Lisha Mizizi na Matawi Yatakua
Matawi ya ushuhuda wako yatapata nguvu kutokana na imani yako ya kina kwa Baba wa Mbinguni na Mwanawe Mpendwa.
Kanisa Dogo la Zamani huko Zwickau
Mwaka wa 2024 ni mwaka muhimu kwangu. Inaadhimisha mwaka wa 75 tangu nilipobatizwa na kuthibitishwa kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho huko Zwickau, Ujerumani.
Uumini wangu katika Kanisa la Yesu Kristo ni thamani kuu kwangu. Kuhesabiwa miongoni mwa watu wa agano wa Mungu, akina kaka na dada, ni mojawapo ya heshima kuu ya maisha yangu.
Ninapofikiria kuhusu safari yangu binafsi ya uanafunzi, akili yangu mara nyingi hurejea kwenye nyumba ya zamani huko Zwickau, ambako nimetunza kumbukumbu za kuhudhuria mikutano ya sakramenti ya Kanisa la Yesu Kristo kama mtoto. Ni huko ambako mche wa ushuhuda wangu ulipokea lishe yake ya awali.
Kanisa hili lilikuwa na kinanda cha zamani kitumiacho upepo. Kila Jumapili mvulana alipangiwa kusukuma juu na chini wenzo imara iliyojaza upepo kinanda ili kukifanya kinanda kifanye kazi. Wakati mwingine nilipata fursa kubwa ya kusaidia katika kazi hii muhimu.
Wakati mkusanyiko ulipoimba nyimbo zetu pendwa za dini, nilisukuma kwa nguvu zangu zote ili kinanda kisiishiwe upepo. Kutoka kwenye kiti cha mwendeshaji viriba, niliweza kuona madirisha mazuri ya kioo, moja likimuonyesha Mwokozi Yesu Kristo na jingine likimuonyesha Joseph Smith katika Kijisitu Kitakatifu.
Bado naweza kukumbuka hisia takatifu niliyopata nilipotazama vioo hivyo vilivyomulikwa na jua wakati nikisikiliza shuhuda za Watakatifu na kuimba nyimbo za Sayuni.
Katika sehemu hiyo takatifu, Roho wa Mungu alishuhudia kwenye akili na moyo wangu kwamba ilikuwa kweli: Yesu Kristo ni Mwokozi wa ulimwengu. Hili ni Kanisa Lake. Nabii Joseph Smith alimuona Mungu Baba na Yesu Kristo na kusikia sauti Zao.
Mapema mwaka huu, nikiwa katika jukumu huko Ulaya, nilipata fursa ya kurejea Zwickau. Kwa huzuni, kanisa pendwa lile la zamani halipo tena. Lilibomolewa miaka mingi iliyopita ili kujenga jengo kubwa la makazi.
Kipi ni cha Milele, na Kipi Sicho?
Ninakiri kwamba ni huzuni kujua kwamba jengo hili pendwa la utotoni mwangu sasa ni kumbukumbu tu. Lilikuwa ni jengo takatifu kwangu. Lakini lilikuwa ni jengo tu.
Kinyume chake, ushahidi wa kiroho nilioupata kutoka kwa Roho Mtakatifu miaka hiyo mingi iliyopita haujapita bado. Na kwa hakika, umekuwa imara zaidi. Vitu nilivyojifunza katika ujana wangu kuhusu kanuni za msingi za injili ya Yesu Kristo zimekuwa ni msingi wangu imara katika maisha yangu yote. Muunganiko wa kimaagano nilioutengeneza na Baba yangu wa Mbinguni na Mwana Wake Mpendwa umebaki pamoja nami—muda mrefu tangu kanisa dogo la Zwickau libomolewe na vioo vile vya picha kupotea.
“Mbingu na dunia zitapita;” Yesu alisema, “lakini maneno yangu hayatapita.”
“Milima itaondoka, na vilima vitaondelewa, lakini wema wangu hautaondoka kutoka kwako, wala agano langu la amani liondolewe, asema Bwana.”
Mojawapo ya mambo muhimu tunayoweza kujifunza katika maisha haya ni tofauti kati ya kilicho milele na kisicho milele. Mara tu tuelewapo hilo, kila kitu hubadilika—uhusiano wetu, chaguzi tuzifanyazo, jinsi tunavyowatendea watu.
Kujua kipi ni milele na kipi sicho ni msingi katika kukuza ushuhuda wa Yesu Kristo na Kanisa Lake.
