“Kuhudumu kupitia Kujitegemea,” Liahona, Agosti 2020
Kanuni za Kuhudumu, Agosti 2020
Kuhudumu kupitia Kujitegemea
Kuwasaidia wengine kuweza kujitegemea ni kutoa na kuhudumu katika njia ya Bwana.
Wengi wa wanafamilia yetu, marafiki zetu na majirani zetu wana hamu ya kuwa zaidi wenye kujitegemea. Kwa kutumia mpango wa Kanisa wa kuwezesha kujitegemea, waumini wa Kanisa wanapata fursa za kutumikia, kutunza, na kuhudumu huku wakiwabariki wengine kwa kanuni ambazo huleta “tumaini, amani na maendeleo makubwa zaidi.”1
“Nilikuwa Nyumbani”
Na Chrissy Kepler, Arizona, Marekani
Nilikuwa na hali ngumu kifedha baada ya talaka, nikijaribu kutafuta njia ya kurudi kazini baada ya kuwa mama wa kukaa nyumbani kwa miaka minane. Pia nilikuwa na hali ngumu kiroho, nikitafuta ukweli na imani, ingawa sikuwahi kukanyaga kanisani tangu nilipokuwa kijana.
Jumapili moja nilikuwa nikifua nguo nyumbani kwa dada yangu mkubwa, Priscilla, muumini wa Kanisa mwenye kushiriki kikamilifu. Nikiwa ningali huko, Priscilla alinialika kuhudhuria kanisani pamoja na familia yake—mwaliko wangu wa kwanza kwa zaidi ya miaka 15.
Mwanzoni nilisita, lakini usiku tu uliopita, nilikuwa nimemwomba Mungu anionyeshe jinsi ya kuwa karibu zaidi na Yeye. Baada ya kuhisi mvuto nafsini, nilihitimisha, “Kwa nini usiende kusikia na kujionea mwenyewe kama mtu mzima kwa moyo na macho yako mwenyewe?”
Tukiwa katika mkutano wa sakramenti, niligundua kipeperushi katika matangazo ya Jumapili kikitangaza kozi ya kuwezesha kujitegemea kwenye mapato binafsi. Sikuwa tayari kurudi kanisani, lakini nilihisi kuvutiwa na kozi hiyo ya wiki 12. Kwa kutiwa moyo na dada yangu na shemeji yangu, nilijisajili, nikitarajia kujifunza jinsi ya kutengeneza bajeti na kulipa madeni pekee. Mafunzo hayo, hata hivyo, yalinibadilisha kiroho.
Nilikuwa nimeshangazwa na ujumbe wa kiroho katika wiki chache za mwanzo darasani, lakini wakati wa somo la tatu, nilizidiwa na hisia za uthibitisho kwamba nilikuwa nyumbani na nilikuwa nikisikia kweli mpya lakini zisizo ngeni. Nilitoka darasani na kuendesha gari moja kwa moja kwenda kumwona Priscilla. Nikitokwa machozi, nilimuuliza, “Ninawezaje kupata hisia zaidi kama hizi maishani mwangu?” Aliandaa mpango wa wamisionari kuanza kunifundisha.
Washiriki wa darasa langu la mafunzo ya kujitegemea walikuja kwenye masomo yangu niliyokuwa nikifundishwa na wamisionari ili kuniunga mkono. Walileta matokeo ya kudumu katika maisha yangu ya kiroho na walinisaidia kukuza ushuhuda juu ya injili na manabii wa siku za mwisho.
Katika muda niliochukua kumaliza kozi, nilifanya mabadiliko kadhaa ya kimwili na kiroho. Nilianza kazi mpya katika kampuni nzuri, na nililipa mikopo kadhaa.
Lakini baraka za kina, na tamu ambazo zilitokana na kozi zilijumuisha kuunda urafiki mzuri, kukuza uhusiano chanya na askofu aliyenitia moyo, kupata ushuhuda juu ya utoaji zaka, kupata kibali changu cha kuingia hekaluni, kupata endaumenti, na kushuhudia watoto wangu wawili wakubwa wakibatizwa.
Safari yangu kuelekea kujitegemea bado taratibu inafunuliwa, lakini kwa safari iliyosalia, nitaenzi mafunzo niliyopata na urafiki niliotengeneza.
“Nilitoka Kwenye Kila Darasa Huku Nikihisi Kupendwa”
Wakati alipotembelea Temple Square katika Jiji la Salt Lake, Utah, akiwa na mwanaye, Vincent, wa miaka 10, mnamo Desemba 2016, Katie Funk alijichukulia kuwa “mwenye kuridhika kuhusu kutokuwepo kwa ukweli wa uwepo wa Mungu.” Aliacha Kanisa akiwa na umri wa miaka 16, akawa mama asiye na mume akiwa na miaka 17, akaanza kujichora mwilini, na kuanza kutumia kahawa. Lakini wakati wa ziara hiyo ya Temple Square, Vincent alihisi Roho Mtakatifu na akamuuliza mama yake kama angeweza kufundishwa na wamisionari.
Licha ya kazi zake mbili, masaa 80 kwa wiki, Katie alijifunza injili pamoja na Vincent, akitafiti majibu ya maswali yake kwenye masomo toka kwa wamisionari. Kufikia msimu wa kiangazi wa 2017, alianza kuhudhuria mikutano ya Kanisa, ambapo alipata kujifunza kuhusu kozi za Kanisa kuhusu kujitegemea.
“Niligundua kwamba zilikuwa kitu ambacho kingeweza kunisaidia,” alisema. “Labda nisingehitaji kufanya kazi mbili au kutegemea wazazi wangu kwa maisha yangu yote yaliyosalia.”
Katie aliita kozi yake kuwa ya “kuimarisha kimwili na kiroho kwa njia ya ajabu,” si kwa sababu ya aliyojifunza tu lakini pia kwa sababu ya jinsi kikundi chake cha mafunzo ya kujitegemea kilivyomkubali na kumhudumia.
© 2020 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Imepigwa chapa Marekani. Idhini ya Kiingereza: 6/19. Idhini ya kutafsiri: 6/19. Tafsiri ya Ministering Principles, August 2020. Swahili. 16723 743