Kanuni za Kuhudumu, Agosti 2019
Je, Naweza Kumsaidia Mtu Fulani Kubadilika?
Ndiyo. Lakini wajibu wako unaweza kuwa tofauti kuliko wazo lako.
Tuliumbwa na uwezo wa kubadilika. Kukua kuelekea uwezo wetu mtakatifu ni lengo la uzoefu wetu wa maisha ya duniani. Mojawapo ya malengo yetu ya msingi ya katika kuhudumu ni kuwasaidia wengine kuja kwa Kristo na kufanya mabadiliko ya lazima kurudi kwenye uwepo Wake. Lakini kwa sababu ya uhuru wa kujiamulia, wajibu wetu katika kuwasaidia kuwa zaidi kama Kristo una kikomo.
Masomo 7 kutoka kwa Mwokozi juu ya jinsi tunavyoweza kuwasaidia wengine kuwa zaidi kama Yeye.
-
Usiogope Kualika Mabadiliko
Mwokozi hakuwa mwoga kuwaalika wengine kuacha njia za zamani nyuma na kukumbatia mafundisho Yake. Aliwaalika Petro na Yakobo kuacha kazi zao na “kuwa wavuvi wa watu”(Marko 1:17). Alimualika mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi “kwenda zake’ na kutofanya dhambi tena” (Yohana 8:11). Alimualika kijana tajiri kuacha mapenzi yake kwenye mambo ya kilimwengu na kumfuata (ona Marko 10:17–22). Sisi vilevile tunaweza kuwa vyote wenye ujasiri na wenye upendo tunapowaalika wengine kufanya mabadiliko na kumfuata Mwokozi.
-
Kumbuka ni Chaguo lao Kubadilika
Aina ya mabadiliko Mwokozi anayotaka hayawezi kulazimishwa. Mwokozi alifundisha na alialika, lakini hakulazimisha. Kijana tajiri “alienda zake kwa huzuni” (Mathayo 19:22). Katika Kapernaumu, wengi wa wafuasi Wake walichagua “kurejea nyuma”, na Aliwauliza wale kumi na wawili kama wao pia wangeondoka (ona Yohana 6:66–67). Baadhi ya wafuasi wa Yohana Mbatizaji walichagua kumfuata Mwokozi, wengine hawakufanya hivyo (ona Yohana1:35–37; 10:40–42). Tunaweza kuwaalika wengine kuwa zaidi kama Yeye, lakini hatuwezi kufanya uamuzi wa kubadilika kwa ajili yao. Na kama bado hawajachagua kubadilika, tusikate tamaa—wala hatupaswi kuhisi kama tumeshindwa.
-
Sali kwa ajili ya Uwezo wa wengine Kubadilika
Wakati wa Sala Yake ya Kuombea, Yesu alimwomba Mungu kwamba wafuasi Wake wangewekwa mbali na uovu, wangekuwa zaidi kama Yeye na Baba, na wangejazwa na upendo wa Mungu (ona Yohana 17:11, 21–23, 26). Na akijua kwamba Petro angehitaji nguvu katika juhudi zake za kukua kwenye jukumu lake, Mwokozi alisali kwa ajili yake (ona Luka 22:32). Sala zetu kwa ajili ya wengine zinaweza kuleta tofauti (ona Yakobo 5:15).
-
Wafundishe Kutegemea Uwezo Wake
Ni kwa kupitia tu kwa Mwokozi ambapo tunaweza kwa kweli kubadilika na kukua kuelekea uwezekano mtakatifu tulionao sote. Yeye ni “njia, kweli, na uzima: mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya [Yeye]” (Yohana 14:6). Ni uwezo Wake ambao unaweza “kufanya vitu dhaifu kuwa vya nguvu” (Etheri 12:27). Ilikuwa imani katika uwezo Wake wa upatanisho ambao ulimwezesha Alma Mdogo kubadilika (ona Aima 36:16–23). Tunaweza kuwafundisha wengine kumtegemea Mwokozi ili kwamba wao pia waweze kuwa na uwezo Wake wa kutakasa katika maisha yao.
-
Watendee kama Wanavyoweza Kuwa
Upendo na kukubalika vinaweza kuwa vichocheo vya nguvu kubwa ya mabadiliko. Mwanamke kisimani alikuwa akiishi na mwanaume ambaye hakuwa mumewe. Wafuasi wa Yesu “walishangazwa kwamba alizungumza na mwanamke” (Yohana 4:27), lakini Yesu alijali zaidi kuhusu kile ambacho angeweza kuwa. Alimfundisha na kumpa fursa ya kubadilika, na alibadilika. (Ona Yohana 4:4–42.)
