Bwana Yesu Kristo Atakuja Tena
Sasa ni wakati wako na mimi wa kujiandaa kwa ajili ya Ujio wa Pili wa Bwana na Mwokozi wetu, Yesu Kristo.
Wapendwa kaka na dada zangu, ninashukuru kwamba Bwana amenibariki kuzungumza nanyi.
Katika mkutano huu, Bwana amezungumza nasi kupitia watumishi Wake. Ninawaasa kujifunza jumbe zao. Zitumieni kama kipimo cha litmasi cha kipi ni kweli na kipi sicho kwa wakati wa miezi sita ijayo.
Utunzaji na uboreshaji wa Hekalu la Salt Lake na maeneo mengine ya Temple Square umekuwa ukiendelea kwa takribani miaka mitano. Matarajio ya sasa yanaonyesha kwamba kazi hii itamalizika mwishoni mwa 2026. Tunawashukuru wale wote wanaofanya kazi kwenye mradi huu mkubwa.
Wakati wa miezi sita iliyopita, tumeweka wakfu au kurudia kuweka wakfu mahekalu tisa katika nchi tano. Kati ya sasa na mwishoni mwa mwaka, tutaweka wakfu mengine ya ziada matano
Leo tunafurahia kutangaza mipango ya kujenga mahekalu 17 zaidi. Tafadhali sikilizeni kwa unyenyekevu wakati nikitangaza maeneo.
-
Juchitán de Zaragoza, Mexico
-
Santa Ana, El Salvador
-
Medellín, Colombia
-
Santiago, Dominican Republic
-
Puerto Montt, Chile
-
Dublin, Ireland
-
Milan, Italy
-
Abuja, Naijeria
-
Kampala, Uganda
-
Maputo, Msumbiji
-
Coeur d’Alene, Idaho
-
Queen Creek, Arizona
-
El Paso, Texas
-
Huntsville, Alabama
-
Milwaukee, Wisconsin
-
Summit, New Jersey
-
Price, Utah
Wapendwa kaka na dada zangu, je, mnaona kinachoendelea mbele ya macho yetu kwa sasa? Ninasali kwamba hatutakosa utukufu wa wakati huu! Bwana kwa hakika anaharakisha kazi Yake.
Je, kwa nini tunajenga mahekalu kwa kasi isiyo na kifani? Kwa nini? Kwa sababu Bwana ametuelekeza kufanya hivyo. Baraka za hekaluni husaidia kuikusanya Israeli pande zote mbili za pazia. Baraka hizi pia husaidia kuwaandaa watu ambao watasaidia kuandaa ulimwengu kwa ajili ya Ujio wa Pili wa Bwana!
Kama nabii Isaya alivyosema, na kama ilivyonukuliwa kwenye wimbo wa Handel wa Messiah, wakati Yesu Kristo atakaporudi, “utukufu wa Bwana utafunuliwa, Na wote wenye mwili watauona pamoja.”
Katika siku ile “uweza wa kifalme utakuwa begani mwake: Naye ataitwa jina lake Mshauri wa Ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani.”
Yesu Kristo ataongoza kutoka kote Yerusalemu ya zamani na Yerusalemu Mpya “iliyojengwa kwenye bara ya Amerika.” Kutoka vituo hivi viwili, ataendesha mambo ya Kanisa Lake.
Katika siku ile Bwana atajulikana kama “Mfalme wa Wafalme, na Bwana wa Mabwana.” Wale ambao watukuwa Naye “wataitwa wateule, na waaminifu.”
Akina Kaka na dada, sasa ni wakati wako na mimi wa kujiandaa kwa ajili ya Ujio wa Pili wa Bwana na Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Sasa ni wakati wa kufanya ufuasi wetu kuwa kitu cha kipaumbele. Katika ulimwengu uliojaa vivuruga mawazo vya kutia kizunguzungu, tunawezaje kufanya hili?
Kuabudu hekaluni mara kwa mara kutatusaidia. Katika nyumba ya Bwana, tunafokasi kwa Yesu Kristo. Tunajifunza kumhusu Yeye. Tunaweka maagano ya kumfuata Yeye. Tunakuja kumjua Yeye. Tushikapo maagano ya hekaluni, tunapata ufikiaji mkubwa wa nguvu ya Mungu ya kuimarisha. Hekaluni, tunapokea ulinzi dhidi ya majaribu ya ulimwengu. Tunapata uzoefu wa upendo msafi wa Yesu Kristo na Baba yetu wa Mbinguni kwa wingi. Tunahisi amani na uhakikisho wa kiroho, dhidi ya dhoruba za ulimwengu.
Hii ni ahadi yangu kwenu: Kila anayemtafuta Yesu Kristo kwa dhati atampata hekaluni. Utahisi rehema Yake. Utapata majibu ya maswali yako magumu. Utaweza kuelewa zaidi shangwe ya injili Yake.
Nimejifunza kwamba swali la msingi zaidi ambalo kila mmoja wetu anatakiwa kulijibu ni hili: Ni kwa nani au kwa kipi nitayakabidhi maisha yangu?
