Mkutano Mkuu
Utakatifu kwa Bwana katika Maisha ya Kila Siku
Mkutano mkuu wa Oktoba 2024


14:17

Utakatifu kwa Bwana katika Maisha ya Kila Siku

Utakatifu kwa Bwana hufanya maisha yetu ya kila siku kuwa matakatifu. Unatuvuta sisi karibu zaidi na kuwa na furaha zaidi kwa Bwana na kila mmoja.

Kukutana tena kwa familia yote ya Gong hivi karibuni kulijumuisha burudani ya maonyesho ya vipaji na kukamilishwa na mashindano ya utani wa baba.

Lakini mashindano haya hayakuwa ya kawaida. Kwenye timu moja alikuwepo Babu (mimi) na wajukuu wawili, miaka 12 na 11. Kwenye timu nyingine ilikuwa programu ya akili mnemba (AI) ikiendeshwa na binamu kufanya utani wa baba katika mtindo wa Gerrit W. Gong. Babu Gerrit Gong dhidi ya akili mnemba ya Gerrit Gong.

Mimi na Wajukuu tulianza.

Je, unamwitaje dinosau anayegongesha gari yake? Migongano ya Dinosau.

Akili mnemba ya Gerrit Gong ilielekezwa—fikiri kama Gerrit W. Gong. Zungumza kama yeye.

Akili mnemba ya Gerrit Gong:—“Hapa kuna utani wa baba kama ulivyosemwa na Gerrit W. Gong, akikumbatia mtindo wake wenye upendo, kujali na kuinua: Kwa nini mti huu mkunjufu unawafanya watu watabasamu? Kwa sababu umekuzwa katika upendo na kuchanua kwa matawi yenye ukarimu. Kama mti ule, sisi pia tunaweza kupata nguvu katika mizizi yetu na shangwe katika kusambaza ukarimu kwa wengine.”

Vyema, wewe unafikiria nini? Na hiyo ndiyo sababu ya kuitwa utani wa baba.

Kote kutuzunguka sisi kuna fursa za kucheka, kufurahia, kuona kwa macho ya shukrani. Yetu ni injili ya shangwe na utakatifu kila siku ya maisha. Utakatifu hubainisha vitu kwa ajili ya dhumuni takatifu. Lakini utakatifu pia unatualika sisi kujaza maisha ya kila siku kwa utakatifu—kushangilia katika mkate wa kila siku katikati ya mibaruti na miiba ya ulimwengu. Ili kutembea na Bwana, lazima tuwe watakatifu, kwani Yeye ni mtakatifu; na ili kutusaidia sisi kuwa watakatifu, Bwana anatualika kutembea pamoja na Yeye.

Kila mmoja wetu anayo hadithi. Mimi na Dada Gong tunapokutana nanyi—waumini na marafiki wa Kanisa katika sehemu na hali nyingi—hadithi zenu za utakatifu kwa Bwana katika maisha ya kila siku zinatusisimua. Mnaziishi K saba: kushirikiana na Mungu, kushiriakiana na jumuiya na kuhurumiana sisi kwa sisi, kuwa na dhamira kuagana na Mungu, familia na marafiki—kuwa na kiini katika Yesu Kristo.

Ushahidi unaoongezeka unaangazia ukweli huu wa kushangaza: Waaminio katika dini kwa wastani wanayo furaha, wana afya, na wameridhika zaidi kuliko wale wasio na msimamo au muunganiko wa kiroho. Furaha na kuridhika kimaisha, afya ya akili na kimwili, maana na dhumuni, tabia na wema, uhusiano wa karibu wa kijamii, hata uthabiti wa kifedha na rasilimali—kwenye kila nyanja, washika dini wanastawi.

Wanafurahia afya bora ya kimwili na kiakili na uridhikaji mkubwa zaidi katika maisha katika umri wote na makundi yote ya kijamii.

