Mkutano Mkuu
Upepo Haukuacha Kamwe Kuvuma
Mkutano mkuu wa Oktoba 2024


9:46

Upepo Haukuacha Kamwe Kuvuma

Tunaweza kuwasaidia wengine kusonga katika safari yao ili wapokee baraka za Mungu.

Mwaka 2015, katika jimbo la Pernambuco, Brazili, wanachama 62 wa Chama cha Sheria cha J. Reuben Clark walishirikiana na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali katika kuchunguza changamoto za kisheria za wakazi katika nyumba nne tofauti za uuguzi. Jumamosi moja, kwa saa tano, mawakili hawa waliwahoji zaidi ya wakazi 200, mmoja baada ya mwingine, ambao kila mmoja alikuwa kiuhalisia amesahaulika na jamii.

Wakati wa mahojiano yao, waligundua uhalifu kadhaa ambao ulikuwa umefanywa dhidi ya wakazi wazee kama vile kutelekezwa, kutendewa vibaya na mgao mbaya wa fedha. Nguzo muhimu ya chama hiki cha sheria ni kuwajali masikini na walio katika uhitaji. Miezi miwili tu baadaye, mwendesha mashtaka alifanikiwa kufungua mashtaka dhidi ya wahusika.

Msaada wao ni mfano mzuri wa mafundisho ya Mfalme Benjamini: “kwani tazama mnapowatumukia wanadamu wenzenu mnamtumikia tu Mungu wenu.”

Mkaazi mmoja niliyemhoji mimi binafsi wakati wa mradi wa huduma za wanasheria bila malipo alikuwa mwanamke wa miaka 93 mwenye moyo wa huruma aitwaye Lúcia. Akishukuru kwa huduma yetu, alisema kwa utani, “Nioe mimi!”

Kwa mshangao, nilijibu: “Angalia kule kwa yule msichana mrembo! Yule ni mke wangu na mwendesha mashtaka wa serikali.”

Kwa haraka alijibu: “Kwa hiyo? Yeye ni kijana, mrembo na anaweza kuolewa tena kwa urahisi. Yote niliyo nayo ni wewe!”

Wakazi wale wazuri hawakuweza kutatuliwa matatizo yao yote siku hiyo. Bila shaka waliendelea kupata shida mara kwa mara kama Wayaredi katika mashua zao katika safari ngumu ya nchi ya ahadi, “walizikwa katika vilindi vya bahari, kwa sababu ya milima ya mawimbi ambayo yaliwapiga.”

Lakini Jumamosi hiyo, wakazi wa nyumba ya uuguzi walijua kwamba bila kujali kutokujulikana kwao duniani, walijulikana kibinafsi na Baba wa Mbinguni mwenye upendo, Mmoja ambaye hujibu hata sala rahisi zaidi.

Bwana wa mabwana alisababisha “upepo mkali” ili kuwasukuma Wayaredi kuelekea baraka zilizoahidiwa. Vivyo hivyo tunaweza kuamua kutumika kama upepo mwanana katika mikono ya Bwana. Kama vile “upepo haukuacha kamwe kuvuma” kwa Wayaredi kuelekea nchi ya ahadi, tunaweza kuwasaidia wengine kuendelea katika safari yao ya kupokea baraka za Mungu.

Miaka kadhaa iliyopita, wakati Chris, mke wangu mpendwa, na mimi tulipofanyiwa usaili kwa ajili ya wito wangu kama askofu, rais wetu wa kigingi aliniomba nisali ili kufikiria majina ya kupendekeza kama washauri. Baada ya kusikia majina niliyopendekeza, alisema ninapaswa kujua mambo machache kuhusu mmoja wa ndugu hawa.

Kwanza, huyu kaka hawezi kusoma. Pili, hakuwa na gari analoweza kutumia kuwatembelea waumini. Tatu, yeye daima—kila wakati—alitumia miwani ya jua kanisani. Licha ya wasiwasi wa dhati wa rais, nilihisi kwa nguvu kwamba bado ninapaswa kumpendekeza kama mshauri wangu na rais wa kigingi aliniunga mkono.

Jumapili ambayo mimi na washauri wangu tulikubaliwa katika mkutano wa sakramenti, mshangao kwenye nyuso za waumini ulikuwa dhahiri. Ndugu huyu mpendwa polepole alielekea kwenye jukwaa, ambapo mwanga wa taa za juu ulimulika kwenye miwani yake ya jua.

Alipoketi kando yangu, nilimuuliza, “Ndugu, una matatizo ya kuona?”

“Hapana,” alisema.

