oskar aliitwa kuwa rais wa tawi.

Waumini wa tawi la Högmarsö walikiheshimu kisiwa kile. Haya ndio yalikuwa Maji yao ya Mormoni. Hapa ndipo mahali walipopata maarifa ya Mkombozi wao.

Baada ya miaka mingi, kadiri walivyoshika maagano yao ya ubatizo, Oskar na Albertina walibadilishwa kwa uwezo wa Yesu Kristo. Walitamani sana kufanya maagano zaidi na kupokea baraka zao za hekaluni. Ili kupata baraka hizo, walihamia kutoka nyumbani kwao huko Uswidi kuja Jijini Salt Lake mnamo 1949. Oskar alitumikia kama kiongozi wa waumini huko Högmarsö kwa zaidi ya miaka 33.

Muunganiko wa nitroglycerin na kieselguhr uliifanya baruti kuwa ya thamani; muunganiko wa injili ya Yesu Kristo na Kanisa Lake ni zaidi ya bei yoyote. Oskar na Albertina walisikia kuhusu injili ya urejesho kwa sababu nabii wa Mungu aliwaita wamisionari, akawapa jukumu na kuwatuma kwenda Uswidi. Kwa mamlaka takatifu, wamisionari walifundisha mafundisho ya Kristo na kwa mamlaka ya ukuhani wakawabatiza Oskar na Albertina. Kama waumini, Oskar na Albertina waliendelea kujifunza, wakiendelea na kuwahudumia wengine. Walikuja kuwa Watakatifu wa Siku za Mwisho kwa sababu walishika maagano waliyofanya.

Mwokozi analielezea Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho kama “kanisa langu” kwa sababu Yeye amelipa mamlaka ya kutimiza madhumuni Yake—kuhubiri injili Yake, kutoa ibada Zake na maagano, na kufanya iwezekane kwa nguvu Zake kuhalalisha na kututakasa sisi. Bila Kanisa Lake, hakuna mamlaka, hakuna kuhubiri kweli zilizofunuliwa katika jina Lake, hakuna ibada au maagano, hakuna madhihirisho ya nguvu za uchamungu, hakuna kubadilishwa kuwa kile Mungu anataka sisi tuwe na mpango wa Mungu kwa ajili ya watoto Wake utakuwa si kitu. Kanisa katika kipindi hiki ni muhimu katika mpango Wake.

Ninakualika ujitoe kwa dhati zaidi kwa Mwokozi, injili Yake na Kanisa Lake. Ufanyapo hivyo, utatambua kwamba muunganiko wa injili ya Mwokozi na Kanisa Lake unaleta nguvu katika maisha yako. Nguvu hii ni zaidi ya ile ya baruti. Itapasua mawe yaliyo katika njia yako, itakubadilisha kuwa mrithi katika ufalme wa Mungu. Na wewe “utajazwa na hiyo shangwe ambayo haiwezi kuelezeka na iliyojaa utukufu.” Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Poda nyeusi ni mchanganyiko wa potasiamu naitreti (saltpeter) salfa, na mkaa. Imeainishwa kama kilipuzi laini au kilipuzi cha hali ya chini kwa sababu ya kiwango cha chini cha uchangukaji, kikiungua kwa kasi ya spidi ndogo kuliko ya sauti. Vilipuzi vya juu au vilipuzi vyenye matokeo ya juu hulipuka kuliko kuungua, vikizalisha wimbi la mshituko wa juu.

  2. Kilipuzi kiliwezesha “mpanuko katika ujenzi wa mahandaki ya gari moshi, mifumo ya mabomba taka, na barabara za chini ya ardhi kote duniani—miradi muhimu ya uhandisi ambayo haingewezekana kutimizwa bila ulipuzi unaodhibitiwa [ambao ulioruhusiwa]. Karibu kila mafanikio makubwa ya uhandisi ya [karne ya 19 na ya 20]—njia za Chini ya Ardhi za London, Daraja la Brooklyn, Reli ya Kuvuka Bara, [na] Mfereji wa Panama—vilitegemea hiki kilipuzi kipya” (Steven Johnson, The Infernal Machine: A True Story of Dynamite, Terror, and the Rise of the Modern Detective [2024], 24).

  3. Kwa sababu nitroglycerin haikuwa faida kibiashara, Ascanio Sobrero hakupata kuwa tajiri kwa sababu ya uvumbuzi wake. Hata hivyo, wakati Alfred Nobel alipojenga kiwanda cha baruti kali huko Avigliana, Italia mnamo 1873, Sobrero aliteuliwa kama mshauri anayelipwa vizuri zaidi katika kutambuliwa kwa ugunduzi wake wa nitroglycerin. Sobrero alishikilia uteuzi huo hadi kifo chake mnamo 1888. (Ona G. I. Brown, The Big Bang: A History of Explosives [1998], 106.)

