“Kushiriki Nuru ya Mwokozi wakati wa Krismasi,” Liahona, Desemba 2020
Kanuni za Kuhudumu, Desemba 2020
Kushiriki Nuru ya Mwokozi wakati wa Krismasi
Wafikirie wale unaowahudumia. Utawezaje kuwasaidia kuwa karibu na Kristo Krismasi hii?
Wakati tunamkumbuka Mwokozi Yesu Kristo mwaka mzima, Krismasi ni msimu ambao tunasherehekea zawadi kubwa zaidi iliyowahi kutolewa: “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee” (Yohana 3:16). Tunapohudumu wakati wa Krismasi, sisi pia tunaweza kutoa zawadi ambazo husaidia wengine kumkaribia Mwokozi. Ni ya kupendeza kujifikiria sisi wenyewe kama wenye kujifananisha na zawadi iliyotolewa na Baba wa Mbinguni.
Bado Ninathamini Zawadi hiyo
Susan Hardy, California, Marekani
Nilipokuwa na umri wa miaka 11, mwalimu wangu wa Shule ya Jumapili, Kaka Deets, aliliambia darasa letu kwamba ikiwa tungekariri Makala za Imani na kumuelezea maana zake, angetununulia maandiko yetu wenyewe.
Kaka na Dada Deets walikuwa wanandoa vijana, waliokuwa wameanza maisha. Sikuwa na uhakika kuwa Kaka Deets angeweza kununua zawadi kwa ajili ya mtu yeyote. Lakini niliamua kwamba ikiwa anafikiria Makala za Imani ni muhimu kukariri, ningeitikia changamoto.
Baada ya kumaliza zote 13, muda ulipita na nikasahau juu ya ahadi yake.
Kisha, Siku ya Krismasi, nilipokea kifurushi kilicho na jina langu juu yake. Nilikifungua na kukuta seti ya maandiko kwa ajili yangu, pamoja na kadi ikinitia moyo nizisome kila wakati. Hiyo ilikuwa mnamo 1972, na mpaka leo bado ninayo maandiko hayo. Ni ya thamani kwangu.
Haikuwa gharama ya zawadi hiyo lakini fadhila aliyonionyesha na ile dhabihu aliyokuwa tayari kuifanya kwa ajili yangu iliniacha na hamu kubwa ya kusoma neno la Mungu. Ninajaribu kufuata mfano wa Kaka Deets wa kuhudumu kwa kutoa zawadi zenye maana kwa wale wanaonizunguka, nikitumaini kuwa naweza kubariki maisha ya wengine kama yeye alivyobariki yangu.
Mwaliko wa Kushiriki
Richard M. Romney, Utah, Marekani
Wakati wale wanaopanga mjumuiko wa Krismasi wa kata yetu waliponiomba nimtembelee mtu fulani ambaye ni muumini asiyeshiriki kikamilifu na kumwalika kushiriki katika programu, lazima nikiri nilikuwa na wasiwasi. Nilikuwa nimekutana na Darren mara moja tu hapo awali, wakati alipokuwa ameshiriki katika shughuli iliyopita ya kata. Alikuwa amevaa chuma cha pikipiki kwenye paji la uso wake. Nywele zake nyeupe ndefu zilikuwa zimefungwa na kutengeneza mkia, alikuwa na ndevu zote nyeupe, na mikono yake ilikuwa imefunikwa na michoro.
Sasa, nikiongozana na mjumbe wa kamati, nilikuwa nimesimama mlangoni kwa Darren, nikijiuliza ni nini angeweza kusema. Alituomba tuingie ndani, na tulimwambia kwa nini tulikuwa pale. Alisema, “Ah, ningependa kufanya hivyo!”