Basi kwa nini unatumia miwani ya jua kanisani?” Niliuliza. “Rafiki yangu, waumini wanahitaji kuona macho yako, na lazima uweze kuwaona vizuri pia.”

Wakati huo huo, alitoa miwani yake ya jua na kamwe hakuitumia tena kanisani.

Ndugu huyu mpendwa alihudumu na mimi hadi nilipopumzishwa kama askofu. Leo, anaendelea kuhudumu kwa uaminifu katika Kanisa na ni mfano wa kujitolea kwa dhati na kujituma kwa Bwana Yesu Kristo. Na bado, miaka kadhaa iliyopita, alikuwa mtu asiyejulikana aliyevaa miwani ya jua aliyekaa kimsingi akisahaulika katika benchi kanisani. Mara nyingi najiuliza, ni ndugu wangapi waaminifu wanaokaa wamesahaulika miongoni mwetu leo?

Iwe tunajulikana au tumesahaulika, majaribu yatakuja kwa kila mmoja wetu. Tunapomgeukia Mwokozi, Yeye anaweza “kuweka wakfu mateso [yetu] kwa faida [yetu]” na kutusaidia kujibu majaribu yetu kwa njia inayowezesha maendeleo yetu ya kiroho. Iwe kwa wakazi wa nyumba za uuguzi, mshiriki wa Kanisa aliyehukumiwa vibaya, au mtu mwingine yeyote, tunaweza kuwa “upepo [ambao] haukukoma kuvuma,” ukileta tumaini na kuwaongoza wengine kwenye njia ya agano.

Nabii wetu mpendwa, Rais Russell M. Nelson, alitoa mwaliko wa kusisimua na wa kutia moyo kwa vijana: “Ninawahakikisha kwa dhati kwamba Bwana ameamuru kila mvulana anayestahili, na mwenye uwezo ajiandae kwa ajili ya kutumikia misheni. Kwa wavulana Watakatifu wa Siku za Mwisho, huduma ya kimisionari ni jukumu la kikuhani. … Kwenu ninyi akina dada wenye uwezo, misheni pia ni kitu chenye nguvu, lakini ni, fursa, ya hiari.”

Kila siku, maelfu ya vijana wanaume na wanawake huitikia wito wa kinabii wa Bwana kwa kuhudumu kama wamisionari. Ninyi mna akili sana, na kama Rais Nelson alivyosema, mnaweza “kuwa na matokeo mazuri zaidi kwa ulimwengu kuliko kizazi chochote kilichopita!” Bila shaka, hiyo haimaanishi kuwa utakuwa toleo bora zaidi la wewe mwenyewe wakati ule unapokanyaga katika kituo cha mafunzo ya umisionari.

Badala yake, unaweza kuhisi kama Nefi, “ukiongozwa na Roho, wala usijue mapema vitu ambavyo [wewe] ungefanya. Hata hivyo [wewe] ulisonga mbele.”

Labda unahisi kutokuwa salama kama Yeremia alivyokuwa na unataka kusema, “Siwezi kusema: kwa maana mimi ni mtoto.”

Unaweza hata kuona mapungufu yako binafsi na unataka kulia kama Musa alivyofanya: “Ee Bwana, mimi si msemaji … : maana mimi si mwepesi wa kusema, na ulimi wangu ni mzito.”

Ikiwa yeyote kati yenu wapendwa vijana wa kiume na wa kike wenye nguvu ana mawazo kama haya hivi sasa, kumbuka kwamba Bwana amejibu, “Usiseme, mimi ni mtoto: maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake.” Na Yeye anaahidi, “Basi nenda, mimi nitakiongoza kinywa chako, na kukufundisha nini cha kusema.”

Mabadiliko yako kutoka nafsi yako ya asili hadi ya kiroho yatatokea “mstari juu ya mstari, amri juu ya amri” unapojitahidi kwa bidii kumtumikia Yesu Kristo katika misheni kupitia toba ya kila siku, imani, utii kamili, na bidii kwenye kazi ili “kutafuta daima, kufundisha toba, na kubatiza waongofu.”

Ingawa unavaa beji ya jina, wakati mwingine unaweza kuhisi kutotambuliwa au kusahaulika. Hata hivyo, lazima ujue kwamba unaye Baba wa Mbinguni aliye mkamilifu, ambaye anakujua wewe binafsi, na Mwokozi, anayekupenda. Utakuwa na viongozi wa misioni ambao, licha ya mapungufu yao, watakutumikia kama ule “upepo [ambao] haukukoma kuvuma” katika kukuongoza katika safari yako ya uongofu binafsi.

