“Kuhudumu kupitia Shughuli za Kanisa,” Liahona, Julai 2020
Kanuni za Kuhudumu, Julai 2020
Kuhudumu kupitia Shughuli za Kanisa
Taarifa ya Mhariri: Makala hii ilitengenezwa kabla ya janga la ulimwengu la COVID-19 Baadhi ya mapendekezo hapo chini hayatatumika katika wakati wa kuzingatia umbali kati ya mtu na mtu lakini yatatumika mara mikutano na shughuli za Kanisa zitakapoanza tena. Kama itahitajika, tafadhali tohoa mapendekezo haya kulingana na miongozo ya sasa ya Kanisa na serikali.
Njia mojawapo tunayoweza kuwahudumia waumini wenzetu wa kata, majirani, na marafiki ni kupitia shughuli za Kanisa. Iwe unapanga shughuli kwa kuzingatia mahitaji au mapendeleo ya mtu fulani unayemhudumia au unawaalika kushiriki katika shughuli au fursa ya huduma kwa wengine, shughuli za kata, kigingi, au hata katika kiwango cha vigingi vingi zinaweza kuwa ni njia zenye maana na zenye kufurahisha za kukuza umoja na kuwaimarisha waumini.
Shughuli za Kanisa zinaweza pia kufungua mlango kwa ajili ya fursa nyingi za kuhudumu. Kwa mfano, shughuli za Kanisa zinaweza kutoa fursa za kushiriki katika miradi ya kutoa huduma ambayo inawabariki wengine na kuleta uhusiano chanya katika jumuiya. Shughuli za Kanisa zinaweza pia kuwa nafasi ya kuwafikia waumini wa Kanisa wasioshiriki kikamilifu na marafiki wa imani nyingine au marafiki wasiojishirikisha na dini.
Kuwajumuisha watu wengi katika shughuli za Kanisa kunatengeneza fursa kwa ajili ya Bwana kubariki na kuimarisha kata na matawi yetu, ujirani wetu na jumuiya zetu.
Kujenga Mahusiano Chanya
Majira ya baridi yalikuwa yanakuja, na David Dickson hakuwa anajua jinsi ya kuipa familia yake joto.
David, mke wake, na mabinti wawili walikuwa punde wamefika kwenye mji huu wa viijijini wa Fredonia, Arizona, Marekani, sura ya nchi yenye mwinuko wa jangwa iliyozungukwa na miteremko ya kupendeza ya rangi nyekundu, vichaka na mimea ya kijani inayomea mwaka mzima.
Nyumba ambayo akina Dickson walipanga ilitegemea jiko la kuchoma kuni kama chanzo kikuu cha kuwapa joto. David kwa haraka alijifunza kuwa kukusanya kuni ilikuwa ujuzi muhimu sana kwa sababu majira ya baridi katika Fredonia yamejaa theluji na barafu.
“Sikuwa na kuni kabisa au msumeno au hata maarifa ya jinsi ya kuutumia!” David anasema “Sikujua kitu cha kufanya.”
Baadhi ya waumini wa kata walimuuliza David kama familia yake ilikuwa na kuni za kutosha kuwafikisha mwisho wa majira ya baridi. “Haikuwachukuwa muda mrefu wao kutambua kuwa sikuwa nazo,” David anasema. “Akidi ya wazee punde wakaomba wanisaidie kukusanya kuni. Nikiwa nimejawa na shukrani, nilikubali ombi lao.”
David mara akagundua kuwa safari hii ya kukusanya kuni ilikuwa ndiyo hasa moja ya shughuli za kata iliyopangiliwa vyema, iliyoandaliwa vyema na iliyohudhuriwa vyema. Asubuhi ya Jumamosi moja, David, akidi ya wazee, na waumini wengine wa kata walielekea milimani katika msafara wa magari na matela.
“Katika mchana mmoja, shukrani kwa zana zao na ujuzi wao, waumini wa kata, waliipa familia yangu rundo la kuni ambazo zilidumu kwa sehemu kubwa ya majira mawili ya baridi,” David anasema. “Muhimu zaidi, nilifundishwa kila kitu nilichohitaji kujua kuhusu kukusanya kuni mimi mwenyewe. Wakati naondoka Fredonia, nilikuwa najua jinsi ya kuutumia msumeno, na nilisaidia sana kwenye shughuli nyingi zaidi za kata za kukusanya kuni kuliko ninavyoweza kuhesabu.”
Shughuli za kata za jinsi hii siyo tu zilijenga mahusiano chanya miongoni mwa waumini wa Kanisa bali pia zilijenga mahusiano chanya na kila mtu katika jumuiya.
