Shangwe ya Ukombozi Wetu
Upendo na nguvu za Yesu Kristo zinaweza kumuokoa kila mmoja wetu kutoka kwa makosa yetu, udhaifu, na dhambi zetu na kutusaidia tuwe kitu kingine zaidi.
Karibu miaka 10 iliyopita nilihisi msukumo wa kupaka rangi picha ya Mwokozi. Ingawa mimi ni msanii, hii ilionekana kidogo ya kuchosha. Ni kwa jinsi gani mimi ningechora picha ya Yesu Kristo inayoonyesha Roho Wake? Ni wapi ningeanzia? Ni wapi ningepata muda?
Hata kwa maswali yangu, niliamua kusonga mbele na kutumaini kwamba Bwana angenisaidia. Lakini ilinibidi kusonga mbele na kuacha yanayowezekana Kwake. Nilisali, nikatafakari, nikatafiti, na kuchora, na nilibarikiwa kupata msaada na nyenzo. Na kilichokuwa turubai nyeupe kikaanza kuwa kitu kingine zaidi.
Mchakato huu haukuwa rahisi. Wakati mwingine haukuonekana kama nilivyotarajia. Wakati mwingine kulikuwa na nyakati za uvuvio wa kuweka mistari na mawazo mengine. Na mara nyingi, nililazimika tu kujaribu tena na tena na tena.
Nilipodhani kuwa mchoro wa rangi ya mafuta ulikuwa umekamilika na kukauka, nilianza kutumia vanishi inayoangaza ili kuukinga dhidi ya uchafu na vumbi. Nilipofanya hivyo, niligundua nywele kwenye mchoro zilianza kubadilika, kutawanyika na kupotea. Kwa haraka niligundua kuwa nilipaka vanishi mapema sana, ile sehemu ya mchoro ilikuwa bado haijakauka!
Kumbe nilikuwa nimefuta sehemu ya mchoro wangu kwa vanishi. Ee, jinsi gani moyo wangu ulifadhaika. Nilihisi kama vile nimeharibu kile ambacho Mungu alinisaidia kufanya. Nililia na kujihisi mgonjwa ndani. Katika huzuni, nilifanya kile ambacho kila mmoja hakika angeweza kufanya katika hali kama ile: nilimpigia simu mama yangu. Kwa hekima na upole alisema, “Huwezi kupata tena kile ulichokuwa nacho, lakini fanya vizuri zaidi uwezavyo kwa kile ulicho nacho.”
Hivyo nilisali na kusihi kwa ajili ya msaada na kuchora usiku kucha ili kurekebisha mambo. Na nakumbuka nilipoangalia mchoro asubuhi—ulionekana mzuri kuliko ilivyokuwa mwanzo. Je, iliwezekana vipi? Nilichodhani lilikuwa ni kosa lisilo na marekebisho ilikuwa ni fursa ya mkono Wake wa huruma kudhihirishwa. Yeye hakuwa amemalizana na mchoro huu, na Yeye hakuwa amemalizana na nami. Shangwe kiasi gani ilijaza nafsi yangu. Nilimtukuza Mungu kwa huruma Yake, kwa muujiza huu ambao si tu uliokoa mchoro bali ulinifundisha upendo Wake na nguvu ya kutuokoa kutoka makosa yetu, udhaifu, na dhambi zetu na kutusaidia tuwe kitu kingine zaidi.
Kadiri kina cha shukrani yangu kwa Mwokozi kilivyoongezeka kwa kadiri alivyonisaidia kwa huruma kurekebisha mchoro “usiorekebika,” ndivyo upendo wangu binafsi na shukrani kwa Mwokozi vilivyoongezeka nilipotafuta kufanya Naye kazi katika udhaifu wangu na kusamehewa makosa yangu. Nitakuwa milele mwenye shukrani kwa Mwokozi wangu kwamba naweza kubadilika na kutakaswa. Yeye ana moyo wangu, na ninatumaini kufanya chochote ambacho Yeye angetaka mimi nifanye na kuwa.
Kutubu huwezesha kuhisi upendo wa Mungu na kumjua na kumpenda katika njia ambazo kamwe tusingeweza kuzijua. Kwa mwanamke aliyeipaka mafuta miguu ya Mwokozi, Yeye alisema, “dhambi Zake, ambazo ni nyingi zimesamehewa; kwani alipenda sana: bali kwa yule aliyesamehewa kidogo, huyo hupenda kidogo.” Alimpenda Yesu sana, kwani Yesu alikuwa amemsamehe mengi.
