Kanuni za Kutumikia, Januari 2020
Ukusanyaji wa Israeli kupitia Kuhudumu
Kuhudumu ni fursa ya kufuata ushauri wa nabii wa kukusanya Israeli.
Rais Russell M. Nelson ametualika kusaidia kukusanya Israeli—”jambo muhimu sana linalofanyika duniani leo.”1
Kwa wale wanaotaka kuwa sehemu ya kazi hii ya kukusanya Israeli, kuhudumu kunaweza kuwa fursa ya ajabu. Ni njia ya kutia moyo kubadili maisha ya watu. Iwe tunahudumu kwa waumini wasioshiriki kikamilifu au kuwaalika kutusaidia tunapowatumikia wale wasio wa imani yetu, kuhudumu kunatoa fursa za kukusanya Israeli.
Kuwaokoa Waumini Wanaorudi
“Pamoja na upendo kama motisha, miujiza itatokea, na tutapata njia ya kuwaleta akina dada na akina kaka zetu “waliopotea” katika kumbatio la pamoja la injili ya Yesu Kristo,” —Jean B. Bingham2
“Nimekuwa nisiyeshiriki kwa takribani miaka sita wakati mume wangu nami tulipohamia mji mpya. Rais wangu mpya wa Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama, alizungumza nami, akiniomba kama angeweza kumtuma dada kunitembelea. Kwa wasiwasi kiasi, nilikubali. Dada huyu alinitembelea kila mwezi, bila kujali mzio wake kwa mbwa—na nina mbwa mwenye upendo sana! Uhudumiaji wake uliendelea kwa miaka miwili, na ulikuwa na adhari kubwa kwangu.
“Ingawa kutembelea kwake kulikuwa kwa kawaida kabisa aghalabu kiushirikiano, mara chache aliniuliza maswali ambayo yalituongoza kwenye mazungumzo ya kiroho. Haya yalinifanya kidogo kuwa na wasiwasi sana, lakini yalinishawishi kuamua ikiwa nitasonga mbele katika injili au kubaki pale nilipokuwa. Uamuzi huu ulikuwa ni jambo gumu kwangu, lakini nilichagua kutembelewa na dada wamisionari.
“Siku niliyokwenda kuhudhuria mkutano wa sakramenti kwa mara ya kwanza katika miaka sita, niliogopa kuingia ndani. Nilipoingia kanisani, dada yangu anayenihudumia alikuwa akinisubiri, na tuliingia pamoja kanisani. Baada ya hapo, alinisindikiza kwenye gari langu, akiniuliza angefanya nini zaidi kunisaidia wakati ninaposonga karibu zaidi kwa Mwokozi.
“Muda na upendo wa dada yangu aliyenihudumia ulisaidia kuniongoza kurudi kwenye ushirika, na ninachukulia juhudi zake kama mojawapo ya zawadi kubwa mno nilizowahi kupewa. Ninashukuru alikuwa pale pembeni mwangu kwenye safari yangu ya kurudi kwenye Kanisa la Mwokozi.”
Jina limefichwa, British Columbia, Canada
Kanuni za Kuzingatia
“Alinitembelea kila mwezi”
Jinsi gani unaweza kuonesha kwamba unawajali zaidi wale unaowahudumia kuliko mambo mengine? (ona Mafundisho na Maagano 121:44).
“Maswali”
Kuuliza maswali sahihi kunaweza kusaidia kusababisha ukadiriaji wa binafsi. Kumbuka kwamba kuhudumia kwetu kuna sababu ambayo inakwenda zaidi ya kuwa ushirikiano.3
“Akinisubiri”
Kila mtu anapaswa kuhisi kukaribishwa (ona 3 Nefi 18:32).
“Pale pembeni mwangu kwenye safari yangu ya kurudi”
Msaada wetu unaweza kufanya tofauti yenye maana kwa wale waliojikwaa kurudi kwa Mwokozi na kuponywa (ona Waebrania 12:12–13).
Kuhudumu na Kukusanya
“Kwa njia yoyote inayoonekana ya asili na ya kawaida kwako, shiriki na watu kwa nini Yesu Kristo na Kanisa Lake ni muhimu kwako. …
“… Jukumu lako ni kushiriki kile kilichopo moyoni mwako na kuishi kulingana na imani zako.” —Mzee Dieter F. Uchtdorf4
Kuhudumu na kushiriki injili huendana pamoja. Hizi ni baadhi ya njia tunaweza kuwakusanya rafiki zetu na majirani wakati tunapohudumia—au kuhudumu wakati tunakusanya marafiki zetu na majirani:
-
Tumikia pamoja. Tafuta fursa kuwaalika marafiki au majirani kujiunga nawe katika kuhudumia mahitaji ya mtu fulani. Waombe wakusaidie kuandaa mlo kwa ajili ya mama mgeni, tembelea jirani mzee, au safisha nyumba ya mtu fulani mgonjwa.
-
Fundisheni pamoja. Fikiria kumwalika rafiki au jirani ambaye hahudhurii kanisani kila mara kuwa mwenyeji wa somo la wamisionari katika nyumba yao kwa ajili ya mtu anayekutana na wamisionari. Au rafiki yako angeweza kukusaidia katika kuwa mwenyeji wa somo katika nyumba yako au kwenda pamoja nawe kwenye somo katika nyumba ya mtu mwingine.
-
Wanyooshee mkono wengine unapoona hitaji. Ahidi kupanga usafiri kwenda kanisani. Waalike Watoto kwenye shughuli za vijana au Msingi. Ni njia zipi zingine ungeweza kuhudumia na kukusanya?
-
Tumia nyenzo zilizotolewa na Kanisa. Kanisa linatoa nyenzo nyingi kwa ajili ya waumini kuwasaidia kushiriki injili. Unaweza kutembelea kupitia sehemu ya the “Missionary” katika Gospel Library app na tembelea ComeUntoChrist.org kwa mawazo juu ya jinsi ya kukuanya Israeli katika jumuiya zetu.
© 2020 by Intellectual Reserve, Inc. All rights reserved. Imepigwa chapa Marekani. Idhini ya Kiingereza: 6/19. Idhini ya kutafsiri: 6/19. Tafsiri ya Ministering Principles, January 2020. Swahili. 16984 743