Kile watafiti wanachokiita “uthabiti wa muundo wa kidini” hutoa ufasaha, dhumuni na mwongozo wa kiungu katikati ya matatizo na mabadiliko ya maisha. Kaya ya watu wa imani na jumuiya ya Watakatifu zinaepukana na kutengwa na kuepuka umati mpweke. Utakatifu kwa Bwana unasema “hapana” kwenye lugha chafu, “hapana” kwenye ujanja wenye hila za kuhujumu wengine, “hapana” kwenye mambo ambayo huzalisha hasira na ubaguzi. Utakatifu kwa Bwana unasema “ndiyo” kwenye utakatifu na staha, “ndiyo” kwenye kuwa kwetu huru zaidi, wenye furaha zaidi, wakweli zaidi, toleo letu bora zaidi tunapomfuata Yeye katika imani.

Je, utakatifu kwa Bwana katika maisha ya kila siku unaonekanaje?

Utakatifu kwa Bwana katika maisha ya kila siku unaonekana kama vijana wawili wakubwa, waliooana kwa kipindi cha mwaka mmoja, wakishirikiana pasipo unafiki kuishi maagano ya injili, dhabihu na huduma katika maisha yao mapya.

Mke anaanza, “katika shule ya upili, nilikuwa mahali pa giza. Nilihisi kama Mungu hakuwepo kwa ajili yangu. Usiku mmoja, ujumbe wa maandishi kutoka kwa rafiki ulisema, ‘Habari umewahi kusoma Alma 36?’

“Nilipoanza kusoma,” mke anasema “nilizidiwa na amani na upendo. Nilihisi nilikuwa ninapewa kumbatio hili kubwa. Niliposoma Alma 36:12, nilijua Baba wa Mbinguni aliniona mimi na alijua kabisa jinsi gani nilivyokuwa ninahisi.”

Mke anaendelea, “Kabla ya sisi kuoana, nilikuwa muwazi kwa mchumba wangu kwamba sikuwa na ushuhuda mkubwa juu ya zaka. Kwa nini Mungu alihitaji sisi tutoe fedha wakati wengine walikuwa na vingi vya kutoa? Mchumba wangu alinisaidia kuelezea kwamba hiyo siyo kuhusu fedha bali kufuata amri ambazo tumetakiwa tutii. Alinipa changamoto ya kuanza kulipa zaka.

“Hakika niliona ushuhuda wangu ukikua,” mke anasema. “Wakati mwingine fedha inakuwa haitoshi, lakini tuliona baraka nyingi na kwa namna fulani mapato yetu yalikuwa yanatosheleza.”

Pia, “katika darasa langu la uuguzi,” anasema “nilikuwa muumini pekee wa Kanisa na mtu pekee aliyeolewa. Mara nyingi niliondoka darasani nikiwa nimekasirika au ninalia kwa sababu nilihisi kama wanafunzi wenzangu walinitenga na walitoa maoni hasi kuhusu imani yangu, kuvaa kwangu gamenti au kuolewa kwangu nikiwa kijana sana.

Lakini anaendelea kusema “Muhula huu uliopita nilikuja kujua namna bora ya kutetea imani yangu na kuwa mfano mzuri wa injili. Ufahamu na ushuhuda wangu ulikua kwa sababu nilijaribiwa katika uwezo wangu wa kusimama peke yangu na kuwa imara katika kitu ninachokiamini.”

Mume kijana anaongeza, “Kabla ya misheni yangu nilipata ofa ya kucheza besiboli chuoni. Ili kufanya uamuzi huu mgumu, niliweka kando ofa hizo na kwenda kumtumikia Bwana. Nisingeweza kubadilisha miaka hiyo miwili na kitu kingine chochote.

“Niliporudi nyumbani,” anasema “nilitarajia kipindi kigumu cha mpito lakini nilijikuta nikiwa imara zaidi, mwepesi na mwenye afya zaidi. Nilikuwa nikirusha mipira vyema zaidi kuliko wakati nilipoondoka. Nilipata ofa nyingi zaidi za kucheza kuliko wakati nilipoondoka, ikijumuisha shule ya ndoto yangu. Na, cha muhimu zaidi,” anasema “ninamtegemea Bwana zaidi kuliko nilivyowahi kuwa.”

