Mkutano Mkuu
Mungu Anawapenda Watoto Wake Wote
Mkutano mkuu wa Oktoba 2024


9:37

Mungu Anawapenda Watoto Wake Wote

Yesu Kristo daima hutuita, na hututumia, watumishi Wake wa kawaida, ili kusaidia kuwaleta watoto Wake Kwake.

Je, Baba yetu wa Mbinguni anatamani nini kutoka kwako wewe? Je, unaelewa kwamba wakati ulipokuwa kwenye maisha yako kabla ya kuja duniani, Baba wa Mbinguni alikuwa akikuandaa kwa ajili ya maisha yako ya duniani? Akizungumza na vijana, Rais Russell M.Nelson alifundisha “Baba Yetu wa Mbinguni amehifadhi wengi wa watoto wake wa kiroho walio wazuri zaidi—pengine … timu Yake iliyo bora zaidi—kwa ajili ya awamu hii ya mwisho.” kwa sababu tulihifadhiwa kwa ajili ya siku hizi za mwisho, ni muhimu kwetu kujifunza kuwa wanafunzi wa Yesu Kristo.

Bwana Yesu Kristo ni Mchungaji Mwema na analijua kundi Lake, na kundi Lake linamjua mchungaji Wao kwa sababu “yeye humuita kondoo wake kwa jina lake.” Yeye daima hutuita, na anatutumia sisi, watumishi Wake wa kawaida, ili kusaidia kuwaleta watoto Wake Kwake.

Zamani kidogo, mimi na rais wa kigingi tulikuwa tukiwatembelea waumini wa Kanisa katika ujirani wa eneo husika. Baada ya kukamilisha matembezi yetu yaliyopangwa, rais wa kigingi aliniuliza ikiwa tungeweza kwenda kuiona familia moja zaidi. Alihisi msukumo kwamba tulipaswa kuzungumza nao.

Tuligonga mlango, na dada alifungua. Alinitazama, lakini hakujua nilikuwa nani, hivyo hakujieleza sana. Nilionyesha kwa mkono wangu kumwelekea rais wa kigingi, ambaye alimsalimu dada huyo kwa kumtaja jina. Punde tu alipomsikia na kumwona, alishangilia. Tukiwa tumesimama pale mlangoni, wote walikumbatiana na kulia pamoja. Hiyo ilianzisha toni ya matembezi yetu. Hatukujua kwamba dada yule alikuwa amepokea tiba ya kemikali ya kansa siku moja kabla. Alihisi kuwa mdhaifu sana kuweza kumhudumia mwanaye kijana mkubwa. Hivyo, nilisaidiana na rais wa kigingi kumvisha nguo mwanaye, na tukamweka kwenye kitimwendo chake. Tulimlisha chakula ambacho dada mwingine mwema kutoka kwenye kata alikileta mapema, na tulisaidia kwenye majukumu mengineyo. Kabla ya kuondoka nyumbani kwao humo, tuliweza kuwapatia baraka.

Yote yaliyokuwa mawazoni mwangu wakati wa ziara hii yalikuwa ni uthibitisho kwamba Yesu Kristo anawapenda kwa dhati. Anawaelewa na anajua kwa njia binafsi maumivu ya hali yao ya kipekee. Sehemu kubwa ya ziara yetu yote ilifanyika katika ukimya. Katika tukio hili hatukutoa mahubiri makubwa wala kushiriki andiko letu pendwa, lakini Bwana alitupatia baraka tele kupitia Roho Wake.

Moja ya sababu kuu ya Baba wa Mbinguni kukuleta hapa wakati huu ni kwamba uweze kutambua uwezo wako kamili. Hubiri Injili Yangu inatufundisha kuwa kama wanafunzi wa Kristo, tunapaswa kuepuka kujilinganisha sisi kwa sisi. Uwezo wako wa kiroho ni wa kipekee, binafsi na wa asili, na Baba yako wa Mbinguni anataka kukusaidia uukuze. Daima kutakuwa na mtu unayeweza kumsaidia ahisi upendo wa Baba yako wa Mbinguni. Uwezo wako ni wa kiungu. Wakati kwa hakika ni muhimu kujitayarisha ili kufanikiwa katika ulimwengu huu wenye mashindano, misheni yako muhimu katika maisha yako yote ni kuwa mwanafunzi wa Yesu Kristo na kufuata misukumo ya Roho. Unapofanya hili, Mungu atayabariki maisha yako; Ataibariki familia yako ya sasa na ya baadaye; na Atayabariki maisha ya watoto Wake unaokutana nao.

Tunaishi katika ulimwengu wenye fursa nyingi. Japo tunakabiliwa na magumu mengi, ninajua yapo kwa sehemu ili kuturuhusu tuwasaidie wengine wahisi upendo wa Baba yetu wa Mbinguni. Rais Nelson alifundisha, “Katika siku zijazo, tutaona madhihirisho makubwa zaidi ya nguvu za Mwokozi ambayo ulimwengu kamwe haujapata kuyaona.” Tunayo fursa ya kuwatunza watu wanaohitaji mkono wa usaidizi, kumbatio, hisia ya faraja au kuwa nao tu katika ukimya. Ikiwa tutasaidia kupunguza mizigo yao, hata kama ni kwa muda tu, basi tutaweza kuona madhihirisho makubwa ya nguvu za Mwokozi katika maisha yao.