Katika “nchi imiminikayo maziwa na asali” utahudumu humo misheni yako, utazaliwa upya kiroho na kuwa mwanafunzi wa maisha yote wa Yesu Kristo unapomkaribia Yeye. Unaweza kuja kujua kwamba haujasahaulika.

Japokuwa baadhi wanaweza kusubiri “siku nyingi” kwa ajili ya ahueni, kwa sababu “hawana mtu” ambaye anaweza kusaidia, Bwana Yesu Kristo ametufundisha kwamba Kwake hakuna mtu anayesahaulika. Kinyume chake, Yeye alikuwa mfano mzuri wa kumtafuta yule mmoja katika kila wakati wa huduma Yake ya duniani.

Kila mmoja wetu—na wale wanaotuzunguka—tunakabiliwa na dhoruba zetu za upinzani na mawimbi ya majaribio ambayo yanatuzamisha kila siku. Lakini “upepo [hautakoma] kuvuma kuelekea nchi ya ahadi … ; na hivyo [tutasukumwa] mbele na upepo.”

Kila mmoja wetu anaweza kuwa sehemu ya upepo huu—upepo ule ule ambao uliwabariki Wayaredi katika safari yao na upepo ule ule ambao, kwa msaada wetu, utabariki wasiotambuliwa na waliosahaulika kufikia nchi zao wenyewe za ahadi.

Ninashuhudia kwamba Yesu Kristo ndiye mwombezi wetu kwa Baba. Yeye ni Mungu aliye hai na anatenda kama upepo mkali ambao daima utatuongoza kwenye njia ya agano. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Chama cha Wanasheria cha J. Reuben Clark ni chama kisicho cha faida kilichoundwa na wanasheria na wanafunzi wa sheria na kupangwa katika sura zaidi ya 100 ulimwenguni. Kiliitwa kwa heshima ya Joshua Reuben Clark Jr., ambaye alihudumu kwa miaka mingi kama mshauri katika Urais wa Kwanza wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

  2. Mosia 2:17.

  3. Pro bono ni aina iliyopunguzwa ya maneno katika Kilatini pro bono publico, ambayo inamaanisha “kwa manufaa ya umma” au “kwa faida ya umma.” Hii ni aina ya kazi ya hiari ambayo, tofauti na kujitolea kwa jadi, inahitaji sifa za kitaaluma, ingawa hakuna malipo.

  4. Etheri 6:6.

  5. Etheri 6:5.

  6. Ona 2 Nefi 2:14, 16.

  7. Etheri 6:8.

  8. Ona Mafundisho na Maagano 84:106.

  9. Ona Ibrahimu 3:25.

  10. 2 Nefi 2:2; ona pia Mafundisho na Maagano 122:7.

  11. Russell M. Nelson, “Kuhubiri Injili ya Amani,” Liahona, Mei 2022, 6.

  12. Russell M. Nelson, “Hope of Israel” (worldwide youth devotional, June 3, 2018), Gospel Library.

  13. 1 Nefi 4:6–7.

  14. Yeremia 1:6.

  15. Kutoka 4:10.

  16. Yeremia 1:7.

  17. Kutoka 4:12.

  18. Ona Mosia 3:19.

  19. 2 Nefi 28:30.

  20. Ona Alma 26:22.

  21. Neil L. Andersen, “The Faith to Find and Baptize Converts” (address given at the seminar for new mission presidents, June 25, 2016), 6.

  22. Ona Kumbukumbu la Torati 11:8–9.

  23. Ona “Becoming Lifelong Disciples of Jesus Christ,” Preach My Gospel: A Guide to Sharing the Gospel of Jesus Christ (2023), 76–100.

  24. Yohana 5:6–7.

  25. Ona Luka 10:29.

  26. Etheri 6:8.

  27. Rais Dallin H. Oaks alitaja picha ya mchoro iliyochorwa na Maynard Dixon iliyopewa jina la Mtu Aliyesahaulika, inayoning’inia katika ofisi yake katika Jengo la Kanisa la Utawala katika Jiji la Salt Lake: “Unaona jua linamulika juu ya kichwa chake. Baba yake wa mbinguni anajua kuwa yuko huko. Anasahauliwa na umati unaopita, lakini katika mapambano yake, Baba yake wa Mbinguni anajua yuko pale. Nimekuwa na picha hii kwa karibu miaka 40, na inazungumza nami na inanikumbusha mambo ambayo ninahitaji kukumbuka” (in Sarah Jane Weaver, “What I Learned from President Oaks about the ‘Forgotten Man,’” Church News, Sept. 18, 2022, thechurchnews.com).