“Ninamkumbuka mwanamke mmoja, siyo muumini wa Kanisa, ambaye alikuwa mgeni katika eneo letu,” David anasema. “Alikuwa amelazimika kuchoma kuni za vipande vya mlango kutoka katika nyumba yake ili kumpatia joto. Mara tulipojua kuhusu mkasa wake, tulihakikisha alikuwa na kuni za kutosha ili kumfikisha hadi mwisho wa majira ya baridi. Alikuwa mwenye shukrani sana hata hakuweza kuongea.”
Jitihada za kuhudumu katika Fredonia zilihakikisha kwamba kila mtu alikaa salama na mwenye joto majira yote ya baridi.
Kuwafikia Wengine
Wakati akihudumu misheni huko Romania, Meg Yost na mwenza wake mara kwa mara waliitembelea familia ambayo ilikuwa haijahudhuria Kanisani kwa siku nyingi. “Akina Stanica walikuwa miongoni mwa waumini wa mwanzo kabisa wa Kanisa katika Romania”, Meg anasema, “na tuliwapenda.”
Wakati muda ulipofika wa kupanga na kuandaa shughuli ya tawi, viongozi waliamua kwamba tawi lingekuwa na “Usiku wa Waanzilishi.” Huu ungekuwa ni usiku wa kuwasherehekea waumini majasiri waliovuka Marekani ili kwenda Bonde la Salt Lake. Pia ingekuwa ni fursa ya kuwaenzi waanzilishi wa Kanisa katika Romania.
“Tulifikiria ingekuwa njia nzuri kwa baadhi ya waumini kutoa ushuhuda juu ya uongofu wao na jinsi walivyoliona Kanisa likikua katika Romania,” Meg anasema. “Mara moja tukafikiria kuwa familia ya Stanica inapaswa kuhusishwa. Tuliwaalika kushiriki, na walikuwa ni wenye shauku!”
Usiku ule wa shughuli, akina Stanica walikuwa bado hawajafika wakati wa kuanza ulipofika.
“Tulikuwa na hofu kwamba pengine wasingekuja,” Meg anakumbuka. “Lakini katika wakati muafaka, nao waliingia kupitia mlangoni. Akina Stanica walitoa ushuhuda mzuri juu ya injili na Kanisa. Pia walipata kuongea na waumini wengine ambao walikuwa hawajaonana nao kwa muda mrefu.”
Waumini wa tawi walifungua mikono yao na kuwakaribisha akina Stanica. Jumapili iliyofuata, Meg kwa furaha alishangazwa kumwona Dada Stanica kanisani.
“Nilipotembelea tawi miezi michache baadae, yeye alikuwa bado akiendelea kuja!” Meg anasema. “Nafikiri nafasi ya kutoa ushuhuda wake na kuhisi ameshirikishwa na anahitajika katika tawi hakika vilimsaidia.”
Mawazo 4 kwa ajili ya kuhudumu kupitia Shughuli za Kanisa
-
Panga shughuli ambazo zinakimu mahitaji: Shughuli ni njia bora ya kukimu mahitaji mengi tofauti. Zinaweza kupangwa ili kukimu mahitaji maalumu ya mtu au kikundi. Zinapaswa pia kukimu mahitaji ya wale wanaoshiriki, iwe hitaji hilo ni kufahamiana vyema zaidi, kujifunza zaidi kuhusu injili, au kuhisi Roho.
-
Mwalike kila mtu: Unapopanga shughuli, fanya jitihada maalumu ya kuwaalika wale ambao wangenufaika kutokana na kushiriki. Pasipo kuwasahau waumini wapya, waumini wasioshiriki kikamilifu, vijana, vijana wakubwa waseja, watu walio na ulemavu, na watu wa imani nyingine. Toa mwaliko ukiwa na mapendeleo yao akilini, na elezea jinsi gani ungependa wao waje.
-
Himiza ushiriki: Wale unaowaalika watapata mengi zaidi kutoka kwenye shughuli hiyo endapo watapata fursa ya kushiriki. Njia mojawapo ya kuhimiza ushiriki ni kuwafanya watu binafsi kutumia vipawa vyao, ujuzi, na vipaji wakati wa shughuli.
-
Mkaribishe kila mmoja: kama rafiki zako wanahudhuria shughuli, fanya kila uwezalo kuwafanya wajisikie wamekaribishwa. Vile vile, kama unawaona watu usiowajua, kuwa rafiki nao na wakaribishe pia!
© 2020 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Imepigwa chapa Marekani. Idhini ya Kiingereza: 6/19. Idhini ya kutafsiri: 6/19. Tafsiri ya Ministering Principles, Julai 2020. Swahili. 16989 743