Kuzika Silaha Zetu za Uasi
Na tuzike—chini, chini kabisa—dalili yoyote ya uasi dhidi ya Mungu katika maisha yetu na tuibadilishe kwa moyo wa hiari na akili iliyo tayari.
Kitabu cha Mormoni kinaandika kwamba takriban miaka 90 kabla ya kuzaliwa kwa Kristo, wana wa Mfalme Mosia walianza kile ambacho kingekuwa misioni ya miaka 14 kwa Walamani. Juhudi zisizo na mafanikio kwa vizazi vingi zilikuwa zimefanywa ili kuwaleta Walamani kwenye kuamini katika mafundisho ya Kristo. Wakati huu, hata hivyo, kupitia hatua za kimiujiza za Roho Mtakatifu, maelfu ya Walamani waliongoka na kuwa wanafunzi wa Yesu Kristo.
Tunasoma, “Na kwa kweli kama vile Bwana aishivyo, kwa hakika vile wengi walivyoamini, au vile wengi walivyoelimishwa kwenye ukweli, kupitia kwa mahubiri ya Amoni na ndugu zake, kulingana na roho ya ufunuo na ya unabii, na uwezo wa Mungu ukifanya miujiza ndani yao—ndio, nawaambia nyinyi, kama vile Bwana aishivyo, vile wengi wa Walamani walivyoamini kuhubiri kwao, na wakamgeukia Bwana, hawakuanguka kamwe kutoka kanisani.”
Muhimu katika uongofu wa kudumu wa watu hawa umeelezwa katika aya inayofuata: “Kwani walipata kuwa watu wenye haki na wakaweka chini silaha zao za uasi, kwamba hawangeweza kupigana na Mungu tena, wala dhidi ya yeyote wa ndugu zao.”
Rejeleo hili la “silaha za uasi” lilikuwa halisi na la lugha ya picha. Ilimaanisha panga zao na silaha zingine za vita lakini pia kutomtii kwao Mungu na amri Zake.
Mfalme wa Walamani hawa walioongoka alieleza kwa njia hii: “Na sasa tazama, ndugu zangu, … vile imekua yote ambayo tungetenda (kwa vile sisi tulikuwa wapotevu zaidi miongoni mwa wanadamu wote) kutubu dhambi zetu na mauaji mengi tuliyotenda, na kupata Mungu kuziondoa kutoka mioyo yetu, kwani ni hii tu tungefanya kutubu ya kutosha mbele ya Mungu kwamba angeondolea mbali hatia yetu.”
Zingatia maneno ya mfalme—toba yao ya dhati ilikuwa imesababisha sio tu msamaha wa dhambi zao, lakini pia Mungu aliondoa madoa ya dhambi hizo na hata hamu ya kutenda dhambi kutoka mioyoni mwao. Kama unavyojua, badala ya kuacha uwezekano wowote wa kurudi kwenye hali yao ya awali ya uasi dhidi ya Mungu, walizika mapanga yao. Na walipozika silaha zao, kwa mioyo iliyobadilika, pia walizika tabia yao za dhambi.
Tunaweza kujiuliza wenyewe ni nini tunaweza kufanya ili kufuata mpangilio huu, “kuweka chini silaha za uasi [wetu],” zozote zile na “kuongolewa katika Bwana” kwamba doa la dhambi na hamu ya kutenda dhambi kuondolewa kutoka mioyoni mwetu na kamwe tusianguke.
Uasi unaweza kuwa wa utendaji au kimyakimya. Mfano wa kawaida wa uasi wa makusudi ni Lusiferi, ambaye, katika ulimwengu wa kabla ya maisha ya duniani, alipinga mpango wa ukombozi wa Baba na kuwakusanya wengine kupinga pia, “na, siku hiyo, wengi walimfuata.” Si vigumu kutambua athari za uasi wake unaoendelea katika wakati wetu wenyewe.
Wapinga-Kristo watatu katika Kitabu cha Mormoni—Sheremu, Nehori, na Korihori—ni mfano hai wa uasi dhidi ya Mungu. Tasnifu ya juu ya Nehori na Korihori ilikuwa kwamba hakuna dhambi; kwa hivyo, hakuna haja ya toba, na hakuna Mwokozi. “Kila mtu anafanikiwa kulingana na akili yake, na … kila mtu alishinda kulingana na nguvu yake; na chochote ambacho mtu alifanya si kosa.” Mpinga Kristo anakataa mamlaka ya kidini, akitaja ibada na maagano kama maonyesho “yaliyoanzishwa na makuhani wa zamani, ili kujitwalia nguvu na uwezo juu yao.”
