Mkutano Mkuu
Ee Vijana wa Haki Tukufu ya Uzaliwa
Mkutano mkuu wa Oktoba 2024


12:33

Ee Vijana wa Haki Tukufu ya Uzaliwa

Mungu anakutumainieni ninyi, watoto wa agano kusaidia katika kazi Yake ya kuwaleta watoto Wake wote nyumbani Kwake salama.

Mzee Stevenson, huu ni mkutano usiosahaulika.

Familia yetu daima ilifurahia kitabu kidogo kilichoitwa Barua za Watoto kwa Mungu. Hapa ziko chache:

“Mungu mpendwa, badala ya kuwaacha watu wafe na kuwaumba wengine wapya, kwa nini usiwe tu na hawa ulio nao sasa?”

“Inakuaje wewe una sheria kumi tu, lakini shule yetu ina mamilioni?

“Kwa nini uweke ugonjwa wa mafindo findo ikiwa utayatoa tu tena?”

Leo hamna muda wa kujibu maswali haya yote, lakini kuna swali lingine ninalosikia mara kwa mara kutoka kwa vijana ambalo ningependa kulishughulikia. Kutoka Ulaanbaatar, Mongolia, hadi Thomas, Idaho, swali ni lile lile: “Kwa nini? Kwa nini Watakatifu wa Siku za Mwisho wanaishi tofauti sana na wengine?”

Ninajua ni vigumu kuwa tofauti—hasa wakati wewe ni kijana na unataka sana watu wengine wakupende. Kila mtu anataka kukubalika na wengine, na hamu hiyo inakuzwa hadi kuwa uwiano usio na afya katika ulimwengu wa leo wa kidigitali uliojaa mitandao ya kijamii na uonevu wa mtandaoni.

Kwa hiyo, kwa mashinikizo hayo yote, kwa nini Watakatifu wa Siku za Mwisho wanaishi tofauti sana hivi? Kuna majibu mengi mazuri: Kwa sababu wewe ni mtoto wa Mungu. Kwa sababu ulihifadhiwa kwa ajili ya siku hizi za mwisho. Kwa sababu wewe ni mwanafunzi wa Yesu Kristo.

Lakini majibu hayo daima hayakutofautishi wewe. Kila mmoja ni mtoto wa Mungu. Kila mmoja ulimwenguni sasa hivi alitumwa katika siku za mwisho. Lakini sio kila mtu anaishi Neno la Hekima au sheria ya usafi wa kimwili kama vile wewe unavyojitahidi kufanya. Kuna wanafunzi wengi shupavu wa Kristo ambao si waumini wa Kanisa. Lakini hawahudumu mishei na kufanya ibada katika nyumba za Bwana kwa niaba ya mababu kama vile ninyi mnavyofanya. Lazima kuwe na zaidi kuliko hilo—na lipo.

Leo ningependa kuzingatia sababu ya ziada ambayo imekuwa na maana sana katika maisha yangu. Mnamo 1988, Mtume kijana aliyeitwa Russell M. Nelson alitoa hotuba katika Chuo Kikuu cha Brigham Young iliyoitwa “Asante kwa Agano,” Ndani yake, wakati huo Mzee Nelson alielezea kwamba wakati tunapotumia haki yetu ya kujiamulia kufanya na kushika maagano na Mungu, tunakuwa warithi wa agano la milele la Mungu analofanya na watangulizi wetu katika kila kipindi. Ikisemwa kwa njia nyingine, tunakuwa “watoto wa agano.” Hiyo inatufanya kuwa wa tofauti. Hiyo inatupatia sisi kufikia baraka zile zile mababu na mabibi zetu walizopokea, ikijumuisha haki ya kuzaliwa.

Haki ya uzaliwa! Yawezekana umeshasikia neno hilo. Tunaimba hata wimbo kulihusu hili: “Ee Vijana wa haki tukufu ya uzaliwa, songeni, songeni, songeni!” Ni neno la kuvutia sana. Lakini linamaanisha nini?

