“Ninyi ni Marafiki Zangu”
Tangazo la Mwokozi “ninyi ni marafiki zangu” ni wito wa wazi wa kujenga mahusiano ya juu na matakatifu miongoni mwa watoto wote wa Mungu.
Katika ulimwengu uliojaa mabishano na mgawanyiko, wakati hukumu na dharau vimechukua sehemu ya mazungumzo safi, na urafiki kutambulika kupitia ubaguzi, nimekuja kujua kwamba kuna mfano wa wazi, rahisi na wa kiungu tunaoweza kuutazama kwa ajili ya umoja, upendo na kuwa sehemu ya. Mfano huo ni Yesu Kristo. Ninashuhudia kwamba Yeye ni muunganishi mkuu.
Sisi ni Rafiki Zake
Mnamo Desemba ya 1832, wakati “matatizo miongoni mwa nchi” yalikuwa “dhahiri zaidi” kuliko wakati wowote tangu kuanzishwa kwa Kanisa, viongozi wa Watakatifu wa Siku za Mwisho huko Kirtland, Ohio, walikusanyika kwa ajili ya mkutano. Walisali “mmoja mmoja na kwa sauti kwa Bwana ili afunue mapenzi yake [kwao].” Katika kutambua sala ya waumini hawa watakatifu katika nyakati za majaribu makali, Bwana aliwafariji, akizungumza kwa Watakatifu mara tatu kwa maneno mawili mazito: “marafiki zangu.”
Yesu Kristo tangu zamani amewaita wafuasi Wake waaminifu marafiki Zake. Mara kumi na nne katika Mafundisho na Maagano Mwokozi anatumia neno rafiki kuelezea uhusiano mtakatifu na wa kupendeza. Siongelei kuhusu neno rafiki kama ulimwengu unavyolifahamu—kumaanisha kuwa na wafuasi wa mitandao ya kijamii na “penda.” Hauwezi kutambuliwa katika tagi au nambari kwenye Instagram au X.
Ninakubali, kama kijana, nakumbuka mazungumzo ya hofu wakati niliposikia maneno ya kuumiza “Tunaweza kuwa marafiki tu?” au “Acha tu tubakie marafiki.” Hakuna kokote katika maandiko matakatifu tunamsikia akisema, “Ninyi ni marafiki zangu tu.” Badala yake, Yeye alitufundisha kwamba, “hakuna upendo mkuu zaidi kuliko upendo wa mtu atoaye uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.” Na “ninyi ndiyo wale ambao Baba amenipa; ninyi ni marafiki zangu.”
Hisia iko wazi: Mwokozi anatuhesabu kila mmoja wetu na kutulinda. Huu ulinzi wa utunzaji si haba au usio muhimu. Bali, ni wa kuinua, kukupeleka juu na wa milele. Ninaona tangazo la Mwokozi “ninyi ni marafiki zangu” kama wito wa wazi wa kujenga mahusiano ya juu na matakatifu miongoni mwa watoto wote wa Mungu “ili kwamba tuwe wamoja.” Tunafanya hili tunapokuja pamoja tukitafuta fursa za kuungana na hisia ya kuwa sehemu ya, kwa wote.
Tu Wamoja Kwake
Mwokozi kwa uzuri alionyesha hili kwenye wito Wake wa “njoo, unifuate.” Yeye alitumia vipawa na sifa binafsi za makundi mbalimbali ya wafuasi katika kuwaita Mitume Wake. Aliita wavuvi, wakereketwa wa dini, akina kaka waliojulikana kwa sifa zao kuu, na hata mkusanya kodi. Imani yao katika Mwokozi na hamu ya kusogea karibu Naye viliwaunganisha. Walimtegemea Yeye, wakamuona Mungu kupitia Yeye, na “wakaziacha nyavu zao mara moja, wakamfuata.”
