Kanuni za Kuhudumu, Machi 2020
Kuhudumu kupitia Huduma za Hekaluni
Wakati tunapowasaidia wengine kufurahia baraka za hekaluni, tunahudumu.
Kuhudhuria hekaluni kuna faida. Rais Russell M. Nelson alifundisha kwamba “hekalu ni muhimu kwa wokovu na kuinuliwa kwetu na kwa familia zetu. …
“… Kila mmoja wetu anahitaji kuimarishwa kiroho kunakoendelea na kufundishwa ambako kuna wezekana tu katika nyumba ya Bwana.”1
Kuhudhuria hekaluni kunahitaji kupanga muda wetu, majukumu, na mali, vilevile kuwa tayari kiroho. Tunahudumia wakati tunapotambua vikwazo ambavyo vinawaweka kaka na dada zetu mbali na hekalu na kuwasaidia kutafuta suluhisho.
Hekalu ni Baraka Yeyote Anaweza Kufurahia
Mmisionari aliyerudi hivi karibuni, Meg, alikuwa anatembea kuelekea milango ya Hekalu la Kona Hawaii alipomuona msichana amekaa peke yake kwenye benchi nje. Meg alihisi kwamba anapaswa kuzungumza na msichana, lakini hakuwa na uhakika aseme nini. Kwa hivyo aliuliza kuhusu maana ya mchoro kwenye kifundo cha mguu cha yule msichana. Hicho kilianzisha mazungumzo ambayo yalimwezesha msichana, Lani, kushiriki hadithi yake.
Lani alimwambia Meg kuhusu juhudi zake za kurudi kwenye ushiriki kamili katika Kanisa, waumini wema waliokuwa wanamsaidia, na matumaini yake ya siku moja kuunganishwa na binti yake mchanga.
Meg alimwalika Lani aje kukaa katika chumba cha kusubiri cha hekalu pamoja naye. Bado wasingeweza kwenda mbele zaidi ndani ya hekalu, lakini wangeweza kuingia kiasi. Lani alikubali, na walikwenda pamoja kupitia lango kuu. Mtumikiaji hekaluni aliwaelekeza kwenye benchi chini ya picha iliyochorwa ya Mwokozi.
Walipokuwa wameketi pamoja, Lani alinong’ona, “Kwa kweli nilitaka kuja hekaluni leo, lakini nilikuwa na wasiwasi.” Kwa sababu Meg alimfuata Roho, alisaidia kujibu sala ya kimya ya Lani.
Mawazo ya Kuwasaidia Wale wasio na Kibali cha Hekaluni
Hata wale ambao hawana kibali cha hekaluni bado wanaweza kubarikiwa na hekalu.
-
Shiriki hisia zako kuhusu jinsi Bwana amekubariki kupitia kazi ya hekaluni.
-
Mualike mtu fulani kuhudhuria sherehe ya ufunguzi wa hekalu au kituo cha wageni. Tafuta sherehe zijazo za ufunguzi wa mahekalu katika temples.ChurchofJesusChrist.org.
-
Angalia picha na jifunze zaidi kuhusu hekalu kwenye temples.ChurchofJesusChrist.org.
Fanya Mahudhurio ya Hekaluni kuwa Rahisi zaidi kwa Wengine
Hata kwa waumini walio na kibali cha hekaluni, kuhudhuria hekaluni kunaweza kuwa changamoto. Baadhi wanaweza kuhitaji kusafiri umbali mrefu. Wengine wanaweza kuwa na watoto wadogo au wanafamilia wazee wanaohitaji matunzo. Tunaweza kufanya kazi kwa pamoja kufanya huduma ya hekaluni iwezekane kwa kila mtu.
Leola Chandler alihisi kuzidiwa na kumtunza mumewe mgonjwa na watoto wao wanne. Kwa hivyo aliamua kutenga muda kila Jumanne kuhudhuria hekalu la karibu. Ikawa chanzo cha amani na uwezo katika maisha yake.
Siku moja alisikia kwamba akina dada wazee wachache katika kata yake walikuwa na shauku ya kutaka kuhudhuria hekaluni, lakini hawakuwa na uwezo wa usafiri. Leola alijitolea kuwapa usafiri. Kwa miaka 40 iliyofuata, mara chache sana alikwenda peke yake hekaluni.2
Leola alibarikiwa, na alibariki wengine alipojitolea kwenda pamoja nao hekaluni.
