Fokasi kwa Yesu Kristo na injili Yake
Tunapopuuza vivuruga mawazo vya ulimwengu na kufokasi kwa Yesu Kristo na injili Yake, tunahakikishiwa ufanisi.
Mwaka 1996, timu ya Nigeria ya wanaume ya mpira wa miguu ilishinda dhahabu kwenye Michezo ya Olimpiki iliyofanyika Atlanta, huko Marekani. Finali ilipoisha, makundi ya furaha yalimwangika mitaani katika kila jiji na mji nchini Nigeria; nchi hii yenye watu milioni 200 ghafla ilibadilishwa kuwa sherehe za kufana mnamo saa nane usiku! Kulikuwa na shangwe ya kuambukiza, furaha, na msisimko pale watu walipokula, kuimba na kucheza ngoma. Wakati huo, Nigeria ilikuwa imeungana, na kila Mnigeria alikuwa ameridhika kuwa Mnaijeria.
Kabla ya Olimpiki, timu hii ilikabiliwa na changamoto nyingi. Wakati mchuano ulipoanza, msaada wao wa kifedha uliisha. Timu ilishindana bila vifaa vinavyofaa, viwanja vya mazoezi, chakula, au huduma za udobi.
Wakati mmoja, walikuwa karibu sana kutolewa kwenye mashindano, lakini timu ya Nigeria walishinda licha ya magumu yote. Wakati huu muhimu ulibadilisha jinsi walivyojitazama. Wakiwa na kujiamini huko kupya, na bidii binafsi na ya timu, na ari ya dhati, walipuuza vivuruga mawazo vingi na kufokasi katika kushinda. Fokasi hii iliwashindia medali za dhahabu na Wanigeria waliibatiza timu yao “Timu ya Ndoto.” Timu ya Ndoto kwenye Olimpiki ya mwaka 1996 huendelea kurejelewa katika michezo ya Nigeria.
Mara timu ya mpira wa miguu walipojifunza kupuuza vivuruga mawazo vilivyowakabili na kufokasi kwenye lengo lao, walifanikiwa zaidi ya kile walichodhani kinawezekana na wakapata shangwe kubwa. (Kama vile ilivyokuwa kwetu sisi huko Nigeria!)
Katika njia inayofanana na hiyo, tunapopuuza vivuruga mawazo vya ulimwengu na kufokasi kwa Kristo na injili Yake, tunahakikishiwa ufanisi zaidi ya kile tunachoweza kufikiria na tunaweza kujisikia shangwe kuu. Rais Russell M. Nelson alifundisha, “Fokasi ya maisha yetu inapokuwa juu ya … Yesu Kristo na injili Yake, tunaweza kujisikia wenye shangwe bila kujali nini kinatokea—au hakitokei—katika maisha yetu.”
Ninasali kwamba Roho Mtakatifu atamsaidia kila mmoja wetu kufuata mwaliko wa Rais Nelson wa kufokasi kwa “Yesu Kristo na injili Yake” ili kwamba tuweze kujisikia wenye shangwe katika Kristo “bila kujali nini kinatokea—au hakitokei—katika maisha yetu.”
Simulizi kadhaa katika Kitabu cha Mormoni zinaelezea wale ambao walibadilisha maisha yao kabisa kwa kufokasi kwa Yesu Kristo na injili Yake.
Fikiria Alma Mdogo. Alma Mdogo aliasi na kupigana dhidi ya Kanisa. Baba yake, Alma, alisali na kufunga. Malaika alimtokea na kumwita Alma Mdogo atubu. Katika wakati ule, Alma alianza kuteseka “uchungu wa nafsi iliyolaaniwa.” Katika saa za kiza, alimkumbuka baba yake akifundisha kwamba Kristo angekuja kulipia dhambi za ulimwengu. Wakati akili yake ilipovutwa—kufokasi—kwenye wazo hili, alimsihi Mungu kwa ajili ya rehema. Shangwe ilikuwa matokeo, shangwe ambayo yeye aliielezea kama isiyo na kifani! Rehema na shangwe ilikuja kwa Alma kwa sababu yeye na baba yake walifokasi kwa Mwokozi.
Kwa wazazi ambao wana watoto ambao wamepotoka, jipeni moyo! Badala ya kujiuliza kwa nini malaika haji kumsaidia mtoto wako kutubu, jua kwamba Bwana amewaweka malaika wa duniani katika njia yake: askofu au kiongozi mwingine au kaka au dada mhudumiaji. Ikiwa unaendelea kufunga na kusali, ikiwa hautajaribu kuweka ratiba au ukomo kwa Mungu, na ikiwa wewe utatumainia kwamba Yeye ananyoosha mkono Wake kusaidia—punde au baadaye—utaona Mungu akigusa moyo wa mtoto wako wakati mtoto anapochagua kusikiliza. Hii ni kwa sababu Kristo ni shangwe—Kristo ni tumaini; Yeye ndiye ahadi “ya mambo mazuri yanayokuja.” Kwa hiyo mtumainie Yesu Kristo kwa mtoto wako, kwani Yeye ndiye nguvu ya kila mzazi na ya kila mtoto.
