Mkutano Mkuu
Mwanamume Aliyenena na Yehova
Mkutano mkuu wa Oktoba 2024


11:8

Mwanamume Aliyenena na Yehova

Joseph Smith “alibarikiwa kufungua kipindi hiki cha mwisho,” nasi tumebarikiwa kutokana na yeye kufanya hivyo.

Kusudi langu siku ya leo na daima ni kushuhudia juu ya Yesu Kristo, kwamba Yeye ni Mwana wa Mungu, Muumbaji na Mwokozi wa ulimwengu, Mponyaji na Mkombozi wetu. Kwa sababu “Kanuni za msingi za dini yetu ni ushuhuda wa Mitume na Manabii, kuhusu Yesu Kristo,” leo ninashiriki nanyi uelewa na ushuhuda wangu juu ya Mwokozi kama vilivyoimarishwa na kufanywa kwa kina kupitia maisha na mafundisho ya mtume mmoja mkuu na nabii.

Mwanzo wa Hekima

Mnamo asubuhi ya siku tulivu na angavu mapema kwenye majira ya machipuko ya mwaka 1820, Joseph Smith mwenye miaka 14 alikwenda kwenye kijisitu karibu na nyumba yake ili kusali kuhusu dhambi zake na kuuliza kuhusu kanisa la kujiunga nalo. Sala yake ya dhati iliyotolewa kwa imani thabiti, ilipokea usikivu wa nguvu kubwa sana kushinda zote za ulimwenguni, ikijumuisha Baba na Mwana. Na ibilisi. Kila moja ya nguvu hizo ilikuwa na shauku ya juu kuhusu sala ile na kuhusu mvulana yule.

Kile ambacho sasa tunakiita Ono la Kwanza kilianzisha mwanzo wa Urejesho wa vitu vyote katika kipindi hiki cha mwisho cha injili. Lakini kwa Joseph, uzoefu ulikuwa pia wa kibinafsi na wa maandalizi. Vyote alivyokuwa akitaka ni msamaha na mwongozo. Bwana alimpa vyote. Maelekezo ya “kutojiunga na [kanisa] lolote” yalikuwa ya kimwongozo. Maneno, “Dhambi zako zimesamehewa” yalikuwa ya ukombozi.

Pamoja na uzuri wa kweli zote tunazoweza kujifunza kutoka lile Ono la Kwanza, pengine kwa Joseph kitu muhimu alichojifunza kilikuwa ni kwamba “Nilijua ushuhuda wa Yakobo ni wa kweli—kwamba mtu aliyepungukiwa na hekima angeweza kumuomba Mungu na kuipata.”

Kama mwanazuoni mmoja alivyosema: “Sababu muhimu ya Ono la Kwanza hivi leo ni kujua kwamba ni asili ya Mungu kuwapa wale wanaopungukiwa hekima. … Mungu aliyejifunua Yeye mwenyewe kwa Joseph Smith kwenye kijisitu kitakatifu ni Mungu ambaye huwajibu vijana katika nyakati za changamoto.”

Uzoefu wa Joseph kwenye kijisitu kitakatifu ulimpa ujasiri kuomba msamaha na mwongozo katika maisha yake yote. Uzoefu wake pia umenipa mimi ujasiri wa kuomba msamaha na mwongozo maisha yangu yote.

Toba ya Kila Mara

Mnamo Septemba 21, 1823, Joseph alisali kwa dhati kwa ajili ya msamaha, ujasiri ambao ulikuja kwa sababu ya uzoefu wake kwenye kijisitu miaka mitatu iliyopita, mbingu zingejibu tena. Na ndivyo ilivyokuwa. Bwana alimtuma malaika, Moroni, kumpa mwongozo Joseph na kumfahamisha kuhusu kumbukumbu ambayo baadae angeitafsiri kupitia kipawa na nguvu za Mungu—Kitabu cha Mormoni.

Takribani miaka 13 baada ya hapo, Joseph na Oliver Cowdery walipiga magoti kwa unyenyekevu, kwenye sala ya kimya kimya kwenye hekalu jipya lililowekwa wakfu la Kirtland. Hatujui walisali kwa ajili ya kitu gani, lakini sala zao inawezekana zilijumuisha kusihi kwa ajili ya msamaha, kwani, wakati wakinyanyuka, Mwokozi aliwatokea na kutamka, “Tazama dhambi zenu zimesamehewa; nanyi ni wasafi mbele zangu.”

Katika miezi hiyo na miaka baada ya tukio hili, Joseph na Oliver wangetenda dhambi tena. Na tena. Lakini katika wakati huo, kwa ajili ya wakati huo, katika kujibu kusihi kwao na katika maandalizi kwa ajili ya urejesho wa funguo za ukuhani ambao ulikuwa karibu kutokea, Yesu aliwatakasa dhambi zao.

Maisha ya Joseph ya toba ya mara kwa mara hunipa ujasiri wa kukikaribia kiti cha neema ili [nami] nipate rehema.” Nimejifunza kwamba Yesu Kristo kweli ni “mwenye hamu ya kusamehe.” Si dhumuni Lake wala asili Yake kuhukumu. Yeye alikuja kutuokoa.

