Mkutano Mkuu
Karibuni kwenye Kanisa lenye Shangwe
Mkutano mkuu wa Oktoba 2024


13:2

Karibuni kwenye Kanisa lenye Shangwe

Kwa sababu ya maisha ya ukombozi na misheni ya Mwokozi, Yesu Kristo, tunaweza—na tunapaswa—kuwa watu wenye shangwe kubwa sana duniani!

Nilibatizwa katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho katika Mkesha wa Krismasi ya mwaka 1987, karibu miaka 37 iliyopita. Hiyo ilikuwa ni siku nzuri sana katika maisha yangu na katika safari yangu ya milele, na nina shukrani nyingi sana kwa ajili ya marafiki walioandaa njia na kuniongoza kwenye maji ya kuzaliwa upya huko.

Iwe ubatizo wako umefanyika jana au miaka kadhaa iliyopita, iwe mnakutana kwenye jengo kubwa la Kanisa lenye kata nyingi au kwenye nyumba ya nyasi, iwe mnapokea sakramenti katika kumkumbuka Mwokozi kwa Kithai au Kiswahili, ningependa niwaambie, karibuni kwenye kanisa lenye shangwe! Karibuni kwenye Kanisa lenye Shangwe!

Kanisa lenye Shangwe

Kwa sababu ya mpango wa upendo wa Baba yetu wa Mbinguni kwa kila mmoja wa watoto Wake, na kwa sababu ya maisha ya ukombozi na misheni ya Mwokozi, Yesu Kristo, tunaweza—na tunapaswa—kuwa watu wenye shangwe kubwa sana duniani! Hata kama tufani za maisha katika ulimwengu wenye matatizo zikija juu yetu, tunaweza kukuza hisia inayoongezeka na ya kudumu ya shangwe na amani ya ndani kwa sababu ya tumaini letu katika Kristo na uelewa wetu wa sehemu yetu katika mpango mzuri wa furaha.

Mtume mkuu wa Bwana, Rais Russell M. Nelson, ameongea kuhusu shangwe inayotokana na maisha yaliyojikita kwa Yesu Kristo takribani katika kila hotuba aliyotoa tangu awe Rais wa Kanisa. Anahitimisha kwa uzuri sana: “Shangwe huja kutoka Kwake na kwa sababu Yake. … Kwa Watakatifu wa Siku za Mwisho, Yesu Kristo ni shangwe!”

Sisi ni waumini wa Kanisa la Yesu Kristo. Sisi ni waumini wa kanisa lenye shangwe! Na shangwe yetu inapaswa kuwa kubwa zaidi tunapokusanyika pamoja kila Sabato katika mikutano yetu ya sakramenti ili kumwabudu chanzo cha shangwe yote! Hapa tunakusanyika na familia za kata zetu na matawi ili kusherehekea sakramenti ya Chakula cha Mwisho cha Bwana, ukombozi wetu kutoka dhambini na kifo, na neema kuu ya Mwokozi! Tunakuja kupata shangwe, kimbilio, msamaha, kutoa shukrani na kuwa sehemu ya, vinavyopatikana kupitia Yesu Kristo!

Je, roho huyu wa pamoja wa shangwe katika Kristo ndiye kile mnachotafuta? Je, hiki ndicho mnachokileta? Labda unadhani hili halihusiani sana na wewe, au labda umezoea tu jinsi mambo yanavyofanywa siku zote. Lakini sote tunaweza kuchangia, bila kujali umri wetu au wito wetu, kuifanya mikutano yetu ya sakramenti iwe iliyojaa shangwe, yenye kufokasi kwa Kristo, yenye kukaribisha inavyowezekana, iliyojaa roho wa shangwe ya unyenyekevu.

Shangwe ya Unyenyekevu

Shangwe ya Unyenyekevu? “Je, hicho ni kitu?” unaweza kuuliza. Sawa, ndiyo, ni kitu! Kwa kina tunampenda, kumcha na kumheshimu Mungu, na staha yetu hutiririka kutoka kwenye nafsi ambayo hushangilia katika upendo mwingi wa Kristo rehema na wokovu! Shangwe hii ya staha kwa Bwana inapaswa kutawala mikutano yetu mitakatifu ya sakramenti.

