Mkutano Mkuu
Siku Ambazo Kamwe Hazitasahaulika
Mkutano mkuu wa Oktoba 2024


14:19

Siku Ambazo Kamwe Hazitasahaulika

Nyakati zijazo zitawapa waumini wa Kanisa kila mahali ongezeko la fursa za kushiriki habari njema za injili ya Yesu Kristo.

Utangulizi

Wapendwa akina kaka na akina dada, historia ya Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho katika kipindi hiki ni nzuri kwa uzoefu wa kiungu ambao huonesha jinsi ambavyo Bwana ameliongoza Kanisa Lake. Hata hivyo, kuna muongo mmoja katika historia yetu, unasimama tofauti juu ya mingine yote—muongo kuanzia 1820 hadi 1830. Tukianza na uzoefu wa Nabii Joseph Smith katika Kijisitu Kitakatifu majira ya kuchipua ya 1820, wakati alipomwona Baba wa Mbinguni na Mwana Wake, Yesu Kristo, na kuendelea hadi Aprili 6, 1830, muongo huo ni tofauti na mwingine wowote.

Moroni akiyotoa mabamba ya dhahabu.
Urejesho wa Ukuhani wa Melkizedeki.
Oliver Cowdery.

Zingatia matukio haya ya kustaajabisha! Nabii kijana alizungumza na malaika Moroni, alitafsiri mabamba ya dhahabu na kuchapisha Kitabu cha Mormoni! Alikuwa chombo ambacho kupitia kwacho Ukuhani wa Haruni na Melkizedeki ulirejeshwa, na hapo alianzisha Kanisa! Oliver Cowdery alielezea vyema kipindi hicho: “Hizi zilikuwa siku ambazo kamwe hazitasahaulika.” Matukio ya kimiujiza yameendelea hadi leo.

Acha niwe jasiri kupendekeza kwamba mwaka huu tumeanza muongo ambao unaweza kuthibitisha kuwa muhimu sana kama vile wowote ule tangu muongo ule wa mwanzo takribani karne mbili zilizopita.

Muongo Wetu

Acha nifafanue. Kati ya sasa 2024 na 2034, tutapata uzoefu wa matukio muhimu ambayo yataleta fursa zisizo kifani za kutumikia, za kuungana na waumini na marafiki na za kutambulisha Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho kwa watu wengi zaidi kuliko hapo kabla.

Kumbukizi ya miaka 100 ya kuzaliwa Rais Nelson.

Hakika tumeshuhudia hivi karibuni nguvu ya nyakati za kihistoria tuliposherehekea pamoja na makumi ya mamilioni kumbukizi ya miaka 100 ya kuzaliwa kwa Rais Russell M. Nelson.

Wakiripoti juu ya siku ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa Rais Nelson, jarida la Newsweek waliandika kichwa cha habari kilichosomeka, “Kiongozi wa Dini Mzee Zaidi Ulimwenguni Anafikisha Miaka 100.” Kisha waliorodhesha viongozi 10 wa imani wazee zaidi ulimwenguni—Rais Nelson akiwa wa kwanza kwenye orodha ambayo iliwajumuisha Papa Francis na Dalai Lama.

Kauli hii kutoka makala ya New York Times huwakilisha mtazamo wa habari nyingi za kimataifa: “Nchini [Marekani] mbio za uchaguzi wa urais ambazo zimechochea tafakuri kuhusu uzee na uongozi, safari ya bwana Nelson inapendekeza kwamba, angalau katika kanisa lake, siku ya kuzaliwa yenye tarakimu tatu si suala la kuleta mawazo. Anabakia mtu maarufu kati ya waumini wa kanisa, ambao wanamwona rais wao si tu kama mtendaji bali kama ‘nabii, mwonaji na mfunuzi.’”

Jinsi gani tuna shukrani kwamba ukumbusho wa siku ya kuzaliwa ya Rais Nelson umetupatia fursa ya kuitambulisha hadhira ya ulimwengu kwa nabii wa Mungu, maadhimisho ambayo kamwe hayatasahaulika.

Jengo la Ofisi ya Kanisa Lililofanyiwa Ukarabati.