Mimi pia nimeona jinsi ambavyo ujenzi wa mahusiano ya juu na matakatifu hutuleta pamoja. Mimi pamoja na mke wangu, Jennifer, tulibarikiwa kuwalea watoto wetu watano huko Jiji la New York. Huko katika jiji lenye mambo mengi, tulitengeneza mahusiano ya thamani na matatatifu pamoja na majirani, marafiki wa shuleni, wenza kibiashara, viongozi wa imani na Watakatifu wenza.
Mnamo Mei ya 2020, wakati ulimwengu ukipambana na kuenea kwa janga la ulimwengu, washiriki wa Tume ya Viongozi wa Kidini ya Jiji la New York walikutana mtandaoni katika mkutano ulioitishwa ghafla. Hapakuwa na ajenda. Hapakuwa na wageni rasmi. Ilikuwa ni ombi tu la kuja pamoja na kujadili changamoto tulizokuwa tunakabiliana nazo kama viongozi wa imani. Vituo vya Kuthibiti Magonjwa vilikuwa ndio vimeripoti kwamba jiji letu ndio kitovu cha UVIKO-19 nchini Marekani. Hii ilimaanisha hakuna tena kukusanyika. Hakuna tena kukutana.
Kwa viongozi hawa wa kidini, kuondoa huduma ya uchungaji, mkusanyiko wa watu na ibada za kila wiki ilikuwa ni jambo la kukatisha tamaa. Kundi letu dogo—ambalo lilijumuisha kadinali, pasta, mwalimu, imamu, mchungaji, kuhani na mzee—walisikiliza, walifariji na kusaidiana wao kwa wao. Badala ya kufokasi kwenye tofauti zetu, tuliona kile tulichokuwa nacho pamoja. Tuliongea kuhusu mambo yamkini na kisha uwezekano. Tuliungana na kujibu maswali kuhusu imani na mambo yajayo. Na kisha tulisali. Ee, tulisali kwa dhati sana.
Katika jiji lenye utofauti mwingi lililojaa mila tofauti na zinazopishana, tuliona tofauti zetu zikitoweka tulipokuja pamoja kama marafiki kwa sauti moja, lengo moja na sala moja.
Hatukuangaliana sisi kwa sisi lakini tuliangalia kuelekea mbinguni pamoja. Tulimaliza kila mkutano uliofuatia tukiwa tumeungana zaidi na tayari kuchukua “sepetu” zetu na kuingia kazini. Muunganiko uliotokea na huduma iliyotolewa kwa maelfu ya watu wa New York ilinifundisha kwamba kwenye ulimwengu wa mgawanyiko, umbali na kutokukubaliana, daima kuna mengi yanayotuunganisha kuliko yanayotutenganisha. Mwokozi alisihi, “Kuweni na umoja; na kama hamna umoja ninyi siyo wangu”
Akina kaka na dada, tunapaswa kuacha kutafuta sababu za kugawanyika na badala yake fursa za “kuwa wamoja.” Yeye ametubariki sisi kwa vipawa vya pekee na sifa ambazo hualika kujifunza kutoka kwa kila mmoja na ukuaji binafsi. Daima huwa nawaambia wanafunzi wangu wa chuo kikuu kwamba kama nikifanya kile wafanyacho na wao wakifanya kile nifanyacho, hatuhitajiani. Lakini kwa sababu hamfanyi nifanyacho na mimi sifanyi kile mfanyacho, tunahitajiana. Na hitaji hilo hutuleta pamoja. Kugawa na kutwaa ni mpango wa adui wa kuharibu urafiki, familia na imani. Ni Mwokozi anayeunganisha.
Sisi tu wa Kwake.
Mojawapo ya baraka ya ahadi ya “kuwa wamoja” ni hisia kubwa ya kuwa sehemu ya. Mzee Quentin L. Cook alifundisha kwamba “msingi wa kuwa sehemu ya, ni kuwa wamoja na Kristo.”
