Mkutano Mkuu
Maisha ya Duniani Yanafanya Kazi!
Mkutano mkuu wa Oktoba 2024


10:59

Maisha ya Duniani Yanafanya Kazi!

Licha ya changamoto ambazo sote tunapitia, Baba yetu mpendwa wa Mbinguni amesanifu mpango wa furaha kiasi kwamba hatujakusudiwa kushindwa.

Kwa miaka kadhaa nilipangiwa kuwa mwalimu wa nyumbani wa dada mmoja kikongwe katika kata yangu. Hakuwa na maisha rahisi. Alikuwa na matatizo kadhaa tofauti ya kiafya na alipitia wakati mgumu katika maisha kutokana na ajali ya utotoni kwenye uwanja wa michezo. Alipewa talaka akiwa na miaka 32 akiwa na watoto wadogo wanne wa kuwalea na kukidhi mahitaji, aliolewa tena akiwa na miaka 50. Mume wake wa pili alifariki dunia yeye akiwa na umri wa miaka 66, na dada huyu aliishi miaka 26 ya ziada kama mjane.

Licha ya changamoto nyingi katika maisha yake marefu, alikuwa mwaminifu katika maagano yake hadi mwisho. Dada huyu alikuwa mwenye shauku ya elimu ya nasaba, mhudhuriaji wa hekaluni, na mkusanyaji na mwandishi wa historia za familia. Ingawa alikuwa na majaribu mengi magumu, na bila shaka wakati mwingine alijihisi huzuni na upweke, alikuwa na uso mchangamfu na mwenye shukrani na utu wenye kufurahisha.

Miezi mitatu baada ya kufariki kwake, mmoja wa watoto wake wa kiume alipata uzoefu wa kustaajabisha hekaluni. Alijua kwa nguvu ya Roho Mtakatifu kwamba mama yake alikuwa na ujumbe kwa ajili yake. Aliwasiliana naye, lakini siyo kwa ono au maneno ya kusikika. Ujumbe bayana ufuatao ulikuja katika akili ya mwana kutoka kwa mama yake: “Ninataka ujue kwamba maisha ya duniani ni muhimu, na ninataka wewe ujue kwamba mimi sasa ninaelewa kwa nini kila kitu kilitokea [katika maisha yangu] katika namna kilivyotokea—na yote ni SAWA.”

Ujumbe huu ni wa kustaajabisha zaidi mtu anapozingatia hali na magumu ambayo dada huyu aliyavumilia na kuyashinda.

Akina kaka na akina dada, maisha ya duniani yanafanya kazi! Yamesanifiwa ili yafanye kazi! Licha ya changamoto, maumivu na magumu tunayokabiliana nayo, Baba yetu mpendwa wa Mbinguni, mwenye hekima na mkamilifu amesanifu mpango wa furaha kiasi kwamba hatujakusudiwa kushindwa. Mpango Wake hutoa njia kwa ajili yetu kuinuka juu ya kushindwa kwetu. Bwana amesema, “Hii ndiyo kazi yangu na utukufu wangu, kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu.”

Hata hivyo, kama tunahitaji kuwa wanufaika wa “kazi na utukufu” wa Bwana, hata “kutokufa na uzima wa milele,” lazima tutegemee kupewa elimu na kufundishwa, na kufaulu kupitia moto wa msafishaji—wakati mwingine hadi kufikia ukomo wetu. Kwa kuepuka kikamilifu matatizo, changamoto na magumu ya ulimwengu huu ingekuwa kukwepa mchakato ambao kwa kweli ni muhimu kwa ajili ya maisha ya duniani kufanya kazi.

Na hivyo, hatupaswi kushangaa wakati nyakati ngumu zinapotufikia. Tutakumbana na hali ambazo zinatujaribu na watu ambao wanatuwezesha kufanyia mazoezi hisani ya kweli na uvumilivu. Lakini tunahitaji kustahimili chini ya magumu yetu na kukumbuka, kama Bwana alivyosema:

“Na yeyote autoaye uhai wake katika kazi yangu, kwa ajili ya jina langu, atauona tena, hata uzima wa milele.

“Kwa hiyo, usiwaogope maadui zako [au matatizo, changamoto au majaribio ya maisha haya], kwani nimeazimia …, asema Bwana, kwamba nitawajaribu ninyi katika mambo yote ikiwa mtakaa katika agano langu … ili muweze kuwa wenye kustahili.”

