Maandiko Matakatifu—Msingi wa Imani
Hatuwezi kudharau upekee wa maandiko matakatifu kote katika uongofu na katika kubaki waaminifu katika injili.
Mimi na mke wangu, Mary, hivi karibuni tuliona fulana yenye picha ya kitabu na ujumbe upande wa mbele ambao unasomeka, “Vitabu: Vyombo Halisi vya Kushikwa kwa Mkono.”
Niliwaza kuhusu ujumbe huu wa kupendeza na jinsi ambavyo vifaa vya kushikwa mkononi vya kila aina vimekuwa muhimu. Baada ya kutafakari zaidi, nilitambua kwamba kifaa changu au hata kile ambacho kimewekewa akili mnemba kupitia programu kamwe havitakuwa muhimu au vya kipekee kama mwongozo wa kiroho ambao huja kutokana na ufunuo wa kiungu.
Iwe cha kushikwa mkononi au kidijitali, Biblia Takatifu na Kitabu cha Mormoni: Ushuhuda Mwingine wa Yesu Kristo vinatoa mwongozo wa kiroho na mafundisho kutoka kwa Yesu Kristo, Mwokozi wa ulimwengu. Tunavithamini vitabu hivi kutokana na kazi yake muhimu kwenye kuweka kumbukumbu ya Mwongozo wa Mungu kwa manabii na watu wa kale na mwongozo viutoao kwa ajili ya maisha yetu binafsi.
Vikiungana na mafundisho ya manabii walio hai, maandiko haya matakatifu yanatoa mwongozo wa kimafundisho kwa ajili yetu sisi katika ulimwengu wa leo. Maandiko haya ni yenye nguvu zaidi yanapotoa maelekezo, usahihishaji, faraja, na tulizo kwa watu binafsi na familia ambao wanatafuta mwongozo kutoka kwa Bwana.
Maandiko, yakiungana na msukumo wa kiungu toka kwa Roho Mtakatifu, huendelea kuwa chanzo cha msingi ambacho kinawezesha uongofu wa wale walio na mioyo iliyovunjika na roho iliyopondeka na wenye nia ya kumfuata Yesu Kristo. Maandiko yanasaidia kujenga msingi ambao unaweza kustahimili jitihada endelevu za adui za kudhoofisha imani.
Waongofu wapya wamebarikiwa na wamekuwa uhai wa Kanisa kote katika historia yake. Mfano mmoja ni wa thamani ya kipekee kwangu mimi. Nilipokuwa askofu kijana, akina dada wawili wamisionari wa kustaajabisha walikuwa wakiifundisha familia ya William Edward Mussman. Baba huyu, mwanasheria mwenye uwezo mkubwa, alikuwa mshauri mkuu wa sheria wa shirika kubwa. Mke wake mwenye kujitoa kwa dhati, Janet, aliisaidia familia hii kujitahidi kuishi zaidi maisha kama ya Kristo.
Mwana na binti yao wenye uwezo wa kipekee, wote wawili wakiwa katika miaka ya mwanzoni ya umri wao wa miaka ya 20, pia walikuwa wakifundishwa. Wote wanne walikuwa wakipokea masomo na walikuwa wakihudhuria Kanisa. Wale akina dada wamisionari walikuwa wamewahimiza kusoma Kitabu cha Mormoni na kusali kwa ajili ya ushuhuda juu ya maandiko hayo matakatifu. Cha kushangaza familia ilisoma Kitabu cha Mormoni chote kwa muda mfupi tu.
Wamisionari wa kigingi, ambao wote wawili hapo kabla walikuwa marais wa Muungano wa Usaidizi kwenye kata, waliongozana nao kwenye mkutano wa sakramenti.
Familia ilipokuwa ikikaribia ubatizo, walipokea mfululizo wa maandiko mbali mbali yenye kukosoa Kanisa. Hii ilikuwa kabla ya intaneti, lakini makaratasi yenye maandishi hayo yalilijaza boksi kubwa.