Kwenye matembezi ya hivi karibuni pamoja na familia yangu huko Ghana nchi ya Afrika Magharibi, nilipendezwa na mila za wazawa. Tulipokuwa tukifika kanisani au nyumbani, tulisalimiwa na maneno “unakaribishwa.” Wakati chakula kilipoandaliwa, mwenyeji wetu angetangaza, “Mnaalikwa.” Salamu hizi rahisi zilitolewa kwa lengo na kwa makusudi. Mnakaribishwa. Mnaalikwa.
Sisi huweka tangazo kama hilo tukufu katika milango yetu ya nyumba za ibada. Lakini alama Wageni Wanakaribishwa haitoshelezi. Je, tunawakaribisha kwa ukunjufu wote wapitao mlangoni? Akina kaka na akina dada, haitoshi tu kukaa kwenye mabenchi. Tunapaswa kuitikia wito wa Mwokozi wa kujenga mahusiano ya juu na matukufu pamoja na watoto wote wa Mungu. Lazima tuishi imani yetu! Baba yangu mara kwa mara alinikumbusha kwamba kukaa tu kwenye benchi siku ya Jumapili hakukufanyi uwe Mkristo mwema na bora kama ambavyo kulala gereji hukukufanyi uwe gari.
Tunapaswa kuishi maisha yetu ili kwamba ulimwengu usituone sisi lakini umuone Yeye kupitia sisi. Hii haifanyiki siku za Jumapili tu. Hufanyika dukani, kwenye kituo cha mafuta, kwenye mkutano wa shule, kwenye mkusanyiko wa majirani—sehemu zote ambazo washiriki waliobatizwa na ambao hawajabatizwa wa familia zetu hufanya kazi na kuishi.
Ninaabudu katika siku ya Jumapili kama ukumbusho kwamba tunahitajiana na kwa pamoja tunamhitaji Yeye. Vipawa vyetu vya pekee na talanta ambazo hututofautisha katika ulimwengu huu hutuunganisha katika sehemu takatifu. Mwokozi anatuita tusaidiane, tunyanyuane na tujengane. Hiki ndicho alichokifanya Yeye alipomponya mwanamke mwenye kuvuja damu, alipomtakasa mwenye ukoma aliyemsihi kwa ajili ya neema Yake, alipomshauri mwana mfalme aliyeuliza afanye nini zaidi, alipompenda Nikodemu ambaye alijua lakini akasita kwenye imani yake, na alipoketi na mwanamke kisimani kinyume na mila za wakati huo lakini kwa mwanamke huyo Yesu alimtangazia misheni yake ya kimasiya. Hii kwangu ndio kanisa—sehemu ya kukusanyika na kuponywa, kurekebisha na kufokasi upya. Kama Rais Nelson alvyofundisha: “Nyavu za injili ni nyavu kubwa sana ulimwenguni. Mungu amewaalika wote waje Kwake. … Kuna nafasi kwa ajili ya kila mmoja.”
Baadhi wanaweza kuwa na uzoefu uliowafanya kuhisi kutokuwa sehemu ya. Ujumbe wa Mwokozi kwako na mimi ni ule ule: “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.” Injili ya Yesu Kristo ni sehemu sahihi kwa ajili yetu. Kuja kanisani hutoa tumaini la siku njema, ahadi kwamba hauko peke yako, na familia inayotuhitaji sana kama tunavyowahitaji. Mzee D. Todd Christofferson anathibitisha kwamba “kuwa wamoja pamoja na Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu pasipo shaka ndio kilele cha kuwa sehemu ya.” Kwa yeyote aliyeondoka na anatafuta nafasi ya kurejea, ninatoa ukweli na mwaliko wa milele: Wewe ni wa sehemu hii. Rudi. Huu ndio wakati.
Katika ulimwengu wa migongano na uliogawanyika, ninashuhudia kwamba Mwokozi Yesu Kristo ni Muunganishi mkuu. Acha nimualike kila mmoja wetu kuwa wenye kustahili kwa ajili ya mwaliko wa Mwokozi wa “kuwa wamoja” na kwa ujasiri kutangaza, Yeye kama alivofanya, “Ninyi ni marafiki zangu.” Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.