Katika nyakati za Agano la Kale ikiwa baba angefariki, mwana mwenye haki ya uzaliwa alikuwa na jukumu la kumtunza mama yake na dada zake. Kaka zake walipokea urithi wao na kuondoka ili kujitafutia ulimwenguni, lakini mwana mwenye haki ya mzaliwa wa kwanza hakwenda popote. Angeoa na kuwa na familia yake mwenyewe, lakini angebakia mpaka mwisho wa siku zake kutawala shughuli za shamba la baba yake. Kwa sababu ya hili jukumu lililoongezwa, alipatiwa kiasi kikubwa cha urithi. Je, kuongoza na kuwatunza wengine ilikuwa jambo kubwa kuombwa? Sivyo ukifikiria urithi wa ziada aliopatiwa.

Leo hatuongei kuhusu utaratibu wako wa kuzaliwa katika familia ya ulimwenguni au kazi za jinsia za Agano la Kale. Tunaongea kuhusu urithi unaopokea kama mrithi mwenza na Kristo kwa sababu ya uhusiano wa kimaagano uliochagua kuwa nao pamoja Naye na Baba yako aliye Mbinguni. Je, ni jambo kubwa Mungu kukutarajia wewe kuishi tofauti na watoto Wake wengine ili uweze kuwaongoza na kuwatumikia vyema? Sivyo ukifikiria baraka—zote, kimwili na kiroho—ambazo wewe umepatiwa.

Je, haki yako ya uzaliwa inamaanisha wewe ni bora kuliko wengine? Hapana, lakini inamaanisha wewe unatarajiwa kuwasaidia wengine kuwa bora. Je, haki yako ya uzaliwa inamaanisha wewe umeteuliwa? Ndiyo, lakini hukuteuliwa kuwatawala wengine, umeteuliwa kuwatumikia wao. Je, haki yako ya uzaliwa ni ushahidi wa upendo wa Mungu? Ndiyo, lakini muhimu zaidi, ni ushahidi wa tumaini Lake.

Ni jambo moja kupendwa na ni jambo lingine kabisa kuaminiwa. Katika mwongozo wa Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana, tunasoma: “Baba yako aliye Mbinguni anakuamini wewe. Amekupa baraka kuu, ikijumuisha utimilifu wa injili na ibada takatifu na maagano ambayo yanakuunganisha wewe Kwake na kuleta nguvu Yake ndani ya maisha yako. Pamoja na baraka hizo huja ongezeko la majukumu. Anajua unaweza kuleta utofauti katika ulimwengu, na hiyo inahitaji, katika hali nyingi, kuwa tofauti na ulimwengu.”

Uzoefu wetu wa duniani ungeweza kulinganishwa na meli ya kuvinjari ambapo Mungu amewatuma watoto Wake wote wanaposafiri kutoka pwani fulani hadi nyingine. Safari iliyojawa na fursa nyingi za kujifunza, kukua, kuwa na furaha na maendeleo lakini pia iliyojawa na hatari. Mungu anawapenda watoto Wake wote na ana shauku kuhusu ustawi wao. Yeye hataki kumpoteza ye yote kati yao, kwa hiyo Yeye anawaalika wale walio tayari kuwa mabaharia Wake—huyo ni wewe. Kwa sababu ya chaguo lako la kufanya na kushika maagano, Yeye anakupa tumaini Lake. Yeye anaamini wewe utakuwa tofauti, wa kipekee, na uliyesimikwa kwa sababu ya kazi muhimu anayokutumainia wewe ufanye.

Fikiria hilo! Mungu anawatumainieni ninyi—kati ya watu wote duniani, watoto wa agano, mabaharia Wake—kusaidia katika kazi Yake ya kuwaleta watoto Wake wote nyumbani Kwake salama. Si ajabu Rais Brigham Young wakati mmoja alisema, “Malaika wote mbinguni wanawaangalia wadogo hawa wachache walio kati ya watu.”

