Mkutano Mkuu
Kumfuata Kristo
Mkutano mkuu wa Oktoba 2024


13:31

Kumfuata Kristo

Kama wafuasi wa Kristo, sisi tunafundisha na tunashuhudia juu ya Yesu Kristo, Mfano wetu Kamili. Kwa hiyo acha tumfuate Yeye kwa kuachana na ubishi.

Mwaka huu mamilioni wamevutiwa na mpango wa kujifunza injili unaojulikana kwa kupitia mwaliko wa Mwokozi wa “Njoo, Unifuate.” Kumfuata Kristo sio zoezi la juujuu au la mara moja moja. Ni dhamira endelevu na njia ya maisha ambayo inapaswa kutuongoza nyakati zote na katika mahali popote. Mafundisho Yake na mifano Yake huelezea njia kwa ajili ya kila mwanafunzi wa Yesu Kristo. Na wote wanaalikwa kwenye njia hii, kwani Yeye anawaalika wote kuja Kwake,“weusi kwa weupe, wafungwa na walio huru, waume kwa wake; … wote ni sawa mbele za Mungu.”

I.

Hatua ya kwanza katika kumfuata Kristo ni kutii kile Yeye anachokieleza kama “amri iliyo kuu katika torati”:

“Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote.

“Hii ndiyo amri iliyo kuu tena ni ya kwanza.

“Na ya pili yafanana nayo, Mpende jirani yako kama nafsi yako.

“Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii.”

Baba na mwanaye wakipeperusha tiara.

Amri za Mungu zinatoa mwongozo na nguvu za kuimarisha katika maisha yetu. Uzoefu wetu katika maisha ya duniani ni kama mvulana mdogo na baba yake wakirusha tiara katika siku ya upepo mwingi. Jinsi vile tiara ilivyopaa juu sana, upepo ulifanya uzi ulioiunganisha kuvutwa toka mikononi mwa mvulana mdogo. Kwa kukosa uzoefu wa nguvu za upepo, alishauri kukata uzi ili kwamba tiara iweze kupaa zaidi. Baba mwenye hekima alishauri hapana, akielezea kwamba uzi ndio ulikuwa unashikilia tiara dhidi ya upepo mkali. Ikiwa tunashindwa kushikilia uzi, tiara haitapaa juu sana. Itabebwa na pepo hizi na hatimaye kuanguka chini ardhini.

Huo uzi muhimu unawakilisha maagano ambayo yanatuunganisha na Mungu, Baba yetu wa Mbinguni na Mwanawe, Yesu Kristo. Tunapoheshimu maagano haya kwa kutii amri Zao na kuufuata mpango Wao wa ukombozi, ahadi Zao zilizoahidiwa zinatuwezesha sisi kupaa hata viwango vya selestia.

Kitabu cha Mormoni mara kwa mara hutangaza kwamba Kristo ni “nuru ya ulimwengu.” Wakati wa kutokea Kwake kwa Wanefi, Bwana aliyefufuka alielezea mafundisho hayo kwa kuwaambia: “Nimewapatia mfano.” “Mimi ni mwangaza ambao mtainua—kwamba mfanye yale ambayo mmeniona nikifanya.” Yeye ni mfano wetu. Tunajifunza kile ambacho Yeye amekisema na kufanya kwa kujifunza maandiko na kufuata mafundisho ya kinabii kama vile ambavyo Rais Russell M. Nelson ametuasa tufanye. Katika ibada ya sakramenti, tunafanya agano kila siku ya Sabato kwamba “daima tutamkumbuka, na kuzishika amri Zake.”

II.

Katika Kitabu cha Mormoni, Bwana ametupa sisi misingi katika kile Yeye alichokiita “mafundisho ya Kristo.” Mafundisho hayo ni imani katika Bwana Yesu Kristo, toba, ubatizo, kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu, kuvumilia hadi mwisho, na kuwa kama mtoto mdogo, ambayo inamaanisha kumtumainia Bwana na kujisalimisha kwa yote ambayo Yeye anahitaji kutoka kwetu.