Kuna faraja na tumaini katika kujua kwamba tunaweza kujaribu tena—kwamba, kama Mzee David A. Bednar alivyofundisha, tunaweza kupokea ondoleo endelevu la dhambi zetu kupitia nguvu ya utakaso ya Roho Mtakatifu kadiri tunavyotubu kwa dhati.
Nguvu ya ukombozi ya Yesu Kristo ni mojawapo ya baraka kubwa zilizoahidiwa za maagano yetu. Tafakari kuhusu hili kadiri unavyoshiriki ibada takatifu za wokovu. Bila hiyo, tusingeweza kurudi nyumbani kwenye uwepo wa Baba yetu wa Mbinguni na wale tuwapendao.
Ninajua kwamba Bwana na Mwokozi, Yesu Kristo, ni mwenye nguvu za kuokoa. Kama Mwana wa Mungu, aliyejitoa dhabihu kwa ajili ya dhambi za ulimwengu na kuyatoa maisha Yake na kuyachukua tena, Yeye anabeba nguvu za ukombozi na ufufuko. Yeye amewezesha kutokufa kwa wote na uzima wa milele kwa wale wanaomchagua. Ninajua kwamba kupitia dhabihu Yake ya upatanisho, tunaweza kutubu na kutakaswa kabisa na kukombolewa. Ni muujiza kwamba Yeye anakupenda wewe na mimi katika njia hii.
Yeye amesema, “Je, hamtarudi kwangu sasa, na kutubu dhambi zenu, na kugeuka, ili niwaponye?” Yeye anaweza kuponya “sehemu chakavu” za nafsi yako—sehemu zilizokaushwa, kali na zenye ukiwa wa dhambi na huzuni—na “kufanya jangwa [lako] kuwa kama Edeni.”
Kama ambavyo hatuwezi kutambua maumivu na kina cha mateso ya Kristo katika Gethsemane na msalabani, vivyo hivyo “hatuwezi kupima mipaka wala kujua kina cha msamaha [Wake] wa kiungu,” huruma na upendo.
Unaweza kuhisi wakati mwingine kuwa sio rahisi kukombolewa, kwamba pengine wewe umetengwa na upendo wa Mungu na nguvu ya ukombozi ya Mwokozi kwa sababu ya unayoyapitia au kwa sababu ya yale uliyoyafanya. Lakini ninashuhudia kwamba hauko mbali na mfiko wa Bwana. Mwokozi “alijishusha chini ya mambo yote” na yupo kwenye nafasi ya kiungu kukuinua na kukutoa gizani na kukuleta kwenye “mwanga wake mkuu.” Kupitia kuteseka Kwake, Yeye ametengeneza njia kwa kila mmoja wetu kushinda udhaifu na dhambi. “Ana nguvu zote za kumwokoa kila mwanadamu anayeamini katika jina lake na kuzaa matunda ya toba.”
Kama vile ilivyohitaji kazi na kusihi kwa ajili ya msaada wa mbinguni ili kurekebisha mchoro ule, pia inahitaji kazi, uaminifu wa moyo, na unyenyekevu kuvuna “matunda ya toba.” Matunda haya yanajumuisha kutumia imani yetu katika Yesu Kristo na dhabihu Yake ya upatanisho, kutoa kwa Mungu moyo uliovunjika na roho iliyopondeka, kukiri na kuziacha dhambi, kurejesha kile ambacho kiliharibiwa kwa kadiri ya uwezo wetu wote, na kujitahidi kuishi kwa uadilifu.
Ili kutubu kweli na kubadilika, ni lazima kwanza tuwe “tumesadikishwa dhambi zetu.” Mtu haoni ulazima wa kutumia dawa mpaka wajue kwamba wanaumwa. Kunaweza kuwepo nyakati ambazo hatupendi kujitazama kwa ndani na kuona kile ambacho kinahitaji uponyaji na marekebisho.
Katika maandishi ya C. S. Lewis, Aslan alitoa hoja kwa maneno haya kwa mtu ambaye amejiingiza mitegoni kwa njia zake: “ Oh [binadamu], jinsi gani kwa werevu unajilinda mwenyewe dhidi ya yale ambayo yangeweza kukufanyia vyema!”
Ni wapi wewe na mimi tunaweza kuwa tunajilinda dhidi ya mambo yote ambayo yangeweza kutufanya tuwe wema?
Acha tusijilinde dhidi ya mambo mazuri ambayo Mungu anatamani kutubariki nayo. Kutoka kwenye upendo na huruma ambao Yeye anatamani sisi tuihisi. Kutoka kwenye nuru na maarifa ambavyo Yeye anatamani kutupatia. Kutoka kwenye uponyaji ambao Yeye anajua tunauhitaji bila shaka. Kutoka kwenye mahusiano ya kina ya maagano Yeye anayoyakusudia kwa ajili ya wana na mabinti Zake wote.
