Mkutano Mkuu
Kuunganishwa kwa Yesu Kristo: Kuwa Chumvi ya Dunia
Mkutano mkuu wa Oktoba 2024


10:49

Kuunganishwa kwa Yesu Kristo: Kuwa Chumvi ya Dunia

Kadiri tunavyobaki tumeunganishwa kwa Bwana, maisha yetu kwa asili yataakisi nuru Yake, na tutakuwa chumvi ya dunia.

Mwokozi alifundisha kwamba wakati “tunapokuwa tumeitwa kwenye injili [Yake] isiyo na mwisho, na kuahidi kwa agano lisilo na mwisho, [sisi] tunahesabika kama chumvi ya dunia.” Chumvi imetengenezwa kwa elementi mbili zilizounganishwa pamoja. Hatuwezi kuwa chumvi peke yetu; ikiwa tunataka kuwa chumvi ya dunia, lazima tuunganishwe kwa Mwokozi, na hilo ndilo ninaloliona ninapochangamana na waumini wa Kanisa ulimwenguni kote—ninawaona waumini waaminifu wa Kanisa waliounganishwa kwa Bwana, waliojitolea katika juhudi zao za kuwatumikia wengine na kuwa chumvi ya dunia.

Msimamo wako imara ni mfano unaong’ara. Huduma yako inatambulika na kuthaminiwa.

Vijana wetu wameonesha ujasiri mkubwa na kujitolea kwa dhati. Kwa ari wameikumbatia kazi ya historia ya familia, na matembezi yao ya mara kwa mara kwenye nyumba ya Bwana ni ushuhuda kwenye msimamo wao. Utayari wao kutenga muda na nguvu ili kuhudumu misheni kote ulimwenguni huakisi imani kubwa na ya kudumu. Hawashiriki tu bali wanaongoza njia katika kuwa wanafunzi waliounganishwa kwa Yesu Kristo. Huduma yao hunururisha nuru na tumaini, ikigusa maisha yasiyo na idadi. Kwenu ninyi, vijana wa Kanisa, tunatoa shukrani zetu za dhati kwa huduma yenu yenye mwongozo wa kiungu. Ninyi si tu kizazi kijacho cha Kanisa bali cha sasa. Na hakika ninyi ni chumvi ya dunia!

Ninampenda Bwana Yesu Kristo na ninahisi kubarikiwa kwa fursa ya kuhudumu sambamba na ninyi katika Kanisa la Bwana. Umoja na nguvu yetu, vilivyojikita katika imani yetu ya pamoja, hutuhakikishia kwamba kamwe hatuko peke yetu katika safari hii. Kwa pamoja, tunaweza kuendelea kuujenga ufalme wa Mungu ulio na mizizi katika huduma, upendo na imani isiyoyumba.

Wakati Yesu Kristo alipofundisha kando ya Bahari ya Galilaya, mara nyingi alitumia vitu vya kila siku vilivyojulikana kwa hadhira yake ili kufikisha kweli muhimu za kiroho. Moja ya vitu hivyo ilikuwa chumvi. Yesu alitamka, “[Ninyi] ni chumvi ya dunia,” kauli iliyojaa maana na umuhimu, hususani kwa watu wa wakati Wake ambao walielewa thamani anuai za chumvi.

Ujuzi wa kale wa uvunaji chumvi katika Algarve, mkoa wa kusini wa nchi yangu ya Ureno, unarudi hadi maelfu ya miaka kwenye kipindi cha Ufalme wa Kirumi. Kwa kasi ya ajabu, mbinu zilizotumiwa na wafanyakazi wa chumvi, waliojulikana kama marnotos, zimebadilika kidogo tangu wakati ule. Mafundi hawa waliojitolea kwa dhati hutumia mbinu ya kizamani, wakifanya kazi yao yote kwa mikono, wakiacha urithi ambao umedumu kwa karne nyingi.