Mume anahitimisha, “Kama mmisionari nilifundisha kwamba Baba wa Mbinguni anatuahidi uwezo katika sala zetu, lakini nyakati zingine ninasahau hilo kwa ajili yangu mwenyewe.”

Hazina yetu ya baraka za utakatifu wa umisionari kwa Bwana ni nyingi na zimejaa. Fedha, muda na hali nyinginezo mara kwa mara siyo rahisi. Lakini wakati wamisionari wa umri wote na asili yoyote wanapoweka wakfu utakatifu kwa Bwana, mambo yanaweza kufanyika katika wakati na njia ya Bwana.

Sasa akiwa na matarajio ya miaka 48, mmisionari mwandamizi anashiriki, “Baba yangu alitaka mimi nipate elimu ya chuo, na sio kwenda misioni. Muda mfupi baada ya hilo, alipata mshtuko wa moyo na akafariki dunia akiwa na umri wa miaka 47. Nilihisi hatia. Je, ningewezaje kuweka mambo sawa na baba yangu?

“Baadaye,” anaendelea “baada ya kutumikia misheni, nilimwona baba yangu katika ndoto. Kwa amani kabisa na aliyeridhika, alikuwa na furaha kwamba nimeweza kutumikia.”

Mmisionari huyu mwandamizi anaendelea, “Kama Mafundisho na Maagano 138 inavyofundisha, ninaamini baba yangu angeweza kutumikia kama mmisionari katika ulimwengu wa roho. Niliona kama baba yangu akimsaidia baba wa babu yangu, ambaye aliondoka Ujerumani akiwa na miaka 17 na alikuwa amepoteana na familia, na akapatikana tena.”

Mke wake anaongeza, “Miongoni mwa kaka watano katika familia ya mume wangu, wale wanne ambao walitumikia misheni ndio wale walio na shahada za vyuo vikuu.”

Utakatifu kwa Bwana katika maisha ya kila siku, unaonekana kama kijana anayerudi kutoka misheni ambaye alijifunza kuacha Mungu ashinde katika maisha yake. Mapema, alipoombwa kumbariki mtu aliyekuwa mgonjwa sana, mmisionari huyu alisema, “Ninayo imani; nitambariki apate ahueni. Lakini tena,” yule mmisionari anasema, “nilijifunza katika wakati huo kusali siyo kwa ajili ya kitu ninachotaka, bali kwa ajili ya kitu Bwana anachojua mtu yule anahitaji. Nilimbariki kaka yule kwa amani na faraja. Baadaye mtu yule alifariki dunia kwa amani.”

Utakatifu kwa Bwana katika maisha ya kila siku unasikika kama cheche inayowaka kutoka upande mmoja hadi mwingine wa pazia ili kuunganisha, kufariji, kuimarisha. Msimamizi kwenye chuo kikuu kimoja anasema anahisi watu anaowajua tu kwa heshima ndio wanaosali kwa ajili yake. Watu hao binafsi walijitolea maisha yao kwenye chuo na waliendelea kujali misheni ya chuo na wanafunzi wake.

Dada mmoja anafanya kila awezalo kila siku, baada ya mumewe kumwacha yeye na watoto. Ninampenda kwa dhati na wengine kama yeye. Siku moja wakati akikunja nguo zilizofuliwa, mkono wake ukiwa juu ya rundo la nguo, alishusha pumzi, “Ya nini yote haya?” Alihisi sauti nyororo ikimhakikishia, “Maagano yako yapo na mimi.”

Kwa miaka 50, dada mwingine alitamani uhusiano na baba yake. “Wakati nakua,” alisema, “kulikuwa na kaka zangu na baba yangu, na kisha kulikuwa na mimi—binti wa pekee. Yote niliyowahi kutaka ni kuwa “mwema kwa baba yangu.