Ninasali kwamba tuweke kando “silaha zozote za vita” ambazo kwa kujua au kutokujua tumechukua kujilinda dhidi ya baraka za upendo wa Mungu. Silaha za kiburi, ubinafsi, woga, chuki, makwazo, unafiki, hukumu zisizo haki, wivu—kitu chochote ambacho kinaweza kutuzuia kumpenda Mungu kwa moyo wetu wote na kushika maagano yetu yote pamoja Naye.
Kadiri tunavyoishi maagano yetu, Bwana anaweza kutupa nguvu na msaada tunaohitaji ili kutambua na kushinda udhaifu wetu, ikijumuisha kupe wa kiroho wa kiburi. Nabii wetu amesema:
“Toba ndiyo njia ya kuelekea usafi, na usafi huleta nguvu.”
“Na lo, ni kiasi gani tutahitaji nguvu Yake katika siku zijazo.”
Kama mchoro wangu, Bwana hajamalizana nasi pale tunapokosea, wala Yeye haondoki pale tunaposita. Uhitaji wetu wa kuponywa na kusaidiwa sio mzigo Kwake, bali ndiyo sababu ya Yeye kuja. Mwokozi Mwenyewe alisema:
“Tazama, nimekuja duniani kuleta ukombozi katika ulimwengu, ili kuiokoa dunia kutoka dhambini.”
“Mkono wangu wa rehema umenyooshwa kwenu, na yeyote atakayekuja, nitampokea; na heri ni wao ambao huja kwangu.”
Kwa hiyo njooni—njooni ninyi nyote msumbukao, wagonjwa na wenye huzuni; njooni na muachane na kazi zenu na mpate pumziko ndani yake Yeye awapendaye sana. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo.
Baba yetu wa Mbinguni na Mwokozi wanakuona. Wanaujua moyo wako. Wanajali kile unachokijali, ikiwa ni pamoja na wale unaowapenda.
Mwokozi anaweza kukomboa kile kilichopotea, ikiwa ni pamoja na mahusiano yaliyovunjika. Yeye ameshatengeneza njia kwa wale wote walioanguka ili kuokolewa—kurejesha uzima katika kile kinachohisi kufa na kukosa thamani.
Kama unahangaika na hali unayohisi unatakiwa uwe umeishinda kwa sasa, usikate tamaa. Kuwa mvumilivu, tii maagano yako, tubu kila mara, tafuta usaidizi wa viongozi wako inapohitajika, na nenda kwenye nyumba ya Bwana kila mara kadiri uwezavyo. Sikiliza na fuata hisia ambazo Yeye anakutumia. Yeye hatatupilia mbali maagano Yake na uhusiano Wake na wewe.
Pamekuwepo na mahusiano magumu na changamani katika maisha yangu ambayo nimehangahika nayo na hakika nimetafuta kuyaboresha. Wakati mwingine nilihisi kama nazidi kuanguka mara nyingi kuliko kawaida. Nilijiuliza, “Je, sikurekebisha mambo wakati uliopita? Hivi hakika sikushinda udhaifu wangu?” Nimejifunza kwa muda sasa kuwa sio kwamba sifai kabisa; bali, kuna mengi ya kufanya na uponyaji zaidi unaohitajika.
Mzee D. Todd Christofferson alifundisha: “Hakika Bwana anatabasamu juu ya mtu anayetamani kuja kwenye kiti cha hukumu akiwa anastahili, ambaye ameamua siku hadi siku kubadilisha udhaifu kuwa nguvu. Toba ya kweli, badiliko la kweli vinaweza kuhitaji kujaribu kila mara, lakini kuna kitu kinachotakasa na kitakatifu katika jitihada hizi. Msamaha wa kiungu na uponyaji hutiririka kiasili kwenye nafsi kama hiyo.”
Kila siku ni siku mpya iliyojaa tumaini na uwezekano kwa sababu ya Yesu Kristo. Kila siku mimi na wewe tunaweza kujua, kama Mama Eva alivyotangaza, “shangwe ya ukombozi wetu,” shangwe ya kufanywa wazima, shangwe ya kuhisi upendo wa Mungu wa kudumu kwako.
Ninajua kwamba Baba yetu wa Mbinguni na Mwokozi wanakupenda. Yesu Kristo ni Mwokozi na Mkombozi wa wanadamu wote. Yu hai. Kupitia dhabihu Yake ya Upatanisho, kamba za dhambi na kifo zilivunjwa milele ili tuweze kuwa huru kuchagua uponyaji, ukombozi, na uzima wa milele tukiwa na wale tunaowapenda. Ninashuhudia juu ya mambo hayakatika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.