Kanuni za Kuhudumu, Machi 2019
Jinsi ya Kushiriki Ushuhuda Kiuhalisia Zaidi
Kuhudumu ni kushuhudia. Uwezo wa kubadilika wa kuhudumu unaweza kuongeza fursa zetu za kushiriki ushuhuda katika njia rasmi na zisizo rasmi.
Tumeweka agano “kusimama kama mashahidi wa Mungu nyakati zote, na katika vitu vyote na katika mahali popote” (Mosia 18:9). Kushiriki shuhuda zetu ni sehemu ya kusimama kama shahidi na ni njia yenye nguvu ya kualika Roho Mtakatifu kugusa moyo wa mtu mwingine na kubadili maisha yake.
“Ushuhuda—ushuhuda halisi, unaotolewa na Roho na kuthibitishwa na Roho Mtakatifu—hubadilisha maisha,” alisema Rais M. Russell Ballard, Rais Mkaimu wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili.1
Lakini kushiriki ushuhuda wetu inaweza kuwa inaogofya au kuleta wasiwasi kwa baadhi yetu. Hiyo yaweza kuwa ni kwa sababu tunafikiria kushiriki ushuhuda wetu kama kitu tunachofanya katika mkutano wa kufunga na kutoa ushuhuda au wakati tunapofundisha somo. Katika mazingira hayo rasmi mara nyingi tunatumia maneno fulani na vifungu vya maneno ambavyo huonekana havifai katika mazungumzo ya kawaida.
Kushiriki shuhuda zetu kunaweza kuwa baraka ya kila siku katika maisha yetu na katika maisha ya wengine pale tunapoelewa jinsi inavyoweza kuwa rahisi kushiriki kile tunachoamini katika mazingira ya kila siku. Haya ni mawazo machache ya kukuwezesha kuanza.
Ufanye Rahisi
Ushuhuda hauhitaji kuanza na kifungu cha maneno, “ningependa kutoa ushuhuda wangu,” na hauhitaji kuhitimishwa na, “Katika jina la Yesu Kristo, amina.” Ushuhuda ni onyesho la kile tunachoamini na kujua kuwa kweli. Hivyo kuzungumza na jirani yako mtaani kuhusu tatizo alilonalo na kusema, “ninajua kwamba Mungu hujibu sala,” kunaweza kuwa kwenye nguvu kama ushuhuda wowote unaotolewa kutoka kwenye mimbari kanisani. Nguvu haiji kutokana na lugha ya madoido; inakuja kutoka kwa Roho Mtakatifu akithibitisha ukweli (ona Mafundisho na Maagano 100:7–8).
Unganisha Mtiririko wa Mazungumzo ya Kawaida
Kama tuko radhi kushiriki, kuna fursa zimetuzunguka za kuunganisha ushuhuda kwenye mazungumzo ya kila siku. Kwa mfano:
-
Mtu anakuuliza kuhusu wikiendi. “Ilikuwa nzuri,” unajibu. “Kanisa lilikuwa hasa kile nilichohitaji.”
-
Mtu anaonyesha huruma baada ya kugundua changamoto katika maisha yako: “pole sana.” Unajibu: “Asante kwa kujali kwako. Ninajua kwamba Mungu atanivusha. Amekuwepo kwa ajili yangu hapo awali.”
-
Mtu anatoa maoni: “Natumai hali hii mbaya ya hewa itabadilika karibuni,” au “Basi hakika limechelewa,” au “Ona foleni hii.” Ungeweza kujibu: “Nina hakika Mungu atasaidia kila kitu kifanikiwe.”
Shiriki Uzoefu Wako
Mara nyingi tunazungumza na wenzetu kuhusu changamoto zetu. Wakati mtu anapokuambia kuhusu kile wanachopitia, unaweza kushiriki wakati ambapo Mungu alikusaidia katika majaribu yako na kushuhudia kwamba unajua Yeye atawasaidia wao pia. Bwana alisema Yeye hutuimarisha katika majaribu yetu “ili muwe mashahidi wangu hapo baadaye, na kwamba mjue kwa hakika kwamba mimi, Bwana Mungu, huwatembelea watu wangu katika mateso yao” (Mosia 24:14). Tunaweza kusimama kama mashahidi Wake pale tunaposhuhudia jinsi Yeye alivyotusaidia katika majaribu yetu.
Jiandae
Kwa baadhi yetu, kushiriki ushuhuda ghafla kunaweza kuogofya. Kuna njia tunazoweza kupanga kabla na “kuwa tayari siku zote kumjibu kila mtu atuulizaye [sisi] habari za tumaini lililo ndani [yetu]” (1 Petro 3:15).