Mbinu hii ya kale huvuna kile kinachoitwa “ua la chumvi.” Ili kuthamini kikamilifu mchakato mgumu wa kuvuna ua la chumvi, ni muhimu kujua mazingira ambayo kwayo ua la chumvi hutengenezwa. Mabwawa ya chumvi ya pwani ya Algarve hutoa mazingira rafiki kwa ajili ya uzalishaji wa chumvi. Maji ya bahari huchepushwa ndani ya mabwawa yenye kina kifupi yajulikanayo kama vikaangio vya chumvi, ambapo huachwa ili yakauke kwenye jua kali. Maji yanapokauka, ua la chumvi hutengeneza fuwele laini juu ya ardhi ya vikaangio vya chumvi. Fuwele hizi ni safi ajabu na zina umbile la kipekee, linaloweza kuvunjika. Hawa Marnotos kwa uangalifu huondoa fuwele kutoka uso wa maji kwa kutumia kifaa maalumu, mchakato unaohitaji ujuzi mkubwa na usahihi. Ureno, chumvi hii yenye kiwango kizuri inaitwa “krimu ya chumvi” kwa sababu inaweza kuondolewa taratibu kama vile krimu inayoinuka juu ya maziwa. Chumvi hii laini inathaminiwa kwa usafi wake na ladha ya kipekee, ikiifanya iwe kiungo cha thamani katika sanaa za upishi.

Kama vile marnotos wanavyoweka juhudi kubwa kuhakikisha wanavuna chumvi ya ubora wa hali ya juu, ndivyo ilivyo kwetu sisi, kama watu wa Bwana wa agano, daima tunafanya kwa uwezo wetu wote ili kwamba upendo na mfano wetu viwe, kadiri iwezekanavyo, taswira halisi ya Mwokozi wetu, Yesu Kristo.

Katika ulimwengu wa kale, chumvi ilikuwa zaidi ya kiungo—ilikuwa dawa ya kuzuia kuoza na ishara ya usafi na agano. Watu walijua kwamba chumvi ilikuwa muhimu kwa ajili ya kuhifadhi chakula na kuleta ladha. Pia walielewa madhara makubwa ya chumvi kupoteza uhalisia wake au ladha kwa kuharibiwa au kuchanganywa.

Kama vile chumvi inavyoweza kupoteza kiini chake, sisi pia tunaweza kupoteza uhai wa kiroho ikiwa imani yetu katika Yesu Kristo inakuwa ya kawaida. Tunaweza kuonekana vilevile kwa nje, lakini bila imani imara ya ndani, tunapoteza uwezo wetu wa kuleta tofauti ulimwenguni na kuleta utu bora zaidi kwa wale wanaotuzunguka.

Hivyo, tunawezaje kuelekeza nguvu na juhudi yetu ili kuleta tofauti na kuwa badiliko ambalo ulimwengu unalihitaji leo? Tunawezaje kutunza uanafunzi na kuendelea kuwa ushawishi chanya?

Maneno ya nabii wetu mpendwa bado yanatoa mwangwi mawazoni mwangu: “Mungu anatutaka tufanye kazi pamoja na tusaidiane. Hiyo ndiyo sababu ametutuma duniani katika familia na kutuweka kwenye kata na vigingi. Hiyo ndiyo sababu anatutaka tutumikiane na kuhudumiana. Hiyo ndiyo sababu Yeye anatutaka tuishi katika ulimwengu lakini tusiwe wa ulimwengu.”

Wakati maisha yetu yanapokuwa yamejawa na lengo na huduma, tunaepuka kutojali kiroho; kwa upande mwingine, wakati maisha yetu yanaponyimwa lengo la kiungu, huduma ya maana kwa wengine, na fursa takatifu za kutafakari na kuvuta taswira, polepole tunazongwa na shughuli zetu wenyewe na mapendeleo binafsi, tukiingia kwenye hatari ya kupoteza ladha yetu. Kinyume cha hili ni kuendelea kujishughulisha katika huduma—kujishughulisha kwa bidii katika kazi njema na kujiboresha sisi wenyewe na jamii tunayoishi nayo.

