Mkutano Mkuu
Kumbatia Zawadi ya Bwana ya Toba
Mkutano mkuu wa Oktoba 2024


11:35

Kumbatia Zawadi ya Bwana ya Toba

Acha tusingojee mambo yawe magumu ndipo tumgeukie Mungu. Acha tusingojee mwisho wa maisha yetu duniani ndiyo tutubu kweli.

Ninashuhudia juu ya Baba wa Mbinguni mwenye upendo. Katika mkutano mkuu wa Aprili 2019, muda baada ya kukubaliwa katika jukumu langu jipya kama Kiongozi mwenye Mamlaka wa Sabini , kwaya iliimba wimbo wa “Nastaajabu” ambao ulipenya moyo na nafsi yangu.

Nashangaa kwamba angeweza kushuka kutoka kwenye kiti cha enzi cha kiungu

Kuokoa nafsi kiburi kama yangu,

Kwamba upendo wake angenionesha,

Kunikomboa, hata kunihalalisha.”

Niliposikia maneno hayo, nilishangaa sana. Nilihisi kwamba licha ya mapungufu na kasoro zangu, Bwana alinibariki kujua kwamba “katika nguvu zake naweza kufanya mambo yote.”

Hisia ya kawaida ya mapungufu, udhaifu au hata kutostahili ni jambo ambalo wengi wetu wakati mwingine hupambana nalo. Mimi bado napambana nalo; nilihisi hivo siku niliyoitwa. Nimehisi hivyo mara nyingi na bado ninahisi hivyo sasa ninapozungumza nanyi. Hata hivyo, nimejifunza kwamba sio mimi pekee niliye na hisia hizi. Kwa kweli, kuna masimulizi mengi katika maandiko ya wale ambao wanaonekana kuhisi hisia kama hizo. Kwa mfano, tunamkumbuka Nefi mtumishi mwaminifu na shujaa wa Bwana. Nyakati fulani, hata yeye alipambana na hisia za kutostahili, udhaifu na mapungufu.

Alisema: “ingawa Bwana ana wema mkubwa, hata kunionyesha kazi yake kuu na ya maajabu, moyo wangu unalia: Ewe mimi mtu mwovu! Ndiyo, moyo wangu unahuzunishwa kwa sababu ya mwili wangu; moyo wangu unahofishwa na dhambi zangu.”

Nabii Joseph Smith alizungumza kuhusu “mara nyingi [alihisi] kulaumiwa kwa udhaifu [wake] na kutokamilika.” Lakini hisia za Joseph za mapungufu na wasiwasi zilikuwa sehemu ya mambo yaliyomsababisha kutafakari, kusoma, kujifunza na kusali. Kama unavyoweza kukumbuka, alienda kusali kwenye kisitu karibu na nyumba yake ili kupata ukweli, amani na msamaha. Alimsikia Bwana akimwambia, “Joseph, mwanangu, umesamehewa dhambi zako. Enenda zako, enenda katika hukumu zangu, na ukazishike amri zangu. Tazama, mimi ni Bwana wa Utukufu. Nilisulubiwa kwa ajili ya ulimwengu ili wote watakaoliamini jina langu waweze kupata uzima wa milele.”

Tamaa ya dhati ya Joseph ya kutubu na kutafuta wokovu wa nafsi yake ilimsaidia kuja kwa Yesu Kristo na kupokea msamaha wa dhambi zake. Hizi juhudi endelevu zilifungua mlango wa Urejesho unaoendelea wa injili ya Yesu Kristo.

Uzoefu huu wa ajabu wa Nabii Joseph Smith unaonyesha jinsi hisia za udhaifu na kutofaa zinaweza kutusaidia kutambua asili yetu ya kuanguka. Kama sisi ni wanyenyekevu, hii itatusaidia kuja kutambua kumtegemea Yesu Kristo na kuchochea ndani ya mioyo yetu hamu ya dhati ya kumgeukia Mwokozi kwa kusudi kamili na kutubu dhambi zetu.

Marafiki zangu, toba ni shangwe! Toba tamu ni sehemu ya mchakato wa kila siku ambapo kupitia, “mstari juu ya mstari, kanuni juu ya kanuni,” Bwana hutufundisha kuishi maisha ambayo kitovu chake ni mafundisho Yake. Kama Joseph na Nefi, tunaweza “kumlilia [Mungu] ili tupate rehema; kwa maana ana uwezo wa kuokoa.” Yeye anaweza kutimiza tamaa au hamu yoyote ya haki na anaweza kuponya jeraha lolote maishani mwetu.