Kwanza, kujiandaa kunaweza kumaanisha kutazama jinsi tunavyoishi. Je, tunamwalika Roho Mtakatifu ndani ya maisha yetu na kuimarisha shuhuda zetu wenyewe kila siku kupitia kuishi kwa haki? Je, tunampa Roho fursa za kuzungumza nasi na kutupatia maneno tunayohitaji kupitia sala na kusoma maandiko? Kama Bwana alivyomshauri Hyrum Smith, “Usitafute kulitangaza neno langu, bali kwanza tafuta kulipata neno langu, na kisha ulimi wako utalegezwa” (Mafundisho na Maagano 11:21).
Pili, kujiandaa kunaweza kumaanisha kutazama mbele na kuzingatia fursa unazoweza kupata siku hiyo au wiki hiyo ili kushiriki ushuhuda wako. Unaweza kujiandaa kwa ajili ya fursa hizo kwa kufikiria kuhusu jinsi zinavyoweza kukupa nafasi ya kushiriki kile unachoamini.
Baki Umejikita kwa Mwokozi na Mafundisho Yake
Rais Ballard alifundisha, “Japokuwa tunaweza kuwa na shuhuda za mambo mengi kama waumini wa Kanisa, kuna kweli za muhimu tunapaswa kufundisha na kushiriki siku zote na kila mmoja wetu.” Kama mifano, aliorodhesha: “Mungu ni Baba yetu na Yesu ndiye Kristo. Mpango wa wokovu umejikita kwenye Upatanisho wa Mwokozi. Joseph Smith alirejesha utimilifu wa injili isiyo na mwisho ya Yesu Kristo, na Kitabu cha Mormoni ni ushahidi kwamba ushuhuda wetu ni wa kweli.” Pale tunapoelezea kweli hizo za kutoka moyoni, tunamwalika Roho kutoa ushahidi kwamba kile tulichosema ni cha kweli. Rais Ballard alisisitiza kwamba “Roho hawezi kuzuiliwa wakati ushuhuda msafi wa Kristo unapotolewa.”2
Mfano wa Mwokozi
Akiwa amechoshwa na safari kupitia Samaria, Mwokozi alitulia kupumzika kisimani na alikutana na mwanamke pale. Alianzisha mazungumzo kuhusu kuchota maji kutoka kwenye kisima. Kwa kutumia jukumu hili la kila siku ambalo mwanamke alikuwa nalo lilimpa Yesu fursa ya kushuhudia juu ya maji yaliyo hai na uzima wa milele unaopatikana kwa wale wanaomwamini Yeye (ona Yohana 4:13–15, 25–26).
Ushuhuda Rahisi Unaweza Kubalidi Maisha
Rais Russell M. Nelson amesimulia kuhusu muuguzi aliyemuuliza swali daktari Nelson wa kipindi hicho baada ya utaratibu mgumu wa upasuaji. “Kwa nini hauko kama madaktari wengine wa upasuaji?” Baadhi ya madaktari wa upasuaji aliowafahamu wangekuwa wepesi kukasirika na kutumia lugha chafu wakati walipofanya utaratibu huo wenye shinikizo kubwa.
Daktari Nelson angeweza kujibu kwa njia nyingine nyingi. Lakini kwa ufupi alijibu, “Kwa sababu ninajua Kitabu cha Mormoni ni cha kweli.”
Jibu lake lilimshawishi muuguzi na mume wake kusoma Kitabu cha Mormoni. Rais Nelson baadaye alimbatiza muuguzi. Miongo kadhaa baadaye, wakati akisimamia mkutano wa kigingi huko Tennessee, Marekani, kama Mtume mpya aliyetawazwa, Rais Nelson alifurahia muunganiko ambao haukutarajiwa na muuguzi yule. Muuguzi alisimulia kwamba mazungumzo yake, yaliyoletwa na ushuhuda rahisi wa daktari Nelson na ushawishi wa Kitabu cha Mormoni, yalisaidia kuelekeza uongofu wa watu wengine 80.3
Mwaliko wa Kutenda
Usiwe na hofu kushiriki ushuhuda wako. Unaweza kuwabariki wale unaowahudumia. Ni kwa jinsi gani utatumia mawazo haya au ya kwako mwenyewe ili kushiriki ushuhuda wako leo?
© 2019 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Imepigwa chapa Marekani. Idhini ya Kiingereza: 6/18. Idhini ya kutafsiri: 6/18. Tafsiri ya Ministering Principles, March 2019. Swahili. 15764 743