Amri za Bwana ni za aina mbili, za kudumu kama vile mafundisho ya Kristo, na za muda. Amri za muda ni zile zilizo muhimu kwa mahitaji ya Kanisa la Bwana au waaminifu katika hali ya muda, lakini zinawekwa kando wakati hitaji linapokuwa limeisha muda. Mfano wa amri za muda ni maelekezo ya Bwana kwa uongozi wa mwanzo wa Kanisa ya kuwahamisha Watakatifu kutoka New York hadi Ohio, hadi Missouri, na hadi Illinois na mwishowe kuwaongoza waanzilishi kuondoka hadi Milima ya Magharibi. Ingawa zilikuwa ni za muda tu, wakati zikiwa zinatumika amri hizi zilitolewa ili zitiiwe.

Baadhi ya amri za kudumu zimechukuwa muda mrefu ili kufuatwa. Kwa mfano, hotuba maarufu ya Rais Lorenzo Snow juu ya sheria ya zaka ilisisitiza amri iliyotolewa zamani lakini bado ilikuwa haifuatwi na wengi wa waumini wa Kanisa. Ilihitaji kusisitizwa tena katika hali ya wakati huo iliyolikabili Kanisa na waumini wake. Mifano ya hivi karibuni ya kusisitiza tena imehitajika pia kwa sababu ya hali za sasa zinazowakabili Watakatifu wa Siku za Mwisho au Kanisa. Hii inajumuisha tangazo juu ya familia lililotolewa na Rais Gordon B. Hinckley kizazi kilichopita, na mwito wa Rais Russell M. Nelson wa hivi karibuni wa Kanisa kujulikana kwa jina lake lililofunuliwa, Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

III.

Mengine katika mafundisho ya Mwokozi wetu yanaonekana kuhitaji kusisitizwa tena katika hali za siku yetu.

Huu ni wakati wa maneno makali na ya kuumiza katika mawasiliano ya umma na hata wakati mwingine katika familia zetu. Tofauti kubwa juu ya masuala ya sera za umma mara nyingi huleta matendo ya ugomvi—hata chuki—katika mahusiano ya umma na binafsi. Mazingira haya ya uhasama wakati mwingine hulemaza hata uwezo wa kutunga sheria juu ya mambo muhimu pale ambapo raia wengi wanaona haja ya dharura kwa ajili ya hatua katika maswala yanayohusu umma.

Je, Wafuasi wa Kristo wanapaswa kufundisha nini na kufanya nini katika wakati huu wa mawasiliano yenye sumu? Je, mafundisho na mifano Yake ilikuwa ipi?

Mwokozi akiwafundisha Wanefi.

Ni muhimu kwamba miongoni mwa kanuni za kwanza Yesu alizofunza wakati alipotokea kwa Wanefi ilikuwa ni kuepukana na ubishi. Wakati Yeye akifunza hili katika muktadha wa migogoro ya kidini kuhusu mafundisho, sababu Yeye alizozitoa kwa uwazi zinatumika kwa mawasiliano na uhusiano katika siasa, sera za umma na mahusiano ya familia. Yesu alifundisha:

“Yule ambaye ana roho ya ubishi siye wangu, lakini ni wa ibilisi, ambaye ni baba wa ubishi, na huchochea mioyo ya watu kubishana na hasira, mmoja kwa mwingine.

“Tazama, hili sio fundisho langu, kuchochea mioyo ya wanadamu kwa hasira, mmoja dhidi ya mwingine; lakini hili ndilo fundisho langu, kwamba vitu kama hivi viondolewe mbali.”

Katika huduma Yake iliyobakia miongoni mwa Wanefi, Yesu alifunza amri zingine zinahusiana kwa karibu na katazo Lake la ubishi. Tunajua kutoka kwenye Biblia kwamba Yeye awali alikuwa amewafundisha kila moja ya hizi katika Mahubiri Yake makuu ya Mlimani, kwa kawaida katika lugha ile ile Yeye aliyoitumia kwa Wanefi. Nitanukuu lugha inayofahamika ya Biblia:

Mwokozi akifundisha Yerusalemu.

