2019
Tunawezaje Kujenga Utamaduni wa Mjumuisho Kanisani?
Julai 2019


ministering

Kanuni za Kuhudumu, Julai 2019

Tunawezaje Kujenga Utamaduni wa Mjumuisho Kanisani?

Tunapotazama kote katika kata na matawi yetu, tunawaona watu wanaoonekana kufaa kirahisi. Kile ambacho hatutambui ni kwamba hata kati ya wale wanaoonekana kufaa, kuna wengi wanaohisi kuachwa kando. Utafiti mmoja, kwa mfano, hivi karibuni uligundua kwamba takriban nusu ya watu wazima wa Marekani waliripoti kuhisi wapweke, kuachwa kando, au kutengwa kutoka kwa wengine.1

Ni muhimu kuhisi kujumuishwa. Ni hitaji la msingi la mwanadamu, na pale tunapohisi kutengwa, inaumiza. Kuachwa kando kunaweza kuleta hisia za huzuni au hasira.2 Wakati hatuhisi kama sisi tunajumuishwa, tunajaribu kutafuta mahala ambapo tunafarijika zaidi. Tunahitaji kumsaidia kila mtu kuhisi kwamba wanastahili kuwa kanisani.

Kujumuisha Kama Mwokozi

Mwokozi alikuwa mfano mkamilifu wa kuwathamini na kuwajumuisha wengine. Wakati alipowachagua Mitume Wake, hakujali cheo, mali, au taaluma ya juu. Yeye alimthamini mwanamke Msamaria pale kisimani, akimshuhudia juu ya utakatifu Wake bila kujali jinsi Wayahudi walivyowadharau Wasamaria (ona Yohana 4). Yeye huangalia moyo na hana upendeleo (ona 1 Samweli 16:7; Mafundisho na Maagano 38:16, 26).

Mwokozi alisema:

Amri mpya nawapa, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi. nanyi mpendane vivyo hivyo.

“Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi” (Yohana 13:34–35).

Tunaweza Kufanya Nini?

Wakati mwingine ni vigumu kujua kama mtu fulani anahisi kama yuko nje. Watu wengi hawasemi—angalau hawasemi kwa uwazi. Lakini kwa moyo wa upendo, mwongozo wa Roho Mtakatifu, na juhudi za kufahamu, tunaweza kutambua wakati mtu fulani hahisi kujumuishwa kwenye mikutano na shughuli za Kanisa.

Dalili za Yakini za Mtu Kuhisi Kutojumuishwa:

  • Ufu wa lugha ya mwili, kama vile mikono kukunjwa kwa nguvu au macho kuelekezwa chini.

  • Kukaa nyuma ya chumba au kukaa peke yake.

  • Kutohudhuria kanisani au kuhudhuria mara chache.

  • Kuondoka kwenye mikutano au shughuli mapema.

  • Kutoshiriki katika mazungumzo au somo.

Hizi zinaweza kuwa dalili za hisia zingine pia, kama vile aibu, wasiwasi, au kutokuwa huru. Waumini wanaweza kuhisi “tofauti” wakati wanapokuwa waumini wapya wa Kanisa, wanapokuwa wametoka nchi tofauti au utamaduni tofauti, au karibuni wamepitia uzoefu wa kiwewe cha mabadiliko ya maisha, kama vile talaka, kifo cha mwana familia, au kurudi mapema kutoka misheni.

Bila kujali sababu, hatupaswi kusita kuwafikia kwa upendo. Kile tunachosema na kile tunachofanya vinaweza kujenga hisia kwamba wote wanakaribishwa na wote wanahitajika.

Baadhi ya Njia za Kuwa Mjumuishaji na Mkaribishaji:

  • Mara zote usikae na mtu yuleyule kanisani.

  • Tazama zaidi ya mwonekano wa nje wa watu ili kuona utu wa kweli. (Kwa mengi juu ya mada hii, ona “Kuhudumu ni Kuwaona Wengine kama Mwokozi Anavyowaona,” Liahona, Juni 2019, 8–11.)

  • Wajumuishe wengine katika mazungumzo.

  • Alika wengine kuwa sehemu ya maisha yako. Unaweza kuwajumuisha katika shughuli ambazo tayari unazipanga.

  • Tafuta na jenga kwenye mambo mnayopenda.

  • Usizuie urafiki kwa sababu tu mtu fulani hafikii matarajio yako.

  • Unapoona jambo la kipekee kuhusu mtu, vutiwa kwenye hilo badala ya kulifunika au kuliepuka.

  • Onyesha upendo na toa sifa za dhati.

  • Chukua muda kufikiria kuhusu kile inachomaanisha hasa wakati tunaposema Kanisa ni kwa ajili ya kila mtu, bila kujali tofauti zao. Ni kwa jinsi gani tunaweza kufanya hili liwe katika uhalisia?

Mara zote si rahisi kuhisi faraja kati ya watu ambao wako tofauti na sisi. Lakini kwa kujaribu, tunaweza kuwa wazuri zaidi kwenye kutafuta thamani katika utofauti na kufurahia michango ya kipekee inayoletwa na kila mtu. Kama Mzee Dieter F. Uchtdorf wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alivyofundisha, tofauti zetu zinaweza kusaidia kutufanya watu bora, wenye furaha: “Njoo, tusaidie kujenga na kuimarisha utamaduni wa kuponya, ukarimu, na rehema kwa watoto wote wa Mungu.”3

Kubarikiwa kwa Mjumuisho

Christl Fechter alihamia nchi nyingine baada ya vita kuharibu nchi yake ya asili. Hakuzungumza lugha vizuri na hakumjua yeyote katika ujirani wake mpya, hivyo mwanzo alihisi kutengwa na mpweke.

Kama muumini wa Kanisa, alikusanya ujasiri wake na kuanza kuhudhuria kata yake mpya. Alihofu kwamba lafudhi yake nzito ingewazuia watu kutaka kuzungumza naye au kwamba angehukumiwa kwa kuwa mwanamke mseja.

Lakini alikutana na wengine ambao hawakutilia maanani tofauti yake na walimkaribisha katika jumuiya yao ya marafiki. Walifika kwa upendo, na punde alijikuta akishughulika kusaidia kufundisha darasa la msingi. Watoto walikuwa mifano mikuu ya kukubalika, na hisia ya kupendwa na kuhitajika iliimarisha imani yake na kusaidia kuchochea upya kujitolea kwake maisha yote kwa Bwana.

Muhtasari

  1. Ona Alexa Lardieri, “Study: Many Americans Report Feeling Lonely, Younger Generations More So,” U.S. News, Mei 1, 2018, usnews.com.

  2. Ona Carly K. Peterson, Laura C. Gravens, and Eddie Harmon-Jones, “Asymmetric Frontal Cortical Activity na Negative Affective Responses to Ostracism,” Social Cognitive and Affective Neuroscience, vol. 6, no. 3 (Juni 2011), 277–85.

  3. Dieter F. Uchtdorf, Dieter F. Uchtdorf, “Amini, Penda, Tenda,” Liahona, Nov. 2018, 48.