Tunapowatendea wengine kama ambavyo wamekuwa badala ya kama wanavyoweza kuwa, tunaweza kuwamisha kusonga mbele. Badala yake, tunaweza kuwasamehe na kusahau makosa yaliyopita. Tunaweza kuamini kwamba wengine wanaweza kubadilika. Tunaweza kusamehe unyonge na kuonesha tabia chanya ambazo hawataweza kuziona ndani yao. “Tuna jukumu la kuona watu binafsi sio kama walivyo bali kama wanavyoweza kuwa.”1
-
Waache Waende kwa hatua Zao Wenyewe
Mabadiliko hukuchukua muda. Sisi sote lazima “tuendelee kwa uvumilivu hadi [tutakapokuwa] tumekamilika” (Mafundisho na Maagano 67:13). Yesu alikuwa na uvumilivu kwa wengine na aliendelea kufundisha hata wale waliompinga, akishuhudia juu ya wajibu aliopewa na Baba yake na kujibu maswali yao (ona Mathayo 12:1–13; Yohana 7:28–29). Tunaweza kuwa wavumilivu kwa wengine na kuwatia moyo wawe wavumilivu kwao wenyewe.
-
Usikate Tamaa Kama Watarejea kwenye Njia za zamani
Baada ya Kristo kufa, hata Petro na baadhi ya mitume wengine walirejea kwenye kile walichokizoea (ona Yohana 21:3). Kristo alimkumbusha Petro kwamba alihitaji “kuwalisha kondoo [Wake]” (ona Yohana 21:15–17), na Petro alirudi kwenye utumishi. Inaweza kuwa rahisi mno kurudi kwenye njia za awali. Tunaweza kuendelea kusaidia kwa kutia moyo kwa upole na mialiko ya kuvutia kuendelea kumfuata Mwokozi na kujitahidi kuwa zaidi kama Yeye.
Waruhusu Wengine Kukua
Mzee Jeffrey R. Holland wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili anaelezea hadithi hii kuhusu kuwaruhusu wengine kukua: “Niliwahi kuelezwa juu ya kijana ambaye kwa miaka mingi alikuwa takribani sehemu kubwa ya kila mzaha katika shule yake. Alikuwa na mapungufu fulani, na ilikuwa rahisi kwa kundi rika lake kumchokoza. Baadaye katika maisha yake alisonga mbele. Hatimaye alijiunga na jeshi na alikuwa na uzoefu wenye mafanikio kule katika kupata elimu na kwa ujumla kuachana na maisha yake ya nyuma. Juu ya yote, kama wengi jeshini wanavyofanya, aligundua uzuri na utukufu wa Kanisa na akawa mshiriki mkamilifu na mwenye furaha ndani yake.
“Kisha, baada ya miaka michache, alirudi kwenye mji wa ujana wake. Wengi wa uzao wake walikuwa wameondoka bali si wote. Inavyoonekana, aliporudi akiwa amefanikiwa hasa na kuzaliwa upya, akili zilezile za zamani ambazo zilikuwepo kabla ziliendelea kuwepo, zikisubiri kurudi kwake. Kwa watu katika mji wake wa nyumbani, alikuwa bado tu ‘yule yule.’ …
“Pole pole juhudi za mtu huyu kuacha kile ambacho kilikuwa kimepita na kushika kwa nguvu zawadi ambayo Mungu ameiweka mbele yake polepole ilipungua mpaka alipokufa katika njia aliyoishi wakati wa ujana wake. … Kibaya zaidi, huzuni kubwa kwamba alipaswa tena kuzungukwa na … wale waliofikiri maisha yake ya zamani yalipendeza zaidi kuliko maisha yake ya baadaye. Walifanikiwa kunyakua kutoka kwenye mshiko wake wa nguvu kile ambacho Kristo alikuwa amemshikisha kwa nguvu. Na alikufa kwa huzuni, ingawa kupitia kosa lake mwenyewe dogo. …
“Waache watu watubu. “Waache watu wakue. Amini kwamba watu wanaweza kubadilika na kufanya vizuri zaidi.”2
© 2019 by Intellectual Reserve, Inc. Inc All rights reserved. Imepigwa chapa Marekani. Idhini ya Kiingereza: 6/18. Idhini ya kutafsiri: 6/18. Tafsiri ya Ministering Principles, August 2019. Swahili. 15769 743