Hata hivyo, kwa wengi, staha humaanisha hili: kukunja mikono yetu kwa nguvu kuzunguka vifua vyetu, kuinamisha vichwa vyetu, kufumba macho na kutulia—kusiko na mwisho Hii inaweza kuwa njia nzuri ya kuwafundisha watoto wenye nguvu nyingi, lakini kadiri tunavyokua na kujifunza, hebu tuone kwamba staha ni zaidi ya hili. Je, hivyo ndivyo jinsi tungekuwa kama Mwokozi angekuwa pamoja nasi? Hapana, kwani “mbele za uso [Wake] ziko furaha tele.”

Ndiyo, kwa wengi wetu badiliko hili katika ibada za sakramenti zitahitaji mazoezi.

Kuhudhuria dhidi ya Kuabudu

Hatukusanyiki kwenye Sabato ili tu kuhudhuria mkutano wa sakramenti na kuweka alama ya vema kwenye orodha ya mambo ya kufanya. Tunakuja pamoja ili kuabudu. Kuna tofauti yenye umuhimu kati ya haya mawili. Kuhudhuria inamaanisha kuwepo pale. Lakini kuabudu ni kwa makusudi kabisa kusifu na kumsujudia Mungu wetu katika njia ambayo hutubadilisha!

Kwenye Jukwaa na katika Mkusanyiko

Kama tunakusanyika kumkumbuka Mwokozi na kwa ukombozi alioufanya uwezekane, nyuso zetu zinapaswa ziakisi shangwe yetu na shukrani! Mzee F. Enzio Busche aliwahi kusimulia hadithi ya wakati alipokuwa rais wa tawi na kijana mdogo kwenye mkusanyiko alimwangalia kwenye jukwaa na kuuliza kwa sauti, “Mwanaume huyo mwenye uso katili anafanya nini hapo?” Wale wanaokaa kwenye jukwaa—wazungumzaji, viongozi, kwaya—na wale wanaokusanyika kwenye umati wanawasiliana hivi “karibu kwenye kanisa la shangwe” kupitia mwonekano wanaokuwa nao kwenye nyuso zao!

Kuimba Nyimbo za Dini

Tunapoimba, je, tunaungana pamoja kumsifu Mungu na Mfalme wetu, bila kujali kiwango cha sauti zetu, au tunamung’unya tu au hatuimbi kabisa? Maandiko yanasema kwamba wimbo wa mwenye haki ni sala kwa [Mungu] ambamo nafsi Yake hufurahia. Kwa hiyo, acha tuimbe! Na kumsifu Yeye!

Hotuba na Shuhuda

Tunakita hotuba na shuhuda zetu kwa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo na matunda ya kuishi kwa unyenyekevu injili Yao, matunda ambayo ni “matamu kupita yote yaliyo matamu.” Kisha kwa hakika “tutakula …mpaka hata [sisi] tushibe, kwamba [sisi] hatutapata njaa, wala … kiu,” na mizigo yetu itakuwa miepesi sana, kupitia kwa shangwe inayotokana na Mwana.

Sakramenti

Lengo tukufu la ibada zetu ni baraka na kupokea sakramenti yenyewe, mkate na maji vinavyowakilisha zawadi ya Bwana wetu ya kulipia dhambi na lengo zima la kukusanyika kwetu. Huu ni “muda mtakatifu wa kufanywa upya kiroho”, tunaposhuhudia upya kwamba tuko radhi kujichukulia juu yetu jina la Yesu Kristo na kufanya tena agano la daima kumkumbuka Mwokozi na kushika amri Zake.

Katika baadhi ya misimu ya maisha, tunaweza kuhudhuria sakramenti kwa mioyo iliyo mizito na mizigo inayotulemea. Wakati mwingine, tunakuja tukiwa huru na pasipo mzigo wa mambo ya kujali na matatizo. Tunaposikiliza kwa dhati kubarikiwa kwa mkate na maji na kushiriki ishara hizo takatifu, tunaweza kuhisi kutafakari juu ya dhabihu ya Mwokozi, masumbuko Yake huko Gethsemane, maumivu yake makali msalabani na huzuni na machungu aliyovumilia kwa niaba yetu. Hicho ndicho kitakuwa kitu kinachopoza nafsi zetu tunapounganisha maumivu yetu kwa Yake. Nyakati zingine, tutatamani kujiuliza kwa mshangao wenye shukrani ya heshima kuhusu huu uzuri na utamu wa zawadi tukufu ya Yesu ambayo imefanya iwezekane katika maisha yetu na milele yetu! Tutashangilia kwa ajili ya kile ambacho bado hakijafika—muunganiko wetu tunaouhifadhi kwa upendo mkubwa na Baba yetu mpendwa na Mwokozi mfufuka.

