Ujumbe wa Urais wa Kwanza
Tunaposonga Mbele Pamoja
Wapendwa akina kaka na akina dada, ninanyenyekezwa kwa kuwa nanyi asubuhi hii. Siku nne zilizopita tulimzika mwanaume mwenye kipaji, nabii wa Mungu—Rais Thomas S. Monson. Hakuna maneno yanayoweza kueleza ukuu na utukufu wa maisha yake. Daima nitahifadhi kwa upendo mkubwa urafiki wetu kwa shukrani kwa yale aliyonifunza. Sasa ni lazima tutazame mbele kwa siku zijazo kwa imani kamili katika Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye hili ni Kanisa Lake.
Siku mbili zilizopita Mitume wote walio hai walikutana katika chumba cha juu cha Hekalu la Salt Lake. Hapo walifanya maamuzi ya kauli moja, kwanza, kuunda upya Urais wa Kwanza sasa na, pili, kwamba nihudumu kama Rais wa Kanisa. Maneno hayatoshi kuwaelezea jinsi nilivyohisi kwa Ndugu zangu—Ndugu ambao wanazo funguo zote za ukuhani zilizorejeshwa kupitia Nabii Joseph Smith katika kipindi hiki cha maongozi ya Mungu—kuweka mikono yao juu ya kichwa changu kunitawaza na kunisimika kama Rais wa Kanisa. Ulikuwa ni uzoefu mtukufu na wa kunyenyekeza.
Kisha lilikuwa ni jukumu langu kumaizi wale ambao Bwana alikuwa amewaandaa wawe washauri wangu. Ni kwa jinsi gani ningechagua wawili tu miongoni mwa Mitume wengine Kumi na Wawili, ninaowapenda kila mmoja kwa dhati? Nina shukrani za dhati kwa Bwana kwa kujibu sala zangu za dhati. Nina shukrani tele kwamba Rais Dallin Harris Oaks na Rais Henry Bennion Eyring wako tayari kuhudumu pamoja nami kama Mshauri wa Kwanza na Mshauri wa Pili mtawalia. Rais Dieter F. Uchtdorf amerejea katika nafasi yake katika Akidi ya Mitume Kumi na Wawili. Tayari amekwishapokea majukumu makuu ambayo ana uwezo wa kipekee wa kuyatimiza.
Ninatoa shukrani kwake na Rais Eyring kwa huduma yao kuu kama washauri wa Rais Monson. Wamekuwa wenye uwezo kamili, wenye kujitolea, na walio na msukumo. Tunatoa shukrani nyingi sana kwao. Kila mmoja sasa yuko radhi kuhudumu anakohitajika zaidi.
Kama Mtume wa Pili katika ukuu, Rais Oaks pia anakuwa Rais wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili. Hata hivyo, ikizingatia mwito wake katika Urais wa Kwanza na kulingana na taratibu za Kanisa, Rais M. Russell Ballard, ambaye anafuata kwa ukuu, atahudumu kama Rais Mtendaji wa akidi hiyo. Urais wa Kwanza utafanya kazi bega kwa bega na wale Kumi na Wawili kumaizi mapenzi ya Bwana na kusogeza kazi Yake takatifu mbele.
Tunashukuru kwa sala zenu. Zimetolewa kote duniani kwa ajili yetu. Asubuhi baada ya kifo cha Rais Monson, sala kama hiyo ilitolewa na mvulana wa miaka minne aitwaye Benson. Ninanukuu dondoo kutoka kwenye barua aliyoandikwa na mama yake kwa mke wangu, Wendy. Benson alisali, “Baba wa Mbinguni, asante kwamba Rais Thomas S. Monson angeweza kumuona mkewe tena. Asante kwa nabii wetu mpya. Msaidie awe jasiri na asiogope kwamba ni mgeni. Msaidie kukua ili awe mwenye afya na nguvu. Msaidie awe na nguvu kwa sababu ana ukuhani. Na daima tusaidie tuwe wema.”
Ninamshukuru Mungu kwa Watoto kama hawa na kwa wazazi ambao wako makini kuhusu kujitolea kwao, kwenye kusudi na haki—kwa kila mzazi, mwalimu, na mshiriki anayebeba mizigo mizito na bado hutumikia kwa utayari. Kwa maneno mengine, kwa kila mmoja wenu, ninatoa shukrani kwa unyenyekevu kabisa.