Tunapohisi kukanganyikiwa au kuwa na wasiwasi kuhusu matatizo yetu au kuhisi kwamba yawezekana tunapokea zaidi kuliko sehemu yetu ya magumu ya maisha, tunaweza kukumbuka kile Bwana alichosema kwa wana wa Israeli:

“Nawe utaikumbuka njia ile yote Bwana Mungu wako aliyokuongoza miaka hii arobaini katika jangwa, ili akunyenyekeze, kukujaribu kuyajua yaliyo moyoni mwako kwamba [utashika] amri zake, au sivyo.”

Kama Lehi alivyomfundisha mwanawe Yakobo:

“Umeteseka kwa masumbuko na huzuni nyingi. … Walakini, … [Mungu] ataweka wakfu masumbuko yako kwa faida yako. … Kwa hivyo, ninajua kwamba wewe umekombolewa kwa sababu ya utakatifu wa Mkombozi wangu.”

Kwa sababu maisha haya ni uwanja wa majaribio na “shida zinapotuzonga na kutisha amani yetu,” inasaidia kukumbuka ushauri huu na ahadi inayopatikana katika Mosia 23 kuhusiana na changamoto za maisha: “Walakini—yeyote atakayeweka imani yake [kwa Bwana] yeye atainuliwa juu siku ya mwisho.”

Kama kijana, binafsi nilipitia hisia nyingi za maumivu na aibu ambazo zilikuja kama matokeo ya matendo yasiyo ya haki kutoka kwa mtu mwingine, ambazo kwa miaka mingi ziliathiri ustahili wangu binafsi na hisia ya kustahili mbele za Bwana. Hata hivyo ninatoa ushahidi binafsi kwamba Bwana anaweza kutuimarisha sisi na kutubeba juu katika magumu yoyote tunayoitwa kupitia wakati wa safari yetu katika bonde hili la majonzi.

Tunafahamu uzoefu wa Paulo:

“Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi kwa wingi wa mafunuo hayo [niliyopokea], nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi.

“Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu, kwamba kinitoke.

“Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha: maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu.” Basi nitajisifia udhaifu wangu ili uweza wa Kristo ukae juu yangu.”

Sisi hatujui “mwiba katika mwili” wa Paulo ulikuwa ni nini. Yeye hakuchagua kuelezea kama ilikuwa maradhi ya kimwili, kiakili au mapungufu wa kihisia, au majaribu. Lakini hatuhitaji kujua hilo ili tujue kwamba yeye alihangaika na kumsihi Bwana kwa ajili ya msaada na kwamba mwishowe, nguvu ya Bwana na uweza ndivyo vilivyomsaidia.

Kama Paulo, ilikuwa kupitia msaada wa Bwana kwamba hatimaye niliimarishwa kihisia na kiroho na mwishowe nilitambua baada ya miaka mingi kwamba daima nimekuwa mtu wa thamani na mwenye kustahili baraka za injili. Mwokozi alinisaidia kushinda hisia zangu za kutostahili na kutoa msamaha wa dhati kwa mkosaji. Hatimaye nilielewa kwamba Upatanisho wa Mwokozi ulikuwa zawadi binafsi kwangu na kwamba Baba yangu wa Mbinguni na Mwanawe wananipenda mimi kikamilifu. Kwa sababu ya Upatanisho wa Mwokozi, maisha ya duniani yanafanya kazi.

Wakati mwishowe nilipobarikiwa kutambua namna Mwokozi alivyoniokoa na kusimama nami wakati wote wa hayo niliyopitia, kwa uwazi kabisa naelewa kwamba hali hizo za bahati mbaya za ujana wangu zilikuwa ndizo safari na uzoefu wangu binafsi, azimio ambalo kwalo na matokeo ya baadaye hayawezi kuonyeshwa kwa wale walioteseka na wanaoendelea kuteseka kutokana na tabia zisizo za haki za wengine.

Ninatambua kwamba uzoefu wa maisha—mzuri au mbaya—unaweza kutufundisha masomo muhimu. Na sasa ninajua na ninashuhudia kwamba maisha ya duniani yanafanya kazi! Ninatumaini kwamba kama matokeo ya majumuisho ya uzoefu wa maisha yangu—mema na mabaya—ninayo huruma kwa watu wasio na hatia ya matendo ya wengine na huruma kwa wanaodhulumiwa.

Kwa dhati ninatumaini kwamba kama matokeo ya uzoefu wa maisha yangu—mzuri au mbaya—mimi ni mkarimu zaidi kwa wengine, nikiwatendea wengine kama ambavyo Mwokozi angetenda, na ninao uelewa mkubwa zaidi kwa mtenda dhambi, na kwamba ninao uadilifu kamili. Tunapokuja kutegemea neema ya Mwokozi na kushika maagano yetu, tunaweza kutumika kama mifano ya matokeo yenye kufika mbali juu ya Upatanisho wa Mwokozi.

