Mkono Wake Uko Tayari Kutusaidia
Tunapomfikia Yesu Kristo kwa imani, Yeye anaweza kuwepo pale daima.
Nilipokuwa mtoto, kama familia tulienda likizoni kwenye ufuo wa pwani ya nchi yangu ya asili, Chile. Nilifurahi kutumia siku kadhaa kufurahia majira ya joto na familia yangu. Pia nilifurahishwa kwa sababu nilifikiri kwamba hatimaye ningeweza kujiunga na kufanya yale ambayo kaka zangu wawili wakubwa kwa kawaida walifanya ili kujifurahisha kwenye maji.
Siku moja kaka zangu walienda kucheza mahali ambapo mawimbi yalikuwa yakipiga, na nilijiona ni mzima na nimekomaa vya kutosha kuwafuata. Niliposogea kuelekea eneo hilo, niligundua mawimbi yalikuwa makubwa kuliko yale yaliyokuwa yakitokea ufukweni. Ghafla, wimbi lilinijia na kwa kasi na kunishtua. Nilihisi kama nguvu ya asili ilikuwa imenitawala, na nikaburutwa kwenye kilindi cha bahari. Sikuweza kuona au kuhisi sehemu yoyote nilipokuwa nikirushwa huku na huko. Nilipofikiri kwamba huenda safari yangu duniani inakaribia mwisho, nilihisi mkono ukinivuta kuelekea juu. Hatimaye, niliweza kuona jua na kuvuta pumzi yangu.
Ndugu yangu Claudio alikuwa ameona majaribio yangu ya kuwa mtu mzima na alikuja kuniokoa. Sikuwa mbali kutoka ufukweni. Ingawa maji yalikuwa ya kina kifupi, nilichanganyikiwa na sikugundua nisingeweza kujiokoa mwenyewe. Claudio aliniambia kwamba nilihitaji kuwa mwangalifu na, ikiwa nilitaka angeweza kunifundisha. Licha ya galoni za maji nilizokuwa nimemeza, kiburi changu na hamu ya kuwa mvulana mkubwa kilikuwa na nguvu zaidi, na nikasema, “Ni sawa.”
Claudio aliniambia nilihitaji kushambulia mawimbi. Nilijiambia mwenyewe hakika ningeshindwa vita dhidi ya kile kilichoonekana kuwa ukuta mkubwa wa maji.
Wimbi kubwa jipya lilipokaribia, Claudio alisema kwa haraka: “Niangalie; hivi ndivyo unavyofanya.” Claudio alikimbia kuelekea kwenye wimbi lililokuwa likija na kuingia ndani yake kabla halijaisha nguvu yake. Nilivutiwa sana na kupiga mbizi kwake huko kwamba nilipoteza mtazamo wa wimbi lililofuata. Kwa hiyo tena nilitupwa kwenye vilindi vya bahari na kurushwa na nguvu za asili. Sekunde chache baadaye, mkono ulinishika, na nikavutwa tena juu ya maji na hewa. Mwali wa kiburi changu ulikuwa unazimika.
Wakati huu, kaka yangu alinialika nipige mbizi pamoja naye. Kulingana na mwaliko wake, nilimfuata, tukaruka pamoja. Nilihisi kana kwamba ninashinda changamoto ngumu zaidi. Hakika, haikuwa rahisi sana, lakini nilifanya hivyo, shukrani kwa msaada na mfano ulioonyeshwa na ndugu yangu. Mkono wake uliniokoa mara mbili; mfano wake ulinionyesha jinsi ya kukabiliana na changamoto yangu na kuwa mshindi siku hiyo.
Rais Russell M. Nelson ametualika kufikiria selestia, na ninataka kufuata ushauri wake na kuutumia kwenye hadithi yangu ya majira ya jotoi.
Nguvu ya Mwokozi juu ya Adui
Ikiwa tunafikiri selestia, tutaelewa kwamba katika maisha yetu tutakabiliana na changamoto ambazo zinaonekana kuwa kubwa kuliko uwezo wetu wa kuzishinda. Katika maisha ya hapa duniani, tunakabiliwa na mashambulizi ya adui. Kama mawimbi ambayo yalikuwa na nguvu juu yangu siku hiyo ya kiangazi, tunaweza kuhisi kutokuwa na nguvu na kutaka kujiachia kwenye hatima yenye nguvu zaidi. Hayo “mawimbi mabaya” yanaweza kutuzonga kutoka upande hadi upande. Lakini usisahau ni nani aliye na uwezo juu ya mawimbi hayo, na kwa kweli, juu ya vitu vyote. Huyo ni Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Yeye ana uwezo wa kutusaidia kutoka katika kila hali mbaya au isiyofaa. Bila kujali kama tunahisi kuwa karibu Naye, bado anaweza kutufikia tulipo kama tulivyo.
Tunapomfikia kwa imani, atakuwepo daima, na kwa wakati Wake, atakuwa tayari na radhi kushika mikono yetu na kutuvuta hadi mahali salama.