Usikosee Matawi kwa Mizizi
Injili ya urejesho ya Yesu Kristo, kama Nabii Joseph Smith alivyofundisha, “hukumbatia vyote, na kila kitu cha ukweli.” Lakini hiyo haimaanishi kwamba ukweli wote una thamani sawa. Baadhi ya kweli ni za msingi, muhimu, zenye mzizi wa imani yetu. Zingine ni viambatisho au matawi—zenye thamani, lakini ikiwa tu zimeunganishwa na zile za msingi.
Nabii Joseph Smith alisema pia, “Kanuni za msingi za dini yetu ni ushuhuda wa Mitume na Manabii, kuhusu Yesu Kristo, kwamba alikufa, akazikwa, na akafufuka tena siku ya tatu, na kupaa mbinguni; na mambo yote mengine ambayo yanahusiana na dini yetu ni viambatisho tu.”
Kwa maneno mengine, Yesu Kristo na dhabihu yake ya kulipia dhambi ni msingi wa ushuhuda wetu. Vitu vingine vyote ni matawi.
Hii haimaanishi kwamba matawi si muhimu. Mti unahitaji matawi. Lakini kama Mwokozi alivyowaambia wanafunzi Wake, “Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu.” Bila muunganiko kwa Mwokozi, kwenye lishe inayopatikana kwenye mizizi, tawi hunyauka na kufa.
Pale inapohusiana na kulisha shuhuda zetu za Yesu Kristo, huenda wakati mwingine tunakosea matawi kwa mizizi. Hili lilikuwa kosa ambalo Yesu aliliona kwa Mafarisayo wa siku Yake. Waliweka umakini mkubwa kwa vitu vidogo sana vya sheria kiasi cha kuacha kile ambacho Mwokozi alikiita “mambo makuu”—kanuni za msingi kama “haki na rehema na imani.”
Kama unataka kulisha mti, haurushii maji kwenye matawi. Unamwagilia kwenye mizizi. Vivyo hivyo, kama unataka matawi yako ya ushuhuda kukua na kuzaa matunda, lisha mizizi. Kama huna uhakika kuhusu mafundisho fulani au jambo au kipengele cha historia ya Kanisa, tafuta uwazi kwa imani yako kwa Yesu Kristo. Tafuta kuelewa dhabihu Yake kwako, upendo Wake kwako, mapenzi Yake kwako. Mfuate Yeye kwa unyenyekevu. Matawi ya ushuhuda wako yatapata nguvu kutokana na imani yako ya kina kwa Baba wa Mbinguni na Mwanawe Mpendwa.
Kwa mfano, kama unataka ushuhuda imara wa Kitabu cha Mormoni, fokasi kwenye ushahidi wake wa Yesu Kristo. Gundua jinsi Kitabu cha Mormoni kinavyomshuhudia Yeye, kile kinachokifundisha kumhusu Yeye na jinsi kinavyokualika na kukuvuvia kusonga Kwake.
Kama unatafuta uzoefu wa maana zaidi katika mikutano ya Kanisa au hekaluni, jaribu kumtafuta Mwokozi katika ibada takatifu tunazopokea huko. Mtafute Bwana katika nyumba Yake takatifu.
Kama unahisi kuchoka au kuzidiwa na wito wako wa Kanisa, jaribu kufokasi huduma yako kwa Yesu Kristo. Ifanye iwe ni dhihirisho la upendo Kwake.
Lisha mizizi, na matawi yatakua. Na baada ya muda, yatazaa matunda.
Wenye Shina na Kujengwa katika Yeye
Imani imara katika Yesu Kristo haitokei kwa usiku mmoja. Sivyo, katika ulimwengu huu, ni miiba na michongoma ya dukuduku ndivyo hukua kwa pamoja. Mti wenye afya, uzaao matunda ya imani huhitaji juhudi za makusudi. Na sehemu muhimu ya jitihada hiyo ni kuhakikisha kwamba tumekita mizizi madhubuti katika Yesu Kristo.
Kwa mfano: Mwanzoni, tunaweza kuvutwa kwenye injili ya Mwokozi na Kanisa kwa sababu tunavutiwa na waumini marafiki au kwa askofu mwema au usafi wa jengo la kanisa. Mambo haya hakika ni ya muhimu ili kukua kwa Kanisani.
Hata hivyo, kama mizizi ya ushuhuda wetu kamwe havitakua kwa kina zaidi ya hayo, nini kitatokea tutakapohamia kwenye kata yenye jengo linalovutia kidogo, yenye waumini wasio marafiki sana na askofu husema kitu kinachotukera?
