Kumwamini Baba Yetu
Mungu hutuamini sisi kufanya chaguzi nyingi muhimu, na katika mambo yote, anatutaka tumwamini Yeye.
Mnamo Juni 1, 1843, Addison Pratt aliondoka Nauvoo, Illinois, kwenda kuhubiri injili huko Visiwa vya Hawaii, akimwacha mke wake, Louisa Barnes Pratt, kuitunza familia yao changa.
Mateso yalipoongezeka huko Nauvoo, yakiwalazimisha Watakatifu kuondoka, na baadaye huko Winter Quarters walipokuwa wakijiandaa kuhamia Bonde la Salt Lake, Louisa alikabiliwa na uamuzi wa kusafiri au la. Ingelikuwa rahisi kubaki na kumsubiri Addison ili arudi kuliko kusafiri peke yake.
Katika matukio yote mawili, alitafuta ushauri wa nabii Brigham Young, ambaye alimtia moyo kusafiri. Licha ya ugumu mkubwa na kusita kwake binafsi, kwa mafanikio alifanya safari kila wakati.
Mwanzoni, Louisa alipata shangwe kidogo katika safari. Hata hivyo, punde akaanza kukaribia, uwanda mpana wa nyasi za kijani, maua pori yenye rangi rangi, na vishamba vidogo kwenye kingo za mito. “Mawazo yangu ya huzuni yalianza kutoweka pole pole,” aliandika, “na hapakuwa tena na mwanamke alikuwa bila furaha katika kombania yote.”
Hadithi ya Louisa imenivutia kwa kina sana. Nimestaajabishwa na utayari wake wa kuweka kando mapendeleo yake binafsi, uwezo wake wa kumwamini Mungu, na jinsi kutumia imani yake kulivyomsaidia kuona hali kwa njia tofauti.
Yeye amenikumbusha kwamba tunaye Baba mpendwa wa Mbinguni, ambaye anatujali mahali popote tulipo, na kwamba tunaweza kumwamini Yeye zaidi kuliko mtu au kitu chochote.
Chanzo cha Ukweli
Mungu hutuamini sisi kufanya chaguzi nyingi muhimu, na katika mambo yote, anatutaka tumwamini Yeye. Hii ni vigumu zaidi hasa wakati uamuzi wetu, au maoni ya umma, yanatofautiana na mapenzi Yake kwa watoto Wake.
Baadhi wanapendekeza kwamba tunapaswa kuweka upya mipaka kati ya kilicho sahihi na kisicho sahihi kwa sababu wanasema ukweli unaweza kulinganishwa, uhalisia unajieleza wenyewe, au Mungu ni mwema sana kiasi kwamba Yeye hajali kuhusu kile tunachofanya.
Wakati tunapotafuta kuelewa na kukubali mapenzi ya Mungu, inasaidia kukumbuka kwamba kuelezea mipaka kati ya sahihi na kisicho sahihi si jukumu letu. Mungu ameweka mipaka hiyo Yeye Mwenyewe, kulingana na kweli za milele kwa faida na baraka zetu.
Hamu ya kuzibadili kweli za Mungu za milele ina historia ndefu. Ilianza kabla ya ulimwengu kuanza, wakati Shetani alipoasi dhidi ya mpango wa Mungu, akitafuta kwa ubinafsi kuharibu haki ya mwanadamu ya kujiamulia. Kwa mpangilio kama huu, watu kama Sheremu, Nehori, na Korihori wametoa sababu kwamba imani ni upumbavu, ufunuo si muhimu, na chochote tunachotaka kufanya ni sahihi. Kwa bahati mbaya, mara kwa mara, uchepukaji wa namna hii kutoka kwenye kweli za Mungu umesababisha huzuni kuu.
Wakati baadhi ya mambo yanaweza kutegemea muktadha, siyo kila kitu kinahitaji hivyo. Rais Russell M. Nelson kwa uthabiti amefundisha kwamba kweli za Mungu zenye kuokoa ni dhahiri, zenye kujitegemea, na kufafanuliwa na Mungu Mwenyewe.