Kitabu cha Mormoni: Ushuhuda Mwingine wa Yesu Kristo, mimi na wewe tunaweza kupata simulizi zisizo na idadi za watu ambao walijifunza jinsi ya kuja kwa Yesu Kristo kupitia toba ya kweli.

Ningependa kushiriki nanyi mfano wa rehema nyororo za Bwana kupitia uzoefu ambao ulitokea katika kisiwa pendwa cha nyumbani kwangu cha Puerto Rico

Ilikuwa katika mji wangu wa Ponce ambapo dada Kanisani, Célia Cruz Ayala, aliamua kwamba angeenda kumpa rafiki yake Kitabu cha Mormoni. Alikifunga na kwenda kupeleka zawadi hii, yenye thamani zaidi kwake kuliko almasi au rubi, yeye alisema. Akiwa njiani, mwizi mmoja alimsogelea, akakwapua mkoba wake na kukimbia na zawadi hiyo maalumu ndani ya mkoba.

Aliposimulia hadithi hii kanisani, rafiki yake alisema, “Nani anajua? Labda hii ilikuwa fursa yako kushiriki injili!”

Ndiyo, siku chache baadaye, unajua nini kilitokea? Célia alipokea barua. Ninashikilia barua hiyo ambayo Célia alishiriki na mimi, mkononi mwangu leo. Inasema:

“Bi. Cruz:

“Nisamehe, nisamehe. Huwezijua jinsi ninavyosikitika kwa kukushambulia. Lakini kwa sababu ya hilo, maisha yangu yamebadilika na yataendelea kubadilika.

“Kitabu hicho [Kitabu cha Mormoni] kimenisaidia katika maisha yangu. Ndoto ya huyo mtu wa Mungu imenitikisa. … Ninakurudishia [dola] zako tano, kwa maana siwezi kuzitumia. Nataka ujue kuwa ulionekana kuwa na mng’ao juu yako. Nuru hiyo ilionekana kunizuia [nisikudhuru, kwa hivyo] badala yake nilikimbia.

“Nataka ujue kwamba utaniona tena, lakini utakaponiona, hutanitambua, kwa maana nitakuwa kaka yako. … Hapa, ninapoishi, sina budi kumtafuta Bwana na kwenda kwenye kanisa ambalo wewe ni sehemu ya.

“Ujumbe ulioandika katika kitabu hicho umenitoa machozi. Tangu Jumatano usiku sijaweza kuacha kuusoma. Nimesali na kumwomba Mungu anisamehe, [na] ninakuomba unisamehe. … Nilidhani zawadi yako iliyofunikwa ni kitu ninachoweza kuuza. [Badala yake,] imenifanya nitake [kubadilisha] maisha yangu. Nisamehe, nisamehe, nakuomba.

“Wako, rafiki mtoro.”

Akina kaka na akina dada, nuru ya Mwokozi inaweza kutufikia sote, bila kujali hali zetu. “Haiwezekani kwa wewe kuzama chini zaidi ya pale nuru isiyo na mwisho ya Upatanisho wa Kristo inapoangaza.” alisema Rais Jeffrey R. Holland.

Kwa mpokeaji asiye tarajiwa wa zawadi ya Célia, ya Kitabu cha Mormoni, kaka huyu aliendelea kushuhudia zaidi juu rehema za Bwana. Ingawa ilichukua muda kwa kaka huyo kujisamehe, alipata shangwe katika toba. Ni muujiza ulioje! Dada mmoja mwaminifu, Kitabu cha Mormoni kimoja, toba ya dhati, na nguvu za Mwokozi viliongoza kwenye furaha ya utimilifu wa baraka za injili na maagano matakatifu katika nyumba ya Bwana. Wanafamilia wengine walifuata na kukubali majukumu katika shamba la mzeituni la Bwana, ikijumuisha huduma ya umisionari.

Tunapokuja kwa Yesu Kristo, njia yetu ya toba ya dhati hatimaye itatupeleka kwenye hekalu takatifu la Mwokozi.

Ni nia njema iliyoje ya kujitahidi kuwa msafi—kustahili utimilifu wa baraka zilizowezeshwa na Baba yetu wa Mbinguni na Mwanawe kupitia maagano matakatifu ya hekaluni! Kuhudumu mara kwa mara katika nyumba ya Bwana na kujitahidi kushika maagano matakatifu tunayofanya huko kutaongeza hamu yetu na uwezo wetu wa kupata mabadiliko ya moyo, uwezo, akili na nafsi vilivyo muhimu kwetu kuwa zaidi kama Mwokozi wetu. Rais Russell M. Nelson ameshuhudia: “Hakuna cho chote kitakachofungua mbingu zaidi [kuliko kuabudu hekaluni]. Hakuna cho chote!”