Ninashiriki mfano wa mwisho kwamba maisha ya duniani yanafanya kazi.

Shangazi na mama wa Mzee Hales.

Shangazi wa Mzee Hales, Lois VandenBosch, na mama yake, Klea VandenBosch.

Mama yangu hakuwa na safari rahisi maisha yake yote hapa duniani. Hakupokea nishani au heshima ya ulimwenguni na hakuwa na fursa ya kielimu zaidi ya shule ya upili. Alipatwa na polio akiwa mtoto, iliyosababisha maumivu maisha yake yote na kukosa faraja katika mguu wake wa kushoto. Kama mtu mzima, alipitia magumu mengi na hali zenye changamoto kimwili na kifedha lakini alikuwa mwaminifu kwenye maagano yake na alimpenda Bwana.

Mama yangu alipokuwa na umri wa miaka 55 dada yangu mkubwa aliyenifuatia alifariki dunia, akiacha nyuma mtoto mchanga wa kike wa miezi nane, mpwa wangu, akiwa hana mama. Kwa sababu kadhaa, Mama aliishia kwa sehemu kubwa kumlea mpwa wangu kwa miaka 17 iliyofuatia, mara nyingi katika hali ngumu. Na bado, licha ya matukio haya, kwa furaha na kwa hiari aliitumikia familia yake, majirani, na waumini katika tawi, na alihudumu kama mfanyakazi wa ibada katika hekalu kwa miaka mingi. Katika miaka kadhaa ya mwisho ya uhai wake, Mama aliteseka aina fulani ya kupungukiwa akili, mara kwa mara alichanganyikiwa, na alizuiliwa kwenye nyumba ya uuguzi. Cha kusikitisha, alikuwa peke yake wakati alipofariki bila kutarajia.

Miezi kadhaa baada ya kufariki kwake, niliota ndoto ambayo kamwe sijaweza kusahau. Katika ndoto yangu, nilikuwa nimekaa ofisini kwangu katika Jengo la Utawala la Kanisa. Mama aliingia ofisini humo. Nilijua alikuwa ametoka katika ulimwengu wa roho. Daima nitakumbuka hisia niliyokuwa nayo. Hakusema chochote, lakini alinururisha urembo wa kiroho ambao sijawahi kuuona kabla na ambao ninapata ugumu kuuelezea.

Uso wake na umbile lake hakika vilikuwa vizuri mno. Ninakumbuka kumwambia, “Mama, umekuwa mrembo sana!” nikirejelea uwezo wake wa kiroho na urembo. Alinitambua—tena pasipo kuzungumza. Nilihisi upendo wake kwangu, na hapo nilijua kwamba yuko na furaha na ameponywa kutokana na shughuli za ulimwengu na changamoto na kwa hamu anasubiri “ufufuko mtukufu.” Ninajua kwamba kwa Mama, maisha ya duniani yalifanya kazi—na kwamba yanafanya kazi kwetu sisi pia.

Kazi na utukufu wa Mungu ni kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu. Uzoefu wa maisha ya duniani ni sehemu ya safari hiyo ambayo inaturuhusu sisi kukua na kuendelea kuelekea kutokufa kwa binadamu na uzima wa milele. Hatukuletwa hapa ili tushindwe bali tufaulu katika mpango wa Mungu kwa ajili yetu sisi.

Kama Mfalme Benjamini alivyofundisha: “Ningetamani kwamba mtafakari juu ya hali ya baraka na yenye furaha ya wale wanaotii amri za Mungu. Kwani tazama, wanabarikiwa katika vitu vyote, vya muda na vya kiroho; na kama watavumilia kwa uaminifu hadi mwisho watapokewa mbinguni, kwamba hapo waishi na Mungu katika hali ya furaha isiyo na mwisho.” Kwa maneno mengine, maisha ya duniani yanafanya kazi!

Ninashuhudia kwamba tunapopokea ibada za injili, tunapoingia katika maagano na Mungu na kisha kuyashika maagano hayo, kutubu na kuwatumikia wengine, na kuvumilia hadi mwisho, tunaweza pia kuwa na hakikisho na tumaini kamilifu katika Bwana kwamba maisha ya duniani yanafanya kazi! Ninashuhudia juu ya Yesu Kristo na kwamba utukufu wa siku zetu za usoni pamoja na Baba yetu wa Mbinguni unawezeshwa kwa neema na Upatanisho wa Mwokozi. Katika jina la Yesu Kristo, amina.