Mapema majira haya ya kuchipua, jengo lililofanyiwa ukarabati huko Temple Square—likiwa na maonyesho ya bendera za kimataifa zikiwakilisha nchi ambapo Kanisa linatambulika—lilifunguliwa. Njia ya kuingilia ina kielelezo cha mnara wa matale wenye maneno yafuatayo ya kinabii: “Na itakuwa katika siku za mwisho, kwamba mlima wa nyumba ya Bwana utawekwa imara juu ya milima, nao utainuliwa juu ya vilima; na mataifa yote watauendea makundi makundi.”

Kwa kweli matukio ya kumbukumbu ambayo yatatukia kipindi cha miaka 10 ijayo yanajumuisha dhihirisho moja kuwa unabii huu wa Isaya unatimia.

Hekalu la Salt Lake.

Tafakari idadi kubwa ya matembezi ya wazi kwa wote mahekaluni na uwekaji wakfu ambavyo vimepangwa kufanyika kwa muongo unaofuata, uwezekano mkubwa wa mahekalu 164 na zaidi. Fikiria makumi ya mamilioni ya ninyi na marafiki zenu mkitembea katika nyumba ya Bwana. Kiini cha kiishara cha matukio haya kitakuwa uwekaji wakfu upya wa Hekalu la Salt Lake na shughuli zinazohusiana na hili. Hizi hakika zitakuwa siku ambazo kamwe hazitasahaulika.

Kuanzishwa kwa Kanisa.

Mwaka 2030 utaleta fursa ulimwenguni kote ya kukumbuka miaka mia mbili ya uanzishwaji wa Kanisa. Ingawa ni mapema kusema jinsi Kanisa litakavyotambua hatua hii kubwa, itaturuhusu kualika familia, marafiki, wafanyakazi wenza na wageni waalikwa “kuja na kuona” na kuelewa vyema matokeo yenye nguvu Kanisa iliyonayo katika maisha ya waumini wa Kanisa.

Olimpiki ya Majira ya Baridi ya 2002 huko Jijini Salt Lake.

Mnamo 2034, maelfu ya waheshimiwa, wageni na wanariadha kutoka kote ulimwenguni watajaza mitaa ya Jiji la Salt Lake, jukwaa kwa ajili ya Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi. Pengine hakuna onyesho kubwa zaidi la umoja ulimwenguni kote zaidi ya lile linalodhihirishwa katika Michezo ya Olimpiki. Macho ya ulimwengu yatakuwa juu ya Kanisa na waumini wake, wakimudu fursa lukuki za kujitolea, kuhudumu na kushiriki habari njema kupitia matendo ya ukarimu—tukio ambalo halitasahaulika kamwe.

Hakika nyakati hizi zijazo zitawapa waumini wa Kanisa kila mahali ongezeko la fursa za kushiriki habari njema za injili ya Yesu Kristo kupitia maneno na matendo, muongo ambao hautasahaulika kamwe.

Habari Njema

Katika mkutano wiki chache kabla ya siku yake ya kuzaliwa, Rais Nelson alishiriki sababu ya yeye kuthamini kirai “habari njema.” Kwa kuliangalia tu neno, alisema, kirai kinaashiria shangwe na furaha. Lakini “habari njema” humaanisha mengi zaidi ya hilo. Alifafanua kwamba kirai hiki kinatoka kwenye neno la kiasili la Kigiriki euangelion, ambalo kiuhalisia humaanisha “habari njema” au “injili.” Furaha na shangwe katika maisha haya na yajayo mara zote imeunganishwa na injili ya Yesu Kristo. Hivyo kirai “habari njema” huchukua maana hizi mbili katika namna ya kupendeza.

“Wanaume [na wanawake] wapo, ili wapate shangwe.” Baba wa Mbinguni alitoa mpango wa furaha ambao huwezesha shangwe kupitia baraka Zake. Hizi ni pamoja na kuishi katika uwepo Wake milele kama familia. Upatanisho wa Yesu Kristo ni kiini kwenye mpango wa Mungu wa kutukomboa. Ili kupokea uzima wa milele, ni lazima tuje kwa Kristo. Tunapofanya hivyo “na kuwasaidia wengine kufanya vivyo hivyo, tunashiriki katika kazi ya Mungu ya wokovu na kuinuliwa.”