Akina dada hao wamisionari walinialika kama askofu aliyekuwa na umri wa miaka 34 kusaidia kujibu maswali yaliyokuwa yameibuliwa. Tulipokusanyika katika sebule yao, boksi kubwa lenye vipeperushi vya ukosoaji wa Kanisa lilikuwa katikati ya chumba. Nililiendea jukumu hili kwa sala. Wakati wa sala ya ufunguzi, Roho alininong’oneza kwamba “Yeye tayari anajua kwamba ni kweli.” Hii ilikuwa muhimu. Wamisionari waliamini kwamba wanafamilia wengine waliobaki walikuwa tayari na ushuhuda. Walikuwa hawana uhakika kuhusu baba.
Mara moja nilimwambia kwamba Roho ameniambia kwamba tayari anao ushuhuda. “Je, hii ilikuwa kweli?” Alinitazama kwa umakini na kusema kwamba Roho alikuwa amemthibitishia ukweli juu ya Kitabu cha Mormoni na Kanisa.
Kisha nikamuuliza kama ingekuwa na ulazima wa kurejelea vipeperushi vile, kama wamekwisha kuwa na uthibitisho wa kiroho.
Baba alijibu kwamba isingekuwa na ulazima. Wanafamilia wengine walikubaliana na jibu lake.
Alisema alikuwa na swali la kipekee: Sababu moja ya wao kupokea maandishi mengi yanayopingana na Kanisa ilikuwa kwamba wao walikuwa washiriki wa imani nyingine. Cha ziada, alikuwa ameweka ahadi kubwa ya kusaidia ujenzi wa jengo jipya la ibada kwa dhehebu lile la awali. Aliniambia kwamba akina dada wamisionari walimfundisha kuhusu umuhimu wa kulipa zaka, jambo ambalo kwa shukrani alilikubali, lakini alijiuliza kama ingekuwa siyo sahihi kuheshimu pia ahadi aliyofanya kabla. Nilimhakikishia kwamba kuitimiza ahadi itakuwa ni heshima na ni sahihi.
Familia yote ilibatizwa. Mwaka mmoja baadaye waliunganishwa kama familia katika Hekalu la Oakland California. Nilipewa heshima ya kuwepo. Kijana wa kiume alimaliza shule ya sheria, akafaulu mitihani ya Uwakili ya California, na mara moja akahudumu misheni kwa uaminifu nchini Japan. Nimeangalia kwa miaka mingi kadiri vizazi vinavyofuatia wanavyobaki waaminifu katika injili. Nilipewa heshima ya kufanya uunganishaji wa mmoja wa wajukuu wao wa kike.
Uongofu unaotokea katika siku zetu ni wa kushangaza vile vile. Juni iliyopita Kocha Andy Reid, kocha wa Kansas City Chiefs pamoja nami, pamoja na wengine tukiwakilisha imani yetu na imani nyinginezo, tulizungumza katika tukio la imani mbalimbali katika Kanisa la Riverside huko jijini New York. Kocha Reid alisisitiza juu ya nafasi ya pili na kuitikia mialiko na fursa, ambacho ndicho kile injili ya Yesu Kristo husisitiza. Asubuhi iliyofuata, tukiwa na wake zetu Tammy Reid na Mary, tulihudhuria mkutano wa sakramenti katika Kata ya Manhattan. Lilikuwa ni tukio la kiroho. Palikuwa na waongofu wengi wapya katika mkusanyiko ule. Waumini watano waliobatizwa karibuni, wanaume wanne na mvulana mmoja, walikuwa miongoni mwa washiriki wenye Ukuhani wa Haruni waliopitisha sakramenti. Ninayo furaha kuripoti kwamba kumiminika huku kwa waumini wapya wa Kanisa vilevile kunatokea kote katika Kanisa.
Tunashukuru kwa ongezeko hili linaloonekana kwa wale wanaoitikia mialiko hii mitakatifu, wanaobadili maisha yao, na kukubali fursa ya kumfuata Yesu Kristo. Wanaingia kwenye njia ya agano kupitia imani, toba, ubatizo na uthibitisho kama ilivyofundishwa katika Biblia Takatifu na Kitabu cha Mormoni.