“Wapendeni maadui zenu, wabariki wanao walaani, wafanyie mazuri wale ambao wanawachukia, na muwaombee wale ambao wanawatumia kwa madharau na kuwadhulumu.”

Hii ni mojawapo ya amri za Kristo zinazojulikana sana—ya kimageuzi sana na ngumu sana kufuata. Lakini bado ni sehemu ya msingi sana ya mwaliko Wake kwa wote kumfuata Yeye. Kama vile Rais David O. McKay alivyofundisha, “Hakuna njia bora ya kuonyesha upendo kwa Mungu zaidi ya kuonyesha upendo bila choyo kwa wanadamu wenzetu.”

Pande zinazopingana kwenye upatanishi.

Hapa kuna mafundisho mengine ya msingi juu ya Yeye ambaye ni mfano wetu: “Heri wapatanishi: maana hao wataitwa wana wa Mungu.”

Wapatanishi! Ingebadilishaje uhusiano wetu binafsi ikiwa wafuasi wa Kristo wangeachana na maneno makali na ya kuumiza katika mawasiliano yao yote.

Katika mkutano mkuu mwaka uliopita, Rais Russell M. Nelson alitupatia changamoto hizi:

“Njia moja rahisi sana ya kumtambua mfuasi wa kweli wa Yesu Kristo ni kwa kuangalia huruma kiasi gani mtu huyo huwaonyesha wengine. …

“… Wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo ni wapatanishi.

“… Njia moja nzuri sana ya kumkumbuka Mwokozi ni kuwa wapatanishi. …

Akihitimisha mafundisho yake: “Ubishi ni uchaguzi. Upatanishi ni uchaguzi. Unayo haki yako ya kujiamulia kuchagua ubishi au mapatano. Ninawasihi mchague kuwa wapatanishi, sasa na daima.”

Maadui yamkini wanapaswa kuanza kwa kutambua jambo la pamoja ambalo juu yake wote wanakubaliana nalo.

Kufuata Mfano wetu Kamili na nabii Wake, tunahitaji kufanya kile kijulikanacho sana kama Sheria ya Dhahabu: “Yote mtakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na Manabii.” Tunajitahidi kupenda na kutenda mema kwa wote. Tunahitaji kuepukana na ubishi na kuwa wapatanishi katika mawasiliano yetu yote. Hii haimaanishi kulegeza sharti la kanuni zetu na vipaumbele vyetu bali kuachana na kuwashambulia wengine kwa ukali kwa sababu ya kanuni na vipaumbele vyao. Hicho ndicho Mfano wetu Kamili alichofanya katika huduma Yake. Huo ndio mfano Yeye aliotuwekea wakati alipotualika sisi tumfuate Yeye.

Katika huu mkutano mkuu miaka minne iliyopita, Rais Nelson alitoa changamoto ya kinabii kwa ajili ya siku yetu wenyewe:

“Je, wewe uko radhi kuacha Mungu ashinde katika maisha yako? Je, wewe uko radhi kuacha Mungu awe na ushawishi muhimu zaidi katika maisha yako? Je, utaruhusu maneno Yake, amri Zake, na maagano Yake, yashawishi kile unachofanya kila siku? Je, utaruhusu sauti Yake ichukue kipaumbele cha juu zaidi ya sauti zingine zote?”

Bwana Yesu Kristo.

Kama wafuasi wa Kristo, sisi tunafundisha na tunashuhudia juu ya Yesu Kristo, Mfano wetu Kamili. Kwa hiyo acha tumfuate Yeye kwa kuachana na ubishi. Tunapofuata sera zetu pendwa katika vitendo vya umma, acha tustahili kwa ajili ya baraka Zake kwa kutumia lugha na mbinu za wapatanishi. Katika mahusiano ya familia zetu na binafsi, acha tuepukane na kile kilicho cha ukali na chenye chuki. Acha tutafute kuwa watakatifu, kama vile Mwokozi wetu, ambaye jina Lake takatifu ninalishuhudia na kuomba baraka Zake ili kutusaidia kuwa Watakatifu. Katika jina la Yesu Kristo, amina.