Kama wanafunzi wa Yesu Kristo, Watakatifu wa Siku za Mwisho wanaweza kuleta tofauti chanya ulimwenguni. Tunaweza kutoa hisia ya shangwe ambayo huakisiwa katika nyuso zetu—shangwe tunayoishiriki kwa maneno ya upendo na matendo ya ukarimu. Tuwe majirani wema, waajiriwa wema na wafanyakazi wema. Hebu tujitahidi kuwa Wakristo wema nyakati zote.

Bwana amerejesha injili Yake pamoja na ibada muhimu ili kwamba watoto wa Baba wa Mbinguni waweze kuwa na ahadi zote zinazotuunganisha Kwake. Kwa kuwasaidia dada zetu na kaka zetu katika changamoto zao za kila siku, na tukumbuke pia kuwasaidia wafanye na washike ahadi hizi takatifu kwa Baba yao wa Mbinguni ili kwamba Yeye awaahidi baraka tele kwa ajili ya maisha haya na milele yote. Ahadi hizi zinafanywa ziwezekane kupitia Urejesho wa injili ya Yesu Kristo na funguo Zake za ukuhani pekee.

Kwa maneno mengine, tunaweza kuwasaidia wengine wabaki kwenye njia ya agano. Baadhi yetu tunachepuka kutoka kwenye njia mara kadha wa kadha, na hivyo lazima tukumbuke kwamba kwa Baba yetu wa Mbinguni, daima tunao uwezekano wa kurejea. Hata ikiwa njia yetu si kamilifu sana, Mwokozi daima anatukumbusha kwamba “kadiri [tunavyotubu] na [kutafuta] msamaha, kwa kusudi halisi, [tutasamehewa].”

Moja ya mbinu za adui leo ni kutufanya tudhani na kuamini kwamba hakuna njia ya sisi kubadilika au kwamba hatuna tena tumaini. Dhana hii angamizi huwafanya wengi wetu kuacha kujaribu. Na ni katika wakati huu ambapo upendo wetu, maneno yetu ya kutia moyo na uungaji mkono, muda wetu na usaidizi wetu vinaweza kumpa mtu tumaini la kutosha kujaribu kwa mara nyingine tena.

Pengine unawaza, “SAWA, lakini nani atanitumikia mimi?” Kwa kwenda na kuyabariki maisha ya kaka zetu na dada zetu, tutakusanya shuhuda ambazo zitajaza maisha yetu kwa imani katika Bwana Yesu Kristo. Shuhuda hizi zitafufua ari yetu ya sisi kujaribu tena zaidi. Roho Mtakatifu atatuhuisha na kutusaidia kwa shuhuda zilizofanywa upya ili kushughulikia magumu yetu wenyewe na majaribu binafsi. Wakati wowote tunapotafuta kuyabariki maisha ya wengine, Bwana huleta rehema juu yetu hata zaidi na zaidi; Hutuimarisha na kutusaidia katika maisha yetu.

Tafadhali kumbuka kwamba Bwana Yesu Kristo, ni Mwokozi wako na hukuelewa binafsi. Anajua jinsi ambavyo inahitajika ili kutimiza wito na jinsi inavyohitajika kuacha vitu nyuma ili kuwasaidia watoto wa Mungu. Yeye anao uwezo wa kukubariki katika yote ikiwa unamwamini na huna mashaka.

Wapendwa kaka zangu na dada zangu, siku ile wakati kiongozi wa ukuhani alipohisi msukumo wa sisi kumtembelea yule mama na mwanae ambao hawakuwepo kwenye ajenda yetu, ninatamka kwamba Mungu alijua kwamba walituhitaji. Na hatimaye, ilikuwa ni mimi ambaye nilihudumiwa. Katika siku ile, nilipokea moja ya masomo makubwa ya upendo wa Mwokozi kwa ajili yetu.

Ninashuhudia kwamba Yesu Kristo ni Mwokozi wa ulimwengu, kwamba Yu hai, kwamba aliishi na kufa kwa ajili yako na yangu, na kwamba alifufuka kwa ajili yako na yangu ili kwamba tuweze kutumainia miunganiko ya selestia iliyojaa shangwe tukiwa na wale ambao tayari wako upande mwingine wa pazia. Ninajua kwamba anakuelewa wewe na mimi kikamilifu. Yeye anaelewa kila moja ya nyakati zetu ngumu, na Anao uwezo wa kutusaidia katika nyakati hizo ambapo tunahisi zaidi kuwa waathirika. Ninajua kwamba Bwana Yesu Kristo na Baba yetu wa Mbinguni walimtokea Joseph Smith ili kurejesha injili katika siku hizi. Ninajua kwamba nabii wetu mpendwa, Rais Russell M. Nelson, ni nabii wa Bwana, na ninashuhudia juu ya haya katika jina la Yesu Kristo, Amina.