Hatuwezi kudharau upekee wa maandiko matakatifu kote katika uongofu na katika kubaki waaminifu katika injili. Manabii wa kale katika Kitabu cha Mormoni walijua kuhusu kazi ya Yesu Kristo na walifundisha injili Yake. Kitabu cha Mormoni kinatusaidia tusogee karibu zaidi na Mungu kadiri tunavyojifunza, kuelewa na kutumia mafundisho yake. Nabii Joseph Smith alifundisha “mwanamume [au mwanamke] angesogea karibu zaidi na Mungu kwa kuishi kanuni za [kitabu] kuliko kitabu kingine chochote.”
Ili kujua kwamba Kitabu cha Mormoni ni neno la Mungu, tunahitaji kukisoma, kutafakari, na kusali kukihusu, na kisha kutenda kulingana na kanuni zake. Nabii Moroni aliahidi kwamba Mungu angefunua ukweli juu ya kitabu hiki kwetu sisi pale tunaposali kwa moyo wa dhati, kwa kusudi halisi na kwa imani katika Kristo. Kujifunza Kitabu cha Mormoni ni muhimu kwa ajili ya uongofu wa kudumu.
Tunapotafakari uhusiano kati ya Biblia na Kitabu cha Mormoni kama kifaa kishikwacho mkononi, mtu angeweza kuuliza swali. Unadhani ingesaidia na kuleta ufafanuzi kiasi gani kwa vitabu viwili kama Bwana angetamka kwamba vingeunganishwe pamoja na “kuwa kimoja mkononi mwako”? Hicho ndicho Bwana alichotamka kuhusiana na “kijiti cha Yuda,” Biblia, na “kijiti cha Yusufu,” Kitabu cha Mormoni.
Katika nyanja nyingi za kipekee, Kitabu cha Mormoni kinatoa mafundisho ya msingi ambayo yanaimarisha na kujenga juu ya Biblia. Mafundisho juu ya Upatanisho wa Yesu Kristo ni mfano muhimu.
Biblia hutoa maelezo sahihi juu ya huduma ya duniani ya Yesu Kristo, ikijumuisha kifo Chake na Ufufuko. Kitabu cha Mormoni kiko wazi zaidi kuhusu Upatanisho wa Yesu Kristo, kitu ambacho manabii walikielezea kwa kina kabla ya kifo Chake.
Kichwa cha habari cha Alma mlango wa 42 kinaakisi mafundisho ya kipekee juu ya Upatanisho wa Yesu Kristo.
Kinasomeka: “Maisha ya duniani ni wakati wa majaribio kumwezesha mtu kutubu na kumtumikia Mungu—Anguko limeleta kifo cha kimwili na cha kiroho kwa binadamu wote—Ukombozi huja kupitia toba—Mungu Mwenyewe hulipia dhambi za ulimwengu—Rehema ni kwa wale ambao wanatubu—Wengine wote wako chini ya hukumu ya Mungu—Rehema huja kwa sababu ya Upatanisho—Ni wale tu wenye toba ya kweli wanaokolewa.”
Rais Russell M. Nelson amesema, “Ninaahidi kwamba unaposoma Kitabu cha Mormoni kwa sala kila siku, utafanya maamuzi mazuri—kila siku.” Yeye pia anaahidi kwamba kama “kila siku utajizamisha mwenyewe kwenye Kitabu cha Mormoni, unaweza kukingwa dhidi ya maovu ya siku.”