Ujumbe huu wa habari njema ya injili ya Yesu Kristo ni ujumbe muhimu zaidi duniani. Na hapo ndipo vijana na vijana wakubwa wa Kanisa wanapoingia.

Kwa Ajili ya Nguvu Kwa Vijana

Sasa, wakati muongo huu ujao unaweza kuwa umejaa siku ambazo kamwe hazitasahaulika kwa kila muumini wa Kanisa, hii inaweza kuwa kweli hususani kwenu ninyi kizazi kinachoinukia. Mpo hapa duniani sasa kwa sababu mlichaguliwa kuwa hapa sasa. Mnazo nguvu na uwezo wa kuwa wanafunzi wa Kristo katika njia zisizo na kifani.

Rais George Q. Cannon alifundisha, “Mungu amehifadhi roho kwa ajili ya kipindi hiki cha maongozi ya Mungu ambazo zina ujasiri na ari ya kukabiliana na ulimwengu, na nguvu zote za mwovu [na] … kuijenga Sayuni ya Mungu wetu bila kuhofia matokeo.”

Kwa sababu ya hilo, ninatamani kuzungumza nanyi enyi wa kizazi kinachoinukia, kuwaalika kupata taswira ya jinsi muongo huu ujao wa kusisimua, usiosahaulika kamwe unavyoweza kuwa kwenu ninyi. Ninatoa pia maneno rahisi ya ushauri na kutia moyo ambayo yatawawezesha katika kipindi cha muongo huu ujao.

Kama vile wengi wenu, nina simu janja ambayo, mara kadhaa na bila kuamrishwa, huvuta pamoja mlolongo wa picha zikionesha kile nilichokuwa nikifanya siku fulani. Mara zote inashangaza kuona jinsi mambo yalivyobadilika kwangu na kwa familia yangu ndani ya miaka michache tu.

Picha ambazo simu yako itatunza kwa miaka 10 kuanzia sasa! Unaweza kujiona ukihitimu shule ya upili au chuo, ukipokea endaumenti yako, kwenda misheni, kufunga ndoa na kupata mtoto wa kwanza. Kwako binafsi, huu utakuwa muongo usiosahaulika kamwe. Lakini itakuwa mara mbili ya hayo ikiwa kwa ari utajitahidi kuwa nuru ya ulimwengu ya jinsi habari njema ya Yesu Kristo inavyoweza kurutubisha na kustawisha si tu maisha yako bali yale ya familia yako, marafiki na wafuasi wa mitandao ya kijamii.

Unaweza ukawa unajiuliza jinsi ya kufanya hili.

Manabii wa Mungu wametufunza kwamba hili hufanyika kupitia shughuli rahisi, zinazojulikana kama majukumu matakatifu yaliyoainishwa: kwanza, kuishi injili ya Yesu Kristo; pili, kuwajali wenye mahitaji; tatu, kuwaalika watu wote waipokee injili; na nne, kuziunganisha familia kwa milele yote. Cha kustaajabisha, kila moja linaweza kufanywa katika njia za kawaida sana na za asili.

Majukumu Matakatifu Yaliyoainishwa

Ninawaahidi huu utakuwa muongo usiosahaulika kamwe kwenu ikiwa mtakumbatia majukumu haya manne matakatifu yaliyoainishwa. Hebu tufikirie kile hii inachoweza kujumuisha.

Majukumu manne matakatifu yaliyoainishwa.
Msichana akisali.

Kwanza, ishi Injili ya Yesu Kristo. Jifunze maneno ya manabii, na jifunze kumpenda Baba yako wa Mbinguni. Funganisha moyo wako Kwake, na jitahidi kutembea katika njia Zake. Inuliwa na “ujasiri wa agano” ambao Mzee Ulisses Soares ameufafanua. Ujasiri huu huja kutokana na kufanya maagano ya kumfuata Yesu Kristo, kwa kujua kwamba Mwokozi hatimaye atakuimarisha na kukuunga mkono.

Acha marafiki zako waone shangwe unayoihisi katika kuishi injili na utakuwa ujumbe bora zaidi wa injili ambao watawahi kuupokea.