Kumuuliza Bwana

Kama sehemu ya ahadi ya “urejesho wa vitu vyote,” Bwana, kupitia Joseph Smith, alileta Kitabu cha Mormoni na mafunuo mengine ambayo yana utimilifu wa injili Yake. Kweli muhimu zilitolewa kwa uwazi na kwa ukamilifu kwa kadiri Joseph alivyorudia rudia kumuuliza Bwana kwa ajili ya maelekezo. Zingatia yafuatayo:

  1. Baba na Mwana wana miili “yenye kushikika kama ya mwanadamu.”

  2. Yesu alijichukulia juu Yake Mwenyewe si tu dhambi zetu, bali pia magonjwa, mateso na udhaifu Wetu.

  3. Upatanisho Wake ulikuwa wa maumivu makali yaliyo sababisha Yeye kutokwa damu kwenye kila kinyweleo.

  4. Tunaokolewa kwa neema Yake “baada ya kufanya yote tuwezayo kufanya.”

  5. Kuna masharti kupata rehema ya Kristo.

  6. Tunapokuja kwa Kristo, Yeye si tu atatatusamehe dhambi zetu, bali pia Yeye atabadilisha asili yetu “kwamba hatuwi tena na hamu ya kutenda uovu.”

  7. Kristo mara zote huamuru watu Wake kujenga mahekalu, ambamo Yeye hujidhihirisha Mwenyewe kwao na huwajalia wao nguvu kutoka juu.

Ninashuhudia kwamba vitu hivi vyote ni vya kweli na muhimu. Vinawakilisha sehemu ndogo tu ya utimilifu ambao ulirejeshwa na Yesu Kristo kupitia Joseph Smith kama itikio la ombi la kujirudia rudia la Joseph la kutaka mwongozo.

Kuendeleza Ufalme Huu

Mnamo 1842, Joseph aliandika vitu vya kustaajabisha ambavyo vingekuja kutokea kwenye kipindi hiki cha mwisho. Alitangaza kwamba wakati wa siku zetu, “wenye ukuhani walio mbinguni wataungana na wale wa duniani, ili kutimiza malengo hayo makuu; na wakati tukiwa tumeungana kwa kusudi moja, kuendeleza ufalme wa Mungu, wenye ukuhani walio mbinguni si watazamaji wasiofanya chochote.”

Katika tamko linalohusiana na hilo kwa Benjamin Johnson, rafiki yake, Joseph alisema “Benjamin [kama nitakufa] sitakuwa mbali nawe, na kama ningekuwa upande mwingine wa pazia, [ningekuwa] bado ninafanya kazi nawe na kwa nguvu iliyoongezwa sana, ili kuendeleza ufalme huu.”

Mnamo Juni 27, 1844, Joseph Smith na Hyrum kaka yake waliuawa. Mwili wa Joseph ulizikwa, lakini ushuhuda wake unaendelea kupiga mwangwi tena na tena kote ulimwenguni na katika nafsi yangu:

“Nilikuwa nimeona ono; nilijua hilo, na nilijua kwamba Mungu alijua, na sikuweza kukataa.”

“Kamwe sikuwaambia nilikuwa mkamilifu; lakini hakuna kosa katika funuo ambazo nimefundisha.”

“Kanuni za msingi za dini yetu ni ushuhuda wa Mitume na Manabii, kuhusu Yesu Kristo, kwamba alikufa, akazikwa, na akafufuka tena siku ya tatu, na amepaa mbinguni; na mambo yote mengine ambayo yanahusiana na dini yetu ni viambatisho tu.”

Kile ambacho kilisemwa juu ya Yohana Mbatizaji kingeweza pia kusemwa juu ya Joseph Smith: “Kulikuwa na mtu aliyetumwa kutoka kwa Mungu, ambaye jina lake lilikuwa [Joseph]. … “Huyo hakuwa ile nuru, bali alikuja ili aishuhudie ile Nuru,” “kwamba wanadamu wote wapate kuamini kwa yeye.”

Ninaamini. Ninaamini na nina uhakika kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Ninashuhudia kwamba Mungu aliye hai ni Baba yetu mwenye upendo. Ninajua hili kwa sababu sauti ya Bwana imesema hivyo kwangu, na vivyo hivyo sauti ya watumishi Wake, mitume na manabii, ikijumuisha na kuanzia na Joseph Smith.

Ninashuhudia kwamba Joseph Smith alikuwa na ni nabii wa Mungu, shahidi na mtumishi wa Bwana Yesu Kristo. “Alibarikiwa kufungua kipindi hiki cha mwisho,” nasi tumebarikiwa kutokana na yeye kufanya hivyo.

Bwana alimuamuru Oliver na sisi sote “Simama pamoja na mtumishi wangu Joseph, kiuaminifu.” Ninashuhudia kwamba Bwana anasimama pamoja na Joseph Mtumishi Wake na Urejesho ulioletwa kupia yeye.

Joseph Smith sasa ni sehemu ya wale wenye ukuhani mbinguni ambao aliwazungumzia. Kama alivyomuahidi rafiki yake, yeye hayuko mbali nasi, na kwenye upande wa pili wa pazia, bado anaendelea kufanya kazi pamoja nasi, na kwa nguvu iliyoongezwa, kuendeleza ufalme huu. Kwa shangwe na shukrani, ninapaza sauti yangu “sifa kwa mwanamume aliyenena na Yehova.” Na juu ya yote, sifa kwa Yehova, ambaye alinena na mtu huyo! Katika jina la Yesu Kristo, amina.