Yaweza kuwa tumezoeshwa kufikiri kwamba lengo la sakramenti ni kukaa kwenye viti na kufikiria tu kuhusu njia zote tulizokosea wakati wa wiki hii. Lakini acha tubadili mtindo huo. Kwa utulivu, tunaweza kutafakari njia nyingi tulizomwona Bwana pasipo kuchoka akitupigania kwa upendo Wake wa ajabu katika wiki hiyo! Tunaweza kutafakari katika kile inachomaanisha “kutambua shangwe ya toba ya kila siku.” Tunaweza kutoa shukrani kwa nyakati ambazo Mwokozi aliingilia mapambano na ushindi wetu na matukio ambayo tulihisi neema Yake, msamaha na uweza uliotupa nguvu ya kushinda magumu yetu na kubeba mizigo yetu kwa ustahimilivu na hata kwa furaha.

Ndio, tunatafakari mateso na udhalimu aliotendewa Mkombozi wetu kwa ajili ya dhambi zetu, na hilo husababisha tafakuri ya makini. Lakini wakati mwingine tunakwama hapo—kwenye bustani, msalabani, ndani ya kaburi. Tunashindwa kusonga kwenye shangwe ya kaburi kufunguka wazi, kushindwa kwa mauti na ushindi wa Kristo dhidi ya yote yanayoweza kutuzuia tusipate amani na kurejea kwenye makazi yetu ya mbinguni. Iwe tunatiririkwa na machozi ya huzuni au machozi ya furaha wakati wa sakramenti, acha iwe kwa heshima ya ajabu kwenye habari njema ya zawadi ya Baba ya Mwanawe!

Wazazi wenye Watoto Wadogo au Wenye Mahitaji Maalumu

Sasa, kwa wazazi wa watoto wadogo au wenye mahitaji maalumu, mara nyingi hakuna kitu kama muda wa utulivu na kutafakari kwa ukimya wakati wa sakramenti. Lakini katika nyakati fupi za wiki, unaweza kufundisha kwa mfano upendo, shukrani na shangwe unayohisi kwa ajili ya Mwokozi na itokayo Kwake kadiri kwa uendelevu unavyowatunza kondoo Wake wadogo. Hakuna juhudi yoyote inayopotea kwenye jukumu hili. Mungu anakujua sana.

Mabaraza ya Familia, Kata, na Tawi

Vivyo hivyo na nyumbani, tunaweza kuanza kuboresha matumaini na matarajio yetu kwa ajili ya muda wetu wa kanisani. Katika mabaraza ya familia, tunaweza kujadili jinsi kila mtu anavyoweza kuchangia katika njia bora za kuwakaribisha wote kwenye kanisa la shangwe! Tunaweza kupanga na kutarajia kuwa na uzoefu wenye shangwe kanisani.

Mabaraza ya kata na matawi yanaweza kutazamia na kutengeneza utamaduni wa shangwe yenye staha kwa ajili ya saa yetu ya sakramenti, yakibainisha hatua zinazotekelezeka na ishara zinazoonekana ili kusaidia.

Shangwe

Shangwe huonekana tofauti kwa watu tofauti. Kwa baadhi inaweza kuwa salamu za msisimko mlangoni. Kwa wengine, inaweza kuwa kuwasaidia watu kwa ukimya kuhisi vizuri kwa kutabasamu na kukaa karibu nao kwa moyo mwema na mkunjufu. Kwa wale wanaohisi kutengwa au kuwa pembeni, ukunjufu wa karibisho hili utakuwa muhimu. Hatimaye, tunaweza kujiuliza ni vipi Mwokozi angependelea saa yetu ya sakramenti iwe. Ni kwa jinsi gani angependelea kila mmoja wa watoto Wake wakaribishwe, kutunzwa, kulishwa na kupendwa? Je, Yeye angependa tuhisi nini pale tunapokuja kufanywa upya kupitia kumkumbuka na kumwabudu Yeye?