Pili, fikia kwa huruma ili kuwajali wenye mahitaji. Kizazi chenu kwa njia isiyo ya kawaida huwakumbuka sana wenye uhitaji. Popote majanga yanapotokea na waumini wa Kanisa wanapoharakisha kuondoa vifusi na kuwafariji wanaoteseka, inaonekana kwamba wengi wa waliovalia fulana za “Mikono ya Usaidizi” ni vijana na wale wa miaka ya ishirini. Ni asili yenu “kubeba mzigo wa mmoja na mwingine” na “kuwafariji wale wanaohitaji kufarijiwa.” Kwa kufanya hili “tunatimiza sheria ya Kristo.”

Watoto wakikusanya jibini kwa ajili ya wale wenye uhitaji.

Evan, mvulana mdogo wa darasa la watoto, aliamua kutumia mapumziko yake ya kiangazi kwa kukusanya bidhaa kwa ajili ya mkate wenye karanga na jibini ili kutoa msaada kwenye hifadhi ya chakula ya eneo lake. Alipata mradi huo kwenye tovuti ya JustServe. Evan mdogo aliwaandikisha darasa lake lote la shuleni kusaidia kukusanya chupa 700 za jibini! Waruhusu watu unaowatumikia wajue kuwa kuwajali kwako kuna kiini kwenye upendo wako kwa Mungu na tamanio lako la kumtendea jirani yako kama unavyojitendea.

Wamisionari huko Brazili.

Tatu, waalike wote waipokee injili. Mwaka huu tumefungua misheni mpya 36 ulimwenguni kote ili kuweza kuwapokea wote wanaotamani kutumikia misheni. Katika kipindi ambapo vijana wengi hujiondoa kwenye shughuli za pamoja za kidini, hii ni ya kustaajabisha na huelezea asili tukufu ya shuhuda zenu. Iwe mnatumikia muda wote ama la, tafadhali tambueni uwezo wenu mkubwa wa kushawishi makundi rika yenu kadiri mnavyowapenda, kushiriki na kuwaalika watafiti injili ya Yesu Kristo.

Vijana kwenye Hekalu la Preston England.

Nne, ziunganishe familia kwa milele yote. Ninapotembelea mahekalu ulimwenguni kote, ninastaajabia idadi kubwa ya vijana waliosimama wakingojea kwenye eneo la ubatizo na ongezeko la idadi ya vijana wakubwa wakihudumu kama wahudumu wa ibada. Hivi karibuni kundi la vijana zaidi ya 600 kutoka Scotland na Ireland walisafiri hadi Hekalu la Preston Uingereza, kufanya zaidi ya ibada 4,000, nyingi ambazo zilikuwa kwa ajili ya mababu zao wenyewe waliofariki! Ninawahimiza mjishughulishe katika historia ya familia, mtumie muda hekaluni na kwa umakini mjiandae kuwa aina ya mwanamume au mwanamke aliye tayari kufunga ndoa na mwenza mwenye kustahili kama wewe ndani ya hekalu. Jenga mpangilio katika maisha yako sasa wa kufanya hekalu liwe sehemu ya kawaida ya maisha yenu.

Hitimisho

Wapendwa kaka zangu na dada zangu, marafiki zangu wapendwa vijana, yawezekana kukawepo na magumu kwa kila mmoja wetu katika siku za mbeleni. Hata hivyo, tunapouingia muongo huu wa nyakati zisizo na kifani, na tushiriki habari njema kupitia shughuli rahisi za kuishi, kujali, kualika na kuunganisha. Tunapofanya hivyo, Bwana atatubariki kwa uzoefu usiosahaulika kamwe.

Ninashuhudia kwamba wale wanaomwendea Bwana kwa moyo wa dhati na kusudi halisi, wale walio na jina la Mwokozi midomoni mwao na Roho Mtakatifu kwenye nafsi zao, wale wanaojiingiza kwenye hija hii kuu na tukufu, mtagundua na kupata uzoefu wa baraka tele za selestia na kupokea ushahidi kwamba Mungu anakusikia, anakujua na anakupenda. Utakuwa na uzoefu wa siku zisizosahaulika kamwe. Katika jina la Yesu Kristo, amina.