“Ni Mimi”
Hisani ya Kristo—hudhihirishwa katika uaminifu kamili kwa mapenzi ya uungu—ipo toka kitambo na inaendelea kuwepo na huendelea kuendelea.
Ni siku ya Sabato, na tumekusanyika kuzungumza juu ya Kristo na Yeye kusulubiwa. Najua Kristo Yu hai.
Fikiria tukio hili kutoka katika wiki ya mwisho ya maisha ya Yesu duniani. Umati ulikuwa umekusanyika, ikijumuisha askari wa Kirumi waliojihami kwa marungu na mapanga viunoni. Wakiongozwa na maofisa kutoka kwa makuhani wakuu ambao walikuwa na tochi mikononi, kombania hii yenye ari haikuwa imekuja kuteka mji. Usiku huu walikuwa wanamtafuta mtu mmoja tu, mtu ambaye hakujulikana kubeba silaha, bila mafunzo ya kijeshi, au kujihusisha na kupigana wakati wowote katika maisha Yake yote.
Askari walipokuwa wanakaribia, Yesu, katika juhudi ya kuwalinda wanafunzi Wake, alisonga mbele na kusema, “Ni nani mnayemtafuta? Wao wakamjibu, “Yesu Mnazareti.” Yesu akawaambia, “Ni mimi. … Punde … alipowaambia, Ni mimi, walirudi nyuma, wakaanguka chini.”
Kwangu mimi, huo ni mojawapo ya mistari yenye kusisimua sana katika maandiko yote. Miongoni mwa mambo mengine, unaniambia wazi kwamba kuwa tu kwenye uwepo wa Mwana wa Mungu—Yehova mkuu wa Agano la Kale na Mchungaji Mwema wa Agano Jipya ambaye habebi silaha ya aina yoyote—kwamba kusikia tu sauti ya Kimbilio hili kutoka kwa Dhoruba, huyu Mfalme wa Amani inatosha kuwafanya wapinzani wajikwae wakitaka kukimbia, wakirundikana kwa fujo na kulifanya kundi lote kutamani wangepangiwa kazi za jikoni usiku huo.
Siku chache tu kabla, wakati Yeye alipoingia jijini kwa shangwe, “mji wote ulitaharuki,” maandiko yanasema, wakiulizana, “Ni nani huyu?” Ninaweza tu kuwaza kwamba “Ni nani huyu?” ni swali ambalo liliwakanganya askari hao waliokuwa sasa wanauliza!
Jibu la swali hilo halingeweza kuwa katika mwonekano Wake, kwani Isaya alikuwa ametoa unabii karne saba mapema kwamba “Yeye hana umbo wala uzuri; Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani.” Haikuwa katika mavazi Yake ya ustarabu au katika ukwasi Wake mwingi wa kibinafsi, ambavyo vyote Yeye hakuwa navyo. Haingewezekana kuwa wa mafunzo yoyote ya kitaalamu katika masinagogi ya eneo hilo kwa sababu hatuna ushahidi wowote kwamba Yeye aliwahi kujifunza kutoka kwa yeyote kati yao, ingawa hata katika ujana Wake Yeye angeweza kuwakanganya sana wasomi na wanasheria, akiwashangaza na mafundisho Yake “kama mtu aliyekuwa na mamlaka.”
Kutoka kwenye fundisho Lake hilo ndani ya hekalu mpaka kuingia kwake Yerusalemu kwa ushindi na huku kukamatwa, kusiko haki, Yesu mara kwa mara aliwekwa kwenye hali ngumu, zisizoeleweka ambazo daima alikuwa mshindi—ushindi ambao hatuna melezo yake isipokuwa kwa kupitia vinasaba vya kiungu.
Na bado katika historia nzima wengi wamerahisisha, hata kushusha thamani ya mfano wetu kumhusu Yeye na ushahidi Wake wa Yeye ni nani. Wameshusha thamani wema Wake kuwa kitu cha kujidai, haki Yake kuwa hasira, rehema Yake kuwa uhuru. Sisi tunapaswa tujihadhari na mitazamo miepesi kuhusu Yeye ambayo inapuuza mafundisho tuyaonayo magumu kwetu. “Upuuzi” huu umekuwa wa kweli hata kuhusu wema Wake wa juu, upendo Wake.
Wakati wa huduma Yake duniani, alifundisha kwamba kuna ya amri mbili kuu. Zimefundishwa katika mkutano huu na daima zitafundishwa: “Mpende Bwana Mungu wako [na] mpende jirani yako kama nafsi yako.” Iikiwa sisi tutamfuata Mwokozi kwa uaminifu katika hizi sheria mbili muhimu zilizoungana bila kuchanganulika, tunapaswa kushikilia kwa nguvu kile ambacho Yeye kwa kweli alisema. Na kile ambachoYeye kwa kweli alisema kilikuwa, “Kama mnanipenda, zishikeni amri zangu.” Jioni ile ile, Yeye alisema “pendaneni; kama nilivyowapenda ninyi.”
Katika maandiko hayo, virai hivyo vya kustahilisha vinafafanua ukweli, upendo kama wa Kristo—wakati mwingine huitwa hisani—ni vya muhimu sana.
Vinafafanua nini? Je, Yesu alipenda vipi?
Kwanza, Yeye alipenda kwa “moyo [Wake] wote, uwezo, akili na nguvu,” ikimpatia Yeye uwezo wa kuponya maumivu ya kina na kutangaza uhalisia wa ukweli mgumu. Kwa kifupi, Yeye ni mtu ambaye anatoa neema na anasisitiza ukweli kwa wakati huo huo. Kama Lehi alivyosema katika baraka yake kwa mwanawe Yakobo, “Ukombozi unakuja kupitia Masiya Mtakatifu; kwani amejaa neema na kweli.” Upendo Wake huruhusu kumbatio wakati linapohitajika na kikombe kichungu kama inahitajika kimezwe. Kwa hiyo tunajaribu kupenda—kwa moyo wetu wote, uwezo, akili na nguvu—kwa sababu hii ndiyo njia ambayo Yeye anatupenda sisi.