Mawazo ya Kuwasaidia Wengine Kuhudhuria Hekaluni
Unawezaje kuwasaidia wengine kwenda hekaluni mara kwa mara? Unaweza kukuta kwamba mawazo sawa na hayo yamekusaidia wewe pia.
-
Nendeni pamoja. Jitolee kutoa au panga usafiri kwa ajili ya mtu fulani. Inaweza kumtia moyo mtu mwingine kuhudhuria hekaluni pia.
-
Waombe wanafamilia yako au kata kukusaidia kufanya ibada kwa niaba ya mababu zako, hususani unapokuwa na majina mengi ya familia tayari kwa kufanyiwa ibada.
-
Jitolee kukaa na watoto ili wazazi waweze kuhudhuria hekaluni. Au panga kuchukua zamu kuwatunza watoto wa mwenzako.
Wakati Hekalu Liko Mbali Sana
Chandradas “Roshan” na Sheron Antony wa Colombo, Sri Lanka, waliamua kuunganishwa katika hekalu. Rafiki zao Ann na Anton Kumarasamy walifurahia sana juu yao. Lakini walijua kwamba kufika Hekalu la Manila Ufilipino haikuwa rahisi au gharama nafuu.
Roshan na Sheron walikuwa wamedunduliza fedha zao na kuweka nafasi ya usafiri wa ndege miezi mingi kabla ili kupata usafiri wa anga ambao wangeweza kuumudu. Hatimaye, siku ilifika. Hata hivyo, wakati wa kupumzika Malaysia kusubiri kusafiri zaidi, waligundua kwamba kuendelea kwenda Ufilipino, walihitaji ama visa au walihitaji kutumia shirika la ndege tofauti. Ilikuwa haiwezekani kupata visa, na wasingeweza kumudu kununua tiketi kwenye shirika lingine la ndege. Lakini wasingeweza kuvumilia wazo la kurudi nyumbani bila kuunganishwa.
Bila uhakika wa nini kingine cha kufanya, Roshan alimpigia simu Anton. Anton na Ann walifanya kila wawezalo kutaka kuwasaidia. Walikuwa ni moja kati ya wanandoa wachache huko Sri Lanka waliounganishwa hekaluni, na walijua ilikuwa ni baraka kiasi gani. Lakini hivi karibuni walikuwa wametumia akiba yao kumsaidia mwanafamilia aliyekuwa na uhitaji, na hawakuwa na pesa za kutosha kuwasaidia Roshan na Sheron kununua tiketi kwa ajili ya usafiri mpya wa anga.
Nchini Sri Lanka ni kawaida kwa bwana arusi kumnunulia bibi arusi mkufu wa dhahabu ili kwamba aweze kuwa na fedha kiasi ikiwa mumewe atafariki. Ann aliamua kuuza mkufu wake kusaidia kununua tiketi mpya. Zawadi yake ya ukarimu iliwawezesha Roshan na Sheron kukamilisha miadi yao hekaluni Manila.
“Ninajua gharama ya kuunganishwa hekaluni,” Ann alisema. “Nilijua Sharon na Roshan wangekuwa nguvu kubwa katika tawi. Sikutaka wakose fursa hii.”3
Mawazo ya Kuwasaidia Wale Wasioweza Kuhudhuria Hekaluni
Unaweza kuitwa kuwahudumia wale wasioweza kabisa kuhudhuria hekaluni au kuhudhuria mara kwa mara kwa sababu ya umbali au gharama. Lakini unaweza bado kupata njia za kuwasaidia kufurahia baraka za hekaluni.
-
Fundisha au shirikini kwa pamoja katika madarasa ya matayarisho ya hekaluni au historia ya familia.
-
Wape picha ya hekalu wakaning’inize nyumbani mwao.
-
Kama umewahi kuwa hekaluni, shiriki hisia zako kuhusu uzoefu wako na ushuhuda wako wa ibada za hekaluni.
-
Wasaidie kujifunza zaidi kuhusu maagano waliyoyafanya na jinsi ya kuyatunza. Fikiria kutumia “Kuelewa Maagano Yetu na Mungu: Maelezo ya Jumla ya Ahadi Zetu za Muhimu Sana, katika Liahona ya Julai 2012
© 2020 na Intellectual Reserve, Inc. All rights reserved. Imepigwa chapa Marekani. Idhini ya Kiingereza: 6/19. Idhini ya kutafsiri: 6/19. Tafsiri ya Ministering Principles, March 2020. Swahili. 16985 743