Rafiki zangu wapendwa, je, mnajiona kuwa hamtoshi? Je, unahisi hustahili? Je, una jishuku wewe mwenyewe? Labda unaweza kuwa na wasiwasi na kujiuliza: Je ninatosha! Je, nimechelewa sana? Kwa nini naendelea kushindwa wakati ninajaribu kwa kadiri niwezavyo?

Akina kaka na akina dada, hakika tutafanya makosa katika maisha yetu tukiwa njiani. Lakini tafadhali kumbuka kwamba, kama Mzee Gerrit W. Gong alivyofundisha: “Upatanisho wa Mwokozi wetu hauna kikomo na ni wa milele. Kila mmoja wetu hupotoka na kupungukiwa. Tunaweza, kwa muda, kupotea njia. Mungu kwa upendo anatuhakikishia [kwamba] licha ya pale tulipo au kile tulichokifanya, hakuna mahali ambapo hatuwezi kurudi. Yeye anasubiri kwa utayari kutukumbatia.”

Mke wangu mpendwa, Cari Lu, pia amenifundisha, sisi sote tunahitaji kutubu, kurudisha wakati nyuma na kuweka upya muda wetu kwenye “saa sifuri” kila siku.

Vikwazo vitakuja. Acha tusingojee mambo yawe magumu ndipo tumgeukie Mungu. Acha tusingojee mpaka mwisho wa maisha yetu duniani ndiyo tutubu kwa dhati. Badala yake, hebu sasa, bila kujali ni sehemu gani ya njia ya agano tuliyopo, tuzingatie nguvu za ukombozi za Yesu Kristo na juu ya hamu ya Baba wa Mbinguni kwetu ya sisi kurudi Kwake.

Nyumba ya Bwana, maandiko Yake matakatifu, manabii na mitume Wake watakatifu hutupatia msukumo wa kujitahidi kusonga kuelekea utakatifu binafsi kupitia mafundisho ya Kristo.

Na Nefi akasema: “Na sasa, tazama, ndugu zangu wapendwa, hii ndiyo njia; na hakuna njia nyingine wala jina lililotolewa chini ya mbingu ambalo mwanaume [na mwanamke] anaweza kuokolewa katika ufalme wa Mungu. Na sasa, tazama, hili ndilo fundisho la Kristo, na fundisho pekee na la kweli la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu.”

Mchakato wetu wa “upa-ta-nisho” na Mungu unaweza kuonekana kuwa wenye changamoto. Lakini mimi na wewe tunaweza kusimama, kutulia, na kumtegemea Mwokozi, na kutafuta na kutenda juu ya kile ambacho Yeye angetaka sisi tubadilishe. Ikiwa tutafanya hivyo kwa nia kamili, tutashuhudia uponyaji Wake. Na fikiria ni jinsi gani uzao wetu watabarikiwa tunapokumbatia zawadi ya Bwana ya toba!

Mfinyanzi Mkuu alimfundisha baba yangu, kwa kielezo na kutusafisha, ambavyo inaweza kuwa vigumu. Hata hivyo, Mponyaji Mkuu pia atatusafisha. Nimepata uzoefu huo na ninaendelea kupata nguvu hiyo ya uponyaji. Ninashuhudia kwamba nguvu hiyo huja kupitia imani katika Yesu Kristo na toba ya kila siku.

Ni ajabu kwangu angenithamini

Kiasi cha kufa!”

Ninashuhudia juu ya upendo wa Mungu na uwezo usio na kikomo wa Upatanisho wa Mwanawe. Tunaweza kuhisi kwa kina tunapotubu kwa dhati na kwa moyo wote.

Rafiki zangu, mimi ni shahidi wa Urejesho mtukufu wa injili kupitia Nabii Joseph Smith na mwongozo wa kiungu wa sasa wa Mwokozi kupitia nabii na mnenaji Wake, Rais Russell M. Nelson. Ninajua Yesu Kristo yu hai na kwamba Yeye ni Mponyaji Mkuu wa nafsi zetu. Ninajua na kushuhudia kwamba mambo haya ni ya kweli, Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. “Nastaajabu,” Nyimbo za Dini,, na.106.

  2. Alma 26:12.

  3. 2 Nefi 4:17; ona pia mstari wa 18–19

  4. Joseph Smith—Historia ya 1:29.

  5. Joseph Smith, “History, circa Summer 1832,” 3, josephsmithpapers.org; herufi kubwa na tahajia za maneno zimebadilishwa.