“Kisha, mama yangu akafariki dunia! Yeye alikuwa kiungo cha pekee kati yangu na baba yangu.

“Siku moja,” dada huyo anasema “nilisikia sauti ikisema, ‘mwalike baba yako na uende naye hekaluni.’ Huo ukawa mwanzo wa miadi ya siku mbili kwa mwezi pamoja na baba yangu kwenye nyumba ya Bwana. Nilimwambia baba yangu kuwa ninampenda. Naye aliniambia kuwa ananipenda pia.

“Kutumia muda katika nyumba ya Bwana kumetuponya. Mama yangu asingeweza kutusaidia sisi huku duniani. Ilimchukua yeye kuwa upande mwingine wa pazia ili kurekebisha kile kilichovunjika. Hekalu lilikamilisha safari yetu ya uponyaji kama familia ya milele.”

Baba anasema, “Uwekaji wakfu wa hekalu lilikuwa tukio kuu la kiroho kwangu mimi na binti yangu wa pekee. Sasa tunahudhuria pamoja na kuhisi upendo wetu ukiimarishwa.

Utakatifu kwa Bwana katika maisha yetu ya kila siku unajumuisha nyakati nyororo pale wapendwa wetu wanapofariki dunia. Mapema mwaka huu, mpendwa mama yangu, Jean Gong, alifariki siku kadhaa kabla ya kumbukizi ya siku yake ya 98 ya kuzaliwa.

Kama ungemwuliza mama yangu, “Ungependa rocky road, chokoleti ya tangawizi nyeupe au aiskrimu ya stroberi?” Mama angesema, “Ndiyo, tafadhali, naweza kuonja kila moja?” Nani angeweza kusema “hapana” kwa mama yako, hususani pale anapopenda ladha zote za maisha?

Siku moja nilimwuliza Mama ni maamuzi gani yamechonga maisha yake zaidi.

Alisema, “Kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho na kuhama kutoka Hawaii kuja bara, mahali ambapo nilikutana na baba yako.”

Alibatizwa alipokuwa na umri wa miaka 15, muumini pekee katika familia yake kubwa kujiunga na Kanisa letu, mama yangu alikuwa na imani ya maagano na alitumainia katika Bwana ambaye aliyabariki maisha yake na vizazi vyote vya familia yetu. Ninamkumbuka mama yangu, kama unavyowakumbuka washiriki wa familia yako. Lakini ninajua mama yangu hajapotea. Ni kwamba tu hayupo hapa sasa. Ninamheshimu yeye na wote wanaofariki kama mifano iliyo jasiri ya utakatifu wa kila siku kwa Bwana.

Bila shaka, utakatifu kwa Bwana katika maisha ya kila siku unajumuisha kuja mara kwa mara zaidi kwa Bwana katika nyumba Yake takatifu. Hii ni kweli, iwe sisi ni waumini wa Kanisa au marafiki.

Marafiki watatu walikuja kwenye ziara ya kuzuru Hekalu la Bangkok Thailand.

“Hapa ni mahali pa uponyaji mkuu,” alisema mmoja wao.

Katika kisima cha ubatizo, mwingine alisema, “Niwapo hapa, nataka nioshwe niwe safi, na nisitende dhambi tena.”

Wa tatu alisema, “Je, unaweza kuhisi nguvu za kiroho?”

Kwa maneno sita matakatifu, mahekalu yetu yanatualika na kututangazia:

“Utakatifu kwa Bwana.”

“Nyumba ya Bwana.”

Utakatifu kwa Bwana hufanya maisha yetu ya kila siku kuwa matakatifu. Hutuleta karibu zaidi na kuwa wenye furaha zaidi kwa Bwana na kila mmoja na hutuandaa kuishi na Mungu Baba yetu, Yesu Kristo na wale tuwapendao.

Kama alivyofanya rafiki yangu, unaweza kujiuliza kama Baba wa Mbinguni anakupenda wewe. Jibu ni la hakikisho, ndiyo kabisa! Tunaweza kuhisi upendo Wake pale tunapofanya utakatifu kwa Bwana kila siku kuwa wetu, furaha na milele. Na tufanye hivyo, ninaomba katika jina takatifu la Yesu Kristo. amina.

