Mkutano Mkuu
“Tazama Mimi ni Mwangaza Ambao Mtainua Juu”
Mkutano mkuu wa Oktoba 2024


13:29

“Tazama Mimi ni Mwangaza Ambao Mtainua Juu”

Tunainua juu nuru ya Bwana tunaposhikilia kwa nguvu maagano yetu na tunapomuunga mkono nabii wetu aliye hai.

Kwenye shuhuda nyingi za mkutano huu, nami naongeza ushahidi wangu wa kitume kwamba Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu, Bwana na Mwokozi wetu, Mkombozi wa watoto wote wa Baba yetu. Kwa Upatanisho Wake, Yesu Kristo amefanya iwezekane kwetu sisi, kama ni wenye kustahili, kurudi katika uwepo wa Baba yetu wa Mbinguni na kuwa pamoja na familia zetu milele.

Mwokozi hajajitoa kutoka katika safari yetu ya duniani. Kwa siku mbili zilizopita tumemsikia Yeye akinena nasi kupitia viongozi Wake wateule ili tuweze kujongea karibu zaidi na Yeye. Mara kwa mara, kwa upendo Wake ulio safi na rehema, Yeye anatusaidia tunapokabiliwa na changamoto za maisha. Nefi anaeleza: “Mungu wangu amekuwa msaada wangu, ameniongoza katika mateso yangu. … Yeye amenijaza upendo Wake.”

Upendo huo ni dhahiri tunaposaidiana katika kazi Yake.

Tunamuidhinisha nabii wetu aliye hai kwenye mkutano mkuu, na Urais wa Kwanza, Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, Viongozi Wakuu wenye Mamlaka, na Maafisa wa Kanisa. Kuidhinisha inamaanisha kumkubali mtu mwingine, kumpa usikivu, kuwa waaminifu katika tumaini lao, kuyafanyia kazi maneno yao. Wananena kwa mwongozo wa Bwana, wanaelewa mambo yalivyo sasa, kushuka kwa maadili ya jamii, na jitihada za adui zinazoongezeka za kuzuia mpango wa Baba. Katika kuinua juu mikono yetu, tunaahidi kuunga mkono, sio tu kwa wakati ule bali katika maisha yetu ya kila siku.

Kuidhinisha inajumuisha kuwainua marais wetu wa vigingi, na maakofu, viongozi wa akidi na wa vikundi, walimu, na hata waelekezi wa kambi katika kata na vigingi. Karibu zaidi na nyumbani, sisi tunawainua wake zetu na waume, watoto, wazazi, familia na jamaa, na majirani. Wakati tunapoinuana sisi kwa sisi tunasema, “niko hapa kwa ajili yako, siyo tu kuinua viganja vya mikono yako ‘inaponing’inia chini’ bali kuwa faraja na nguvu kando yako.”

Dhana ya kuinua msingi wake ni katika maandiko. Katika maji ya Mormoni, wale waumini wapya wa Kanisa waliobatizwa karibuni walitoa ahadi ya “kubeba mizigo ya mmoja na ya mwingine, ili iwe miepesi; … [kuwafariji] wale ambao wanahitaji kufarijiwa, na kusimama kama mashahidi wa Mungu nyakati zote na katika vitu vyote, na katika mahali popote.”

Kwa Wanefi, Yesu alisema: “Inueni juu nuru yenu kwamba iangaze juu ya dunia. Tazama mimi ni mwangaza ambao mtainua.” Sisi tunainua juu nuru ya Bwana tunaposhikilia kwa nguvu maagano yetu na tunapomuunga mkono nabii wetu aliye hai anaponena maneno ya Mungu.

Rais Russell M. Nelson alisema, wakati akihudumu katika akidi ya Mitume Kumi na Wawili, “Kuwaidhinisha kwetu manabii ni ahadi binafsi kwamba tutafanya kwa kadiri ya uwezo wetu kuunga mkono vipaumbele vyao vya kinabii.”

Kumwinua nabii ni kazi takatifu. Hatukai tu kimya bali kwa kujishughulisha kumlinda, kufuata ushauri wake, kufundisha maneno yake na kumwombea.

Mfalme Benjamini, katika Kitabu cha Mormoni, aliwaambia watu, “Mimi niko kama ninyi, kwa unyonge wa kila aina mwilini na akilini; lakini nimechaguliwa … na nikaruhusiwa kwa mkono wa Bwana … na nimelindwa na kuhifadhiwa kwa uwezo wake usio na kipimo, ili niwatumikie kwa uwezo wote, akili, na nguvu ambazo Bwana amenipatia.”

Kuinua mikono ya Musa.