Uchaguzi wangu wa kumfuata Yesu Kristo ni wa muhimu zaidi ambao nimewahi kufanya. Wakati wa mafunzo yangu ya udaktari, nilipata ushuhuda wa utakatifu wa Mungu Baba na Mwanawe, Yesu Kristo. Tangu hapo Mwokozi wetu amekuwa mwamba ambao juu yake nimejenga maisha yangu. Uchaguzi huo ulileta utofauti kwenye yote! Uchaguzi huo umewezesha chaguzi zingine nyingi kuwa rahisi sana. Uchaguzi huo umenipa dhumuni na mwongozo. Pia umenisaidia kukabiliana na tufani za maisha. Acha nishiriki mifano miwili:
Kwanza, wakati Dantzel mke wangu alipofariki ghafla, sikuweza kumfikia mtoto wetu yoyote. Nilikuwa peke yangu, niliyekata tamaa na mwenye kulia kwa ajili ya msaada. Nashukuru, kupitia Roho Wake, Bwana alinifundisha sababu ya kwa nini Dantzel alikuwa amerudishwa nyumbani. Kwa uelewa huo, nilipata faraja. Kadiri muda ulivyoenda, niliweza kuzoea huzuni yangu. Baadaye, nilimuoa Wendy mke wangu mpendwa. Yeye alikuwa kitovu cha mfano wangu wa pili.
Wakati Wendy pamoja nami tukiwa kwenye jukumu katika nchi ya mbali, wanyang’anyi wenye silaha waliweka bunduki kichwani kwangu ili kunipiga risasi. Lakini risasi haikutoka. Katika uzoefu huo, maisha yetu wote wawili yalikuwa yametishwa. Hata hivyo, Wendy na mimi tulihisi amani isiyozuilika. Ilikuwa ni amani “ipitayo akili zote.”
Akina kaka na dada, Bwana atawafariji ninyi pia! Yeye atawaimarisha. Yeye aawabariki kwa amani, hata katikati ya machafuko.
Tafadhali sikilizeni ahadi hii ya Yesu Kristo kwenu: “Nitakuwa mkono wenu wa kuume na wa kushoto, na Roho wangu atakuwa mioyoni mwenu, na malaika wangu watawazingira, ili kuwabeba juu.”
Uwezo wa kuwasaidia wa Mwokozi hauna ukomo. Mateso yake yasiyoelezeka huko Gethsemane na Kalvari yalikuwa kwa ajili yenu! Upatanisho Wake usio na mwisho ni kwa ajili yenu!
Ninawasihi kutenga muda kila wiki—katika maisha yenu yote—kuongeza uelewa wenu wa Upatanisho wa Yesu Kristo. Moyo wangu hupata huzuni kwa ajili ya wale ambao wamekwama dhambini na hawajui namna ya kutoka. Ninahuzunika kwa ajili ya wale ambao wanahangaika kiroho au ambao wanabeba mizigo mizito wao wenyewe kwa sababu hawaelewi Yesu Kristo alifanya nini kwa ajili yao.
Yesu Kristo alijichukulia mwenyewe dhambi zako, mateso yako, kuvunjika moyo kwako, na magonjwa yako. Huna haja ya kuyabeba mwenyewe! Yeye atakusamehe unapotubu. Yeye atakubariki na kile unachohitaji. Yeye atatibu nafsi yako iliyojeruhiwa. Unapojifunga nira pamoja Naye, mzigo wako utakuwa mwepesi Kama utafanya na kushika maagano ya kumfuata Yesu Kristo, utagundua kwamba nyakati za maumivu za maisha yako ni za muda. Mateso yako “yatamezwa kwenye shangwe ya Kristo.”
Si mapema wala muda haujapita wa wewe kuwa mfuasi wa kweli wa Yesu Kristo. Kisha utapata uzoefu mkamilifu wa baraka za Upatanisho Wake. Pia utakuwa na ufanisi zaidi katika kusaidia kuikusanya Israeli.
Kaka na dada zangu wapendwa, katika siku ijayo, Yesu Kristo atarudi duniani kama Masiya wa milenia. Hivyo leo ninawaasa kuweka wakfu tena maisha yenu kwa Yesu Kristo. Ninawaasa kusaidia kuikusanya Israeli iliyotawanyika na kuuandaa ulimwengu kwa ajili ya Ujio wa Pili wa Bwana. Ninawaasa kuongea kuhusu Kristo, kushuhudia kuhusu Kristo, kuwa na imani katika Kristo na kufurahia katika Kristo!
Njoo kwa Kristo na “jitoe [nafsi] yako yote” Kwake. Hii ndio siri ya shangwe maishani!
Mazuri bado yako njiani, kaka na dada zangu, kwa sababu Mwokozi anakuja tena! Mazuri bado yako njiani kwa sababu Bwana anaharakisha kazi Yake. Mazuri bado yako njiani wakati tunapogeuza mioyo na maisha yetu yote kwa Kristo.
Ninatoa ushahidi wangu wa dhati kwamba Yesu Kristo ni mwana wa Mungu. Mimi ni mfuasi Wake. Ninashukuru kuwa mtumishi Wake. Kwenye Ujio Wake wa Pili, “utukufu wa Bwana utafunuliwa na kila mwili utauona.” Siku hiyo itajawa na shangwe kwa wenye haki!
Kupitia nguvu za funguo takatifu za ukuhani nilizonazo, ninatamka ukweli huu kwenu na kwa ulimwengu wote! Katika jina la Yesu Kristo, amina.