Muhtasari

  1. Kutoka nyakati za Agano la Kale, tunafundishwa, “Takaseni nafsi zenu basi, iweni watakatifu, kwa kuwa mimi ni mtakatifu” (Mambo ya Walawi 11:44). Tunapaswa kutembea katika utakatifu mbele za Bwana (ona Mafundisho na Maagano 20:69), simama mahali patakatifu (ona Mafundisho na Maagano 45:32), itakase siku ya Sabato (ona Kutoka 20:8), vaa mavazi matakatifu (ona Kutoka 29:29), tumia mafuta ya upako mtakatifu (ona Kutoka 30:25), ubarikiwe na manabii watakatifu (ona Mafundisho na Maagano 10:46), na tutegemee maandiko matakatifu (ona Mafundisho na Maagano 20:11), sheria takatifu (ona Mafundisho na Maagano 20:20), malaika watakatifu (ona Mafundisho na Maagano 20:6). Utakatifu kwa Bwana umekusudiwa kubariki nyanja zote za maisha yetu ya kila siku.

  2. Ona Musa 6:34.

  3. Ona “Religion and Spirituality: Tools for Better Wellbeing?,” Gallup Blog, Oct. 10, 2023, news.gallup.com. “Kote ulimwenguni, watu wenye dhamira kubwa kiroho au dini wana maisha mazuri katika hali nyingi”—ikijumuisha hisia chanya, hisia za lengo, kuunganika na jumuiya na kuunganika na jamii (Faith and Wellness: The Worldwide Connection between Spirituality and Wellbeing [2023], 4, faithandmedia.com/research/gallup).

  4. Kila uzoefu ulionukuliwa unashirikiwa—na upendezwaji wangu na shukrani—katika maneno ya watu waliohusika na kwa ruhusa yao.

  5. Leo katika Kanisa, vijana watu wazima wa umri wa 18–35 (ikijumuisha wote vijana waseja na vijana waliooana) na vijana watu wazima (umri wa miaka 36–45) wanafikia theluthi moja (asilimia 32.5) ya idadi ya waumini wa Kanisa. Kati ya waumini wa Kanisa milioni 5.623, jumla ya vijana watu wazima wa umri wa miaka 18–35 hufikia milioni 3,625 (kati yao 694,000 wameoana) na vijana watu wazima wa umri wa miaka 36–45 hufikia milioni 1.998 Vijana wetu na watu wazima waseja ni wenye sifa bainifu, kila mmoja ni wa thamani. Kila mmoja wao anayo hadithi ya imani, utafutaji, ustahimilivu na huruma. Mfano uliotolewa hapa unawakilisha kiasi kikubwa sana cha hadithi na uzoefu wa vijana na watu wazima waseja ninapokutana nanyi katika mazingira mengi na hali kote Kanisani.

  6. Kwa sasa, wamisionari 77,500 wanahudumu katika misioni 450 ulimwenguni kote. Hii inajumuisha vijana wamisionari wanaofundisha, vijana wamisionari watoa huduma, na wanandoa wenza, lakini siyo wamisionari waandamizi 27,800 watoa huduma na watu wa kujitolea wa wa muda mrefu. Kila hadithi ya mmisionari, kuanzia maandalizi hadi huduma na kurudi, ni binafsi na iliyojaa utakatifu kwa Bwana katika uzoefu binafsi.