Vile vile, katika umri wa miaka 100, Rais Nelson amelindwa na kuhifadhiwa na Bwana. Rais Harold B. Lee, wakati huo akiwa mshiriki wa Urais wa Kwanza, alitoa mfano wa Musa akisimama juu ya kilele cha kilima Refidimu. “Mikono ya [Rais wa Kanisa] yawezekana ikachoka,” yeye alisema. “Inaweza kuelekea kushuka chini kwa uchovu nyakati zingine kwa sababu ya majukumu mazito, lakini tunapoinua juu mikono yake, na tunapoongoza chini ya maelekezo yake, bega kwa bega, malango ya jahanamu haitawashinda nyinyi na dhidi ya Israeli. Usalama wenu na wetu unategemea kwenye ikiwa tutamfuata au kutomfuata yule ambaye Bwana amemweka kuliongoza kanisa lake. Yeye anamjua anayemtaka aliongoze kanisa lake, na yeye hatafanya makosa.”

Rais Nelson anayo mengi kutokana na miaka mingi ya kumtumikia Bwana. Ukomavu wake, uzoefu wake mpana, hekima na mwendelezo wa kupokea mafunuo ni wa kufaa mahususi kwa ajili ya siku yetu. Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho linauandaa ulimwengu kwa ajili ya siku ambayo ‘dunia itajawa na kumjua Bwana’ (Isaya 11:9). … Kazi hii inahalalishwa na tangazo takatifu lililotolewa miaka 200 iliyopita. Iilikuwa na maneno sita pekee: “Huyu ni Mwanangu Mpendwa. Msikilize Yeye!” (ona Historia ya—Joseph Smith 1:17). ”

Rais Nelson pia amesema: “Hakujawahi kuwepo na kipindi kama cha sasa katika historia ya ulimwengu ambapo maarifa juu ya Mwokozi wetu ni ya msingi na muhimu sana binafsi kwa kila nafsi ya mwanadamu. Fikiria jinsi migogoro ya uharibifu ulimwenguni kote—na katika maisha yetu binafsi—itakavyotatuliwa kwa haraka kama sisi sote tukichagua kumfuata Yesu Kristo na kutii mafundisho Yake.”

Akina kaka na akina dada, tunahitaji kufanya zaidi mambo yenye kuinua na kupunguza kunung’unika, kushika zaidi neno la Bwana, njia Zake, na nabii Wake, ambaye amesema: mojawapo ya changamoto zetu kuu leo ni kubainisha ukweli wa Mungu na bandia za Shetani. Ndiyo sababu Bwana alituonya sisi “tuombe daima, … ili [tuweze] kumshinda Shetani, na … kuepuka mikono ya watumishi wa Shetani ambayo hufanya kazi za [adui] [Mafundisho na Maagano 10:5; msisitizo umeongezwa].”

Kuweka wakfu upya Hekalu la Manti Utah.

Aprili iliyopita, mimi na Dada Rasband tulipewa heshima ya kuungana na nabii na Dada Nelson kwa ajili ya uwekaji upya wakfu wa Hekalu la Manti, Utah.

Rais Nelson alimshangaza kila mtu alipoingia kwenye chumba. Ni wachache wetu tu tuliojua kwamba anakuja. Katika uwepo wake, mara moja nilihisi nuru na joho la kinabii analobeba. Mwonekano wa shangwe kwenye nyuso za watu wakimwona nabii ana kwa ana utabaki nami milele.

Katika sala ya uwekaji upya wakfu, Rais Nelson alimsihi Bwana kwamba nyumba Yake takatifu kimsingi ingewainua juu wote walioingia ndani ya hekalu hili “ili waweze kupokea baraka takatifu na wabakie wenye kustahili na waaminifu kwenye maagano yao … kwamba hii ipate kuwa nyumba ya amani, nyumba ya faraja, na nyumba ya ufunuo binafsi kwa wote wanaoingia milango hii wakiwa wenye kustahili.”

Sisi sote tunahitaji kuinuliwa na Bwana kwa amani, kwa faraja, na zaidi ya yote kwa ufunuo binafsi kukabili hofu, giza na ugomvi unaouzingira ulimwengu.

Kabla ya ibada, tulisimama nje juani pamoja na Rais na Dada Nelson ili kutazama machweo mazuri. Muunganiko wa Rais Nelson kwenye vizazi vya eneo hili ni wa kina sana. Mababu wanane wa baba yake walihamia na kuishi katika bonde hili linalolizunguka hekalu hili, kama ilivyokuwa kwa baadhi ya mababu zangu. Babu wa baba yangu Andrew Anderson alihudumu kwenye kundi la waanzilishi wa awali ambao walifanya kazi ya ujenzi huo kwa miaka 11 ili kukamilisha Hekalu la Manti, hekalu la tatu katika Milima ya Rocky.