Uchaguzi Wetu
Tunayechagua kumwamini ni moja ya chaguzi muhimu za maisha. Mfalme Benjamini aliwafundisha watu wake, “Mwamini Mungu; amini kwamba yupo … ; amini kwamba anayo hekima yote … ; amini kwamba mwanadamu hafahamu vitu vyote Bwana anavyoweza kufahamu.”
Kwa bahati nzuri, tunayo maandiko na mwongozo kutoka kwa manabii walio hai ili kutusaidia kufahamu kweli za Mungu. Kama ufafanuzi zadi ya tulionao unahitajika, Mungu huutoa kupitia manabii Wake. Na Yeye atajibu sala zetu za dhati kupitia Roho Mtakatifu tunapotafuta kuelewa kweli ambazo bado hatujazielewa kikamilifu.
Mzee Neil L. Andersen aliwahi kufundisha kwamba hatupaswi kushangaa “kama nyakati fulani mtazamo [wetu] binafsi mwanzoni hauafikiani na mafundisho ya nabii wa Bwana. Hizi ni nyakati za kujifunza,” alisema “za unyenyekevu, wakati tunapopiga magoti kusali. Tunasonga mbele kwa imani, tukimwamini Mungu, tukijua kwamba baada ya muda tutapokea ufasaha zaidi wa kiroho kutoka kwa Baba wa Mbinguni.”
Nyakati zote, itasaidia kukumbuka mafundisho ya Alma kwamba Mungu anatoa neno kulingana na usikivu na jitihada tunayotoa kwa neno Lake. Kama tunatii neno lake, tutapokea zaidi, kama tunapuuza ushauri Wake, tutapokea kidogo na kidogo zaidi hadi hatupokei chochote. Upotevu huu wa maarifa haimaanishi kwamba ukweli ulikuwa sio sahihi badala yake, inaonyesha kwamba tumepoteza uwezo wa kuelewa ukweli huo.
Mtegemee Mwokozi
Huko Kapernaumu, Mwokozi alifundisha kuhusu utambulisho Wake na misheni Yake. Wengi waliona maneno Yake kuwa magumu kusikiliza, yakiwapeleka kwenye kugeuza migongo yao na “[kutotembea] pamoja na Yeye.”
Kwa nini waliondoka?
Kwa sababu hawakupenda kitu alichokisema. Hivyo, wakiamini uamuzi wao wenyewe, walienda zao, wakijinyima wenyewe baraka ambazo zingekuja kwao kama wangebaki.
Ni rahisi kwa kiburi chetu kuja katikati yetu sisi na ukweli wa milele. Tunapokuwa hatuelewi, tunaweza kusimama, kuruhusu hisia zetu zitulie, na kisha kuchagua jinsi ya kujibu. Mwokozi anatusihi “tumtegemee [Yeye] katika kila wazo, tusiogope.” Tunapofokasi kwa Mwokozi, imani yetu inaweza kuanza kushinda wasiwasi wetu.
Kama Rais Dieter F. Uchtdorf alivyotuhimiza kufanya: “tafadhali, kwanza tilia shaka mashaka yako kabla ya kutilia shaka imani yako. Kamwe tusiruhusu mashaka yatushikilie mateka na kutuzuia kupata upendo wa kiungu, amani, na karama zinazokuja kupitia imani katika Bwana Yesu Kristo.”
Baraka Huja kwa Wale Wanaobakia
Wakati siku ile wanafunzi wakiondoka kutoka kwa Mwokozi, Yeye kisha akawauliza wale Kumi na Wawili, “Je, ninyi nanyi mwataka kuondoka?”
Petro akajibu:
“Bwana, twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
“Nasi tumesadiki, tena tumejua ya kuwa wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.”
Mitume wale waliishi katika ulimwengu ule ule, na walikabiliana na mashinikizo yale yale ya kijamiii kama ya wale wanafunzi walioenda zao. Hata hivyo, katika wakati huu, walichagua imani yao na kumwamini Mungu, na hivyo kujihifadhia baraka ambazo Mungu huwapa wanaobaki.