    Uzoefu mwingi wa wamisionari unarejelea mpangilio wa kiroho. Hii inajumuisha ushuhuda binafsi wa kualika bila choyo na kuwasaidia wengine kuja kwa Yesu Kristo na wa mmisionari kuwa mwanafunzi wa Yesu Kristo na mmisionari wa Hubiri Injili Yangu. Wamisionari wa Hubiri Injili Yangu wamebadilika, hata kugeuzwa, kwa uzoefu wa ushuhuda wao. Wanajifunza kuwapenda watu binafsi, mahali, lugha na tamaduni. Wanatimiza unabii wa kuleta habari njema ya utimilifu wa injili ya Yesu Kristo kwa mataifa, ukoo na watu katika nchi nyingi. Wanapata uzuri katika na kuishi na kila mwenza. Wanafanya kazi na waumini, viongozi, na marafiki katika hali nyingi na asili nyingi, na mengine mengi.

    Wamisionari wa Hubiri Injili Yangu wanakuza imani na kujiamini. Wanajenga uhusiano uliowekwa wakfu. Wanajifunza utiifu ambao huleta baraka na miujiza. Katika njia zingine nyingi mno za kibinafsi, hakika wanakuwa na kujua kwa agano: “Mimi ni mwanafunzi wa Yesu Kristo, Mwana wa Mungu” (3 Nefi 5:13).

  7. Baadhi ya wengi wa waumini wetu wa Kanisa walio waaminifu na jasiri, akina dada na akina kaka, wanajikuta wakikabiliana na hali ambazo kamwe hawakuzitarajia na kamwe hawangeweza kuzichagua. Hawa Watakatifu wanaendelea, siku baada ya siku, kila mara wakimngojea Bwana. Bwana anamjua kila mmoja, na kama mfano huu unavyoshiriki kwa unyenyekevu, hamu ya kumhimiza na kumuimarisha kila mmoja wetu katika wakati Wake na njia Yake.

  8. Kuna utashi mwingi wa uhusiano kwa wazazi na watoto. Nina shukrani sana kwa kila hali ambayo kwayo, hata baada ya miaka mingi, upatanishi, msamaha, na agano la kuwa wa mahala fulani vinatengenezwa au kurejeshwa. Dada huyu hataki mtu yeyote amfikirie vibaya baba yake. Yeye anasema, “Yeye ni mwema na kiongozi mwaminifu na baba mzuri.

  9. Kitendawili cha uzazi ni kwamba watoto wanatengenezwa kwa jinsi walivyolelewa, na bado kwa kawaida wanakumbuka kidogo juu ya miaka ya mapema wakati mama zao bila kuchoka, bila uchoyo waliwalea. Maneno hayatoshi kuelezea ukweli ambao uelewa wangu, upendo, na shukrani kwa baba yangu na mama, ulivyopanuka na kuzama kwa kina nilipokuja kuwa mume, mzazi, na babu. Kuakisi asili ya vizazi ya mpango wa furaha, tunaweza, katika vioo vya hekaluni vya milele, kujiona kama mama, bibi, bibi mkuu katika mwelekeo mmoja na kama binti, mjukuu, kitukuu katika mwelekeo mwingine.

  10. Leo takribani asilimia 60 ya waumini wa Kanisa ulimwenguni kote wanaishi ndani ya maili 50 (kilomita 80 au kiasi cha mwendo wa saa moja katika maeneo mengi) kutoka nyumba Bwana. Katika miaka inayokuja, mahekalu yaliyotangazwa yatakapokamilika, takribani robo tatu ya waumini wa Kanisa wataishi ndani ya saa moja kufika nyumba ya Bwana. Kutengemea na hali, hilo ni tumaini la kutosha kuja kila mara kwa Bwana katika nyumba Yake takatifu, hivyo kubariki vizazi vya wanafamilia wa thamani na sisi wenyewe na uzao wetu.

  11. Juu ya mahekalu yetu, maandishi ya kawaida ni “utakatifu kwa Bwana: Nyumba ya Bwana.” Mahekalu machache yanajumuisha zaidi ya maandishi haya, kama vile kuongezwa kwa jina la Kanisa. Mahekalu machache maandishi yake yamegeuzwa: “nyumba ya Bwana, utakatifu kwa Bwana” (katika Atlanta, Los Angeles, San Diego) Maandishi ya Hekalu la Logan yanaelezea, “utakatifu kwa Bwana.”