Mfano wa siku za mwisho wa uasi wa makusudi wenye mwisho wa furaha ni masimulizi kuhusu William W. Phelps. Phelps alijiunga na Kanisa mwaka 1831 na aliteuliwa kuwa mpiga chapa wa Kanisa. Alihariri machapisho kadhaa ya awali ya Kanisa, aliandika nyimbo nyingi, na kutumika kama mwandishi wa Joseph Smith. Kwa bahati mbaya, aligeuka dhidi ya Kanisa na Nabii, hata kufikia hatua ya kutoa ushahidi wa uongo dhidi ya Joseph Smith katika mahakama ya Missouri, ambapo ilichangia Nabii kuweka gerezani.
Baadaye Phelps alimwandikia Joseph akimwomba msamaha. “Ninaijua hali yangu, wewe unaijua, na Mungu anaijua, na ninataka kuokolewa kama marafiki zangu watanisaidia.”
Katika majibu yake Nabii alisema: “Ni kweli kwamba tumeteseka sana kutokana na tabia yako. … Hata hivyo, kikombe kimenywewa, mapenzi ya Baba yetu wa Mbinguni yamefanywa, na bado tuko hai. … Njoo, ndugu mpendwa, kwa kuwa vita vimepita, kwa kuwa marafiki wa kwanza ni marafiki tena.”
Kwa toba ya dhati, William Phelps alizika “silaha zake za uasi,” alipokelewa tena katika ushirika kamili, na kamwe hakuanguka tena.
Labda aina ya uasi wa kuchukiza zaidi dhidi ya Mungu, hata hivyo, ni ule wa kimyakimya—kupuuza mapenzi Yake katika maisha yetu. Wengi ambao kamwe hawangeweza kuonyesha uasi waziwazi bado wanaweza kupinga mapenzi na neno la Mungu kwa kufuata njia yao wenyewe bila kujali maelekezo ya kiungu. Ninakumbushwa kwa wimbo uliotungwa miaka mingi iliyopita na mwimbaji Frank Sinatra na mstari wa juu kabisa, “Nilifanya kwa njia yangu.” Hakika katika maisha kuna nafasi nyingi za mapendeleo na chaguzi binafsi, lakini linapokuja suala la wokovu na uzima wa milele, wimbo wetu wa dhima unapaswa kuwa, “Nilifanya kwa njia ya Mungu,” kwani hakika hakuna njia nyingine.
Kwa mfano, chukua mfano wa Mwokozi kuhusiana na ubatizo. Alijisalimisha kwenye ubatizo kama onyesho la uaminifu kwa Baba na kama mfano kwetu:
“Anawaonyesha watoto wa watu kwamba, kulingana na mwili anajinyenyekeza mbele ya Baba, na kumshuhudia Baba kwamba yeye atakuwa mwaminifu kwake katika kutii amri zake. …
“Na akawaambia watoto wa watu: Nifuateni mimi. Kwa hivyo, ndugu zangu wapendwa, je, tunaweza kumfuata Yesu tusipokubali kushika amri za Baba?”
Hakuna “njia yangu” iwapo tunataka kufuata mfano wa Kristo. Kujaribu kupata njia tofauti kwenda mbinguni ni kama ubatili wa kufanya kazi kwenye Mnara wa Babeli badala ya kumtafuta Kristo na wokovu Wake.
Panga na silaha nyingine ambazo Walamani waongofu walizizika zilikuwa silaha za uasi kwa sababu ya jinsi walivyozitumia. Aina hizo hizo za silaha mikononi mwa watoto wao, zikitumika katika ulinzi wa familia na uhuru, hazikuwa silaha za uasi dhidi ya Mungu hata kidogo. Ndivyo ilivyokuwa kwa silaha kama hizo mikononi mwa Wanefi: “Kwani hawakuwa wanapigania utawala wala uwezo lakini walipigania maskani yao na uhuru wao, wake zao na watoto wao, na vyao vyote, ndiyo, kwa kanuni zao za kuabudu na kanisa lao.”
Kwa njia hiyo hiyo, kuna mambo katika maisha yetu ambayo yanaweza kuwa vuguvugu au hata mazuri lakini ambayo hutumiwa kwa njia isiyo sahihi huwa “silaha za uasi.” Maneno yetu, kwa mfano, yanaweza kujenga au kukebehi. Kama Yakobo alivyosema:
“Bali ulimi hakuna awezaye kuufuga; ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti.
“Kwa huo twamhimidi Mungu Baba yetu, na kwa huo twawalaani wanadamu waliofanywa kwa mfano wa Mungu.
“Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu, haifai mambo hayo kuwa hivyo.”
Kuna mengi leo katika katika mazungumzo ya umma na ya binafsi ambayo ni ya nia ovu na roho ya udhalilishaji. Kuna mengi ya mazungumzo ambayo ni machafu na matusi, hata miongoni mwa vijana. Aina hii ya usemi ni “silaha za uasi” dhidi ya Mungu, “zilizojaa sumu ya mauti.”