Kama nilivyosema, nilivutiwa na wazo la kifaa cha asili kishikwacho mkononi—kitabu. Hata hivyo, ninatambua upekee wa ajabu wa intaneti katika ulimwengu wa leo. Kifaa kimoja cha kushika mkononi kinaweza kutoa taarifa ambayo kihistoria imejaza maktaba kubwa. Tunayo shukrani kuishi katika wakati kama huu. Kipekee ninayo shukrani kwamba kinaruhusu vitabu vitakatifu na taarifa za Kanisa kupatikana kidijitali. Intaneti ni zana yenye nguvu kwa ajili ya kujifunza injili. Leo hii, watu wengi hushiriki injili na marafiki kwa kutumia teknolojia. App ya Kitabu cha Mormoni, kwa mfano, ni njia ya kupendeza ya kuwatambulisha marafiki kwenye Kitabu cha Mormoni na kuweza kwa urahisi kushiriki katika njia za kawaida na za asili mahali popote uwapo.
Wakati intaneti inatoa baraka nyingi, kwa bahati mbaya, kama vipeperushi vilivyoandikwa vinavyokosoa Kanisa kama nilivyoeleza awali, pia imekuwa ikitumiwa kutengeneza mashaka na kudhoofisha imani katika kanuni za injili zenye thamani. Inaweza kuwa sehemu ya “uovu wa siku yetu” ambao Rais Nelson ameutaja.
Adui na wale wanaomsaidia, kwa kujua ama kwa kutokujua, wametengeneza katika intaneti, kitu kilicho sawa sawa na lile boksi lililojaa makaratasi yaliyoandikwa taarifa zenye kukosoa Kanisa nilizoeleza hapo awali, zikikusudiwa kukuweka wewe mbali na ukweli wa Mungu.
Maswala yaliyoibuliwa ili kutengeneza mashaka kwa miaka mingi yamekuwa yale yale. Huu ni ukweli maalumu unapolinganisha siku yetu na miaka ya 1960 nilipokuwa katika miaka yangu ya 20.
Maandiko yanatufundisha kutumia maamuzi na kuwa na hekima katika mambo yote. Intaneti inaweza kutumika kwa njia chanya au njia ya uharibifu.
Kwa wote waumini wa muda mrefu na wale wapya wanapojifunza injili wanahitaji kuwa wenye kusudi kuhusu kile wanachotazama. Usifurahie ukosefu wa maadili, kukosa uaminifu au taarifa zisizo za uadilifu. Ukifanya hivyo, mkusanyiko wa taarifa unaweza kukuongoza kwenye njia ambayo inaangamiza imani na kuharibu maendeleo yako ya milele. Unaweza kutendewa kwa njia chanya au hasi. Tafuta uadilifu na epuka intaneti hasi yenye uraibu ambayo itachukua muda wako na kukuacha na hisia mbaya. Jaza maisha yako na mambo chanya, mawazo mema, kuwa mwenye shangwe, burudika lakini epuka upumbavu. Kuna tofauti. Makala ya imani ya kumi na tatu ni mwongozo wa kustaajabisha. Juu ya yote, jizamishe wewe mwenyewe mara kwa mara katika Kitabu cha Mormoni, jambo ambalo litamvuta Roho katika maisha yako na kukusaidia kutambua ukweli na uongo.
Ushauri wangu kwa wale ambao kwa njia yoyote ile wamechepuka kutoka kwenye njia ya agano ni rudini kwenye maandiko matakatifu, mwongozo wa manabii, heshima kwenye mambo ya dini nyumbani na muziki wenye kujenga imani. Kila nafsi ni ya thamani kwa Bwana. Tunakuhitaji! Bwana anakuhitaji wewe, na wewe unamhitaji Yeye. Daima utakaribishwa. Wakati wa miaka yangu mingi katika huduma ya Kanisa nimewapenda watu wema ambao walirudi katika njia ya agano na kisha kuhudumu na kumbariki kila mtu waliyempenda au waliyekutana naye.
Maandiko matakatifu na manabii walio hai ni njia kuu ambayo Baba wa Mbinguni mwenye upendo hufanya mpango Wake wa furaha kupatikana kwa watoto Wake wote.
Ninatoa ushahidi wangu wa uhakika juu ya uungu wa Yesu Kristo na uhalisia wa Upatanisho Wake, katika jina la Yesu Kristo, amina.