  6. Ona Mosia 4:11–12.

  7. Rais Russell M. Nelson alifundisha: “Wakati tunapochagua kutubu, tunachagua kubadilika! Tunamruhusu Mwokozi atubadilishe kuwa toleo zuri zaidi la sisi wenyewe. Tunachagua kukua kiroho na kupokea shangwe—shangwe ya ukombozi katika Yeye. Tunapochagua kutubu, tunachagua kuwa zaidi kama Yesu Kristo!” (“Tunaweza Kufanya Vizuri Zaidi na Kuwa Bora Zaidi,” Liahona, Mei 2019, 67.)

  8. 2 Nefi 28:30.

  9. Alma 34:18.

  10. Kaka zangu na dada zangu, Kitabu cha Mormoni ni cha thamani kiasi gani kwenu? Kama utapewa almasi au rubi au Kitabu cha Mormoni, utachagua nini? Kwa kweli, ni kipi kilicho cha thamani kubwa kwako?” (Russell M. Nelson, “Kitabu cha Mormoni: Maisha Yako Yangekuwaje Bila Hicho?Liahona, Nov. 2017, 61).

  11. In F. Burton Howard, “Missionary Moments: ‘My Life Has Changed,’” Church News, Jan. 6, 1996, thechurchnews.com; see also Saints: The Story of the Church of Jesus Christ in the Latter Days, vol. 4, Sounded in Every Ear, 1955–2020 (2024), 472–74, 477–79.

  12. Jeffrey R. Holland, “Wafanyakazi katika Shamba la Mizabibu, Liahona, Mei 2012, 33.

  13. Je, tunaweza kusimama kwa sekunde moja na kufikiria kuhusu kizazi chetu? Kwa sababu ya mtazamo wetu finyu, hatuwezi kukiona sasa, lakini nia yetu ya kumgeukia Bwana kwa kusudi kamili la moyo—kubadilika, kutubu na kukumbatia Injili ya Yesu Kristo—inaweza kuathiri vizazi! Hebu tafakari baraka za ziada zinazoweza kuchanua kutokana na unyenyekevu, upole na imani ya nafsi moja katika Yesu Kristo hata katika hali ngumu zaidi!

  14. Undani wa taarifa hizi ulisimuliwa tena na Dada Célia Cruz katika mazungumzo ya binafsi na Mzee Jorge M. Alvarado mnamo Septemba 10, 2024.

  15. Russell M. Nelson, “Furahia Katika Zawadi ya Funguo za Ukuhani,” Liahona, Mei 2024, 122.

  16. Tunapojikuta tunauliza maswali kama haya, ni muhimu kukumbuka maneno ya Mtume Paulo:

    “Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? …

    “Lakini, katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.

    “Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo,

    “Wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu” (Warumi 8:35, 37–39).

  17. Gerrit W. Gong, “Mwako Wetu wa Imani,” Liahona,, Nov. 2018, 41.

  18. Nefi ni mfano mzuri wa hili? Yeye alieleza:

    “Amka, nafsi yangu! Usitumbukie tena katika dhambi. Shangilia, Ewe moyo wangu, na usimpatie adui wa nafsi yangu mahali.

    “Ewe Bwana, je, utaikomboa nafsi yangu? Je, utaniopoa kutoka mikononi mwa maadui zangu? Je, utanifanya kwamba nitetemeke nikiona dhambi?” (2 Nefi 4:28, 31).

  19. Rais Dallin H. Oaks alifundisha: “Wakati mtu amepitia mchakato wa toba, Mwokozi hufanya zaidi ya kumtakasa mtu huyo kutoka kwa dhambi—Pia humpa nguvu mpya. Yeye pia alimpa nguvu mpya. Uimarishwaji huo ni muhimu kwetu ili kuelewa lengo la utakaso, ambalo ni kurudi kwa Baba yetu wa Mbinguni. Ili kuruhusiwa kuingia kwenye uwepo Wake, lazima tuwe zaidi ya wasafi. Lazima pia tuwe tumebadilishwa kutoka mtu dhaifu kimaadili ambaye amefanya dhambi kuwa mtu imara na mwenye msimamo wa kiroho ili kuishi katika uwepo wa Mungu” (“Upatanisho na Imani,” Ensign, Apr. 2010, 33–34).

  20. 2 Nefi 31:21.

  21. Tunaheshimu familia zetu na Baba yetu wa Mbinguni kwa kukumbatia toba na kujitahidi kuishi maisha mazuri.

  22. Nyimbo za Dini, na. 193.