Mfano mwingine: Je, ni halali kutumaini kwamba kama tukishika amri na kuunganishwa hekaluni, tutabarikiwa na familia kubwa, yenye furaha yenye watoto makini na watiifu, wote wanabakia hai Kanisani, wanatumikia misheni, wanaimba kwaya kwenye kata na kujitolea kusafisha ukumbi wa ibada kila Jumamosi asubuhi?
Ni matumaini yangu kuwa sote tutayaona haya katika maisha yetu. Lakini vipi ikiwa haitatokea? Tutabakia kwa Mwokozi bila kujali hali ilivyo—kumwamini Yeye na muda Wake?
Tunapaswa kujiuliza: Je, ushuhuda wangu u katika kile nitumainiacho kutokea katika maisha yangu? Je, unategemea matendo au mitazamo ya wengine? Au umejengwa imara katika Yesu Kristo, “wenye shina na kujengwa katika Yeye,” bila kujali hali zinazobadilika za maisha?
Desturi, Tabia na Imani
Kitabu cha Mormoni husimulia watu waliokuwa “wakamilifu kwa kuweka masharti ya Mungu.” Lakini Korihori mwenye mashaka alitokea, akifanyia mzaha injili ya Mwokozi, akiita “ya kipumbavu” na “desturi za kijinga za babu zao.” Korihori alipotosha “mbali mioyo ya wengi, na kuwafanya kubeba juu vichwa vyao kwa uovu.” Lakini hakuweza kuwadanganya wengine, kwa sababu kwao, injili ya Yesu Kristo ilikuwa zaidi ya tamaduni.
Imani ni imara ikiwa na mizizi mirefu katika uzoefu binafsi, dhamira binafsi kwa Yesu Kristo, bila kujali tamaduni zetu ni zipi au kile wasemacho wengine na kufanya.
Ushuhuda wetu utapimwa na tutajaribiwa. Imani si imani kama haitapimwa. Imani si imara kama haitapingwa. Hivyo usikate tamaa kama unapitia majaribu ya imani au maswali yasiyojibika.
Hatupaswi kutarajia kuelewa kila kitu kabla ya kutenda. Hiyo si imani. Kama Alma alivyofundisha, “Imani siyo kuwa na ufahamu kamili wa vitu.” Kama tukisubiri kutenda mpaka pale majibu ya maswali yetu yatakapojibiwa, tunazuia mema tuwezayo kukamilisha, na tunazuia nguvu ya imani yetu.
Imani ni nzuri kwa sababu hutokea hata kama baraka haziji kama ilivyotumainiwa. Hatuwezi kuona yajayo, hatujui majibu yote, lakini tunaweza kumwamini Yesu Kristo tunapoendelea kusonga mbele na juu kwa sababu Yeye ni Mwokozi na Mkombozi wetu.
Imani huvumilia majaribu na yasiyojulikana ya maisha kwa sababu imekita mizizi vyema katika Yesu Kristo na injili Yake. Yesu Kristo na Baba yetu wa Mbinguni ambaye Alimtuma, kwa pamoja wanaunda chombo kisichoyumba, cha kutegemea kikamilifu kwa imani yetu.
Ushuhuda siyo kitu unachojenga mara moja na kusimama milele. Ni zaidi kama mti ambao unaulisha kila mara. Kupanda neno la Mungu katika moyo wako ni hatua tu ya kwanza. Ushuhuda wako unapoanza kukua, ndipo kazi halisi huanza! Na hapo “utaulisha kwa uangalifu mkuu, kwamba uweze kupata mizizi, kwamba upate kukua, na kututolea matunda.” Inahitaji “jitihada kuu” na “subira kwa neno.” Lakini ahadi za Bwana ni za kweli: “Mtavuna zawadi ya imani yenu, na bidii yenu, na subira, na uvumilivu, mkingojea mti kuwatolea matunda.”
Wapendwa wangu akina kaka na dada, marafiki zangu wapendwa, kuna sehemu yangu ambayo inakumbuka kanisa dogo la zamani la Zwickau na madirisha yake yenye michoro. Lakini kwa miaka 75 iliyopita, Yesu Kristo ameniongoza kwenye safari ya maisha ambayo ni ya kufurahisha kuliko nilivyowahi kudhania. Yeye amenifariji katika mateso yangu, amenisaidia kutambua mapungufu yangu, ameponya majeraha yangu ya kiroho na kunilisha katika imani yangu inayokua.
Ni ombi langu la dhati na baraka kwamba daima tutalisha mizizi ya imani yetu katika Mwokozi, katika mafundisho Yake na katika Kanisa Lake. Juu ya hili ninashuhudia—katika jina takatifu la Mwokozi wetu, Mkombozi wetu, Bwana wetu—katika jina la Yesu Kristo, amina.