Mwokozi na Mfano Wake wa Kuhudumu
Ikiwa tunafikiria selestia, tutamtambua Yesu Kristo kama mfano usio na dosari wa huduma. Kuna mpangilio kwa ajili yetu katika maandiko wakati Yeye au wanafunzi Wake wanamfikia mtu anayehitaji msaada, uokoaji, au baraka wanapomfikia kwa mikono yao. Kama katika hadithi yangu, nilijua kaka yangu alikuwapo, lakini kuwa pale kwa ajili yangu haikutosha. Claudio alijua niko taabani, na akaenda kunisaidia kuniinua kutoka kwenye maji.
Mara kwa mara, tunafikiri kwamba tunahitaji tu kuwa pale kwa ajili ya mtu mwenye uhitaji, na mara nyingi kuna mengi zaidi tunaweza kufanya. Kuwa na mtazamo wa milele kunaweza kutusaidia kupokea ufunuo ili kutoa usaidizi kwa wakati unaofaa kwa wengine wenye uhitaji. Tunaweza kutegemea mwongozo na maongozi ya Roho Mtakatifu ili kutambua ni aina gani ya usaidizi unaohitajika, iwe ni usaidizi wa muda kama vile faraja ya kihisia, chakula, au usaidizi wa kazi za kila siku, au mwongozo wa kiroho ili kuwasaidia wengine katika safari yao ya kujiandaa, kufanya na kuheshimu maagano matakatifu.
Mwokozi Yupo Tayari Kutuokoa
Wakati Petro, Mtume mkuu, “alipotembea juu ya maji, kumwendea Yesu … aliogopa; akaanza kuzama”; ndipo “akalia, akisema, Bwana, niokoe.” Yesu alijua imani ambayo Petro alikuwa ametumia kuja Kwake juu ya maji. Pia alifahamu hofu ya Petro. Kulingana na simulizi hiyo, Yesu “mara … akanyosha mkono wake, akamshika,” akisema maneno yafuatayo: “Ewe mwenye imani haba, kwa nini uliona shaka?” Maneno yake hayakuwa ya kumkemea Petro bali kumkumbusha kwamba Yeye, Masiya, alikuwa pamoja naye na wanafunzi.
Ikiwa tunafikiria selestia, tutapokea uthibitisho katika mioyo yetu kwamba Yesu Kristo kwa hakika ni Mwokozi wetu, Mtetezi wetu kwa Baba na Mkombozi wetu. Tunapotumia imani Kwake, Yeye atatuokoa kutoka kwa hali yetu ya kuanguka, zaidi ya changamoto zetu, udhaifu, na mahitaji yetu katika maisha haya ya muda, na kutupa zawadi kuu zaidi ya zote, ambayo ni uzima wa milele.
Mwokozi Hakati Tamaa Juu Yetu
Kaka yangu hakukata tamaa juu yangu siku hiyo bali aling’ang’ania ili niweze kujifunza jinsi ya kufanya mwenyewe. Aliendelea, hata kama hilo lilihitaji kuniokoa mara mbili. Aliendelea, hata kama sikuweza kufanya mwanzoni. Aliendelea ili niweze kushinda changamoto hiyo na kufanikiwa. Ikiwa tunafikiria selestia, tutatambua kwamba Mwokozi wetu atakuwa pale mara nyingi inavyohitajika ili kutoa msaada ikiwa tunataka kujifunza, kubadilika, kushinda, kukabiliana au kufanikiwa katika chochote kitakacholeta furaha ya kweli na ya milele katika maisha yetu.
Mikono ya Mwokozi
Maandiko hutoa ishara na umuhimu wa mikono ya Mwokozi. Katika dhabihu Yake ya upatanisho, mikono Yake ilitobolewa na misumari ili kumtundika msalabani. Baada ya Ufufuo Wake, aliwatokea wanafunzi Wake katika mwili mkamilifu, lakini alama katika mikono Yake zinabaki kama ukumbusho wa dhabihu Yake isiyo na kikomo. Mkono Wake utakuwa hapo kila wakati kwa ajili yetu, hata kama hatuwezi kuuona au kuuhisi mwanzoni, kwa sababu alichaguliwa na Baba yetu wa Mbinguni kuwa Mwokozi wetu, Mkombozi wa wanadamu wote.
Ikiwa ninafikiria selestia, najua kwamba hatujaachwa peke yetu katika maisha haya. Ingawa ni lazima tukabiliane na changamoto na majaribu, Baba yetu wa Mbinguni anajua uwezo wetu na anajua tunaweza kustahimili au kushinda matatizo yetu. Ni lazima tufanye sehemu yetu na kumgeukia kwa imani. Mwanawe Mpendwa, Yesu Kristo, ndiye mwokozi wetu na atakuwepo daima. Katika jina Lake, jina takatifu la Yesu Kristo, amina.