  4. Kwa historia ya poda nyeusi, baruti na baruti kali, ona Brown The Big Bang, 1–121.

  5. Injili ya Yesu Kristo ni sawa katika maana na mafundisho ya Kristo.

  6. Ona Mosia 18:7, 20; 25:15, 22.

  7. Mosia 18:10.

  8. Ona 2 Nefi 31:13.

  9. Ona Mosia 18:17; 25:18, 23; Alma 4:4–5; Helamani 3:24–26; 3 Nefi 28:18, 23.

  10. Ona 2 Nefi 31:12–14; Mosia 18:10.

  11. Kanisa ni ufunguo wa kutoa maagano matakatifu kwa watoto wa Baba wa Mbinguni. Hii ndio kwa nini, wakati wa endaumenti hekaluni, waumini wanafanya agano la kushika sheria ya kuweka wakfu. Hii inamaanisha kwamba wanatoa muda wao, vipaji na kila kitu ambacho Bwana amewabariki navyo ili kujenga Kanisa la Yesu Kristo hapa duniani” (Kitabu cha Maelezo ya Jumla: Kuhudumu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, 27.2, Gospel Library).

  12. Ona Russell M. Nelson, “Hazina za Kiroho,” Liahona, Nov. 2019, 77.

  13. Ona Mosia 18:22; Musa 6:68; Mwongozo wa Maandiko, “Wana na Mabinti wa Mungu,” Gospel Library.

  14. Ona 3 Nefi 27:13–21.

  15. Ona Makala ya Imani 1:5.

  16. Ona Russell M. Nelson, “Shangilia katika Zawadi ya Funguo za Ukuhani,” Liahona, Mei 2024; 3 Nefi 27:9–11.

  17. Mwokozi “alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu” ili kwamba “sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, … ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu.” (Waefeso 4:11, 13–14).

  18. Syncretism ni jina la istilahi ya muunganisho wa dini tofauti, tamaduni au dhana za watu au kikundi.

  19. Ona Joseph Smith—Historia ya 1:19.

  20. Ona “Urejesho wa Utimilifu wa Injili ya Yesu Kristo: Tangazo kwa Ulimwengu la Maadhimisho ya Miaka Mia Mbili,” Gospel Library. Tangazo hili lilisomwa na Rais Russell M. Nelson kama sehemu ya ujumbe wake katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa 190, Aprili 5, 2020, huko jijini Salt Lake, Utah (ona “Msikilize Yeye,” Liahona, Mei 2020, 91–92).

  21. Tunaweza kufikia nguvu za Mungu kwa kuwa na imani katika Yesu Kristo, kutubu dhambi zetu na kuyashika maagano tuliyofanya na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo katika ibada kama vile ubatizo, endaumenti na sakramenti.

  22. Ona Mwongozo wa Maandiko, “Uhalalishaji,” Gospel Library.

  23. Ona Mwongozo wa Maandiko, “Utakaso,” Gospel Library.

  24. Ona Moroni 10:32–33.

  25. Ona Waebrania 4:15; ona pia tanbihia.

  26. Ona Mafundisho na Maagano 19:15–18.

  27. Ona Isaya 53:4–12.

  28. Waebrania 12:2.

  29. Mosia 15:23.

  30. Moroni 7:27–28; ona pia Mafundisho na Maagano 45:3–5.

  31. Ona Mosia 18:30.

  32. Ona Inger Höglund and Caj-Aage Johansson, Steg i Tro: Jesu Kristi Kyrka av Sista Dagars Heliga i Sverige 1850–2000 (2000), 66–67.

  33. Mafundisho na Maagano 115:4.

  34. Ona Mafundisho na Maagano 84:19–21.

  35. Ikiwa utapokea kile Kanisa la Bwana linachotoa, utakamilishwa na Kristo kabla ya Kanisa lake kukamilishwa, kama daima litakuwepo. Lengo Lake ni kukukamilisha wewe, wala si Kanisa Lake. Lengo Lake kamwe halijakuwa, kistiari, kugeuza kieselguhr kuwa almasi; lengo Lake limekuwa kukusafisha wewe uwe dhahabu safi, kukuokoa na kukuinua kama mrithi mwenza na Yeye katika ufalme wa Baba yetu wa Mbinguni. Basi hilo linahitajika kuwa lengo lako, pia. Uchaguzi ni wako.

  36. Helamani 5:44.