Wakati unapotazama ndani ya meli hii ya kuvinjari inayoitwa ulimwengu, unaweza kuona watu wengine wameketi kwenye viti vya kupumzika wakinywa, wakicheza kamari katika kasino, wamevaa nguo ambazo hazifichi mwili wao, wakipitia bila kusita kwenye simu zao za mkononi, na kupoteza muda wao mwingi wakicheza michezo ya kieletroniki. Lakini badala ya kushangaa, “Kwa nini mimi siwezi kufanya hivyo?,” unaweza kukumbuka kwamba wewe sio abiria wa kawaida. Wewe ni baharia. Una majukumu ambayo abiria hawana. Kama Dada Ardeth Kapp wakati mmoja alivyosema, “Hauwezi kuwa mwokozi kama unafanana na waogeleaji wengine ufukweni.”

Na kabla haujavunjwa moyo na wajibu wote wa ziada, tafadhali kumbuka kwamba mabaharia wanapokea kitu fulani ambacho abiria wengine hawapati: malipo. Mzee Neil L Andersen alisema, “Kuna nguvu za kiroho za kufidia kwa ajili ya wenye haki,” ikijumuisha “hakikisho kuu, uthibitisho mkuu na kujiamini kwa hali ya juu ,” Kama vile Ibrahimu wa kale, wewe unapokea furaha nyingi sana na amani, haki kuu, na maarifa mengi sana. Malipo yako sio tu nyumba huko mbinguni na njia zilizotengenezwa kwa dhahabu. Ni rahisi kwa Baba wa Mbinguni kukupatia tu vyote alivyo navyo. Hamu Yake ni kukusaidia wewe kuwa kama Yeye alivyo. Basi, kujitoa kwako kwa dhati kunadai mengi zaidi kutoka kwako kwa sababu hivyo ndivyo Mungu anavyokufanya wewe kuwa zaidi.

Ni “mengi kuyataka kwa yeyote, lakini wewe sio mtu yeyote”! Ninyi ni vijana wa haki tukufu ya uzaliwa. Uhusiano wenu pamoja na Mungu na Yesu Kristo ni uhusiano wa upendo na uaminifu ambao kwao unaweza kufikia kipimo kikubwa cha neema Yao—usaidizi Wao wa kiungu, endaumenti ya nguvu, na nguvu zenye kuwezesha. Nguvu hizo sio ndoto ya mchana, hirizi ya bahati au unabii wa kujiridhisha. Ni halisi.

Unapotimiza majukumu ya haki yako ya uzawa, kamwe hauko peke yako. Bwana wa Shamba la Mizabibu anafanya kazi shambani pamoja na wewe. Wewe unafanya kazi bega kwa bega na Yesu Kristo. Kwa kila agano jipya—na uhusiano wako na Yeye unapokuwa wa kina—mnakumbatiana kwa nguvu na kwa nguvu zaidi mpaka mnaposhikamana pamoja. Katika hiyo ishara takatifu ya neema Yake, utapata vyote viwili hamu na nguvu ili kuishi sawa sawa na jinsi Mwokozi alivyoishi—tofauti na ulimwengu. Umepata hili kwa sababu Yesu Kristo amekupata wewe!

Katika 2 Nefi 2:6 tunasoma, “Kwa hivyo, ukombozi unakuja kupitia Masiya Mtakatifu; kwani amejaa neema na kweli.” Kwa sababu Yeye amejaa ukweli, Yeye anakuona jinsi vile ulivyo—mapungufu, udhaifu, majuto, na yote. Kwa sababu Yeye amejaa neema, Yeye anakuona vile unavyoweza kuwa. Yeye anakutana na wewe pale ulipo na kukusaidia kutubu na kuwa bora, kushinda na kuwa.

“Ee Vijana wa haki tukufu ya uzaliwa, songeni, songeni, songeni!” Ninashuhudia kwamba mnapendwa—mnaaminiwa—leo, katika miaka 20, na milele. Msiuze haki yenu ya uzaliwa kwa chakula cha dengu. Msibadilishane kila kitu kwa kitu bure. Msiache ulimwengu uwabadilishe wakati ninyi mlizaliwa ili muubadilishe ulimwengu. Katika jina la Yesu Kristo, amina.