Sifa ya pili ya hisani ya Yesu ilikuwa ni utiifu Wake kwa kila neno litokalo kinywani mwa Mungu, daima akiwianisha mapenzi na tabia Yake kwa yale ya Baba Yake wa Mbinguni.
Wakati alipowasili bara la Amerika kufuatia Ufufuko Wake, Kristo aliwaambia Wanefi: “Tazama, Mimi Ndimi Yesu Kristo. … Na nimekunywa kutoka kwa kikombe kichungu ambacho Baba amenipatia, … ambamo ndani yake nimevumilia mapenzi ya Baba … kutoka mwanzo.”
Juu ya njia tofauti tofauti ambazo Yeye angeweza kujitambulisha Mwenyewe, Yesu alifanya hivyo kwa kutangaza utiifu Wake kwa mapenzi ya Baba—pasipo kujali kabisa kwamba ilikuwa punde tu kabla ya muda wa hitaji Lake kuu, Mwana huyu Mzaliwa wa Pekee wa Mungu alihisi kutelekezwa na Baba Yake. Hisani ya Kristo—inayojidhihirisha katika uaminifu kamili kwa mapenzi matakatifu—upo na unaendelea kuwepo, sio tu katika siku rahisi na za faraja lakini hasa hata katika siku za kiza na zilizo ngumu sana.
Yesu alikuwa “mtu wa huzuni,” maandiko yanasema. Alipitia huzuni, uchovu, kuvunjika moyo na upweke wa hali ya juu. Katika nyakati hizi na nyakati zote, upendo wa Yesu haushindwi, na wala wa Baba Yake. Kwa upendo uliokomaa, wa kweli—aina ya ule unaotoa mfano, unaowezesha, na unaohamishika—upendo wetu pia hautashindwa.
Kwa hiyo, kama nyakati zingine kwa kadiri unavyojaribu, ndivyo inavyoonekana kuwa vigumu sana; kama vile unavyojaribu kufanyia kazi vizuizi na mapungufu yako, unagundua kuna mtu au kitu kinachoazimia kujaribu imani yako; kama unafanya kazi kwa bidii sana, bado unahisi nyakati za uoga zikikukamata, kumbuka kwamba imekuwa hivyo kwa baadhi ya watu waaminifu wa ajabu katika kila kipindi. Pia kumbuka kwamba kuna nguvu katika ulimwengu inayoazimia kupinga kila kitu kizuri unachojaribu kufanya.
Kwa hiyo, iwe katika wingi na pia katika umasikini, iwe katika pongezi za binafsi na pia ukosoaji wa umma, iwe katika vipengele vitakatifu vya Urejesho na pia katika mapungufu ya binadamu ambayo yatakuwa sehemu yake, tunabakia kwenye njia ya Kanisa la Kristo la kweli. Kwa nini? Kwa sababu kama vile Mkombozi wetu, tulijiandikisha kwa ajili ya kozi yote—sio kwa jaribio fupi bali hadi mtihani wa mwisho. Shangwe katika hili ni kwamba Mwalimu Mkuu ametupatia sisi sote majibu ya wazi kabla ya kozi kuanza. Zaidi ya hayo, tuna walimu wengi ambao hutukumbusha majibu hayo katika kila kipindi wakati tuwapo njiani. Lakini bila shaka, hakuna kati ya haya yatazaa matunda kama tunakwepa darasa.
“Mnamtafuta nani?” Kwa mioyo yetu yote tunajibu, “Yesu wa Nazareti.” Wakati Yeye anaposema, “Ni mimi,” tunapiga goti na kukiri kwa ulimi wetu kwamba Yeye ni Kristo aliye hai, kwamba Yeye peke yake alilipia dhambi zetu, kwamba Yeye alikuwa anatubeba hata wakati tulipodhani ametutelekeza. Tutakaposimama mbele Yake na kuona vidonda katika mikono Yake na miguu, tutaanza kuelewa kile ilichomaanisha Kwake kubeba dhambi zetu na kuzoea huzuni, kuwa mtiifu kabisa kwa mapenzi ya Baba Yake—yote hayo sababu ya upendo safi kwetu. Ili kuwatambulisha wengine kwenye imani, toba, ubatizo, kipawa cha Roho Mtakatifu na kupokea baraka zetu katika nyumba ya Bwana—hizi ni “kanuni na ibada” za msingi ambazo zinafunua upendo wetu kwa Mungu na jirani na kwa shangwe kuonyesha mfano wa Kanisa la kweli la Kristo.
Akina kaka na dada, ninashuhudia kwamba Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni chombo ambacho Mungu ametoa kwa ajili kuinuliwa kwetu. Injili inayofundishwa na Kanisa hili ni ya kweli, na ukuhani unaolihalalisha siyo zao. Ninashuhudia kwamba Russell M. Nelson ni nabii wa Mungu wetu, kama vile watangulizi Wake walivyofanya na kama vile warithi Wake watakavvofanya. Na siku moja huo mwongozo wa kinabii utaongoza kizazi kumwona Mjumbe wetu wa Ukombozi akishuka kama vile “radi … itokavyo mashariki,” na tutatamka, “Yesu wa Nazareti.” Kwa mikono milele iliyonyooshwa na upendo usio na unafiki, Yeye atajibu, “Ni mimi.” Ninaahidi hivyo kwa nguvu za kitume na mamlaka ya jina Lake takatifu, hata Yesu Kristo, amina.