Hitimisho

Mwanzoni mwa safari yangu ya imani, shangwe katika Yesu Kristo ilikuwa ni uvumbuzi wangu wa kwanza mkubwa, na ilibadilisha ulimwengu wangu. Kama bado hujatambua shangwe hii, anza kuitafuta. Huu ni mwaliko wa kupokea zawadi ya Mwokozi ya amani, nuru na shangwe—kuifurahia, kuishangaa na kuishangilia, kila Sabato.

Amoni katika Kitabu cha Mormoni alitoa hisia za moyo wangu aliposema:

“Sasa si tunayo sababu ya kufurahi? Ndiyo, nasema kwenu, hakujakuwa na [watu] ambao walikuwa na sababu kubwa hivyo ya kufurahi kama sisi, tangu mwanzo wa dunia; ndiyo, na shangwe yangu imenichukua mbali, hata kwa majivuno kwa Mungu wangu; kwani ana uwezo wote, hekima yote, na akili yote; anaelewa vitu vyote, na ni Kiumbe cha huruma, hata kwenye wokovu, kwa wale ambao watatubu na kuamini kwa jina lake.

“Sasa kama hii ni kujivuna, na hata iwe hivyo nitajivuna; kwani haya ni maisha yangu na mwangaza wangu, … shangwe yangu na shukrani yangu nyingi.”

Karibuni kwenye kanisa lenye shangwe! Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Rais Russell M. Nelson alifundisha: “Furaha ina nguvu, na kufokasi juu ya ya shangwe huleta nguvu ya Mungu katika maisha yetu. “Jinsi ilivyo katika vitu vyote, Yesu Kristo ni mfano wetu wa mwisho, ‘ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba’ [Waebrania 12:2]. Fikiria hayo! Ili Yeye aweze kuvumilia uzoefu wa kuteseka uliowahi kuvumiliwa duniani, Mwokozi wetu alifokasi kwenye shangwe! Na nini ilikuwa furaha ambayo iliwekwa mbele Zake? Hakika inajumuisha shangwe ya kusafisha, kuponya, na kutuimarisha; shangwe ya kulipia dhambi za wote watakaotubu; shangwe ya kutuwezesha wewe na mimi kurudi nyumbani—safi na wenye kustahili—ili kuishi na Wazazi wetu wa Mbinguni na familia. Kama tunalenga katika furaha itakayokuja kwetu, au kwa wale tuwapendao, nini tunachoweza kuvumilia ambacho sasa kinaonekana kushindikana, kichungu, cha kutisha, kisicho haki, au haiwezekani?” (“Shangwe na Kunusurika Kiroho,” Liahona, Nov. 2016, 82-83).

  2. Zaburi 16:11.

  3. F. Enzio Busche, “Lessons from the Lamb of God,” Religious Educator 9, no. 2 (2008).

  4. Mafundisho na Maagano 25:12.

  5. Ona Zaburi 100:1.

  6. Alma 32:42

  7. Ona Alma 33:23.

  8. Kitabu cha Maelekezo ya Jumla: Kuhudumu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, 29.2.1.1, Maktaba ya Injili.

  9. Ona Russell M. Nelson, mission leadership seminar, June 2019;; imenukuliwa katika Dale G. Renlund, “Msimamo Usioyumba kwa Yesu Kristo,” Liahona, Nov. 2019, 25.

  10. Rais Gordon B. Hinckley alifundisha: “Wakati wewe, kama kuhani, unapopiga magoti kwenye meza ya sakramenti na kutoa sala, iliyotokana na ufunuo, unauweka umati wote kwenye agano na Bwana. Je, hili ni jambo dogo? Ni jambo muhimu na lisilo na kifani.( “The Aaronic Priesthood—a Gift from God,” Ensign, Mei 1988, 46.

    “Wale wanaoandaa, kubariki au kupitisha sakramenti wanahudumia ibada hii kwa wengine kwa niaba ya Bwana. Kila mmoja anayeshikilia ukuhani anapaswa kutekeleza jukumu hili kwa mtazamo mkunjufu, mtazamo wa staha. Anapaswa kuwa nadhifu, msafi, kuvaa vizuri. Mwonekano binafsi unapaswa kuakisi utakatifu wa ibada” (“Priesthood Ordinances and Blessings,” Family Guidebook [2006], 22).

  11. Alma 36:21

  12. Russell M. Nelson, “Nguvu ya Kasi ya Kiroho,” Liahona, Mei 2022, 98.

  13. Ona Mosia 24:13–15.

  14. Ona Yohana 3:16–17.

  15. Alma 26:35–37.