Kaka zangu na dada zangu wapendwa, ni baraka iliyoje sisi sote tuliyonayo leo kuwa wa Kanisa la Yesu Kristo na kuwa na fursa ya kuhudumu katika Kanisa Lake. Hali zetu zinaweza kutofautiana, lakini sote tunaweza kuleta tofauti.

Wakumbuke marnotos, wafanyakazi wa chumvi; wanatumia vifaa rahisi kuvuna fuwele bora zaidi, chumvi bora zaidi. Sisi pia tunaweza kufanya mambo rahisi ambayo, kwa juhudi endelevu katika matendo madogo madogo na yenye maana, yanaweza kukuza uanafunzi wetu na msimamo kwa Yesu Kristo. Hapa ni njia nne rahisi lakini zenye nguvu tunazoweza kujitahidi kuwa “chumvi ya dunia”:

  1. Kuiweka nyumba ya Bwana kuwa kiini cha kujitoa kwetu kwa dhati. Wakati huu ambapo mahekalu yapo karibu kuliko ilivyokuwa kabla, kuwekea kipaumbele kuabudu ndani ya nyumba ya Bwana kutatusaidia kufokasi kwenye kilicho muhimu zaidi na kuyakita maisha yetu katika Kristo. Ndani ya hekalu, tunapata umuhimu wa imani yetu katika Yesu Kristo na kiini cha kujitoa kwetu kwa dhati Kwake.

  2. Kuwa na kusudi katika juhudi zetu za kuwaimarisha wengine kwa kuishi injili pamoja. Tunaweza kuziimarisha familia zetu kupitia juhudi endelevu na za makusudi za kuleta kanuni za injili ndani ya maisha yetu na nyumba zetu.

  3. Kuwa radhi kukubali wito na kuhudumu katika Kanisa. Huduma katika mikusanyiko yetu huturuhusu kuungana mkono mmoja kwa mwingine na kukua pamoja. Wakati kuhudumu siyo daima rahisi, lakini daima huleta thawabu.

  4. Na mwisho, kutumia mawasiliano ya kidijitali kwa lengo. Leo, vifaa vya mawasiliano ya kidijitali huturuhusu tuunganike kuliko ilivyowahi kuwa hapo kabla. Kama vile wengi wenu, ninatumia vifaa hivi kuunganika na akina kaka na akina dada katika kanisa na familia na marafiki zangu. Ninapounganika nao, ninahisi kuwa karibu nao; tunaweza kuhudumiana katika nyakati za uhitaji ambapo hatuwezi kuwepo kimwili. Vifaa hivi bila shaka ni baraka, lakini bado vifaa hivi hivi vinaweza kutuvuta mbali kutoka kwenye kina cha michangamano yenye maana na hatimaye kutusababisha kuvutwa kwenye mazoea yanayopoteza muda wetu katika shughuli zisizo za maana. Kujitahidi kuwa chumvi ya dunia hujumuisha zaidi ya kupandisha mlolongo wa matukio kwenye skrini ya inchi 6 (sentimita 15).

Tunapoifanya nyumba ya Bwana kuwa kiini katika maisha yetu, kwa makusudi kuwaimarisha wengine kwa kuishi injili, kukubali miito ya kuhudumu, na kutumia vifaa vya kidijitali kwa lengo, tunaweza kuhifadhi uhai wetu wa kiroho. Kama vile chumvi katika hali yake ya usafi ilivyo na nguvu ya kuwezesha na kuhifadhi, ndivyo ilivyo imani yetu katika Yesu Kristo pale inapolishwa na kulindwa kwa kujitoa kwetu kwenye huduma na upendo kama wa Kristo.

Kadiri tunavyobaki tumeunganishwa kwa Bwana, maisha yetu kwa asili yataakisi nuru Yake, na tutakuwa chumvi ya dunia. Katika juhudi hii, si tu tunayaimarisha maisha yetu wenyewe bali pia kuziimarisha familia zetu na jumuiya zetu. Na tujitahidi kuendeleza muunganiko huu na Bwana na kamwe tusipoteze ladha yetu, na tuwe chembe ndogondogo za chumvi ambazo Bwana anatutaka tuwe. Katika jina la Yesu Kristo, amina.