Bwana yu katika Usukani
Tunaposonga mbele pamoja, ninawaalika kufikiria kuhusu njia tukufu ambayo kwayo Bwana anaongoza Kanisa Lake. Wakati Rais wa Kanisa anapofariki, hakuna fumbo kuhusu nani ataitwa kuhudumu katika nafasi hiyo. Hakuna ufanyaji uchaguzi, hakuna ufanyaji kampeni, lakini ufanyaji kazi mtulivu wa mpango mtakatifu wa urithi, ulioandaliwa na Bwana Mwenyewe.
Kila siku ya huduma ya Mtume ni siku ya kujifunza na kujiandaa kwa ajili ya majukumu zaidi katika siku zijazo. Inachukua miongo mingi ya huduma kwa Mtume kusonga kutoka kwenye kiti cha cheo kidogo hadi kiti cha cheo kikuu katika duara. Katika muda huo, anapata uzoefu wa moja kwa moja katika kila sehemu ya kazi ya Kanisa. Pia huja kuwafahamu vyema watu wa ulimwenguni, ikijumuisha historia zao, tamaduni zao, lugha zao wakati majukumu yanampeleka tena na tena kote duniani. Mchakato huu wa urithi wa uongozi katika Kanisa ni wa Kipekee. Sifahamu chochote kingine kama hiki. Hilo lisitustahajabishe, kwa sababu hili ni Kanisa la Bwana. Hatendi kazi kulingana na njia za wanadamu.
Nimehudumu katika Akidi ya Kumi na Wawili chini ya Marais watano wa awali wa Kanisa. Nimetazama kila Rais akipokea ufunuo na kuitikia ufunuo huo. Bwana daima amewaelekeza na daima atawaelekeza na kuwatia msukumo manabii Wake. Bwana yu katika usukani. Sisi ambao tumetawazwa kushuhudia jina Lake takatifu kote duniani tutaendelea kutafuta kujua mapenzi Yake na kuyafuata.
Baki katika Njia ya Agano
Sasa, kwa kila muumini wa Kanisa ninasema, baki katika njia ya agano. Kujitolea kwako kumfuata Mwokozi kupitia kufanya maagano Naye na Kisha kuyaishi maagano hayo kutafungua mlango kwa kila baraka ya kiroho na fadhila iliyoko kwa wanaume, wanawake, na watoto kila mahali.
Kama Urais mpya, tunataka kuanza na mwisho akilini. Kwa sababu hii, tunazungumza nanyi leo kutoka hekaluni. Mwisho ambao kila mmoja wetu hujitahidi ni kupata endaumenti kwa uwezo kutoka juu katika Nyumba ya Bwana, kuunganishwa kama familia, uaminifu katika maagano yaliyofanywa katika hekalu ambayo hutufanya tustahili baraka kubwa zaidi ya Mungu—ile ya uzima wa milele. Ibada za hekaluni na maagano unayofanya huko ni muhimu katika kuimarisha maisha yako, ndoa yako, na uwezo wako wa kupinga mashambulizi ya adui. Kuabudu kwako hekaluni na huduma yako kule kwa niaba ya mababu zako vitakubariki na ufunuo zaidi wa kibinafsi na amani na vitaimarisha kujitolea kwako kubaki katika njia ya agano.
Sasa, ikiwa umechepuka kutoka njiani, naomba nikualike kwa matumaini yote moyoni mwangu tafadhali rudi. Haijalishi matatizo yako yoyote, changamoto zako zozote, kuna nafasi yako katika hili, Kanisa la Bwana. Wewe na vizazi ambavyo havijazaliwa mtabarikiwa kwa matendo yenu kuweza kurejea sasa katika njia ya agano. Baba Yetu wa Mbinguni anawapenda watoto wake, na anataka kila mmoja wetu arudi nyumbani Kwake. Hili ndilo lengo kuu la Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho—kumsaidia kila mmoja wetu kurudi nyumbani.
Ninatoa upendo wangu wa dhati kwenu—upendo ambao umekua kwa kipindi cha miongo mingi ya kukutana nanyi, kuabudu nanyi, na kuwahudumia. Agizo letu takatifu ni kwenda katika kila taifa, ukoo, ndimi, na watu, kusaidia kuuandaa ulimwengu kwa Ujio wa Pili wa Bwana. Hili tutafanya kwa imani katika Bwana Yesu Kristo, tukijua ya kwamba Yupo katika usukani. Hii ni kazi Yake na Kanisa Lake. Sisi ni watumishi Wake.
Ninatangaza kujitolea kwangu kwa Mungu Baba yetu wa Milele na Mwana Wake, Yesu Kristo. Ninawajua, ninawapenda, na ninahidi kuwatumikia—pia nanyi—kwa kila pumzi iliyosalia katika maisha yangu. Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.