Alifanya kazi ya kushangaza, kusaidia kufanya shughuli hiyo kuwa na maana kwa wengi. Muda mfupi baadaye, mimi na mwenzangu mhudumiaji tuliombwa kumtembelea Darren mara kwa mara. Mara zote anaonekana kufurahia kutuona, na tumekuwa na mazungumzo mazuri. Ninashukuru msukumo wa kumualika kushiriki katika programu ya shughuli ya kata uliongoza kwenye kuwa na uhusiano mzuri.
Kuhudumia wengine wakati wa Krismasi
Hapa kuna mambo kadhaa unayoweza kufanya ili kuhakikisha wale unaowahudumia watajua unawafikiria, hasa katika kipindi hiki cha mwaka.
-
Wakati mwingine kupiga simu au ujumbe wa maandishi hufanya maajabu. Kuanzisha mazungumzo kwa salamu rahisi ya “Halo, unaendeleaje?” kunaweza kuleta utofauti.
-
Jiunge kwenye sherehe zao wakati inapofaa. Krismasi inaweza kuwa wakati mzuri wa kujifunza juu ya imani tulizonazo zinazofanana. Unaposhiriki imani na kuwasikiliza wengine, unafungua mlango wa uelewa mkubwa.
-
Waombee kwa jina. Muombe Baba wa Mbinguni akusaidie kufikiria njia za kuwaleta karibu na Mwanawe.
-
Zawadi ndogo mara nyingi hukumbukwa vyema. Zawadi sio lazima ziwe zilizochanganuliwa ili ziweze kupendwa. Zawadi ya wakati, zawadi ya kusikiliza, kushiriki picha au kumbukumbu—hizi zote zinaweza kuwa zawadi za moyoni.
-
Toa zawadi ya ushuhuda. Waombe washiriki nawe upendo wao wa Mwokozi, na jitolee kushiriki upendo wako Kwake pamoja nao.
-
Waalike wengine kuhudhuria ibada ya Krismasi. Watu wengine wanataka kuabudu lakini hawajui waende wapi. Waalike waje kuabudu pamoja nawe.
-
Jaza nyumba zao kwa amani. Acha wafahamu kuwa wamisionari wana ujumbe maalum wa Krismasi ambao wanaweza kuushiriki, ambao utaleta tumaini na upendo mioyoni mwao.
Kuwahudumia Wote kama Mkutano
Mahitaji ya kila mkutano ni ya kipekee. Wengine hufaidika kwa kuandaa shughuli kubwa. Mikutano mingine inaweza kufaidika kutokana na kitu kidogo na rahisi. Wale wanaohusika katika kupanga na kuandaa shughuli kwa sala wanafikiria jinsi ya kukidhi mahitaji ambayo yapo.
-
Waumini kutoka vigingi vitatu huko Paris, Ufaransa, walisaidia kuunga mkono mkutano wa Light the World ambao ulijumuisha onyesho la talanta na maonyesho ya mitindo. Waliandaa vitu ambavyo walivigawa kwa wakimbizi na watu wanaopitia ukosefu wa makazi.
-
Kigingi Kikuu cha Charlotte North Carolina kilifanya tukio la “Krismasi kote Ulimwenguni” kwa ajili ya jamii, pamoja na mjumuiko kumsherehekea Kristo kupitia chakula, utamaduni wa kimataifa wa Krismasi, muziki, miradi ya huduma, na onyesho la watoto la kuzaliwa kwa Yesu.
-
Waumini wa Kigingi cha Vero Beach Florida walijiunga katika ukumbusho wa jamii wa kwa nini tunasherehekea Krismasi. Wanasesere walitolewa kama misaada kwa jumuia za kutoa misaada. Kwaya ya watoto wa msingi ilifanya onyesho, na makanisa mengi yalikuwa na vibanda vilivyoonyesha taarifa.
-
Kigingi cha Jacksonville Florida South kiliwasilisha onyesho la Mkombozi wa Ulimwengu kwa jamii.
© 2020 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Imepigwa chapa Marekani. Idhini ya Kiingereza: 6/19. Idhini ya kutafsiri: 6/19. Tafsiri ya Ministering Principles, December 2020. Swahili. 16727 743