Mara alipopata shangwe katika Kristo, Alma Mdogo aliishi kwa hiyo shangwe. Na ni kwa jinsi gani alidumisha shangwe kama hiyo hata wakati wa magumu na majaribu? Alisema hivi:
“Tangu wakati huo hadi sasa, nimefanya kazi bila kukoma, [ili] nilete nafsi za watu kutubu; kwamba ningewaleta wapate kuonja shangwe kuu ambayo niliionja. …
“… Na … Bwana hunipa shangwe kuu katika matunda ya kazi yangu. …
“Na nimesaidiwa wakati wa majaribu na matatizo ya kila aina.”
Shangwe katika Kristo ilianza kwa Alma wakati alipoonyesha imani katika Yeye na kulilia rehema. Kisha Alma alitendea kazi imani katika Kristo kwa kufanya kazi ili kuwasaidia wengine kuonja shangwe sawa na ile. Jitihada hizi endelevu zilizalisha shangwe kuu ndani ya Alma hata katika majaribu na taabu za kila aina. Unaona,“Bwana anapenda jitihada”, na jitihada zikifokasi Kwake huleta baraka. Hata majaribu makali “yalimezwa katika shangwe ya Kristo.”.
Kundi lingine katika Kitabu cha Mormoni ambalo lilimfanya Yesu Kristo na injili Yake fokasi ya maisha yao na wakapata shangwe ni wale ambao walianzisha mji wa Helamu—mahali ambapo wangeweza kuwalea watoto na kufurahia uhuru wa kutekeleza dini yao. Watu hawa wema wakiishi maisha mazuri walitiwa utumwani na makundi ya wanyang’anyi na walipokonywa haki yao ya kibinadamu ya msingi ya kutekeleza dini. Wakati mwingine mambo mabaya hutokea kwa watu wema:
“Bwana anaonelea vyema kuwarekebisha watu wake; ndiyo, anajaribu subira na imani yao.
“Walakini—yeyote atakayeweka imani yake kwake, yeye atainuliwa juu siku ya mwisho. Ndiyo, na hivi ndivyo ilivyokuwa kwa watu hawa.”
Ni kwa jinsi gani watu hawa walivumilia kupitia majaribu yao na mateso? Kwa kufokasi kwa Kristo na injili Yake. Taabu zao hazikuwatambulisha wao, badala yake, kila mmoja wao alimgeukia Mungu, yawezekana walijitambulisha kama mtoto wa Mungu, mtoto wa agano, na mwanafunzi wa Yesu Kristo. Walipokumbuka wao walikuwa akina nani na kumlingana Mungu, walipata amani, nguvu, na hatimaye shangwe ya Kristo.
“Alma na watu wake … walimimina mioyo yao kwa [Mungu]; na alijua mawazo ya mioyo yao.
“Na ikawa kwamba sauti ya Bwana iliwafikia katika mateso yao, ikisema: lnueni vichwa vyenu na msherehekee, kwani ninajua agano ambalo mlifanya nami; na nitaagana na watu wangu na kuwakomboa kutoka utumwani.”
Kama jibu, Bwana “aliifanya mizigo … mabegani [mwao] iwe miepesi. … Ndiyo, Bwana aliwaimarisha kwamba wabebe mizigo yao kwa urahisi, na walinyenyekea kwa furaha na subira kwa mapenzi ya Bwana.” Fahamu kwamba Watakatifu hawa waliacha taabu zao, kuteseka kwao, na majaribu yao yamezwe katika shangwe ya Kristo! Kisha, katika wakati ufaao, Yeye alimwonyesha Alma njia ya kutorokea, na Alma—nabii wa Mungu—aliwaongoza salama.
Tunapofokasi kwa Kristo na kumfuata nabii Wake, sisi pia tutaongozwa kwa Kristo na kwenye shangwe ya injili Yake. Rais Nelson alifundisha: “Shangwe ina nguvu, na kufokasi kwenye shangwe huleta nguvu za Mungu katika maisha yetu. Kama ilivyo katika vitu vyote, Yesu Kristo ni mfano wetu wa mwisho, ‘ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba’ [Waebrania 12:2].”
Mama yangu hivi karibuni aliaga dunia; ilinishitua. Ninampenda mama yangu na sikutegemea kumpoteza akiwa kijana hivyo. Lakini kupitia kufariki kwake, mimi na familia yangu tulipata uzoefu wa huzuni na shangwe. Ninajua kwa sababu yake Yeye, mama hajafa—yu hai! Na ninajua kwa sababu ya Kristo na funguo za ukuhani zilizorejeshwa kupitia Nabii Joseph Smith, nitakuwa pamoja na yeye tena. Huzuni ya kumpoteza mama yangu imemezwa na shangwe ya Kristo! Ninajifunza kwamba “kufikiria selestia” na “kuacha Mungu ashinde” hujumuisha kufokasi kwenye shangwe inayopatikana katika Kristo.
Yesu anatualika: “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.” Katika jina la Yesu Kristo, amina.