Tulipokuwa tumesimama na Rais Nelson, tulipata fursa ya kumwinua na kumsaidia nabii wa Mungu katika kusherehekea uwekaji upya wakfu wa nyumba takatifu ya Bwana. Ilikuwa siku ambayo sitaisahau.

“Tunajenga mahekalu ili kumpa heshima Bwana,” Rais Nelson alisema siku ile takatifu. “Yamejengwa kwa ajili ya kuabudu na siyo kwa ajili ya maonyesho. Tunafanya maagano matakatifu yenye upekee wa milele ndani ya kuta hizi takatifu.” Tunaikusanya Israeli.

Rais Nelson na manabii waliokuwa kabla yake wameyalea mahekalu matakatifu katika mikono yao. Leo, kote ulimwenguni, tunazo nyumba takatifu za Bwana 350 ambazo zinafanya kazi, zimetangazwa, au ziko katika hatua za ujenzi. Kama nabii, tangu mwaka 2018, Rais Nelson ametangaza mahekalu 168.

“Katika wakati wetu,” amesema, “muunganiko wote, mkamilifu, na ulio kamili wa vipindi vyote, funguo, na nguvu vinapaswa kuunganishwa pamoja (ona Mafundisho na Maagano 128:18). Kwa ajili ya malengo haya matakatifu, mahekalu matakatifu sasa yanasambaa duniani. Ninasisitiza tena ya kwamba ujenzi wa mahekalu haya huenda usibadilishe maisha yenu, lakini huduma yenu hekaluni hakika itabadilisha.”

“Mwokozi na mafundisho Yake ndiyo moyo wa hekalu,” Rais anasema. “Kila kitu kinachofundishwa ndani ya hekalu, kupitia maelekezo na kupitia Roho, huongeza uelewa wetu juu ya Yesu Kristo. Ibada Zake muhimu hutuunganisha Kwake kupitia maagano matakatifu ya ukuhani. Kisha, tunaposhika maagano yetu, Yeye hutubariki kwa nguvu Yake ya uponyaji na yenye kuimarisha.

“Wale wote wanaoabudu hekaluni,” Rais Nelson alisema, “watakuwa na nguvu za Mungu na malaika ‘watawahudumia.’ [Mafundisho na Maagano 109:22]. Ni kwa kiasi gani hii huongeza kujiamini kwako kujua kwamba, kama mwanamume au mwanamke au [kijana anayehudhuria hekaluni] aliyekingwa na nguvu za Mungu, huhitaji kuyakabili maisha peke yako? Ni ujasiri gani unaupata kwa kujua kwamba malaika hakika watakusaidia?

Malaika wakitufikia ili kutuinua inaelezwa katika maandiko wakati Yesu alipopiga magoti chini kwa unyenyekevu katika Bustani ya Gethsemane. Kwa kuteseka Kwake alitoa Upatanisho usio na mwisho. “Hapo,” Rais Nelson anaeleza, “tendo moja pekee la upendo kati ya yote yaliyoandikwa katika historia lilifanyika. Pale Gethsemane, Bwana ‘aliteseka maumivu ya watu wote, kwamba wote … wapate kutubu na kuja Kwake.’[Mafundisho na Maagano 18:11].”

“Uniondolee kikombe hiki,” Yesu Kristo aliomba, “walakini si mapenzi yangu, bali yako, yatimizwe.

Na hapo malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu.”

Tunao malaika wametuzunguka sisi leo. Rais Nelson amesema, “[Hekaluni,] utajifunza jinsi ya kufungua pazia kati ya mbingu na dunia, jinsi ya kuwaomba malaika wa Mungu ili wakuhudumie wewe.”

Malaika huleta nuru. Nuru ya Mungu. Kwa Mitume Wake Wanefi, Yesu alisema, “Tazama mimi ni mwangaza ambao mtainua.” Tunapomwidhinisha nabii wetu, tunashuhudia yeye ameitwa na Mwokozi wetu, ambaye ni “nuru … ya ulimwengu.”

Rais Nelson, kwa niaba ya waumini na marafiki wa Kanisa la Bwana kote ulimwenguni, tunahisi kubarikiwa kuyainua mafundisho yako, kuinua mfano wako wa maisha kama ya Kristo, na kuinua ushuhuda wako wa dhati juu ya Bwana na Mwokozi wetu, aliye Mkombozi wetu sisi sote.

Ninatoa ushahidi wangu wa kitume kwamba Yesu Kristo ndiye “nuru … ya ulimwengu.” Na sisi sote, kama wanafunzi Wake, “tuinue juu” mwangaza Wake. Katika jina la Yesu Kristo, amina.