Fikiria mfano mwingine wa kitu ambacho kimsingi ni kizuri lakini ambacho kinaweza kugeuzwa dhidi ya maagizo ya Mungu—kazi ya mtu. Mtu anaweza kupata kuridhika katika taaluma, wito, au huduma, na sisi sote tunafaidika na kile ambacho watu waliojitolea na wenye vipaji katika nyanja nyingi za juhudi wamekamilisha na kuunda.
Hata hivyo, inawezekana kwamba kujitolea kwenye kazi inaweza kuwa fokasi ya juu kabisa ya maisha ya mtu. Kisha mengine yote yanakuwa ya pili, ikiwa ni pamoja na chochote ambacho Mwokozi anaweza kuomba kufanywa katika muda na talanta ya mtu. Kwa wanaume na wanawake vile vile, kuacha fursa halali za ndoa, kushindwa kuambatana na, na kumwinua mwenza wake, kushindwa kulea watoto wake, au hata kuepuka kwa makusudi baraka na majukumu ya kulea watoto kwa ajili tu ya sababu ya maendeleo ya kazi kunaweza kubadilisha mafanikio ya kujivunia kuwa aina ya uasi.
Mfano mwingine unahusu utu wetu wa kimwili. Paulo anatukumbusha kwamba tunapaswa kumtukuza Mungu katika mwili na roho na kwamba mwili huu ni hekalu la Roho Mtakatifu, “ambalo mnalo kutoka kwa Mungu, na ninyi si mali yenu.” Basi, tuna maslahi halali katika kutumia muda kutunza miili yetu vizuri kadiri tuwezavyo. Wachache wetu tutafikia kilele cha utendaji ambao tumeona hivi karibuni katika mafanikio ya Olimpiki na Paralimpiki, na baadhi yetu tunakabiliwa na athari za umri, au kile Rais M. Russell Ballard alichokiita “ribiti zinazolegea.”
Hata hivyo, naamini inampendeza Muumba wetu tunapojitahidi kutunza zawadi Yake ya ajabu ya mwili wa nyama na mifupa. Itakuwa ni alama ya uasi kwa mtu kuumbua au kuchafua mwili wake, au kuutumia vibaya, au kushindwa kufanya kile mtu anachoweza ili kufuata mtindo wa maisha yenye afya. Wakati huo huo, upuuzi na kushughulikia sana umbile la mtu, muonekano, au uvaaji vinaweza kuwa aina ya uasi kwa upande mwingine, na kusababisha mtu kuabudu zawadi aliyopewa na Mungu badala ya Mungu.
Mwishowe, kuzika silaha zetu za uasi dhidi ya Mungu kunamaanisha tu kuukubali ushawishi wa Roho Mtakatifu, kumvua mtu wa asili, na kuwa “mtakatifu kupitia upatanisho wa Kristo Bwana.” Hii humaanisha kuweka amri ya kwanza kuwa kwanza katika maisha yetu. Humaanisha kumuacha Mungu ashinde. Ikiwa upendo wetu kwa Mungu na uamuzi wetu wa kumtumikia kwa uwezo wetu wote, akili, na nguvu zetu zote vitakuwa kigezo ambacho kwacho tunapima vitu vyote na kufanya maamuzi yetu yote, tutakuwa tumezika silaha zetu za uasi. Kwa neema ya Kristo, Mungu atasamehe dhambi zetu na uasi wa zamani na ataondoa doa la dhambi hizo na uasi kutoka kwenye mioyo yetu. Baada ya muda, Yeye ataondoa hata tamaa yoyote ya uovu, kama alivyowafanyia wale Walamani waongofu wa zamani. Baada ya hapo, sisi pia “kamwe hatutaanguka.”
Kuzika silaha zetu za uasi kunaleta shangwe ya kipekee. Pamoja na wale wote ambao wamewahi kuongoka kwa Bwana, “tunaletwa kuimba [wimbo wa] upendo wa ukombozi.” Baba yetu wa Mbinguni na Mwanawe, Mkombozi wetu, wamethibitisha jukumu lao lisilo na mwisho la furaha yetu ya juu zaidi kupitia upendo na dhabihu ya kipekee. Tunapata uzoefu wa upendo wao kila siku. Hakika tunaweza kulipiza kwa upendo na uaminifu wetu wenyewe. Na tuzike—chini, chini kabisa—dalili yoyote ya uasi dhidi ya Mungu katika maisha yetu, tuibadilishe kwa moyo wa hiari na akili iliyo tayari. Katika jina la Yesu Kristo, amina.