Pengine wewe, kama mimi, wakati mwingine unajikuta ukiwa pande zote mbili za uamuzi huu. Tunapoona kwamba ni vigumu kuelewa au kukumbatia mapenzi ya Mungu, ni ya faraja kukumbuka kwamba Yeye anatupenda sisi jinsi tulivyo, popote tulipo. Na Yeye ana kitu kilicho bora kwa ajili yetu sisi. Kama tutamfikia Yeye, Yeye atatusaidia.
Wakati kumfikia Yeye inaweza kuwa vigumu, kama vile yule baba aliyetafuta uponyaji kwa ajili ya mwanae alivyoambiwa na Mwokozi “mambo yote yanawezekana kwake yeye aaminiye,” Katika nyakati zetu za masumbuko, nasi pia tunaweza kupaza sauti, “Nisaide kutokuamini [kwangu].”
Kuweka Mapenzi Yetu Chini ya Yale Yake.
Mzee Neal A. Maxwell wakati fulani alifundisha kwamba “uwekaji wa mapenzi ya mtu chini ndicho kitu binafsi cha kipekee tulicho nacho cha kuweka juu ya madhabahu ya Mungu.” Ndio maana Mfalme Benjamini alikuwa na shauku kubwa kwamba watu wake wawe “kama mtoto mdogo, mtiifu, mpole, mnyenyekevu, mvumilivu, mwenye upendo tele, aliye tayari kukubali vitu vyote ambayo Bwana anaona sahihi kuyaweka juu yake, hata kama vile mtoto hunyenyekea kwa baba yake.”
Mara zote, Mwokozi huwa mfano kamili kwa ajili yetu. Akiwa na moyo mzito, akijua kazi ya uchungu iliyompasa kufanya, Yeye alijinyenyekeza kwenye mapenzi ya Baba Yake, akitimiza kazi Yake ya kimasiya na kufungua ahadi ya umilele kwako wewe na mimi.
Uchaguzi wa kuweka mapenzi yetu chini ya mapenzi ya Mungu ni kitendo cha imani ambacho kipo kwenye moyo wa uanafunzi wetu. Katika kufanya uchaguzi huo, tunagundua kwamba haki yetu ya kujiamulia haipunguzwi, badala yake, inakuzwa na kupewa thawabu kwa uwepo wa Roho Mtakatifu, ambaye huleta dhumuni, shangwe, amani, na tumaini ambavyo hatuwezi kuvipata pengine popote.
Miezi kadhaa iliyopita, mimi na rais wa kigingi tulimtembelea dada mmoja na kijana wake mkubwa katika kigingi chao. Baada ya miaka mingi nje ya Kanisa, wakitangatanga kwenye njia ngumu, na zisizo rafiki, dada alirejea. Wakati wa kumtembelea kwetu, tulimuuliza kwa nini amerejea.
“Niliyavuruga maisha yangu,” alisema, “na nilijua nilihitaji kuwa wapi.”
Kisha nilimwuliza amejifunza nini katika safari yake.
Akiwa na hisia, alitushirikisha kwamba amejifunza kwamba alihitajika kuhudhuria Kanisani vya kutosha ili kuvunja tabia ya kutokufika Kanisani na kwamba alihitaji kubaki hadi patakapokuwa mahali alipotaka kuwa. Kurudi kwake hakukuwa rahisi, lakini kadiri alivyotumia imani katika mpango wa Baba, alihisi Roho akimrudia.
Kisha akaongeza, “Nimejua mwenyewe kwamba Mungu ni mwema na kwamba njia Zake ni bora kuliko zangu.”
Ninatoa ushuhuda wangu juu ya Mungu, Baba yetu wa Milele ambaye anatupenda, juu ya Mwanawe, Yesu Kristo, ambaye alituokoa sisi. Wanayajua maumivu yetu na changamoto zetu. Hawatatuacha kamwe na wanajua kikamilifu jinsi ya kutusaidia. Tunaweza kujipa moyo, tunapowaamini Wao zaidi kuliko yeyote au kitu kingine chochote Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.